NAIJUA teolojia ya Kikristo inayotumika, na hivyo ninamjua adui wangu, lakini yeye hanifahamu. Kwa maana hiyo, adui yangu tayari ameshindwa vita hata kabla haijaanza.
Heko Precision kwa Twiga Stars lakini...
KAMPUNI ya ndege ya Precision Air imetoa msaada wa tiketi zenye thamani ya Sh. milioni 27.8 kwa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) inayojiandaa kucheza na Namibia mjini Windhoek kuwania nafasi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC).
Meneja Mauzo wa PrecisionAir, Tuntufye Mwambusi alisema wakati wa kukabidhi msaada huo kwamba wameamua kusaidia kwa sababu timu hiyo huibuka kidedea katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
Ni kweli kabisa, kwani mwaka juzi Twiga Stars ilifaulu kucheza fainali za AWC zilizofanyika Afrika Kusini.
Pia Julai mwaka jana timu hiyo ilifuzu kucheza kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) nchini Zimbabwe. Katika michuano hiyo ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu.
Na kana kwamba hiyo haitoshi, Septemba pia mwaka jana Twiga Stars ilishiriki Michezo ya Afrika mjini Maputo, Msumbiji baada ya kufuza kucheza michuano hiyo.
Hiyo ni rekodi nzuri. Angalau mashabiki wa soka wanakuwa na kitu cha kupumulia katika kujipa faraja maana timu za soka za wanaume mara nyingi huwatia simamzi. Inakuwa ni maumivu matupu.
Kwa mfano, timu za taifa za Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na ile ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) zilishindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani wa Dar es Salaam, tena katika kilele cha sherehe za kutimiza Miaka 50 za Uhuru wa Tanganyika kuwapa raha mashabiki wa soka nchini.
Msaada huo wa Precision Air umekuja wakati muafaka kwani Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), tayari lilikuwa limeanza kupata wakati mgumu wa jinsi ya kuiwezesha timu hiyo ishiriki michuano hiyo ya Afrika kwa ufanisi.
Inasikitisha kuona kwamba pamoja na juhudi zote zinazoonyeshwa na wasichana hao katika soka la kiwango cha kimataifa, bado timu hiyo haijapata mfadhili wa nguvu kama ilivyo Taifa Stars ama kama ilivyo Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kwa kweli tunahitaji mashirika au kampuni zenye moyo wa Precision Air nyingi tu katika juhudi za kukuza soka letu.
Baada ya mwanzo kutoa punguzo la nauli kwa timu ya Taifa ya wavulana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) iliyoshiriki michuano ya COSAFA nchini Botswana, Precision Air ndiyo sasa imejitokeza kuwa mkombozi wa wasichana hao. Hongera sana.
Kampuni hiyo imetangaza pia azma yake yake ya kushirikiana na TFF katika kuisafirisha Twiga Stars, Ngorongoro Heroes na ile ya wavulana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwenye nchi ambazo ndege yao inafika.
Hata hivyo, pamoja na haja ya wadau mbalimbali kujitokeza kutoa msaada kwa Twiga Stars, bado kuna umuhimu mkubwa kwa TFF kukabiliana na changamoto ya kufanya soka la wanawake kuvuma na kuvutia wasichana wengi zaidi.
Mkazo mkubwa iwe ni kueneza soka la wanawake kwenye shule kuanzia za msingi, za sekondari hadi vyuoni.
Kwa kufanya hivyo, timu zitakuwa nyingi na hiyo itafanya ligi zitakazochezwa kuwa za kuvutia zaidi. Hebu tulifanye soka la wanawake lishamiri kama ilivyokuwa netiboli katika miaka ya 1980.
Wasichana waliojiingiza katika soka kwa wakati huu wameonyesha njia. Licha ya kupigana vilivyo kwenye soka la kimataifa, baadhi yao wamekonga nyonyo hata za wazungu wa Sweden kwa kupokelewa kucheza soka lao huko.
Hakika soka la wanawake likishamiri kwa maana ya kuwa na ligi ngumu ambazo zitatoa wachezaji maarufu, mashirika na makampuni mengi yatapigana vikumbo kutaka kujitangaza kupitia soka lao.
Wadau wa soka nchini hawana budi kushikamana kuhakikisha kwamba soka la wanawake nchini linakwenda mbele, kwani katika miaka hii ya sasa katika ulimwengu wa soka wa Tanzania ‘hakunaga’ kama Twiga Stars.
Add new comment