- Si siri, nasi twamhitaji King Cobra wetu
WIKI iliyopita hakuna habari zilizonisisimua katika duru za kimataifa kushinda zile zilizotawala vyombo vya habari vya Zambia.
Habari hizo ni hatua ya Rais Michael Sata kurejesha serikalini umiliki wa kampuni kubwa ya simu ya nchi hiyo – Zamtel.
Kilichotokea huko Zambia ni kile ambacho nilimtarajia Rais wetu, Jakaya Kikwete, angekifanya alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, lakini hakukifanya, na hajakifanya hata sasa anapomaliza awamu yake ya pili na ya mwisho ya uongozi.
Lakini kabla ya kulijadili hilo, nirejee kwanza kwenye hatua hiyo ya aina yake iliyochukuliwa na Rais huyo wa Zambia ambaye ni maarufu nchini humo kwa jina la utani la King Cobra.
Wakati wa kampeni za urais za mwaka jana, King Cobra aliwaahidi Wazambia kwamba kama watamchagua kuingia Ikulu, moja ya mambo atakayoyafanya haraka ni kuirejesha Zamtel mikononi mwa umiliki wa serikali kwa kuwa iliuzwa kifisadi kwa kampuni ya LapGreen ya Libya.
Nina hakika ahadi hiyo ya King Cobra ni miongoni mwa zilizowafanya wapiga kura wa Zambia wampigie kura nyingi zilizomwezesha kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Tofauti na marais wengine wa Afrika ambao wakati wa kampeni huwaahidi wapiga kura kuwa wakichaguliwa urais watapambana na ufisadi lakini wakishaingia ikulu hawafanyi kitu, Michael Sata yeye alianza mara moja kutekeleza ahadi zake dhidi ya ufisadi.
Novemba mwaka jana aliunda timu maalumu ya wataalamu kuchunguza mauzo ya kampuni hiyo ya umma kwa mwekezaji huyo kutoka Libya (LapGreen). Timu hiyo iliongozwa na Waziri wa Sheria, Sebastian Zulu.
Katika ripoti yake, timu hiyo ilithibitisha kile ambacho Wazambia wengi walikuwa wakikilalamikia kwa muda mrefu; yaani kwamba Zamtel iliuzwa kwa ‘bei poa’ kwa kampuni hiyo ya Libya.
Kwa maneno mengine, bei ambayo LapGreen iliuziwa Zamtel na Serikali ya Rais wa wakati huo, Rupiah Banda, ilikuwa hailingani na thamani halisi ya kampuni hiyo. Licha ya kuwa na mali nyingi (majengo nk) Zamtel iliuzwa kwa dola milioni 257 tu.
Lakini pia timu hiyo iligundua kwamba kulikuwa na ufisadi mkubwa ulioshamiri katika ngazi zote za mchakato wa kuiuza kampuni hiyo ya umma kwa mwekezaji huyo wa Libya.
Ni baada ya kuipokea ripoti hiyo na kuisoma, King Cobra aliamua, wiki iliyopita, kushambulia kwa kuirejesha kampuni hiyo serikalini.
Alifanya hivyo kwa kutengua mauzo hayo, kusimamisha akaunti zake na kuvunja bodi iliyokuwepo na kuweka mpya.
Ingawa pia, wiki hiyo hiyo, Rais Sata alitengua mauzo ya benki iliyokuwa ya umma ya Finance Bank iliyouzwa kwa dola milioni 5.4 tu kwa kampuni ya Afrika Kusini inayoitwa First Rand Group, utenguzi wa mauzo ya Zamtel ndio uliopokewa kwa furaha kubwa mno na Wazambia wengi.
Ndugu zangu, kilichonisisimua kuhusu King Cobra si tu ujasiri aliojipa wa kufanya kitu ambacho marais wengi wa Afrika (akiwemo Kikwete wetu) hawana ujasiri wa kukifanya, lakini pia ni namna alivyoliendesha zoezi la kuirejesha kampuni hiyo mikononi mwa serikali kwa ufanisi mkubwa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Zambia, hakuna huduma zozote zilizotetereka Zamtel wakati wa utekelezaji wa mchakato huo. Aidha, hakuna ajira hata moja iliyopotea kati ya 1,700 zilizomo katika kampuni hiyo.
Labda nisisitize hapa mapema kabisa kwamba King Cobra, hakuchukizwa na kuuzwa kwa Zamtel kwa LapGreen ya Libya; bali alichukizwa na kitendo cha kampuni hiyo ya umma kuuzwa kwa ‘bei poa’ mno kiasi cha kuwafanya Wazambia wote waonekane ni mabwege.
Kwa maana hiyo, LapGreen au kampuni nyingine yoyote inaweza kuanzisha mazungumzo mengine na Serikali ya King Cobra ya kuinunua upya Zamtel – tofauti tu ni kwamba safari hii itauzwa kwa bei stahiki, na si ya kutupa!
Tukirejea ya kwetu hapa nyumbani Tanzania, swali la kujiuliza ni hili: Je, tuna fundisho lolote tunalolipata kutoka katika hicho kilichojiri Zambia wiki iliyopita?
Jibu langu ni kwamba lipo funzo kubwa tunalolipata; nalo ni kwamba ipo siku moja hayo yaliyotokea Zambia yatatokea pia Tanzania.
Kwa maneno mengine, watawala wetu waliosimamia uuzwaji wa makampuni yetu ya umma kwa “bei poa” baada ya kukatiwa ten percent zao, hawako salama kabisa kama ambavyo pia hazipo salama kabisa hizo kampuni zilizoyanunua.
Ningeweza kutaja hapa orodha ndefu ya makampuni yetu mengi ya umma yaliyouzwa kwa ‘bei poa’ za kifisadi (ya hivi karibuni ikiwa UDA), lakini niishie tu kwenye uuzwaji wa iliyokuwa benki ya umma – NBC (1997) Limited.
Nimechagua kuzungumzia NBC tu kuliko makampuni yetu mengine ya umma yaliyouzwa kifisadi, kwa sababu mauzo hayo ya NBC yalipigiwa kelele mno na Watanzania wengi akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, lakini aliyekuwa Rais wetu, Ben Mkapa (Mr. Clean?), aliziba masikio yake kwa pamba!
Benki hiyo iliyokuwa imesheheni raslimali nyingi, yakiwemo majengo karibu miji mikuu ya mikoa yote na wilaya, iliuzwa na Mr. Clean wetu kwa Sh. bilioni 15 tu kwa ABSA ya Afrika Kusini!
Tena jambo la kushangaza ni kwamba wakati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, akiendesha kampeni ya kuinusuru benki hiyo ya umma isiuzwe, Mr. Clean alikuwa akiendelea na mchakato huo kwa kasi; huku wakati huo huo akiwa ameomba mkopo wa Sh. milioni 500 kutoka ABSA kwa ajili ya kampuni aliyoianzisha na mkewe ya ANBEM.
Hapo, huhitaji kuwa msomi kuuona mgongano wa kimaslahi (conflict of interest) wa waziwazi katika uuzaji huo wa NBC.
Na pengine ndiyo maana uuzaji wa benki hiyo unaisumbua nafsi ya Mkapa mpaka leo, na pengine ndiyo sababu vilevile hupendelea kujikosha kuhusu uuzaji huo kila anapopata fursa nzuri ya kufanya hivyo kama alivyofanya wakati wa kampeni za ubunge za Igunga, Septemba mwaka jana.
Akihutubia mkutano wa kampeni huko Igunga, Mkapa alisema hivi: “Wakati naingia madarakani kulikuwa na benki moja ya biashara – NBC, lakini ilikuwa inaomba ruzuku serikalini; kitu ambacho hakikuwa sahihi.
“Tukaibinafsisha kwa kuwa huwezi kuwa na benki ya biashara inayoomba ruzuku. Wanasema nimeuza benki yetu, si hivyo. Nimeuza madeni yetu na kusaidia nchi.”
Huo ndio umekuwa utetezi wa Mkapa kila mara anapozungumzia uuzaji wa NBC; kwamba eti aliiuza kwa kuwa ilikuwa inaomba ruzuku serikalini! Anasahau kwamba tuhuma zinazomwandama si tu kuuza benki ya umma kwa mwekezaji aliyekuwa na maslahi naye ya kibiashara (ABSA), lakini kuiuza kwa ‘bei poa’ mno sawa na ya kutupa!
King Cobra (Michael Sata) hamshutumu Rais aliyemtangulia, Rupiah Banda, kwa kuiuza Zamtel kwa NetGreen ya Libya; bali anamtuhumu kwa kuiuza kampuni hiyo kwa ‘bei poa’ mno!
Nasi katika Tanzania hatumtuhumu Mkapa kwa kuiuza NBC kwa ABSA, lakini kwa kuiuza kwa ‘bei poa’ mno sawa na ya kutupa – bei inayotufanya Watanzania tuonekane wote mabwege!
Nina hakika hata kama itaundwa timu ya wataalamu leo (miaka 15 baada ya mauzo hayo) na kuchunguza bei ambayo NBC (1997) iliuzwa kwa ABSA, bado matokeo yataonyesha kwamba kwa mali iliyokuwanazo zama hizo (majengo mikoa yote), bei ya shilingi bilioni 15 haikuwa stahiki yetu hata kidogo!
Nihitimishe hivi: Yaliyotokea Zambia, wiki iliyopita, yanatuthibitishia kwamba tunachohitaji Tanzania ni kumpata King Cobra wetu atakayechunguza mashirika yetu yote ya umma yaliyouzwa kifisaadi, na kisha kutengua mauzo hayo; hata kama miaka 20 imepita tangu yauzwe!
Kwa maneno mengine, watawala waliojineemesha kifedha kwa kuuza mashirika yetu ya umma kifisadi, wasijione salama kabisa hata kama miaka 20 itapita hawajaguswa. Vivyo hivyo kwa hao ‘wawekezaji’ walioyanunua kwa bei poa.
Na wala sizungumzii NBC peke yake. Nazungumzia pia viwanda vyote vya nguo, nazungumzia pia viwanda vyote vya ngozi, nazungumzia pia mashamba ya Mbarali na ya mkonge, nazungumzia pia migodi yetu, nazungumzia pia mashirika kama UDA nk, na nazungumzia pia nyumba zetu za serikali katika maeneo maalumu ambazo wakubwa waliuziana wenyewe kwa wenyewe kwa bei poa.
Tunachosubiri tu Watanzania ni kumpata King Cobra wetu; yaani rais mpya mwenye ari na nia ya kweli ya kupambana na ufisadi, atakayewapindulia meza mafisadi kwa kutengua mauzo hayo na kuyarejesha mashirika hayo serikalini ili yauzwe upya!
Nina hakika Kikwete siye rais huyo tunayemsubiri kumpindulia meza Mkapa na wenzake waliouza mali za umma kwa ‘bei poa’.
Lakini pia naamini King Cobra wetu hawezi kuibukia CCM hii ya sasa iliyopoteza kabisa mwelekeo!
Tafakari.
Maoni ya Wasomaji
Very well said Mbwambo.....
Very well said Mbwambo......hakika rais Sata wa Zambia ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wetu...cha msingi na kutia matumaini ni kuwa iko siku nasi watanzania tutapata kiongozi wa namna ya Sata..atakayeshughulikia uuzaji haramu wa mali za umma tz...sio tu mashirika ya umma bali hata migodi yote ya madini inayoendeshwa kwa manufaa ya wageni wachache.Mi na hakika kuwa nchi wala haiitaji kuwa na viongozi wengi aina ya Sata bali hata rais tu akiwa makini na mzalendo anaweza kuleta mabadiliko makubwa kwani kinachotumaliza tz ni ukosefu wa utawala wa sheria(rule of law)....kama unashughulikia wezi wa mali za umma kwa kuwafilisi na kuwaswaga jela hata discipline inakuwepo nchini...watu wataogopa kuiba(chukua mifano ya nchi kama china wanavyofanya kwa wezi)lakini kwa yanayoendelea sasa kwa watawala tulio nao ni kilio na msiba mkubwa kwa watanzania....hamna anaemwadhibu mwenzake kwa kuwa wote manyang'au.....wakigombania kutumaliza kama nchi.....inauma...
Tutampata King Cobra wetu
Tutampata King Cobra wetu kama na sisi wapiga kura tutatanguliza uzalendo zaidi kuliko matumbo yetu, na tukajitokeza kwa wingi kupiga kura kwa kiongozi mwenye ari na uchu wa nchi yetu. Kikwete na CCM ni uozo wa kupindukia!!
Hongera kwa kuandika makala
Hongera kwa kuandika makala nzuri. Mimi si mwana siasa lakini nawaza kwa sauti tuu kuwa hilo ulilolisema ni vyema likatokea, lakini wasiwasi wangu ni kuwa ikiwa CCM itachukuwa uongozi tena 2015, kweli Watanzania tutakuwa tumekwisha kabisa kabisa. Nakaa nikisali na kuomba kila siku isije ikatokea hivyo. Mungu Ibariki Tanzania. Amen
Wale wote waliouza mashirika
Wale wote waliouza mashirika ya uma kwa bei chee ipo siku watakiona.Hiyo dhambi waliyonayo ni yakudumu.
Makala Nzuri kama nyingine
Makala Nzuri kama nyingine ulizoisha andika!
Makala hii umeifupisha mno. Nilitarajia ungeenda mbali na kutaja watu kama James Welfensohn, ambaye alikuwa Rais wa Benki Kuu ya Dunia, kati ya mwaka 1995 hadi 2005. Bwana huyu au Rais huyu wa Benki ya Dunia wakati huo anasifika kwa kutetea nchi maskini, hasa kuhakikisha nchi maskini zinasamehewa madeni makubwa na ambayo hayalipiki.
Inaelezwa kuwa Baba wa Taifa, Nyerere, aliposikia uuzwaji wa Benki ya Biashara, NBC, alitaka kujua kwa nini?. Maana alijua, rejea hotuba yake ya Mei Mosi 1995 kuwa mashrika yanayouzwa ni yale yanayojiendesha kwa hasara, NBC haikuwa miongoni mwao. Hata hivyo ilipouliza viongozi wa wakati huo, ikiwemo AnnBEn, walimueleza kuwa Benki ya Dunia na IMF wametupa masharti kuwa lazima taasisi za fedha ziwe huru ikiwa ni pamoja na NBC kuuzwa.
Baba wa Taifa, hakuwa mtu wa kukubali majibu mapesi kwenye suala la Kitaifa. Inaelezwa pia kuwa Baba wa Taifa ikiwa safarini Amerika aliomba kukutana na Rais wa Benki ya Dunia wakati huo, Bwana Wolfesohn, na kumuuliza kuwa kwa nini mnalazimisha Serikali yetu ya Tanzania iuze Benki wa Watu wote, yaani NBC. Jibu lake ilikuwa ni kuwa si sisi, ila Serikali yenu ndiyo inataka Benki hiyo iuzwe!!
Hapo ndipo unaona umuhimu wa kuhitai naji Rais wa aina ya Micheal Sata au King Cobra.
Ipo siku Mungu atatusaidia tumpate King Cobra.
Makala Nzuri kama nyingine
Makala Nzuri kama nyingine ulizoisha andika!
Makala hii umeifupisha mno. Nilitarajia ungeenda mbali na kutaja watu kama James Welfensohn, ambaye alikuwa Rais wa Benki Kuu ya Dunia, kati ya mwaka 1995 hadi 2005. Bwana huyu au Rais huyu wa Benki ya Dunia wakati huo anasifika kwa kutetea nchi maskini, hasa kuhakikisha nchi maskini zinasamehewa madeni makubwa.
Inaelezwa sehemu nyingi kuwa Baba wa Taifa, Nyerere, aliposikia uuzwaji wa Benki ya Biashara, NBC, alitaka kujua kwa nini. Viongozi wa wakati huo walimueleza kuwa Benki ya Dunia na IMF wametupa masharti kuwa lazima taasisi za fedha ziwe huru ikiwa ni pamoja na NBC kuuzwa.
Baba wa Taifa, hakuwa mtu wa kukubali majibu mapesi kwenye suala la kitaifa. Inaelezwa pia kuwa Baba wa Taifa ikiwa safarini Amerika aliomba kukutana na Rais wa Benki ya Dunia wakati huo, Bwana Wolfesohn, na kumuuliza kuwa kwa nini mnalazimisha Serikali yetu ya Tanzania iuze Benki wa Watu wote, yaani NBC. Jibu lake ilikuwa ni kuwa si sisi, ila Serikali yenu ndiyo inataka Benki hiyo iuzwe!!
Hapo ndipo unaona umuhimu wa kuhitai naji Rais wa aina ya Micheal Sata au King Cobra
Makala yako ni nzuri sana na
Makala yako ni nzuri sana na namshukuru Mungu kukupa uhai.
Mimi naomba nikuuzie wazo langu japo najua litaonekana archaic na kichekesho kidogo!
Unaonaje ifike muda nafasi ya urais nayo tukodishe mgeni inapotokea kuwa na rais mwananchi ambaye haleti tija?
Kwa nini?
Kama kila uchaguzi utakuwa haufanyi vetting ya kuleta kiongozi mzuri ambaye anakuwa na interest za nchi yake at heart na anakuwa tayari kufanya maamuzi ya kweli na haki, na sio kubanwa na maslahi ya familia na maswahiba, basi ni wazi mfumo wetu wa chaguzi utakuwa umefeli!
Kama rais wa nchi anaweza kuona udhaifu wa mashirika ya serikali kwamba hayatendi kulingana na matarajio (mfano Netgroup Solution na Tanesco) je yeye huyu rais mwenyewe pale utendaji wake unapokuwa wa hovyo kama huyu tuliye naye unaonaje tutangaze kutaka rais mwingine kutoka nje ya nchi!
Sio kwamba nchi yetu inakuwa imeishiwa na watu wazuri, lah hasha, mfumo wetu unawafungia nje na wenyewe wanakaa kimya!
Vile vile, kama tunaleta the so called expatriates kuja kutufundisha kwenye idara nyeti kama jeshi, central bank, na hata usalama wa taifa na nyingine nyingi tu, je huyu wa juu kabisa ambaye hata akisafiri mara ngapi hajifunzihuko aendako ugaibuni?!
Inauma sana kama tunashindwa kuendelea kwa sababu ya uongozi! Ukikaa na watu wa Ulaya na ukaona wanavyoendesha nchi zao ambazo hazina rasilimali kama zetu, ni aibu sana kwetu waafrika- hatuna nidhamu ya maisha kwa wananchi wetu!
Tujadili!
Tuna miaka is chini ya 20 ya
Tuna miaka is chini ya 20 ya ku subiri mpaka tump ate huyo sata wetu naamini in katika Hawa vijana wanaochipukia Sasa hivi ndimo tuna mkombozi wetu . Lakini kwa wakati huo tutakuwa na Marengo mabovu na mahandaki tu badala ya makampuni na migodi.
Yamkini Tanzania tulipoteza
Yamkini Tanzania tulipoteza nafasi ya kumpata King Kobra wetu katika uchaguzi uliopita uliojaa hila na mizengwe na kumwibua huyu JK ambaye kwa vitendo vyake amethibitisha kuwa mstari wa mbele kama mpiganaji dhidi ya wanyonge wadhulumiwa. Chini yake mafisadi wako peponi na damu ya uchumi wa nchi inazidi kutiririka kuelekea kuzimu. Kibaya zaidi ni kampeni za wezi na vibaka inayopamba moto sasa ya kumsimika kibaka mwingine - Lowassa eti amrithi JK. Ikiwa hilo litatendeka; basi watanzania watahesabiwa kama walaaniwa wa walaaniwa. Mimi naamini kama Mbwambo anavyoamini kwamba hakuna King Cobra wa kutokea CCM hata awe nani na atokee wapi. Kwa maana nyingine hata kama Slaa, Lipumba, Mbowe, Mbatia au mpinzani yeyote " akiongoka" na kugombea uongozi kupitia CCM hawezi kuwa king Cobra na badala yake atakuwa "king Mjusi". Lakini kwa upande mwingine mpinzani yeyote toka chama kingine zaidi ya CCM anaweza kabisa kuwa "king cobra" Mungu atuepushe na ushetani wa CCM.