Makala
Glovu za ngumi zinapokuwa nzito..!
Julius Sarota
Toleo la 135
26 May 2010
WANAMASUMBWI waingiapo ulingoni huvaa glovu zinazoendana na uzito wao, na kwa kawaida wanaoingia ulingoni kupigana ni lazima wawe na uzito ulio sawa au unaokaribiana.

Kanuni na taratibu nyingine zaidi ya uzito unaolingana, ni uwepo wa refa anayetoa mamuzi kuhusu mchezo unavyoendelea. Refa huyu huwa ndani ya ulingo.

Tatu, kuna majaji wanaokaa pembeni ya ulingo. Kazi ya majaji ni kutoa pointi kwa kila mchezaji anapompiga mwenzake ngumi maeneo  yanayoruhusiwa; hasa pointi muhimu ni pale kipigo kwa mpinzani wako kinapokuwa maeneo ya uso au sehemu ya mbele ya kichwa .

Pointi hizo, kama mmoja wapo hakupigwa kile wanamasumbwi wanachoita “pigo la ushindi” (knock –out), hujumlishwa ili kumpata mshindi wa pointi.

Hata hivyo, kuna refa wengine ambao siyo rasmi. Refa hao wasio rasmi wana mamlaka sawa na yule refa rasmi aliye ndani ya ulingo. Hao wasio rasmi ni wawili; kuna waliopo kona nyekundu na kuna waliopo kona ya bluu.

Kona nyekundu wanakaa kocha, wasaidizi wa kocha na wataalamu wengine wa mmojawapo wa mabondia waliopo ulingoni.

Vivyo hivyo, kona ya bluu wanakaa kocha, wasaidizi wake na wataalamu wengine wa mpiganaji aliyepo kona ya bluu.

Marefa hawa ambao si rasmi huweza kutoa uamuzi wa mchezo unaoendelea. Uamuzi wao unamaliza mchezo bila refa rasmi kupinga. Kwa mfano; kona mojawapo ikiona mchezaji wake amezidiwa na mpinzani, hutupa taulo ndani ya ulingo na mara moja refa rasmi husimamisha mchezo. Ushindi humwendea yule bondia mwingine.

Refa rasmi naye anaweza kuokoa bondia, lakini ni pale anapoona mmojawapo kaelemewa kiasi cha kukaribia kutokutoa upinzani wa aina yeyote au mchezaji anayetakiwa kuokolewa ameonyesha kukosa uwezo wa kurusha ngumi za kujitetea dhidi ya mpinzani wake.

Kanuni na taratibu za mchezo wa ngumi hufanya niufurahie; hasa pale tunapotafakari kwamba kona yako inaweza ikuokoe usiendelee kupigwa hadi ukaumizwa.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, nadhani mwaka 1997, wakati akichangia mada ya utandawazi kwa viongozi wa Serikali, mjini Dodoma, alieleza kuwa nchi tajiri zinaposhinikiza utandawazi bila ya masharti ya kusaidia nchi changa, ni kuzionea nchi maskini.

Alisema kufanya hivyo ni sawa na kumruhusu Nyerere aiingie ulingoni na Mike Tyson, ambapo matokeo ni wazi kuwa Nyerere atapata pigo la ushindi (knock out)!
Katika kipindi hicho cha miaka ya mwishoni mwa 1990, Mike Tyson alikuwa ni bingwa wa uzito wa juu wa masumbwi duniani. Wapinzani wake wengi katika kipindi hicho walipigwa mapema na ‘pigo la ushindi’.

Mara nyingi Mike Tyson alitoa kwa wapinzani wake ‘pigo la ushindi’ hata kabla ya raundi ya nne kati ya raundi 12 zinazotakiwa kuchezwa ili mechi imalizike kwa pointi za majaji kujumlishwa kupata mshindi.

Si nia katika makala hii kujadili kanuni na taratibu za mchezo wa ngumi, ila kuutumia mchezo huu kwa lengo la kuhitaji tuelewane. Hii inatokana, kwa mtazamo wangu, kuwa mchezo wa siasa unafurahisha na kuvutia watazamaji kama ulivyo mchezo wa ngumi!

Michezo yote, siasa na ngumi inafurahisha. Hata hivyo, katika mchezo wa siasa ukianza kuelemewa na kuanza kuyumbayumba katika chama chako, (kambi yako) hasa katika siasa za nchi za Afrika, hawatakuokoa. Matazamio makubwa ni kuokolewa na kambi ya chama kimojawapo cha waliokuwa wapinzani wako.

Kama ukiyumbayumba na kuokolewa na taulo la mpinzani wako, inaonyesha kuwa siasa uliingia kwa malengo ya kujitafutia maslahi binafsi na si maslahi ya wananchi walio wengi na ambao una wawakilisha.

Kwa lugha ya kimchezo wa ngumi, ni sawa na kuiingia ulingo wa siasa lakini glovu ulizoingia nazo zimekubana na usipoangalia utapigwa knock out.

Tabia ya kuyumbayumba ni tabia ya mtu asiye na itikadi ya dhati ya uumini wake katika kuleta maendeleo kwa wananchi walio wengi.

Tabia nyingine ya siasa za Kiafrika ni wanasiasa wake, walio wengi, kutokuchagua wapigane na nani. Ni wazi kuwa ukichagua kukipigana na tajiri , tarajia kushindwa kwa knock out; hasa kama moyo wako haukuwa umejengeka kwa itikadi uliyoiamini kwa dhati kabisa kuwa umeingia siasa kuokoa walio wengi.

Tumepata kusikia, nchini petu, wanasiasa wakisema bila uoga kuwa baadhi ya wawekezaji wamerubuni viongozi wetu hadi wakasaini mikataba ndani ya hoteli, tena ya nje ya nchi. Lakini kabla jua halijatua, wanasiasa hao hao wanasema: Watanzania ee, jitajirisheni kwa kununua hisa huko nje ya nchi za wawekezaji wale wale ambao walituhumiwa kurubuni viongozi wetu kufanya mikataba hotelini!

Asilimia 80 ya Watanzania ambao ndiyo tunatarajia wasaidiwe wajikomboe  wanaishi vijijini kwa dhiki kubwa -  afya zao nduni, watoto wao wengi wanasoma wakiwa wamekaa chini kwa kuwa hawana madawati, na kilimo chao ni cha jembe la mkono na hakiwapi uwezo wa kula na kusaza.

Leo tunapiga mbiu na kutangaza: Ndugu zangu eee, neendeni mkanunuwe hisa za makampuni yanayochimba madini nchini! Hivi kweli wanajua hisa katika makampuni ni nini? Au tunaongelea matajiri wanaoshi mjini; hasa jiji la Dar es Salaam?

Tungeweza kuwasaidia Watanzania hao wa vijijini kwa kuwahamasisha kuwa baada ya msimu wa mazao, sehemu ya mapato ya mauzo wayatumie kuingia mkataba na wenye maduka vijijini ili kupanua mtaji wa duka/maduka hapo vijijini.

Wanasheria wa kuandika mikataba wanaweza kuwasaidia kuandika mikataba midogo kama hiyo kwa malipo kidogo. Na wala hatuzungumzii mikataba ya ushirika; maana hiyo ina utaratibu tofauti, na wala hatuongelei SACCOS; bali mikataba ya mtu kupewa hisa kiasi cha mtaji wake.

Wanaweza wasiwe watu wengi. Lakini wakiwa na mkataba unaoleweka na rekodi za mauzo zikiwekwa vizuri, ni wazi watajua faida ni kiasi gani na kugawana kwa kuzingatia mtaji wa kila mmoja.

Watu wa namna hii wanaweza kujineemesha pole pole, na hatimaye kuweza kununua vitendea kazi kama matrekta na kuajiri wengine. Kwa njia hiyo, wananchi vijijini watajitajirisha pole pole!

Lakini kuhamasisha wananchi kama hao kununua hisa za makampuni ya nje zinazouzwa kwa dola, si siasa za kuleta maendeleo ya wapiga kura walio wengi; bali ni siasa ya kujitafutia umaarufu kwenye televisheni, magazeti na redio.

Kama kuna wanasiasa wa namna hiyo, wanafaa waitwe watu wanaoyumbayumba kama ndara (flip – flop).

Neno hilo la kuyumbayumba kama ndara linatumika sana kwenye kampeni katika uchaguzi kwenye nchi zile zenye siasa za kushindana kwa hoja, sera na msimamo wa kusimamia masuala ya msingi.

Kwa mfano, mwaka 2001, niliona kwenye televisheni ya CNN, muhtasari wa mdahalo wa wagombea wa uwaziri mkuu nchini Australia.

Katika mdahalo huo, mgombea wa chama cha kiliberali, Bw. John Howard, alitumia muda mwingi kumtuhumu mpinzani wake, Bw. Kim Beasley wa chama cha Leba kuwa hafai kuongoza nchi kwa kuwa ni mtu anaye flip – flop.

Suala alilolitumia Bw. Howard kumtuhumu mpinzani wake huyo kuwa anayumbayumba kama ndara lilihusu jinsi ya kushughulikia wakimbizi.

Wakati wakiendelea na kampeni kuna meli ilikamatwa ikiwa baharini na wakimbizi takriban 200 wakitoka nchi ya Afghanistan. Meli ile kabla ya kukamatwa ilipata matatizo na uhai wa watu ukawa mashakani.

Matatizo hayo ndiyo yalisababisha waliokuwa wanaiongoza meli hiyo waombe msaada uliosababisha wakamatwe. Bila tatizo hilo, walitaka waingie kimya kimya.

Bwana Howard akawa na msimamo kwamba, watu hao hata kama meli yao imepata matatizo hawataruhusiwa kukanyaga ardhi ya nchi yake, hasa kwa kuwa walikuwa wanaingia kisivyo halali. Hivyo, alitaka warudishwe kwao.

Mpinzani wake akasema kwa kuwa wamepata matatizo, kiubinadamu waruhusiwe kuingia Australia na wapelekwe kwenye makambi yanayoshughulikia wakimbizi na kila mmoja achunguzwe kibinafsi, wasihukumiwe wote kwa pamoja.

Bwana Howard akapata mwanya kwamba mpinzani wake anayumbayumba kama ndara; maana sheria ya nchi inasema wakimbizi waonakuja kwa njia isiyo halali kama walivyokuwa wanataka kuitumia wasiruhusiwe kuingia.

Katika uchaguzi, Bwana Howard alipata ushindi kama tulivyozoea kuuita Tanzania ‘ushindi wa kishindo’. Ilisemekana angeweza kushinda, lakini ushindi wa kishindo umetokana na wananchi wengi wa nchini kwake kumuona mwenye msimamo thabiti wa kusimamia masuala ya msingi.

Kwa wenzetu, mwanasiasa mwenye kuyumbayumba kama ndara hana nafasi.

Suala lingene ambalo wanasiasa wa nchi zetu maskini wanalo ambalo nalo kwa kiasi fulani ni sawa na kuyumbayumba kama ndara, ni majibu ya kukatisha tamaa.

Sikumbuki kwa usahihi ni mwaka gani hasa, lakini kati ya mwaka 2001 na 2003 hivi, kuna mwanasiasa alisema baadhi ya yale yaliyomo kwenye ilani ya uchaguzi iliyowapa ushindi hayatekelezeki.

Kwa wenzetu ambapo kinywa kikikosea hata kidogo kinaweza kuwakosesha ushindi, majibu ya kwamba baadhi ya masuala mliosimamia kwenye kampeni hayatekelezeki, ni sawa na kusema uchanguzi unaofuata mmejipa nafasi ndogo ya kushinda au mnaweza kubanwa mjiuzulu hata kabla ya uchaguzi.

Majibu ya wenzetu huwa ni ya kujenga. Kama kuna suala mlikuwa mnalisimamia kisera na mmebaini kuwa kwa wakati huo halitekelezeki, majibu ya kuwapa matumaini wananchi ni kusema kwa sasa suala hili tunaliahirisha na tutalianzisha au kulishughulikia baada ya  miaka mitatu hivi.

Baada ya miaka mitatu inawezekana uchaguzi ukawa umeisha pita na mnaweza kuwa mmeshinda au kushindwa, na hivyo kupata muda tena wa kutafakari sera mbadala ya lile ambalo mmesema halitekelezeki.

Kwa mfano, nimesoma katika mtandao kuwa Serikali ya sasa ya Australia iliingia madarakani na mojawapo wa sera yake kuu ilikuwa kushughulikia, wakiingia madarakani, suala la kupunguza madhara ya ongezeko la gesi ya ukaa kutoka viwandani.

Waliahidi kuwa hata kama nchi nyingine zilizoendelea zimeshindwa kupunguza matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani, hasa kuongezeka kwa joto kutokana na nchi zenye viwanda kutoa viawango wa juu vya hewa ya ukaa, wao (Australia) watabana viwanda vitimize viwango. Na Australia itakuwa ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine zilizoendelea katika suala hilo.

Hata hivyo, serikali hiyo, kukiwa uchaguzi umekaribia, wameeleza kuwa sera hiyo kwa sasa hawataitekeleza ila wanaiahirisha hadi baada ya miaka mitatu.

Kabla ya kuhitimisha makala hili, tuangalie msemo wa wahenga unaosema kiatu usichokivaa huwezi kujua kinabana namna gani. Kama wewe si mwanasiasa kwa nini ujadili siasa?

Wanasiasa wengi wa Tanzania huwa na jibu zuri sana kwa swali la namna hiyo. Jibu lao huwa: Siasa tuachie sisi, au kama unataka nawe ingia ulingoni tupambane.

Ni kweli siasa za nchi za Kiafrika huwezi kujua waliozivaa zinawabana namna gani, hasa jinsi ya kutenganisha namna ya kusaidia walio wengi ambao ni masikini wa vijijini dhidi ya matajiri wachache na wawekezaji wa nje.

Na tumalizie makala hii kwa kuangalia tulichojifunza. Suala kubwa ni kuwa tusiingie kwenye siasa kwa malengo binafsi, hasa kujitajirisha. Hili ndilo tumelilinganisha na kuvaa glovu zinazoendana na uzito wa itikadi yako ya unavyotaka wananchi walio wengi wachangie na kushiriki kuleta maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla.

Pili, tumejifunza kwamba tukiwa wanasiasa tusiwe watu wa kuyumba yumba kama ndara (flip – flop). Tatu, tukiwa wanasisa tusiwe na majibu yasiyotoa matumani au yenye kupunguza hamasa ya wananchi. Majibu kama sera hii au suala hili halitekelezeki yanapunguzu matumaini. Msomaji tafakari!!

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Julius Sarota
jsarota@hotmail.com

Toa maoni yako