Makala
Haya ni matokeo sawia kwa CHADEMA wakati huu
Mwandishi Wetu
Toleo la 208
19 Oct 2011

TAKRIBAN wiki tatu sasa zimepita tangu umalizike uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Igunga mkoani Tabora. Ni Dk. Kafumu  wa CCM ndiye aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa mshindi wa uchaguzi huo; huku akifuatiwa kwa karibu na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Uchaguzi huo, tofauti na maeneo mengine, ulitawaliwa na ushindani mkubwa baina ya vyama vya siasa; huku kila kimoja kikijinadi kuwa na uwezo na nia ya kusaidia wananchi wa Igunga katika kusukuma gurudumu la maendeleo la jimbo lao.

Wapo waliojinadi kuwa na hazina ya wapiga kura na hivyo kuhitaji ziada kidogo tu ili walitwae jimbo hilo, wengine wakaamua kufunika kombe ili mwanaharamu apite kwa kuwarudisha kama wafalme wale waliowatuhumu kuwa ni sumu katikati yao kwa ajili ya kusaidia harakati za ushindi huku wengine wakijipanga kwa kuwaandaa wananchi kulinda ushindi kwa kadri wanavyoweza.

Kimsingi, chanzo cha ushindani huo ni matokeo ya historia ya jimbo lenyewe lililoachwa wazi na Rostam Azizi aliyeng’atuka kwa madai ya kuchoshwa na siasa uchwara za CCM.

Ni huyu ndiye aliyetawala fikra za Watanzania wengi wakati sakata la Richmond lililopokuwa bado vuguvugu, akaweza kupuuza chochote alichotuhumiwa kwa kuwa kimya na pengine kuibuka kwa kutumia wasemaji na vyombo anavyomiliki kutoa matamko tofauti ambayo hayakuweza kuponya maumivu ya Watanzania ambao mpaka sasa bado wanauguza kidonda hicho.

Ni yeye anayetuhumiwa kuwa alisimamia harakati za uchaguzi wa 2005 ndani ya CCM uliomwezesha  Rais Kikwete kuingia madarakani kwa kuwa jemedari wa kupambana na makundi yaliyompinga Kikwete na mwishowe akafanikiwa.

Kwa hakika, huyu ni moja ya nguzo muhimu za CCM ambayo imeamua kung’oka na kuacha chama kikiwa hoi; huku kasi ya upepo wa kisiasa nao ukiongezeka kwa kasi ya ajabu. Walichokisahau CCM ni kuwa ujemedari wa Azizi haukuwa katika umoja kama chama; bali katika utengano na makundi, hawakushtuka mapema.

Naikumbuka siku alipokuwa anazungumza na wana-Igunga kwa maana ya kuwaaga na kuwapa uamuzi wake wa kuachia madaraka yote ya kisiasa ndani ya CCM. Wapo waliotokwa na machozi wapo walioapa kuwa hawatoipa kura tena CCM na mengine mengi. Upande wa pili walionekana waliokuwa watendaji wenzake ndani ya CCM hiyo hiyo huko Mbeya na kwingineko wakijinadi kuanza kufanikiwa katika jitihada zao za kukisafisha chama dhidi ya mafisadi ambao walidai walichangia kukiharibu chama.

Hata hivyo, sherehe za ushindi huo hazikuzingatia muda ambao kama chama walimuhitaji Rostam Azizi na wenzie Edward Lowassa na Andrew Chenge waondoke ndani ya siku 90 na badala yake kung’atuka huko kulifanyika baada ya muda huo kupita.

Ilionekana wazi kuwa wakati CCM wakihimiza kujisafisha ili waongeze uungwaji mkono toka kwa wananchi hasa wanachama wao waliowapoteza, walisahau pia hata nyuma ya Rostam kuna wana-CCM ambao, japo kwa uchache, walikuwa na umuhimu mkubwa kwao kama chama.

Ikawa ni furaha ya muda tu; kwani baadae wakagundua kuwa Rostam Azizi ni muhimu; hasa katika kuhakikisha kuwa wanapata ushindi jimboni Igunga. Wakasahau machafu yake, wakampigia magoti, wakamrejesha jukwaani ili amnadi Kafumu ili tu ushindi uende kwao.

Walifanikiwa, wakalitwaa jimbo; japo wakati huu wakifuatiwa kwa karibu sana na CHADEMA tofauti na CUF waliojinadi kuwa walikuwa na hazina ya wapiga kura elfu kumi na moja jimboni humo. Lakini ni nani afurahie ushindi huo wa CCM Igunga?

Kwa jinsi hali ya mambo ilivyokuwa, isingewezekana ushindi kwenda Upinzani; hasa ukizingatia uwepo wa serikali yote ya CCM katika jimbo hilo; huku wakijikita katika kutoa ahadi - sio kama wagombea; bali kama viongozi wa serikali, na hivyo kufanya wapinzani watumie nguvu nyingi kwa kuwa wao zao ni ahadi tu ambazo utekelezaji wake ni mpaka walipate jimbo lenyewe.

Zikatumika mbinu tofauti za kiujanjaujanja kwa kutumia viongozi wa serikali wa wilaya husika na wengineo ili tu kuhakikisha wanatimua vumbi kwa wapinzani na kuandaa mapito sawia kwa CCM. Ukweli ukadhihirika kuwa, pamoja na mbinu zote hizo, shughuli haikuwa rahisi kwa CCM kama ambavyo ilishuhudiwa katika matokeo.

Kimsingi, katika hali ambayo wengi wenu msingeweza kuitabiri, mimi naona CHADEMA walistahili ushindi huo walioupata na sio zaidi ya hapo. Natoa sababu zangu na nitaruhusu kukosolewa ikibidi.

Kwanza, Igunga ni jimbo lililoachwa wazi na mtu ambaye anatuhumiwa na CHADEMA na wapinzani wote kwa ujumla kuwa ni fisadi. Hivyo; ninaona isingekuwa haki wala busara kwa CHADEMA kurithi jimbo hilo moja kwa moja toka kwa mtu mwenye tuhuma za uchafu ambazo hazijawahi kusifiwa wala kupongezwa na CHADEMA wala mpinzani mwingine yeyote.

Mikono ambayo ingewakabidhi ushindi huo ingekuwa ni ya mtu mwenye tuhuma za uchafu, busara ambazo wangetakiwa kuzienzi kwa uzoefu pengine ni za yule yule  mtuhumiwa uchafu, na hivyo nadhani ushindi huu wa CHADEMA  ulitosha kwa sasa.

Pili, ni namna ya uongozi wa jimbo lenyewe na mazoea ya wananchi; hasa katika utatuzi wa matatizo ya wananchi. Mbunge aliyetoka alikuwa anaifanya kazi hiyo akitumia jeuri yake ya pesa na kutoihitaji hata serikali. Hili lingekuwa kikwazo  kikubwa kwa mbunge wa CHADEMA kama angeshinda.

Wananchi wangepima utendaji wa mbunge wao kwa kulinganisha na aliyetangulia bila kutofautisha mbinu zinazotumiwa na wawili hao. Hivyo ni rahisi kwa CHADEMA kupimwa kuwa wameshindwa kwa kuwa utendaji wao ungetegemea zaidi ushirikiano wa serikali, na sio uwezo binafsi wa mbunge kama ilivyokuwa kwa Rostam Azizi.

Mimi naona hili lingerahisisha na kuongeza ushindani hapo mwaka 2015 na pengine kurahisisha njia kwa CCM, kwa kuwa hata serikali yenyewe inaongozwa na CCM.

Tatu, ni kuwa CHADEMA haikuwahi kuwa na dhamira ya wazi ya kujiimarisha kisiasa wilayani Igunga kabla ya uchaguzi huu. Kwa kupitia ushindi huu walioupata wa kushika nafasi ya pili kwa kujizolea kura zaidi ya 23,000, ni dhahiri sasa CHADEMA hicho kinaweza kuwatumia wapiga kura hawa katika kujitengenezea mtandao wa matawi jimboni hapo.

Matawi hayo yanaweza kutumika hata kusaidia maeneo mengine ya Tabora ambayo hayana uwakilishi wa upinzani kwa wakati huu. Hili naliona kuwa ni njia nzuri ya ushindi hapo mwaka 2015, na hivyo CHADEMA wana sababu nyingi za kisayansi kufurahia ‘ushindi’ huo wa Igunga kuliko CCM.

Mwisho, ni kwa jinsi CHADEMA walivyoweza kupambana na hujuma na mbinu tofauti za kuwadhoofisha zilizokuwa zikifanywa na CCM kupitia watawala, wanasiasa na hata makundi mengine ya kijamii.

Sote tunakumbuka suala la DC kuvuliwa mtandio lilivyozua mtafaruku wakati wa kampeni. Tunakumbuka pia masanduku ya kura feki yalivyodakwa usiku na Mh. Mdee. Tunakumbuka ununuzi wa shahada za wapiga kura na shutuma za kuhamasisha vurugu,. Tunakumbuka pia mawaziri wa serikali kuingilia kampeni na kutoa ahadi kinyume na taratibu, na pengine kubwa zaidi likiwa hili la kushughulikia matatizo ya uchaguzi ya ngazi ya tawi katika ngazi ya jimbo. Hilo nalo ni kubwa na baya kwa NEC.

Kuna wakati Mwalimu Nyerere aliwahi kunena mwaka 1995 alipokuwa anazungumzia tatizo la uongozi ndani ya CCM, kwa kusema kuwa CCM inaweza kuendelea kushinda kutokana na mazoea ya watu na hata udhaifu katika upinzani.

Matamshi haya  sasa yanaanza kufifia kwa kuwa upinzani unaonekana kuzichachafya hasa ngome za CCM, na hivo pengine ni ishara kuwa upinzani unafanyia kazi matamshi haya wakati CCM bado wanaenda kwa mazoea ya wananchi wao.

Sidhani kama hilo linaweza kuwaongezea tena kipindi kingine madarakani. Hata kwa kusoma tu matokeo ya Igunga, mtu anaweza kuona namna kazi ilivyo kubwa kwa CCM mwaka 2015.

Mpaka sasa hazijaonekana jitihada za wazi ndani ya chama na serikali ya CCM ya kutaka kuendelea kuwa madarakani kwa kuwa mwananchi ambaye ndiye mpiga kura analia siku zote kwa ugumu wa maisha, mgao wa umeme, ufisadi, ukosefu wa ajira na magumu mengine mengi.

Kama Zambia wameweza, nina imani katika CCM hii wapinzani wanaweza kujiandikia historia mpya ifikapo 2015.

Nihitimishe kwa kusema kwamba, makuzi ya kidemokrasia ni pamoja na kuheshimu matokeo, na kwa hilo hongereni CHADEMA kwa kuyakubali matokeo ya Igunga na kuendelea kuwadhihirishia Watanzania kuwa fujo mnazosingiziwa kuzianzisha ni moja ya hujuma ambazo mnahitaji kuungwa mkono ili kuzitokomeza.

Mwandishi wa makala hii Joseph Migunda anapatikana kwa Email ya mijaceez@gmail.com au Simu: 0752711364

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako