Makala
Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro na Miaka 50 ya Uhuru yenye mafanikio
Mwandishi Wetu
Toleo la 216
9 Dec 2011

Utangulizi na historia

HIFADHI ya Ngorongoro (NCA) ilianzishwa mwaka 1959 kwa sheria ya hifadhi namba 413 ya mwaka  1959 ya matumizi mseto ya bonde la Ngorongoro ikilenga uhifadhi bora wa  maliasili, kuendeleza maslahi ya jamii za asili za bonde hilo na kukuza utalii.

Eneo hili ni la ukubwa wa kilometa za mraba 8,292 linaambaa katika sehemu kubwa ya Wilaya ya Ngorongoro, ambayo ni Tarafa nzima ya Ngorongoro, wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, na likipakana na maeneo ya mikoa mingine nchini kama Mkoa wa Mara na Shinyanga.

Bonde la Ngorongoro ambalo ni maarufu sana duniani ndiyo sehemu pekee katika Afrika na duniani kote, ambako wanyama pori na binadamu (Wamaasai) wanaishi pamoja kwa amani bila shida yoyote.

Eneo la kreta ya Ngorongoro au bonde la Ngorongoro ndilo eneo maarufu na kivutio kikuu cha maelfu ya watalii wanaotembelea  Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kila mwaka kutoka kote duniani  kwa ajili ya kujifunza na kujifurahisha kwa kuona jinsi wanyama lukuki wanavyoishi ndani ya bonde hili, wakizunguka huku na kule kwa ajili ya kujipatia chakula na maji wakati wote.

Maeneo megine muhimu katika bonde la Ngorongoro ni eneo la Olduvai Gorge, eneo ambalo inaaminika ndipo mwanzo wa binadamu wa kwanza hapa duniani alipoishi na hili linabainishwa bayana na ugunduzi wa wataalamu wa masuala ya kale  Dk. Louis Leakey na mkewe Dk. Mary Leakey wa mwaka 1959 katika bonde la Oldupai, ugunduzi huo ni pamoja na ule wa  nyayo za binadamu wa kale au zamadamu huko Laetoli mwaka 1978. Eneo hili liko pia katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Bonde la Ngorongoro lina heshima kubwa duniani kutokana na kutangazwa kuwa ni eneo la Urithi wa Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambalo makao makuu yake ni mjini Paris, Ufaransa. Heshima hiyo ya Ngorongoro imetokana na ukweli kwamba ni hapa tu duniani ambako wanyama wanaishi pamoja na binadamu katika nyendo za kila siku za maisha kwa miaka mingi.

Julai mwaka jana katika kutambua umuhimu wa Hifadhi ya Ngorongoro, Kamati ya masuala ya Urithi wa Dunia ikiketi katika kikao chake cha 34 mjini Brasilia, Brazil, ililiorodhesha eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kama ni eneo la Utamaduni la Urithi wa Dunia katika masuala ya utamaduni. Awali tangu mwaka 1979, kama ilivyokwishakuelezwa, eneo hilo lilikuwa limeorodheshwa kama eneo la Asili la Urithi wa Dunia.

Kamati ilitoa uamuzi wake kutokana na kumbukumbu za ajabu na za kuaminika kisayansi kuhusiana na mabadiliko ya binadamu katika eneo hilo katika sehemu ya ardhi kutoka mbuga ya wanyama ya Serengeti kaskazini magharibi mwa Tanzania hadi sehemu ya mashariki ya Bonde la Ufa.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ilianzishwa mwaka 1959. Tangu wakati huo eneo hili linatumika kwa matumizi mseto ya ardhi. Hii ikiwa ni pamoaja na shughuli za uhifadhi wa wanyama pori na ufugaji wa mifugo mbalimbali  kama vile  ng’ombe unaofanywa na wananchi wa jamii ya Kimaasai  ambao hufuga mifugo yao kijadi. Kitendo hiki cha kufuga mifugo huku kukiwa na wanyama pori ni kivutio kikubwa cha aina yake kwa watalii na wapiga picha wa luninga na magazeti na watalii wanaotembelea  hifadhi hii.

Eneo hilo linajumuisha kireta maarufu ya Ngorongoro ambayo ni kubwa kuliko zote duniani na bonde la Olduvai lenye urefu wa kwenda chini wa kilometa 14 na ambalo ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kale duniani ambako watafiti wa masuala ya binadamu wa kale, Dk. Louis Leakey na mkewe Mary Leakey, walifanya ugunduzi mwingi wa mambo ya kale ya kufutia na kusisimua kuhusu historia ya binadamu wa kale zaidi duniani ambao bado unaendelea hadi sasa kupitia kwa wataalamu wa mambo ya kale na historia  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Colorado, Marekani na vingine vya Hispania, Korea ya Kusini na Afrika Kusini.

Utafiti mwingi wa mambo ya kale umekwisha kufanyika katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kwa miaka 80 na kutoa ushahidi mwingi wa kuishi mwanadamu katika eneo hilo kwa karibu miaka milioni nne iliyopita.

Ushahidi huo ni pamoja na mabaki ya nyayo za mwanadamu katika eneo la Laetoli zikionyesha maendeleo ya binadamu kuweza kusimama wima na ushahidi wa mabadiliko ya binadamu kutoka akiwa kama mnyama aina ya australopiths kwenda homo erectus hadi homo sapiens; na mabaki yanayoonyesha maendeleo katika utaalamu wa kuchonga mawe hadi matumizi ya vyuma.

Eneo lote hilo linaonyesha kuwa bado lina mambo mengi yanayohusiana na maendeleo na mabadiliko ya binadamu hadi binadamu wa sasa, tabia na uhusiano wake na viumbe wengine.

Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lina manufaa makubwa duniani katika kuhifadhi viumbe mbalimbali kutokana na kuwapo viumbe ambao wako hatarini kutoweka kama vile faru weusi. Idadi kubwa ya wanyamapori wanaishi katika kireta ya Ngorongoro na maeneo yanayoizunguka kwa mwaka mzima, na uhamaji wa wanyama kama nyumbu, pundamilia na swala na wengine kwenda uwanda wa kaskazini.

Ukweli huo, pamoja na muundo wa ajabu wa kireta ya Ngorongoro, ndio ulikuwa msingi wa awali wa  kulifanya eneo hilo kuwa eneo la Asili la Urithi wa Dunia.

Ni kwa ajili ya umuhimu huu kwamba Bonde la Ngorongoro liliundiwa mamlaka, yaani Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA) ambayo, pamoja na mambo mengine, inahakikisha kwamba eneo hilo linaendelea kuwa eneo la urithi wa dunia linalojiendesha lenyewe kutokana na mapato ya ndani, likiwezesha kupatikana kwa faida kwa ajili ya jamii za asili za eneo hilo na kuhakikisha kwamba mazingira ya eneo yanalindwa na kutunzwa kwa ubora mkubwa, kwa vile mbali na maliasili zake, hili pia ni eneo muhimu kwa mafunzo ya mambo ya kale kwa vizazi vijavyo vya dunia.

Kwa maana hii NCAA imekuwa ikishirikiana na jamii zinazoishi ndani ya hifadhi,wakiwamo pia Wadatoga na Wahzabe na kwa utaalamu wa hali ya juu, kutunza mazingira, maliasili na vyanzo vya historia vilivyopo na wakati huohuo, kuzihudumia jamii hizo zinazoishi ndani ya hifadhi, wafanyakazi, watalii kwa huduma za msingi za afya, elimu na maji na nyinginezo.

Kati ya mambo ya msingi ambayo NCAA imedhamiria kufanya ni kuhakikisha na kuendelea kuboresha hadhi ya Bonde la Ngorongoro kama Hifadhi ya Dunia na eneo la maajabu ya nane ya dunia kwa:

 • Kutoa huduma bora za jamii kwa wakazi wa asili wa Hifadhi ya Ngorongoro;
 • Kusimamia kwa utaalamu wa hali ya juu maliasili, utamaduni na vyanzo vya historia ya kale vilivyomo;
 • Kuwa na wafanyakazi wanaojituma, bora na wenye utaalamu wa hali ya juu kuhusu masuala yote yanayohusu uhifadhi wa wanayama pori na mambo ya kale;
 • Kuunda na kuwa na sera sahihi zinazotekelezeka;
 • Kutoa huduma za utalii za ubora wa juu zinazokidhi mahitaji na matarajio ya watalii mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo; na 
 • Kuwezesha kuwapo ushirikiano na wadau mbalimbali katika ngazi za wenyeji, watafiti wale wa hapa nchini na wale wa Kimataifa.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikitimiza malengo na matarajio yake kwa kufuata mambo matatu makubwa: kwamba uhifadhi unakuwa ni jambo endelevu; heshima kwa binadamu wote na uwajibikaji kwa wadau.

Kazi/malengo ya NCAA kisheria

 • Kuhifadhi na kuedeleza maliasili za Hifadhi
 • Kukuza utalii ndani ya Hifadhi na kutoa na kuhimiza upatikanaji wa huduma na miundombinu wezeshi kwa ajili ya utalii endelevu
 • Kulinda na kukuza maslahi ya jamii za Kimasai katika Jamhuri ya Muungano zinazojihusisha na ufugaji na uzalishaji maziwa ndani ya Hifadhi
 • Kukuza na kuratibu uanzishwaji na biashara ya mazao ya misitu ndani ya Hifadhi
 • Kujenga barabara, madaraja, viwanja vidogo vya ndege, mejengo na nyugo na kutoa huduma za maji, pamoja na huduma  nyingine, ambazo Bodi ya Wakurugenzi itaona zinafaa kwa ajili ya maendeleo na ulinzi wa Hifadhi ambazo hazitaitia hasara Mamlaka au kuhatarisha uhifadhi wa wanyama pori na eneo zima la Hifadhi ikiwamo misitu na uoto wa asili.
 • Kungia makubaliano ya kutekeleza miradi mbalimbali, ambayo kwa maoni ya Bodi, yatawezesha Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake kama yalivyoainishwa katika sheria iliyoanzisha Mamlaka hii.

Maajabu ya Laetoli na mlima  ‘unaotembea’

Huku Tanzania Bara ikiadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa watu wake Ijumaa, Desemba 9, 2011, ni siku hiyo hiyo pia ndipo mchanga wa ajabu uliotokana na volcano ya mlima Oldonyo Lengai (Mlima wa Mungu kwa Kimaasai)  ulioko Ngorongoro, utakakuwa unatimiza kilometa moja ya safari yake ya miaka 50.

Kwa kawaida haiwezekani kuona rundo la mchanga likisogea au kuhama bila ya kutawanyika, lakini mchanga huu wa ajabu wa volcano wa Ngorongoro ambao sasa upo katika uwanda wa Oldonyo-Gol umekuwa ukisogea umbali wa mita 20 kwa mwaka na hivyo inapofika Ijumaa wiki hii siku ambayo ni kilele cha sherehe ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania  Bara (Tanganyika), unatarajiwa kuwa utakuwa ‘umetembea’ wastani wa kilomita moja nzima tangu Desemba 1961.

Hata hivyo, taarifa zinaonyesha ya kuwa mchanga  huo unaotembea unadaiwa kuwa ulianza safari yake miaka ipatayo 3000 iliyopita baada ya kurushwa kutokana kulipuka kwa  volcano kutoka katika mlima huo wa Oldonyo Lengai  kutoka kwenye kilele cha 'Oldonyo L'engai' au Mlima wa Mungu ulipo upande mwingine mwa Hifadhi ya Ngorongoro karibu na Engaruka.

“Tunatarajia kuweka jiwe la msingi katika eneo ambalo mlima huu wa ajabu utakuwa umefika siku ya tarehe 9, Desemba mwaka huu (leo) tutakapokuwa tunasherekea miaka 50 ya Uhuru wa nchi yetu,” anasema Afisa Mkuu wa Maendeleo ya Utalii wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Asantaeli Melita.

Melita anaongeza kuwa kwa kukadiria umbali ambao mchanga huo mweusi wa volkano na wa ajabu unatarajiwa kuwa utakuwa umetembea katika miaka mingine 50 ijayo, alama nyingine ya makadirio itasimikwa katika eneo ambalo mlima huo utakapokuwa  wakati Tanzania itakapotimiza miaka 100 ya Uhuru tarehe 9 Desemba 2061.

Afisa Uhusiano wa NCAA, Adam Akyoo, anasema kuwa mchanga huo unakisiwa kuwa umekuwa ‘safarini’ kwa zaidi ya miaka 3000 baada ya kurushwa na volkano kutoka kwenye kilichokuwa kilele cha Mlima wa Mungu au ‘Oldonyo L’engai’ ambao una volkano hai inayolipuka hata sasa.

Tayari alama za maeneo ambayo mlima huo umekuwa ukipita zimewekwa katika nyakati tofauti na jiwe la kwanza la msingi liliwekwa mwaka 1969 baada ya hapo alama nyingine zilifuatia katika miaka ya 1976, 1981, 1985, 1990, 1995, 1998 na 2003, huku jiwe jingine la msingi likitarajiwa kusimikwa tarehe 9 Desemba mwaka huu likiwa na rangi za bendera ya Tanzania.

Mchanga unaotembea ni miongoni mwa maajabu kadhaa yaliyoko nchini na husan katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo bado hayajulikani vyema kwa Watanzania wengi kutokana na wananchi wengi kutokuwa na shauku ya kutembelea vivutio mbalimbali vya watalii vilivyoko katika maeneo mbalimbali nchini kama ilivyo kwa mchanga huo.

Pia yafaa ifahamike kuwa mchanga huo ni sehemu takatifu kwa jamii ya Wamaasai kwani akina mama wa jamii hiyo ambao hajajaliwa kupata watoto hupelekwa katika mchanga huo na kufanyiwa tambiko ambapo habari kutoka ndani ya jamii hiyo ya Wamaasai zinasema akina mama wote waliofanyiwa tambiko hilo hatimaye hufanikiwa kupata mimba na kuzaa watoto. 

Waumini wa dini wanaweza wasipendezwe na eneo la “Laetoli” lililo ndani ya Hifadhi ya Mgorongoro, ambako inaaminika, binadamu wa kwanza alitembea duniani. Kwa mujibu wa mafundisho ya dini, watu wamekuwa wakiamini kuwa Mungu ndiye aliyeumba kila kitu; kuanzia dunia, viumbe vyote (akiwamo binadamu) vinavyoishi katika ulimwengu huu ikiwa ni pamoja na nyota zinazoizunguka.

Kwa upande mwingine wanasayansi wanaamini katika nadharia ya ‘mpasuko mkubwa’ wanaodai ulitokea mabilioni ya miaka iliyopita ambao ndio uliosababisha vitu vyote tunavyoviona na kuvishuhudia hivi sasa na kwamba binadamu walitokana na sokwe waliokuwa wanatembea kwa miguu minne kabla ya kuanza kutembea kwa miguu miwili. 

Suala la Laetoli linasemekana lilianza kujitokeza wakati binadamu walipoanza kutembea wima, au kwa miguu yao miwili, alama ambazo sasa haziwezi kufutika ardhini katika eneo hili la Ngorongoro, kutokana na milipuko ya volcano au matukio mengine ya aina hiyo ya asili.

Laetoli ni eneo tepetepe lenye mkusanyiko wa alama za wanyama, lipo kilometa 40 kutoka eneo la Olduvai Gorge kunakovuma upepo na ambako inaaminika binadamu wa kwanza aliishi.

Alama hizo za kale za miguu zilizovumbuliwa na Dk. Mary Leaky zimehifadhiwa katika majivu ya volkano, wanasayansi wakiamini kwamba majivu hayo yanatokana na mlipuko wa volkano ya sadiman yenye urefu wa kilomita 20. Kwa mujibu wa watafiti, mburuzo huo ni ushahidi usiokifani wa binadamu wa kale kutembea kwa miguu miwili zaidi ya miaka milioni 3.6 iliyopita. 

Mtafiti mashuhuri Dk. Mary Leaky alichimbua eneo hilo kati ya mwaka 1978 – 1979 baada ya ugunduzi wake. Mvua ndogo ndogo iligandamiza tabaka hilo la sentimita 15 lenye alama hizo bila kuziharibu nyayo hizo. Nyayo hizo ni za watu watatu, mmoja akiwa anatembea katika nyayo za mwenzake, na hivyo kufanya nyayo za mtu wa kwanza zisigundulike kiurahisi, jopo la Dk. Leakey liliweza kurekodi nyayo hizo kwa kutumia utaalamu mbalimbali, kabla ya kufukia mburuzo huo kwa udongo, mchanga na majabali ya volkano.

Karibu miongo miwili iliyopita, na tena hivi karibuni, Profesa Charles Musiba, Mtanzania na mtaalamu wa Mambo ya Kale anayefundisha katika Chuo Kikuu cha Colorado, Marekani aliongoza kikundi cha wataalamu wenzake  kufukua upya nyayo za Laetoli, na kuzifanya zionekane wazi na kila mtu akiwemo Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Mali Asili na Utalii Mheshimiwa Ezekiel Maige, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Mzee Pius Msekwa pamoja na mamia ya wananchi.

Wakati wa kuona nyayo hizo Profesa Musiba  alieleza miti ya migunga (acacia) ilianza kuota katika eneo hilo ambalo awali lilikuwa mithili ya jangwa itakavyodhibitiwa ili mizizi yake isiharibu nyayo hizo wakati huu michoro ya jengo la kuhifadhi nyayo hizo huko Laetoli ikitayarishwa kwa kuzingatia utaalamu unaotakiwa.

Kutambaa kwa mizizi ya miti hiyo hadi katika eneo la mburuzo kulianza kulitishia kusababisha uharibifu wa nyayo hizo na hifadhi ya eneo hilo muhimu la kihistoria.

Mtaalamu wa masuala ya binadamu wa kale kutoka Chuo Kikuu cha New York, Profesa Terry Harrison, anaendelea kufanya utafiti katika eneo hilo tangu miaka ya mwisho ya 1990 hadi hivi sasa. Taasisi ya Uhifadhi  ya Getty, kwa kushirikiana na Idara ya Mambo ya Kale Tanzania, imechukua hatua zenye lengo la kuhifadhi eneo la mburuzo la Laetoli ambazo ni pamoja na kufukia upya maeneo yaliyochimbwa mwaka 1995 na kuanzisha mpango wa uratibu na matengenezo kwa ajili ya kuhifadhi kwa muda mrefu.

Vifaa na mfumo uliotumiwa kwa ajili ya kufikia tena mburuzo huo hutumika katika maeneo mengi ya mambo ya kale ambayo bila kufanyiwa hivyo yanaweza kuharibiwa na vitu mbalimbali.

Rais Kikwete aingilia kati

Pengine hali ingeweza kubaki hivyo kama si Rais Jakaya Kikwete ambaye miongoni mwa vitu vinavyomvutia ni wanyama pori na maliasili, ambaye mwaka jana alitembelea eneo hilo la Laetoli kujionea nyayo hizo za watu wa kale.

“ Nilishangaa nilipoelezwa kuwa nyayo za watu wa kale zimefukiwa ardhini, na lundo la mawe katika eneo la urefu wa mita 30 ndicho kielelezo cha mahali ambapo binadamu wa kwanza inasemekana walitembea” alisema Rais wakati wa ufukuaji tena wa nyayo hizo zenye  miaka milioni 3.6 iliyopita.

Ni Rais Kikwete ambaye aliamuru nyayo hizo za watu wa kale ziwekwe hadharani kwa manufaa ya wanadamu na utalii. Pale watu watakaporuhusiwa kuwa wanazitembelea zitachangia katika kuinua pato la Taifa kutokana fedha zitakazotozwa watalii watakaokwenda kuona nyayo hizo kutoka nchi mbalimbali duniani.

Kwa vile mburuzo wa nyayo hizo unaelekea eneo moja, wanasayansi wanasema unaweza kuwa ulitokana na kundi la watu. Mtaalamu wa mambo ya binadamu wa kale wa Ujerumani, Ludwig Kohl-Larsen alikuwa wa kwanza kufika Laetoli kuangalia nyayo hizo.

Mwaka 1934 aligundua taya la binadamu wa kale aitwaye australopithecus afarensis ambaye anaaminika ndiye mwenye nyayo hizo. Watu wengi wa mataifa mbalimbali duniani wana shauku kubwa ya kuziona nyayo hizo za binadamu wa kwanza huko Laetoli.

Ngorongoro ambayo pia ni sehemu ya mfumo wa ekolojia wa Serengeti, ni hifadhi ambako hupatikana aina mbalimbali za wanyama na ambayo itaendelea kushika nafasi yake kama eneo ambalo wanyama wote waliopakiwa katika Safina ya Noah, waliteremka baada ya mafuriko, yanayoelezwa katika Biblia. Kwa mpango huo, eneo la Laetoli litaweza kuwa miongoni mwa maeneo muhimu duniani yenye historia ya kale inayomhusu binadamu.

Changamoto na Mafanikio

Wahenga walisema kila masika huja na mbu wake. Na hivyo ndivyo ilivyo kwa Hifadhi ya Ngorongoro ambako maendeleo katika maisha ya binadamu yameleta changamoto nyingi ambazo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu na shughuli za binadamu ndani ya Hifadhi.

Changamoto nyingine ni ongezeko la matukio ya uvamizi wa maeneo ya mazalia ya wanyama ambao nao unatokana na ongezeko la shughuli za binadamu ndani Hifadhi.     

Lakini katikati ya changamoto hizo yamekuwapo mafanikio makubwa. Chini ya usimamizi wa NCAA utalii umeongezeka kwa idadi kubwa zaidi ya watalii kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro; malengo ya huduma kwa wafugaji yamefikiwa kwa kiasi kikubwa na huduma kama za shule, maji na umeme zimesambaa miongoni mwa wanajamii.

Kati ya mafanikio hayo ni pamoja na hatua ya NCAA kuwapa wanawake wajane 85 wa Wilaya ya Ngorongoro mifugo 600 chini ya mpango maalumu wenye lengo la kuinua hali ya maisha yao maarufu EOLOTO.

Hadi sasa utaratibu wa ruzuku ya mifugo hao ambao watagharamia na NCAA kwa kushirikiana na kupitia Baraza la Wafugaji (NPC) umekwisha kusambaza mifugo 245 kwa wajane 35 katika eneo la Ngorongoro. Mifugo hao ambao ni ndama 70 na mbuzi 175 waligawiwa kwa wajane 35, ambao wanatoka katika kata za Kakesio, Endulen na Olbalbal katika Tarafa ya Ngorongoro.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa NPC Mhe. Metui ole Shaudo, Katibu wa  Baraza hilo, Mhe. James Moringe, anasema msaada huo, ambao ni awamu ya kwanza na ukiwa wa thamani ya Sh. milioni 60 uliogharamiwa na NCAA, umewanufaisha wajane wa vijiji saba vya Esere, Olpiro, Endulen, Osinoni, Ngoile, Kakesio na Meshili.

“Tunatarajia kununua mifugo zaidi kwa ajili ya awamu ya pili na mifugo hao watagawanywa katika Kata nne zaidi ambazo ni Ngorongoro, Naiyobi, Nainokanoka na Bulati,” anasema Moringe. Katika awamu ya pili watagawiwa ndama 100 na mbuzi 250 kwa wajane 50 wa vijiji 10 katika kata nne. Vijiji hivyo ni Naiyobi, Alchaniemelok, Alaililai, Sendui, Kapenjiro, Bulati, Irkeepusi, Nainokanoka, Irmisigyo na Oloirobi.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NCAA, Lucas Selelii anasema mpango huo umenuia kuinua maisha ya familia masikini miongoni mwa jamii ya wafugaji katika Tarafa ya Ngorongoro ambao hasa ni Wamasai na Wada’toga.

“Katika mpango huu tunaziainisha familia masikini sana pamoja na wajane ambao tunawapa mifugo kwa kuzingatia kuwa ufugaji ni shughuli pekee iliyoruhusiwa katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambako kilimo na shughuli nyingine za biashara haviruhusiwi,” anasema Mkurugenzi Selelii.

Ng’ombe wapatao 136,000 wanaishi katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro lakini kwa mujibu wa Ofisa Mifugo wa NCAA, Peter Kinyanjui, mifugo mingi wamekufa kutokana na ukame uliolikumbuka eneo la Hifadhi na maeneo mengineya Mkoa wa Arusha mwaka jana.

Mafanikio mengine ya dhahiri ni vituo vya kuchuja samadi kwa ajili ya kufua umeme vitakavyojengwa katika shule mbalimbali za msingi na za sekondari katika Wilaya ya Ngorongoro.

Vituo hivyo vitajengwa na NCAA kwa ushirikiano na Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec) na Ofisa Mwandamizi wa Mifugo wa NCAA, Dk. Justice Muumba, anasema nishati ya kupikia kutokana na samadi inayotolewa na idadi kubwa ya mifugo katika Wilaya ya Ngorongoro ambayo wakazi wake wengi ni wafugaji ni njia muafaka kuhifadhi mazingira hasa misitu na kuondoakana na adha ya akina mama na mabinti zao kutumia muda mwingi kutafuta kuni na kuzibeba umbali mrefu kila siku.

Kwa mujibu wa Dk. Muumba, Shule mbili za Sekondari zitakazonufaika na mradi huo ni za Embaraway na Nainokanoka pamoja na Shule ya Msingi ya Olbalbal na kwamba mpango unafanyika kueneza teknolojia hiyo ya umeme kutokana na samadi katika zahanati, vituo vya afya na taasisi nyingine za umma wilayani.

Naye Mkurugenzi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Hifadhi aya Ngorongoro (NCAA), Bruno Kawasange, anasema ya kuwa teknolojia ya kutengeza gesi kutokana na samadi ina lengo la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa katika juhudi za kutunza mazingira.

Kwa mujibu wa Kawasange, Taarifa ya Ngorongoro ina ng’ombe 150,000 mbali ya mbuzi na kondoo na hivyo kuwezesha upatikanaji wa kiasi cha kutosha cha samadi. Na katika hatua nyingine NCAA imetumia Sh millioni 85 katika mradi wa ng’ombe wa maziwa wenye lengo la kuzinufaisha familia masikini na wananchi hao wafugaji.

Tangu mwaka 2004, NCAA imekuwa ikifundisha elimu ya mazingira katika shule za msingi na sekondari zilizoko tarafa ya Ngorongoro ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Tangu wakati huo hadi mwaka jana, jumla ya wanafunzi 19,600 wamepata elimu hiyo katika Tarafa ya Ngorongoro pekee. Mwaka 2011 NCAA iliwafikia wanafunzi wa Wilaya ya jirani ya Karatu kutokana na umuhimu wao katika kulinda mazingira ya Hifadhi ili waendelee kupata faida zaidi.

Jumla ya shule 29 zimepata mafunzo na wanafunzi wapatao 8,840 wamepata mafunzo haya kwa mara ya kwanza. Changamoto zilizopo ni zile za mahitaji ya miche ya miti ambayo watapanda maeneo ya shule, nia na hamasa ya kufika Ngorongoro ili kujionea wenyewe jinsi raslimali hizi zinavyotunzwa na kulindwa na hivyo kupata mtazamo mpya kuhusu jukumu lao la kulinda mazingira.

Ngorongoro miaka 50 ijayo

Tanzania itajenga makumbusho ya kwanza duniani ya historia halisi ya binadamu itakayokuwa na umbo la kuba, ambayo itajengwa eneo la Ngorongoro kwa gharama ya Sh billion 40.

Rais Jakaya Kikwete aliueleza mpango huo alipozindua rasmi onyesho la nyayo za binadamu zenye umri wa miaka millioni 3.6 ambazo zimekuwa zikihifadhiwa ardhini kwa zaidi ya miaka 15.

Alisema Rais Kikwete: “Nimeiagiza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuanza mipango ya kutekeleza mradi huu na Serikali iko tayari kusaidia katika kugharamia kwa vile mradi huo utakapokamilika utakuwa wa kwanza wa aina yake.”

Makumbusho hayo ya kale yako katika nafasi nzuri ya kuliingiza Taifa mabilioni ya fedha kutokana na maelfu ya wageni watakaoyatembelea kuangalia nyayo halisi za binadamu wa kwanza duniani.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, anasema upembuzi yakinifu wa makumbusho hayo unaendelea lakini kwa vile mradi huo si wa kawaida, sehemu ya eneo hilo ambayo iko wazi (yenye urefu wa mita tatu) ya mburuzo wa nyayo za binadamu lenye urefu wa mita 30 litabakia limefunikwa hadi makumbusho hayo makubwa yatakapokamilika na kuzinduliwa rasmi.

 “Tumeidhihirishia dunia kwamba nyayo za binadamu aliyetembea duniani miaka ipatayo milioni 3.6 iliyopita ziko Tanzania na zimekuwa zimefichwa ardhini kwa miaka 15, ikizingatiwa imekuwepo minong’ono kwamba pengine taarifa hizo zilikuwa ni uongo,” anasema Waziri Maige.

Profesa Charles Musiba, kiongozi wa timu ya ufukuaji huo anasema jengo hilo kubwa la makumbusho hayo ambalo litakuwa na umbo la kuba na lenye teknolojia ya hali ya juu ya kubadili lenyewe hali ya hewa ya ndani, litagharimu dola za Marekani milioni  30 (Shilingi bilioni zaidi ya 35).

Katika hatua nyingine mpango wa kubadilisha maisha ya Wamasai wafugaji, ya kuhamahama kwa kutafuta malisho ya mifugo wao, sasa utawawezesha kufuga ng’ombe kwa biashara na faida na tayari umeanza kuzaa matunda Ngorongoro.

Chini ya mpango huo ambao unamhusisha Rais Jakaya Kikwete, ranchi mpya ya kisasa itakayokuwa na matumizi mbalimbali, yenye thamani ya Sh. bilioni tano, itaanzishwa katika eneo la Kakesio katika Hifadhi Ngorongoro, iwezeshe ufugaji wa kisasa na kwa faida.

Rais Kikwete amepata kutuma kikundi cha wazee na wafugaji kutoka Ngorongoro kutembelea Uganda ambako walikuwa wageni wa Rais Yoweri Museveni na waliweza kujifunza kutoka kwa wafugaji wa Kinyankole ambao wanasemekana wanafaidika kwa kiasi kikubwa sana kutokana na mifugo yao tofauti na Wamaasai.

Hiyo itakuwa ni ranchi kubwa ya ng’ombe katika Afrika Mashariki, itaanzishwa katika Kata ya Kakesio kwenye mpaka wa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha na Wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga. Mradi huu unatekelezwa kwa pamoja kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro.

Ranchi hiyo itaanza na ng’ombe 1000 au zaidi kidogo, lakini baadaye itapanuliwa hadi kuwa na mifugo 2,000 kwa mujibu Meneja Uhusiano wa  NCAA Adam Akyoo. Ranchi hiyo pia itakuwa ya manufaa kwa utalii na kwa kuhifadhi mazingira kwa sababu mifugo ambao walikuwa wamezoea kuzurura ovyo katika maeneo mbalimbali sasa watakuwa katika eneo la ranchi hiyo na hivyo kuliacha eneo kubwa la Ngorongoro kwa wanyama. Na wananchi wa Kimaasai watapata fursa ya kujifunza ufugaji wa kisasa na wenye tija na kuondokana  na kuchunga mifugo mingi isiyokuwa na tija kiuchumi.

Aidha, Akyoo anasema kwa mara ya kwanza wananchi wa Kimasai katika Tarafa  ya Ngorongoro katika kutekeleza mradi huu wataombwa kuchangia ng’ombe mmoja kwa hiari tayari kuingizwa katika mradi huu japo hakuna mwananchi yeyote akayelamishwa kufanya hivyo.

Wananchi watapeleka mifugo yao katika ranchi hiyo ambako watatunzwa kwa kupewa malisho, tiba, uhamilishaji kwa chupa kwa ajili ya kupata ng’ombe bora, na mwisho wa siku fedha zitakazotokana na mifugo hao zitawanufaisha wananchi hao na familia zao.

“Wamasai  walikuwa wakijipatia Sh 60,000 kwa kila ng’ombe na hiyo ilikuwa baada ya miaka sita ya kumchunga, sasa mnyama huyo huyo anaweza kumuingizia mfugaji Sh million 1.2 katika muda huohuo. Pia mmiliki wa mnyama huyo hatapata taabu katika kumtunza, atakachofanya ni kuja tu kuchukua fedha zake.

Matarajio ya ranchi hiyo ni pamoja na kuwa  ni kituo cha kukabili mbung’o Kituo cha Uhamilishaji  kwa chupa, kuwa kama Chama ca Ushirika cha Wafugaji, kiwanda cha kutoa gesi kutokana na kinyesi cha wanyama na kutoa mafunzo ya matunzo mazuri ya mifugo. Ranchi pia itakuwa kama soko la mifugo na watu kutoka sehemu mbalimbali wataweza kuagiza ng’ombe bora wa kisasa na waliotunzwa vizuri.

“Ranchi hiyo inaanzishwa katika eneo ambalo lilikuwa likitumiwa kama njia na wezi wa mifugo na hivyo kuwapo kwake hapa kutachangia kuzuia wizi wa mifugo kati ya Wamaasai na wananchi  wa Meatu,” anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakesio, Stanley Ngorosa.

Katika mradi huohuo, pia patajengwa kiwanda cha kusindika nyama na kiwanda cha kisasa cha maziwa kitajengwa mjini Karatu, vyote hivyo vitakuwa vinachangiwa na nyama na maziwa kutoka katika ranchi hiyo na pia kitatoa ajira kwa mamia ya wanachi wa Ngorongoro.

Tarafa ya  Ngorongoro ambayo ndio eneo lote la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ina jumla ya ng’ombe 136,000 lakini wote hao hawajawanufaisha wafugaji wake jambo ambalo halikumpendeza Rais Kikwete ambaye mwaka 2009 aliingilia kati na kuitaka NCAA kuyabadilisha maisha ya Wamasai hao mara moja.

Meneja uhusiano wa Mamlaka hiyo ya Hifadhi ya Ngorongoro Bwana Akyoo amesema kuwa ili kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa Mamlaka hiyo imetenga jumla ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya kugharamia mradi huo ambao unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Pia Mamlaka hiyo imemwajiri mtaalamu mshauri na mwelekezi kutoka nchini Ufaransa,  Michel Duplat, kwa ajili hiyo.

Mtaalamu huyo wa Kifaransa ambaye amepatikana kutokana na mchakato uliofanyika nchini mwake kwa ushirikiano kati ya ubalozi wa Tanzania  nchini Ufaransa taarifa zake zinaonyesha kuwa amekuwa akisimamia kwa ufanisi mkubwa miradi ya aina hiyo katika nchi mbalimbali duniani zinazoendelea zikiwamo Angola na Sudan. Tayari Duplat ameshatembelea Tarafa yote Ngorongoro kujionea hali ya malisho na mifugo iliyopo hivi sasa ilivyo.

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako