Hisa; Utajirisho usio na kificho

Wakati ananunua hisa za Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) mwishoni mwa mwaka 1998, Zacharia Meshack, 51 (sio jina halisi) alikuwa na mpango wa kuziuza ndani ya kipindi kifupi kama walivyofanya wawekezaji wengine.

Kitu cha kwanza alichofikiria wakati anawekeza ni kuwa pale bei ya hisa itakapopanda kwa kiwango chochote, hata kwa asilimia tano, basi angeweza kuziuza, kwani tayari atakuwa amesharudisha fedha yake aliyowekeza, pamoja na faida.

Awali, Meshack hakufikiria kuwekeza kwa muda mrefu. Kwani TBL ndiyo ilikuwa kampuni ya pili kuwekwa kwenye soko hilo, kwa hiyo hali hiyo haikumpa uhakika kwamba fedha yake ingeongezeka, kutokana na kukua kwa bei ya hisa.

Lakini baada ya kupata ushauri kutoka kwa washauri wa uwekezaji, Meshack aliamua kubadili mawazo yake na kufikiria tofauti na aalivyokuwa akifikiria awali.

Uuzaji wa hisa hizo ulianza mwezi Septemba mwaka 1998, wakati bei ya hisa za awali za TBL ikiwa ni shilingi 550.

Kipindi hicho, kulikuwa na kampuni moja tu iliyoorodheshwa, ambayo ni Tanzania Oxygen Limited, sasa inaitwa TOL Gases. TOL iliorodheshwa kama jaribio, ambapo serikali iliamua kuuza hisa zake inazozimiliki kwenye kampuni hiyo.

Meshack aliamua kununua hisa za TBL baada ya kupata ushauri kutoka kwa mshauri wa uwekezaji ambaye alimueleza manufaa ya kuendelea kuwa na hisa kwa muda mrefu, badala ya kuziuza pale mauzo ya awali yanapokamilika, kama wafanyavyo wawekezaji wengi, hasa wa ndani.

Yeye anaamini kwamba, kabla ya kuamua kuwekeza, alikuwa na mawazo kama ya wawekezaji wengine, kutokana ukweli kwamba, fedha alizopanga kuwekeza hazikuwa za ziada, bali aliamua kujinyima mambo mengine ili awekeze, tena kwa muda mfupi.

Katika zoezi la uuzaji wa hisa za awali za kampuni hiyo, ambazo zilikuwa zikimilikuwa na serikali, Meshack alifanikiwa kununua hisa zenye thamani ya shilingi 220,000, ambazo zilikuwa ni hisa 400.

Baada ya uuzaji wa hisa za awali, ndani ya kipindi fulani, bei ya hisa za TBL zilipanda kwa asilimia zaidi ya 50 na akajikuta mtaji wake umeongezeka hadi kufikia shilingi 330,000 ambazo ni asilimia 50 ya mtaji wake wa awali.

Kiasi hicho cha faida kilikuwa ni kikubwa ikilinganishwa na uwekezaji wowote ule, ukiwemo wa uzalishaji kwenye viwanda, akaunti ya muda maalumu ya benki ama uwekezaji kwenye kilimo, ambavyo vote haviwezi kuleta faida kama ile inayopatikana kwenye soko la hisa.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, uwekezaji kwenye soko la hisa humpa mwekezaji faida ya asilimia zaidi ya 30 kwa mwaka, wakati uwekezaji mwingine ikiwemo amana za muda maalum za benki huzalisha faida ya chini ya asilimia 15.

Baada ya miaka kadhaa, wakati kampuni hiyo ilipotangaza gawio la hisa zake, Meshack na wawekezaji wenzie walipata shilingi 120 kwa kila hisa. Katika kipindi hicho, Meshack alifanikiwa kuweke kibindoni shilingi 48,000 huku thamani ya uwekezaji wake ikiwa imefikia zaidi ya shilingi 500,000.

Kwa kuangalia ukuaji wa uwekezaji, hadi miaka miwili ilipotimia, Meshack tayari alikuwa amepata gawio lake, lakini hata uwekezaji wake tayari ulikuwa umeshafikia shilingi 500,000, ambayo ni takribani asilimia 150 ya uwekezaji wa awali.

Ukilinganisha uwekezaji wa Meshack na mwekezaji mwingine kwenye masoko ya fedha na uzalishaji bidhaa, zikiwemo akaunti maalum ya benki, bado ni eneo ambalo halina hasara nyingi za uwekezaji.

Kwa mfano, iwapo mwekezaji atachukua pesa hiyo ya uwekezaji wa awali wa Meshack wa shilingi 220,000 na kuweka kwenye amana ya muda maalum benki basi atapata chini ya asilimia 20 kwa mwaka.

Kwa hiyo, mwekezaji anayeweka amana yake kwenye benki ya biashara atakuta amana hiyo ikikua kwa asilimia 15 kwa mwaka na kwa miaka miwili basi uwekezaji wake unaweza kuwa umekua kwa asilimia 30, ambayo ni sawa na jumla ya shilingi 273,000.

Kwa haraka haraka utaona kwamba, wakati Meshack kaweka fedha zake kwenye hisa na kupata faida ya shilingi 280,000 ndani ya miaka miwili ama mitatu, wakati yule wa kwenye amana za benki akipata faida ya shilingi 73,000 ambayo ni moja ya tatu.

Mbali na ukuaji wa mtaji wa uwekezaji, Meshack na wawekezaji wenzie kwenye soko la hisa wanapata upendeleo maalum, kwani kwa mujibu wa sheria,uwekezaji kwenye hisa umesamehewa kodi.

Baadhi ya vivutio kwenye soko la hisa kwa mujibu wa mamlaka ya masoko ya mitaji nchini (CMSA) ni kuondolewa kwa kodi ya ukuaji wa mtaji, kuondolewa kwa ushuru wa stempu, kodi kwenye gawio na kuondolewa kwa kodi nyingine nyingi.

Kwa wawekezaji ambao wamewekeza kwenye biashara ambayo haijaandikishwa kwenye soko la hisa, basi utaratibu wa kodi na ushuru hauondolewi, hali inayomfanya mwekezaji kupata kipato kidogo ikilinganishwa na mtu aliyewekeza kwenye hisa zilizoorodheshwa.

Mwaka2012, ambayo ilikuwa ni miaka 14 tangia kuorodheshwa kwenye soko la hisa, bei ya TBL ilikuwa tayari imeshakuwa kubwa. Hii ilitokana na kuendelea kufanya vizuri kibiashara, hali ambayo ilichochea umahitaji ya hisa hizo na kukua zaidi kwa bei.

Kwa mujibu wa ripoti za DSE, mwaka 2012, bei ya hisa ya TBL ilifikia shilingi 2,440. Kwa kuwa Meshack alikuwa bado hajauza hisa zake, tayari uwekezaji wake ulikuwa umefikia shilingi 976,000, ambayo ni zaidi ya mara nne ya ya uwekezaji wa awali.

Hadi kufikia kipindi hicho, akiwa mwekezaji wa kampuni hiyo, ndani ya miaka 14, Meshack alishakuwa ametengeneza zaidi ya shilingi milioni moja kama gawio kwa miaka kumi mfululizo na uwekezaji wake ukiwa umefikia zaidi ya shilingi milioni moja.

Kwa hiyo ndani ya miaka kumi na mminne, Meshack ambaye aliwekeza shilingi 220,000 za awali, mtaji wake uliongezeka hadi kufikia shilingi milioni zaidi ya moja, huku akiwa tayari ameshapata zaidi ya shilingi  milioni moja kama gawio la hisa zake.

Hadi sasa, bei ya hisa za TBL imeshaongezeka hadi kufikia shilingi takribani 11,000, kwa mujibu wa ripoti za DSE, na uwekezaji wa Meshack umeshafikia zaidi ya shilingi milioni 4 huku akiwa tayari ameshapata kiasi kama hicho kama gawio la hisa zake katika kipindi hicho.

Kwa mwaka jana, ambapo kampuni hiyo ilitangaza kutoa gawio la shilingi 600 kila hisa, Meshack ambaye bado analimiki hisa zake alijipatia shilingi 240,000, ambazo ni sawa na kiwango cha uwekezaji wake wa awali miaka 18 iliyopita.

Watanzania wengi wamekuwa wakiliona soko la hisa kama sehemu ambayo haiwahusu. Wengi wanadhani kwamba kuwekeza kwenye soko la hisa ni kwa ajili ya watu wenye vipato vikubwa na vya kati.

Hadi hivi sasa inakadiriwa kuwa soko la hisa la Dar es Salaam lina wawekezaji takribani 400,000 na asilimia zaidi ya 60 ni wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Soko la hisa lina mtaji wa shilingi takribani trilioni 20, ambazo chini ya nusu ya pato la taifa (GDP) kwani wataalamu wanasema kwamba ili nchi iweze kunufaika zaidi na soko la hisa, basi mtaji unatakiwa kuwa angalau nusu ya pato la taifa.

Soko la hisa ni aina mpya ya biashara nchini na wengi wanaogopa kuingia kwa sababu mtindo wa uendeshaji ni mgeni. Pia, wengi wanasita kuwekeza fedha zao wakifananisha mfumo huo na mchezo wa kamari.

Uwekezaji kwenye masoko ya hisa unatafsiriwa na wengi kuwa ni kazi zinazofanywa na matajiri kiasi cha kuweza kuzitumia kwa michezo ya kubahatisha.

Kupitia uuzaji wa hisa hizo, jamii itaweza kujenga uchumi wao, uchumi wa familia zao na taifa kwa ujumla.Hivyo jamii inapaswa kujenga mazingira na utamaduni wa kununua hisa kwani ni msingi mzuri wa kujikwamua kiuchumi na kuendeleza maisha.

Moja wapo ya sifa za hisa inaweza kuuzwa na kununulika kwa makubaliano kati ya mnunuzi na muuzaji au kwa kutegemea bei ya soko kwa kampuni zilizosajiliwa kwenye soko la hisa.

Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) liliwahi kutajwa kuwa soko bora la hisa Afrika kutokana na ushiriki wa uwekezaji mkubwa wa kigeni kwa mwaka 2014 ambao uliwezesha masoko ya hisa ya kikanda kuweka rekodi katika mafanikio kwa wawekezaji kupata marejesho mazuri.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Da es Salaam, Moremi Marwa anasema, matokeo hayo yameonyesha imani kubwa ya wawekezaji katika Soko la DSE kulikosababishwa na kuwapo mageuzi ambayo yana faida kwa uchumi wa Tanzania.

2 thoughts on “Hisa; Utajirisho usio na kificho”

  1. james misana says:

    Mimi ni mwanahisa wa kampuni ya tbl …swali langu ni lini tbl watatoa gawio la mwaka 2017

    1. Raia Mwema says:

      TBL wenyewe kuelekea mwisho wa mwaka ndo watawatangazia wanahisa wao kuwa ni lini watalipa gawio kwa mwaka husika. Inategemea na uamuzi wa management ya TBL kulipa ama kutolipa ulingana na kiasi cha faida kilichopatikana katika mwaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *