Makala
Yanayojiri Jirani
Hasira za Lucy Kibaki kumharibia mumewe?
Allan Sambu
Nairobi
Toleo la 008
19 Dec 2007

KAMA isingekuwa mazoea yake ya kufanya mambo yasiyotarajiwa mbele za watu, basi wengi wangefikiria kuwa shinikizo la uchaguzi limempanda kichwani mke wa Rais wa Kenya,  Mama Lucy Kibaki.

Lakini kwa kuwa ni mazoea yake kufanya yasiyotarajiwa mbele za watu, Wakenya wengi hawakushangaa sana pale alipomparamia mwendeshaji wa shughuli (MC), ama mshereheshaji katika Ikulu ya Nairobi, na kuanza kumtwanga vibao.

Ilikuwa ni katika moja ya hafla kubwa zinazofanyika Ikulu, wakati Rais Mwai Kibaki alipokuwa akiwatunuku nishani watu mbalimbali waliochangia ustawi wa Taifa la Kenya katika kipindi chote cha uhuru wake miaka 44 iliyopita.

Kwa bahati mbaya, wakati akitambulisha wageni mashuhuri, mshereheshaji huyo alikosea jina la mke wa Rais na badala ya kumwita Lucy Kibaki, akamwita kwa jina la Lucy Wambui; jina la hasimu wake mkubwa, Mary Wambui, anayesemekana kuzaa mtoto na Rais Kibaki. Lucy kama walivyo wakenya wengi, analo jina lake la kimila; Muthoni na si Wambui kama lilivyotamkwa na mshereheshaji.

Mara baada ya jina hilo kutamkwa, Lucy alisimama kwa gadhabu kutoka mahali alipokaa na kumfuata mshereheshi huyo, akamkwida na kuanza kumlamba vibao, huku Rais Kibaki na wageni wengine mashuhuri, wakishuhudia kwa mshangao. Haraka haraka, walinzi wa Ikulu wakachukua nafasi yao kwa kumbeba mshereheshaji huyo, Francis Musyimi hadi vyumba vya ndani ya Ikulu na nafasi yake ikachukuliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Francis Muthaura!

Wapigapicha kutoka katika vyombo vya habari waliokuwapo, pia walibanwa na maafisa wa usalama, wakanyang’anywa kamera zao na vipande vilivyonasa sakata hilo vikafutwa kutoka kwenye kamera hizo na baadaye wakarejeshewa kamera zao. Shughuli ikaendelea kama kawaida, huku Lucy akiwa bado amekaa kwenye meza ya wageni mashuhuri!

Hii si mara ya kwanza kwa Lucy kufanya vituko vya aina hiyo. Mwaka 2004, akiwa amevaa pajama, aliwahi kuvamia nyumba ya aliyekuwa Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Kenya, Makhtar Diop, na kuvuruga sherehe ya kumuaga iliyokuwa ikiendelea katika eneo la Muthaiga jijini Nairobi kwa maelezo kuwa anapigiwa kelele.

Kama vile haitoshi, kesho yake, alikwenda kituo cha polisi, akiwa amevaa kaptula fupi mno, hasa kwa mwanamke wa umri wake, na mwenye wajukuu, akishinikiza Diop akamatwe kwa kumpigia kelele nyumbani kwake akiwa amelala. Nyumba binafsi ya Kibaki ni jirani na nyumba aliyokuwa akiishi Diop.

Baada ya magazeti kuzipa uzito habari hizo katika kurasa zake za mbele, Lucy alikwenda katika chumba cha habari cha gazeti la Nation na kuanza kupiga kelele, akiwalaumu waandishi wa habari kwa kumchafulia jina lake na la familia yake. Alikesha katika chumba hicho cha habari akifanya vituko! Na katika moja ya matukio, alimpiga vibao mpigapicha wa televisheni ya KTN (Kenya Television Network), Clifford Derrick, ambaye alikuwa akimnyooshea kamera yake wakati akifanya vituko hivyo.

Makamu wa Rais wa Kenya, Moody Awori, pia aliwahi kuonja hasira za mama huyu mwaka 2004 katika hoteli moja mjini Mombasa, pale alipokosea kwa kumtambulisha kama ‘second lady’ badala ya ‘first lady’ katika sherehe za kuingia mwaka mpya wa 2005. Lucy alimtazama Moody kwa jicho la dharau, halafu akakusanya kilicho chake na kuondoka katika sherehe hiyo, akiwaacha watu wote wakiwa midomo wazi kwa mshangao.

Jitihada za Makamu wa Rais Awori kutaka kumbembeleza kwa kujaribu kumwomba msamaha, akisisitiza kuwa hakukusudia kusema hivyo na kwamba ni ulimi tu ulioteleza, hazikufua dafu na Lucy akasusia kabisa sherehe hizo za mwaka mpya zilizoandaliwa kwa ajili ya vigogo.

Na kwa hakika, akiwa katika mkutano mmoja Mkoa wa Magharibi mapema mwaka huu, Lucy ndiye aliyeitangazia Kenya kuwa mumewe Mwai Kibaki, atawania tena urais wa Kenya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu!

Wengi wanasema kinachomuuma sana Lucy ni pale anapohisi anakejeliwa kuhusiana na Mary Wambui, ambaye Wakenya wote wanajua kuwa ni mke wa pili wa Rais Mwai Kibaki. Katika hatua inayodaiwa kuwa ilichukuliwa na kusimamiwa na Lucy, wakati fulani, Ikulu ililazimika kutoa orodha ya watu wa familia ya karibu ya Rais Kibaki kwa vyombo vya habari, ikiwataja Lucy na watoto wake kuwa ndio pekee familia ya karibu ya kiongozi huyo.

Hata hivyo, Wakenya wengi wanajua kuwa mtoto pekee wa Mary Wambui ambaye anajiita Winnie Mwai, pia ni mtoto wa nje wa Rais Kibaki ambaye ni matunda ya uhusiano wake wa muda mrefu na Mary Wambui.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kwamba hatua ya Awori kumwita kwa wadhifa wa second lady, ulimrejeshea mawazo yale yale kuwa anadhihakiwa kutokana na uhusiano wa mumewe na Mary Wambui. Huyo alikuwa ni Makamu wa Rais, sembuse afisa fulani anayefanya kazi Ikulu chini ya mumewe? Zawadi yake ilikuwa ni kumshikisha adabu kwa kumchapa vibao mbele ya wageni mashuhuri kwa kosa la kumlinganisha na hasimu wake mkuu, Mary Wambui.

Ndiyo maana Desemba 12, mwaka huu alipomzaba kibao mshehereshaji huyo ambaye ni mmoja wa maafisa wakubwa wa Ikulu, Wakenya wengi, wakiwamo wageni mashuhuri waliohudhuria, hawakushangaa na wala hawakulihusisha tukio hilo moja kwa moja na mashinikizo ya kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazofikia kikomo Desemba 27.

Lakini wafuatiliaji wa mambo wanasema kitendo hicho hakiwezi kupita hivi hivi tu na kwamba Wakenya wanaomheshimu Rais Kibaki, wanaendelea kukerwa na tabia ya mwanamke huyo ambaye anaonekana kufanya mambo yanayomharibia mumewe kila mara na kwamba hawakutarajia kitendo hicho kifanywe katika nyakati za mwisho wa kampeni kama hizi.

Mara kadhaa, Lucy ameibuka na kuharibu kabisa jina la mumewe, akijaribu kumwonyesha kuwa hawezi kuidhibiti familia yake na mkewe mbele ya Wakenya, ambao kama walivyo Waafrika wengi, heshima yao kwa wanawake, hasa wenye mekeke kama Lucy Kibaki, si kubwa sana.

Wakenya wanamchukulia Rais Mwai Kibaki kama mtu mpole na asiyependa makuu, lakini kitendo cha mkewe kuendelea kuwakumbusha kwamba bado hawezi kumfanya lolote kwa kuleta rabsha kubwa mbele ya kadamnasi, kinaelezwa na wachunguzi kuwa kinachochea hasira za watu dhidi ya Rais kwa kushindwa kumdhibiti mkewe.

Mchambuzi mmoja, Lycy Oriang, aliandika katika safu zake za uchambuzi katika gazeti la Nation kwamba kitendo kilichofanywa na Lucy Muthoni Kibaki, si kitendo kinachoweza kufanywa na mwanamke wa kawaida. Kwa maneno yake “Mwanamke wa kawaida angesikia makosa hayo, angeinua uso na kutabasamu, lakini si kunyanyuka na kufanya ujinga huo.”

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliwahi kuandika kuwa wakati Wakenya walisubiri kwa hamu kupata ‘first lady’, baada ya miaka 24 ya Rais Daniel arap Moi, sasa wamepata mtu ambaye kwa hakika, vituko vyake vimeanza kuwakera. Ikumbukwe kuwa Moi alikuwa ametengana na mkewe Lena kabla ya kuwa Rais na hakuwahi kumkaribisha katika shughuli zozote za kiserikali kwa muda wote aliokuwa Rais.

Kwa wiki iliyopita, hilo ndilo limekuwa gumzo kubwa katika nyanja za siasa hapa Kenya ukiachilia mbali siasa za kawaida za kuvutana mashati zinazoendelea baina ya wagombea wakuu watatu wa Urais, Kibaki, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka. Baadhi ya watu wanasema, kwa kutania, kwamba huenda mshereheshaji huyo, alitumwa na Odinga kuharibu mambo siku hiyo kwa kumwita mke wa rais Lucy Wambui.

Wanaotoa madai hayo wanahoji ni kwa nini kama mshereheshaji huyo akosee jina hilo na kutaja jina la hasimu wake? Kwa nini asitaje majina mengine ya wanawake Wakikuyu kama Wanjiru ama Njeeri? Wanasema inawezekana hiyo ni sehemu ya kampeni zinazoendelea na kwamba Odinga na watu wake wamefanikisha lengo lao.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako