Hii ni kasoro kwa Waziri Dk. Kigwangala

JANUARI 19 mwaka huu, 2018, Waziri wa Maliasili na Utalii alifanya uteuzi wa wajumbe 11 wa Bodi ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.  Bodi hiyo itaongozwa na Mwenyekiti  Profesa Abiud Kasamila, aliyeteuliwa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, Desemba Mosi, mwaka 2017.

Nimetafakari kwa kina kuhusu muundo wa Bodi hiyo. Nina wajibu wa kutoa mawazo yangu kuhusu uwakilishi wa wanawake na vijana kwenye Bodi husika. Niseme moja kwa moja kwamba uwakilishi wa wanawake kwenye Bodi hiyo hauridhishi. Hili ni pigo jingine kwa wale wenye mtazamo chanya kwenye suala la harakati za kufikia usawa wa jinsia, maarufu kwa sasa kama 50/50.

Sheria inayosimamia uteuzi wa wajumbe wa Bodi haimbani waziri kuzingatia usawa wa kijinsia, inachomtaka waziri huyo ni kuteua watu wenye kuangalia maslahi ya nchi, basi. Huu ni udhaifu wa sheria yetu.

Lakini Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020, kipengele cha 167 (a) (b) kinasema chama tawala kitaielekeza serikali kufanya yafuatayo; (a) kuendelea kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowawezesha wanawake kushika nafasi sawa (50/50) za uongozi katika vyombo vya uamuzi katika ngazi zote.

Nakumbuka mwaka 1995 nikiwa bado katika “umri wa binti” au wazungu wanaita “teenager” habari zilitanda kuhusu Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Wanawake Duniani ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na kufanyika huko Beijing nchini China. Umoja wa Mataifa ulitimiza miaka 50 mwaka huo kwa hiyo mkutano huo ulikuwa wa kipekee.

Nadiriki kusema mkutano wa Beijing hapa Tanzania ulikuwa wa tofauti kwa sababu hakukuwa na kijana wala mzee na pengine hata watoto ambao hatukusikia na pengine kuelewa kuwa kuna jambo kubwa sana limefanyika duniani kuhusu wanawake wote. Mkutano wa Beijing ulikuwa ndio mwanzo wa mabadiliko makubwa duniani wa kuleta maendeleo na usawa wa kijinsia kwenye jamii.

Kama zilivyokuwa nchi nyingi duniani, ushiriki wa Tanzania haukubaki nyuma, mama Getrude Mongella aliongoza ujumbe wa nchi yetu na tuliweka sahihi kwenye Azimio la Kimataifa la Kuhakikisha Nchi zinaweka katiba, sheria na sera zake ziwe na mrengo wa kumpa mwanamke usawa katika nyanja za maendeleo na  kujikwamua kiuchumi.

Ni miaka 23 imepita sasa tangu mkutano ule wa Beijing. Kwa kipindi kilichoendelea Tanzania tumeshiriki maazimio mengi ya kimataifa  kuhusu usawa wa kijinsia. Kwa sasa kubwa tulilonalo na linaloendelea mpaka mwaka 2030 ni malengo endelevu kuelekea 2030 ( SDG’s -Sustainable Development Goals).

Lengo namba tano linahusu usawa wa jinsia (gender equality). Lengo lenye kusisitiza ifikapo mwaka 2030  mataifa yote yawe yamekuwa na usawa wa jinsia na kuwakwamua kiuchumi wanawake na wasichana. Moja ya majukumu ya mataifa katika lengo hili ni kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi sawa kwa wanawake katika nafasi za uongozi na uamuzi kwenye nyanja za kisiasa na kiuchumi, ili kuweza kuwa na uchumi endelevu na wakilishi kwa jamii nzima.

Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mshiriki mzuri wa makongamano haya ya kimataifa imeweza kurudisha nyumbani sera endelevu na njema kwa usawa wa kijinsia na maendeleo.

Kwa kuzingatia hayo yote, niliposoma orodha ya wajumbe wa Bodi ya Ngorongoro iliyoundwa na Waziri Kigwangala nilisikitika na kujiuliza maswali mengi. Je, ni kweli Tanzania yote hii katika wajumbe wa Bodi 11 ni mwanamke mmoja tu mwenye uwezo wa kuyamudu majukumu ya Bodi hiyo?

Je, uwakilishi wa changamoto za wanawake Watanzania na wale wanaoishi eneo la Ngorongoro utafanikiwa vipi kwa mwanamke mmoja tu kuwepo kwenye Bodi? Je, miaka 23 baada ya Beijing na maazimio kadhaa kupita bado huu ndio usawa wa jinsia unaopiganiwa?

Sisemi haya kwa kuwa ningependa kuona namba tu za wanawake kwenye nafasi ambazo hatuna uwezo nazo, hapana. Binafsi naamini  kwamba nchi yetu ina wanawake wenye uwezo sawa na wengi. Na kwa Bodi hii husika ya Ngorongoro naamini kuna wanawake wenye taaluma za utalii na uhifadhi wengi ambao wangeweza kuweka mchango mkubwa miongoni mwa wajumbe wa Bodi.

Sasa tatizo liko wapi? Labda waziri pamoja na mamlaka nyingine za uteuzi zina majibu kwa nini tunaweza kuwa na wajumbe 12 wanaume na mmoja tu mwanamke kwenye Bodi.

Binafsi naamini serikali yetu ina nia nzuri na imekuwa mstari wa mbele katika ngazi za kimataifa kuhakikisha usawa wa kijinsia, ndio maana Tanzania imeweza kutoa mwanamke kuwa kiongozi wa pili wa juu wa nchi, mama Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tanzania pia imekuwa mshiriki mzuri wa makongamano ya kimataifa yanayohusu usawa wa kijinsia. Kwa hili la Bodi ya Ngorongoro na nafasi zingine zote za ujumbe wa Bodi ni tofauti. Nashauri mamlaka husika zingeweka jitihada za makusudi kuhakikisha tunapata usawa wa uwakilishi wa jinsia, yaani Bodi za 50/50. Si jambo gumu tukiamua.

Mwandishi wa makala haya Mariam Mungula, amejitambulisha kuwa ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Jukwaa La Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi Dar es Salaam. Awali, makala hii ilisambazwa katika mitandao ya kijamii lakini tumeichapisha tena hapa ili iweze kusomwa na Watanzania wengi zaidi.

2 thoughts on “Hii ni kasoro kwa Waziri Dk. Kigwangala”

  1. Mussa Alnedy says:

    Muda wote Wazungu wanatuletea sera zitakazo tufanya tukae tukichemsha kichwa namna ya kuzitekeleza kwa kuwa nyingi ya sera hizo sinapingana na yale walio tujenga akilini mwetu kupitia dini miaka mingi ilio pita kwahiyo mnakaa mnaumiza kichwa namna ya kuyatekeleza huku mmnaacha mambo ya msingi ya maendeleo kwamfano mtakaa mkiumiza kichwa namna ya kutekeleza usawa wa kijinsia huku mnaasahau kuangalia ubora na utendaji kiu fanisi alio nao mtu bira kujari huyu mtu ni mwanamke mwanaume au huntha tunakazana kuangalia Beijing wazungu walileta sera gani hebu tujiulize nchi nyingi za Ulaya zimepiga hatua za maendeleo karibia miaka 100 iliopita huwo usawa ulio letwa kuanzia 1995 na kuupigia upatu kila siku je wao wali ufuata enzi wanapambana kuleta maendeleo ya nchi zao

  2. Kaite Kataitika says:

    Mariam, unaandika, “Kama zilivyokuwa nchi nyingi duniani, ushiriki wa Tanzania haukubaki nyuma, mama Getrude Mongella aliongoza ujumbe wa nchi yetu na tuliweka sahihi kwenye Azimio la Kimataifa la Kuhakikisha Nchi zinaweka katiba, sheria na sera zake ziwe na mrengo wa kumpa mwanamke usawa katika nyanja za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.”

    Mama Getrude Mongella hakuwa kiongozi wa ujumbe wa nchi yetu ya Tanzania; wakati huo yeye alikuwa anafanyakazi chini ya Umoja wa mataifa akiwa na wadhifa wa Katibu Mkuu wa Mkutano huo wa Beijing. Kiongozi wa ujumbe wa tanzania alikuwa ni Mama Zakia Meghji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *