Januari 31, 2012, miaka 60 baada ya kuzaliwa kwake, mtu huyu muungwana ambaye leo namzungumzia, aliiaga dunia hii, hivyo kutorudi tena. Ugonjwa ambao bila shaka ni wa malaria ulikuwa umefanya kazi yake.
Mchangamfu, anayeonekana mtu wa kawaida lakini mwenye umbo la heshima, alikuwa anamiliki kampuni ndogo ya ushauri wa utawala mjini Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20.
Familia yake, majirani, wafanyakazi, wateja na marafiki wa karibu, wote walimlilia kwa uchungu. Lakini wapo wengine wachache ambao walishangazwa na jinsi kifo hicho cha ghafla kilivyotokea na kuombolezwa.
Kwa kawaida kifo cha mtu yeyote maarufu hufanya vyombo vyote vya habari nchini kutangaza na kufuatilia kwa makini habari za maombolezo hadi maziko. Lakini kwa kifo hiki haikuwa hivyo.
Haikuwa hivyo kwa ni kifo ambacho hata msitari mmoja haukuchapishwa na hata ‘safa’ moja katika masafa mengi ya redio na televisheni haikusafirisha habari zake.
Ilikuwa inastahili kuwa hivyo kweli? Hebu tujikumbushe kidogo juu ya mtu huyu. Alikuwa ni nani hasa? Jina lake lilikuwa Henry Mapolu. Alikuwa mkufunzi wa idara ya sosholojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia mwaka 1972 hadi 1978.
Katika muda huo mfupi, alifanya kazi maridadi akiongoza tafiti mbalimbali kuanzia zile za utawala wa viwanda, mahusiano ya kazi hadi maendeleo ya vijijini. Tasnifu (thesis) yake ya uzamili (MA) ilihusu Ukulima wa Tumbaku na Mabadiliko ya Jamii Tabora Vijijini.
Alihariri kitabu kimoja, akasaidia kuhariri kingine na akaongeza sura kadhaa katika kitabu hicho. Katika kitabu chake cha kwanza, Workers and Management in Tanzania (kilichochapishwa na Tanzania Publishing House, 1974), Profesa Andrew Coulson wa Chuo Kikuu cha Birmingham Uingereza anakielezea: “Kitakuwa wakati wote ni kitabu bora. Kwa njia nyingi kinaelezea umuhimu wa sosholojia ya mjini katika Tanzania.”
Henry Mapolu alionyesha kipaji chake cha uandishi tangu enzi zake za uanafunzi. Alikuwa mwanaharakati mzuri wa ujamaa, mshiriki mzuri wa chama wanafunzi wa Afrika yote (Pan Africanist Student Organization, na alikuwa mjumbe wa bodi ya jarida la Cheche.
Hata hivyo, hama hicho na jarida hilo, vyote vilifungiwa mwaka 1970 kwa kuonekana kuwa msitari wa mbele mno katika ukosoaji.
Hakukata tamaa, alisonga mbele kuwa mmoja wa waanzilishi na kuwa mhariri mwandamizi wa jarida jingine la vijana lililoitwa MajiMaji. Majarida hayo yalikuwa yakijadili zaidi kisomi masuala mazito yaliyokuwa kwenye chati yanayohusu mambo ya kiuchumi na kijaamii.
Majarida hayo yalichapisha makala nzito za wasomi maarufu waliokuwapo nchini na nje ya nchi. Hiyo ilifanya majarida hayo yasomwe hadi nje ya mipaka ya Tanzania katika nchi za Kenya, Uganda, Marekani, China, Ulaya na kwingineko.
Kama mwanafunzi na msomi, Mapolu, si tu alishiriki katika mabadilishano ya masuala ya kisomi ya wakati huo, lakini pia aliandika barua, maoni na makala na kufanya mapitio ya vitabu katika magazeti mbalimbali na hata ya vyombo vya habari vya taifa.
Henry hakuwa tu mtu wa maneno. Akiwa na wenzake waliokuwa wakereketwa, alifanya kazi katika vijiji vya ujamaa, kwenye miradi ya maendeleo na kampeni za kisomo cha watu wazima.
Alikwenda nyumba hadi nyumba kuchangisha kwa ajili ya vyama vya ukombozi. Maandiko yake maarufu na kazi za kujitolea hazikuwa na maslahi binafsi.
Hadi mwaka 1978, Henry Mapolu alikuwa mwanasosholijia anayekuja juu kawa kasi na alionekana hivyo hapa nyumbani Tanzania na nje. Kazi zake zilitumika katika kozi za vyuo vikuu na zilinukuliwa katika sehemu nyingi.
Pamoja na hivyo, siku moja kutokana na matakwa yake na bila kushawishiwa na ntu yeyote, alivuka msitari na kuajiriwa kama Ofisa Elimu ya Wafanyakazi katika kiwanda cha nguo cha Urafiki mjini Dar es Salaam, kiwanda kikubwa cha nguo ambacho taifa lilikuwa linajivunia.
Ingawa leo inaweza ikaonekana ni kitu cha ajabu, lakini busara ya kufanya kazi hiyo kwenye kiwanda hicho ilikuwa ni moja tu: Ni ukereketwa wake wa elimu kwa umma, akiwa ni mjamaa aliyejitolea kutumikia watu wa kawaida barani Afrika.
Akiwa kwenye kiwanda cha urafiki, alifanya kazi kwa bidii na kuwa mbunifu wakati anaandaa programu ya elimu ya wafanyakazi. Programu hiyo ilihusisha masomo ya watu wazima, masomo ya awali ya uchumi, sheria za kazi, masuala ya kiufundi ya uzalishaji wa nguo, masuala ya kijamii, masuala ya kitaifa na siasa za dunia.
Aliwaajiri wataalam wanaohitajika kuandika majarida yanaoyosomeka kwa urahisi yanayowagusa wafanyakazi au kuwafundisha.
Programu yake ya elimu ilipokewa vizuri na kukubalika vilivyo na wafanyakazi na kuwa na mafanikio makubwa. Ni programu iliyokuwa ya pekee ambayo haijaonekana pengine Afrika. Sehemu ya kozi za programu hiyo baadaye ilichapishwa kuwa kitabu.
Henry alikuwa pia mtu mwenye msimamo. Siku moja asubuhi alisikia kwenye redio kwamba ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya. Ulikuwa ni uteuzi wa Rais.
Kwa wengi wetu, kusika habari hiyo kungefanya turuke juu kwa furaha au kushindwa ujasiri wa kukataa. Lakini Henry hakukubali kazi hiyo aliyopewa kwa njia ya kutangazwa redioni.
Ukweli ni kwamba hakuwa umeshauriwa mapema juu ya kazi hiyo. Kutokana na ukweli huo alikataa kwa kusema: “Hapana, hapana, siikubali.” Na hakutania katika hilo – ilikuwa ni mara ya kwanza na kwa namna ya kipekee katika historia ya Tanzania mtu kukataa uteuzi wa Rais kwa njia hiyo.
Katika miongo miwili ya mwisho ya maisha yake, Henry alijiondoa katika shughuli ambazo zingemfanya aonekane kwenye jamii na kujikita kwenye shughuli za ushauri na za kifamilia.
Tofauti na wenzake wengi wa enzi zake, hakujiingiza kwenye shughuli za kifisadi serikalini au kwenye sekta binafsi kwa kisingizo cha kufanya biashara au kujaribu kujineemesha kwa njia haramu.
Mara chache chache, alifanya au aliandika mapitio ya vitabu. Kazi yake ya mwisho ya kisomi ilikuwa ni ile ya kuchangia kuandika sura katika kuchapisha jarida la wanafunzi kwa ajili ya kitabu cha Cheche: Reminscences of a Radical Magazine (Mkuki na Nyota, 2010).
Henry Mapolu atakumbukwa kwa maandiko yake ambayo yalikuwa ni mfano wa pekee kwa shughuli za kisomi barani Afrika. Uchambuzi wake wa masuala ya maendeleo ya vijijini ulikuwa na mvuto mkubwa.
Umuhimu wake wa wakati huo bado unaendelea kuwapo hadi leo katika harakati za kuwania uhuru wa kweli wa Afrika, ni maandiko ambayo yana umuhimu wa pekee kusoma.
Baada ya kupata habari za kifo chake, wasomi kutoka sehemu mbali mbali walijulishana au waliwajulisha marafiki zake. Wengine waliomfahamu vizuri walieleza juu ya umahiri wake katika nyanja nyingi, heshima aliyokuwa nayo, na jinsi alivyoishi akiwa mtu rafiki wa wengi.
Pia walieleza ni jinsi gani walivyojijifunza kutoka kwake katika masuala aliyokuwa amebobea. Mwandishi wa habari mkongwe, Jenerali Ulimwengu, alimuelezea kama ``kisima cha busara, mtu mwenye uadilifu wa hali ya juu.”
Kwa upande mwingine, Watanzania wengi na watu wa Afrika Mashariki, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyakazi wake katika masomo ya sayansi ya jamii wanamkubali kwamba ni mwana halisi wa Afrika aliyejipambanua.
Wakati nyakati za wakati huu tunapiga domo sana na kutofanya lolote kwa watu wa kawaida, enzi zake haikuwa hivyo. Ukweli ni kwamba nyakati za wakati huu tunapokea dola za wafadhili na kuabudu mawazo na itikadi za magharibi. Tumefanya mchakato wa kuwakabidhi mawazo yetu.
Mimi nilipata fursa ya kujifunza, kufanya kazi na kucheka na Henry Mapolu kwa karibu miongo miwili na nusu. Nilipata fursa pia ya kuwa karibu na familia yake na watu wake wa karibu hivyo nimefadhaika mno na kuondoka kwake.
Kuliko wakati wowote, Afrika inahitaji kukumbuka, kuheshimu na kufuata mawazo na maneno ya wasomi wake waliojitoa kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa bara hilo. Kuzaliwa upya kwa Afrika hakutakuwa mbali ya msukumo unaotoka ndani ya bara hilo kwa njia ya mawazo na vitendo.
Kwa hiyo basi, tunakuaga ukalale mahali pema, comrade Henry Mapolu. Tunakuthamini sana, ulitimiza wajibu wako katika mchakato huu wa Afrika kuzaliwa upya. Siku moja ndoto yako itatimia. Ikiwa hivyo ni wewe utakaotoa miali ya moto angani wakati tunasherehekea.
Maoni ya Wasomaji
Katika kisa kimoja kwenye
Katika kisa kimoja kwenye belays za Aespos, jogoo alidamka kuwika na halafu alas da kchakura chakura kutafuta punje za baraka bila ya mafanikio akamlalamikia Mungu kuwa imekuaje leo hakumpa riziki? Pundekwa mbali akaona mngaro... Kitu kinametameta.... Ilikuwa kifuko chenye vito almasi, lulu, tanzanite, nk. Jogoo akalalama Eh Mungu wangu, ninanjaa na badala y kunipa mtama, mchele au ngano leounanipa vito hivi? Kaka yangu Prof Hirji hivi kwa jogoo kutojua thamani ya vito, kunapinguza thamani ya almasi, dhahabu, au lulu?
R.I.P our real comrade Henry
R.I.P our real comrade Henry Mapolu, I got to know you in a very short period of time but for sure it is as if I knew you ever since, You real have taught me of how an educated, simple, respectful and adorable person should be, may the almighty God find a good place for you to have rest in peace waiting for the eternal salvation. Love you forever and forever praying for you. Mungu alitoa, mungu ametwaa, jina la Bwana libarikiwe.AMEN.
R.I.P We Love you forever and
R.I.P We Love you forever and forever praying for you. Mungu alitoa, mungu ametwaa, jina la Bwana libarikiwe.AMEN.