Hisa za Swala Oil, Yetu Microfinance, Tatepa zadoda sokoni

Mkurugenzi wa Swala Oil and Gas David Ridge Mestress

HISA za kampuni za Yetu Microfinance, Swala Oil and Gas Limited na Kampuni ya uzalishaji ya chai ya TATEPA zimeendelea kudoda kwenye soko la hisa, baada ya kukosa wateja wa kununua kwa kipindi kirefu sasa.

Kampuni hizo ambazo zote ziliorodheshwa awali kwenye soko la hisa la Dar es Salaam zimeonekana kutokuwa na mvuto kwa wawekezaji, kwani kwa muda sasa, hamna maombi ya kununua, japokuwa zimeendelea kuwekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa.

Kwa mujibu wa ripoti za DSE, tangia mwishoni mwa mwaka jana, hisa za kampuni hizo zimeendelea kukaa kwenye soko bila ya kununuliwa, ikilinganishwa na kampuni nyingine za ndani na zile zilizoorodheshwa kwenye masoko ya kigeni.

Ripoti zimeonyesha kwamba baadhi ya wawekezaji wanaotaka kuuza hisa za kampuni hizo bado wanapata wakati mgumu kuziuza kwani hamna mwekezaji yeyote ambaye amepeleka maombi ya kuzinunua, hali inayofanya ziendelee kudorora kwenye soko.

Katika kipindi cha wiki jana, baadhi ya wawekezaji wa kampuni hizo tatu waliendelea kuweka hisa zao kwenye soko, lakini mpaka mwisho wa wiki, hakuna hata ombi moja lililopokelewa kuzinunua hisa hizo.

Ripoti za kila siku za DSE zimeonyesha kwamba katika kipindi cha wiki jana, zaidi ya hisa 29,980 za Swala Oil and Gas Limited zilikuwa sokoni kwa bei ya shilingi 500 lakini hazikuweza kununuliwa kwa wiki nzima.

Katika wiki ya awali, wawekezaji wa Swala waliingiza sokoni hisa 139,980 siku ya kwanza ya wiki ambazo pia hazikununuliwa na siku iliyofuata zaidi ya hisa 110,000 zilipelekwa sokoni pia bila mafanikio.

Hadi mwisho wa wiki, idadi ya hisa zilizokuwa sokoni zilipungua hadi hisa 29,980 siku ya Alhamisi na Ijumaa, lakini nazo zikaambulia patupu baada ya kukosa wawekezaji wa kuzinunua.

Kwa mujibu wa ripoti isiyokaguliwa ya nusu mwaka iliyoishia Juni 30 mwaka jana,  Swala Oil and Gas Plc ilipata hasara ya baada ya kodi ya dola 482,603 (takriban bilioni moja) kutoka hasara ya dola 932,398 (takriban shilingi bilioni 2) za nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

Rasilimali za kampuni hiyo nazo ziliporomoka hadi kufikia dola za Marekani 663,109 (takribani bilioni 1.5) kutoka dola za Marekani 1.5 milioni (takribani bilioni 4) za nusu ya kwanza ya mwaka 2015.

Taasisi ya kutoa mikopo ya YETU Microfinance nayo ilikumbana na hali kama ya Swala kwani hisa zote zilizopelekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa nazo zilidoda kwani hakukuwa na mwekezaji, kutoka nje na ndani ya nchi aliyeonyesha nia ya kuzinunua.

Ripoti za DSE zimeonyesha kwamba katika kipindi cha wiki jana wawekezaji wa YETU waliuza hisa 4,200 siku ya Jumatatu na hisa 12,000 ziku ya Jumanne lakini zote hizo hazikupata wateja wa kununua kwa bei ya shilingi 600 kwa hisa.

Katika siku tatu zilizobaki kwenye wiki ya awali, hisa 10,000 za YETU, ambayo iliorodhesha hisa zake katikati ya mwaka jana zilikuwa zikiingia sokoni takribani kila siku lakini hadi mwisho wa wiki hakukuwa na ombi hata moja la kuzinunua.

Kampuni ya Tatepa, ambayo inajishughulisha na uzalishaji na usindikaji wa zao la chai nayo ilikumbwa na dhahma hiyo kwani hisa zake zote zinazopelekwa sokoni hazipati wawekezaji wa kuzinunua.

Tatepa iliorodheshwa kwenye soko la hisa mwaka 1999 na bei ya hisa kuanzia Septemba mwaka juzi hadi sasa ni shilingi 650, wakati mtaji wa kampuni hiyo kwenye DSE ilikuwa ni shilingi bilioni 12.1 mwaka 2015.

Hata hivyo, hisa za kampuni nyingine za ndani bado zimeendelea kuuzwa kwenye soko tangia mwishoni mwa mwaka jana na nyingi zimekuwa zikipata wanunuzi kwa mara kadhaa.

Kwa sasa idadi kubwa ya wawekezaji kwenye soko la hisa ni wawekezaji wa kigeni kwani ndio wengi wanaonunua hisa kwa sasa, huku idadi kubwa ya wawekezaji wa kigeni wakiuza hisa zao.

Ripoti za wiki jana zimeonyesha kwamba, Kampuni ya Swissport, ambayo inatoa huduma za usafiri wa anga nchini, ndiyo iliyoongoza kwa kuwa na wingi wa hisa zilizofanyiwa biashara kwani ilifanikiwa kuingiza mauzo ya shilingi bilioni 1.6 kwa siku ya Jummanne pekee.

Kampuni hiyo ilifiatiwa na TBL ambayo katika kipindi chote cha wiki ilifanya biashara ya takriban shilingi milioni 800, ambayo ni nusu ya kiasi kilichoingizwa na kampuni ya Swissport Tanzania.

CRDB ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na kiwango kikubwa cha mauzo ya hisa zake kwani ripoti zilionyesha kwamba, kiasi cha shilingi milioni zaidi ya 80 kilipatikana wiki jana.

Kwa muda sasa, CRDB na TBL zimekuwa zikiongoza kwenye mauzo ya hisa tangia mwishoni mwa mwaka jana, kabla ya ujio wa Swissport Tanzania wiki jana.

DSE ilifuatia kwenye orodha za kampuni zilizofanya biashara katika kipindi cha wiki jana baada ya hisa zake zenye thamani ya takriban shilingi milioni 18 kuuzwa na kununuliwa na wawekezaji mbalimbali.

Madalali wa soko wamebainisha kwamba kunuliwa kwa hisa ni matakwa ya wawekezaji na hali ya soko kwa sasa inaonyesha kwamba wengi wao wanapendelea hisa za TBL, DSE, CRDB na NMB kwani ndizo zinafanyiwa biashara kwa wingi kwenye soko.

“Wawekezaji wengi wanapendelea kampuni za kwenye sekta za bia, benki na Saruji ndio maana sekta nyingine  na mvuto kidogo kwa wawekezaji,” alisema mmoja wa madalali aliyeongea na Raia Mwema.

Akiongelea kuhusu biashara ya wiki iliyopita, meneja Masoko ya bidhaa wa DSE Patrick Mususa alisema kwamba mauzo yalipanda hadi kufikia shilingi bilioni 2.5 kutoka shilingi milioni 550 za wiki ya awali.

Idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa nazo ziliongezeka hadi kufikia hisa 868,000 za wiki jana kutoka hisa 530,000 za wiki ya awali. Kampuni ya Swissport iliongoza katika mauzo kwa asilimia 65.3.

Hata hivyo, Mususa alisema kwamba ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko umepungua kutoka shilingi trilioni 19.1 had shilingi trilioni 18.7 huku mtaji wa kampuni za ndani nao ukipungua kwa shilingi milioni 400.

Viashiria vya kampuni  zilizoorodheshwa katika soko (DSEI) kimeshuka kwa pointi 45 hadi pointi 2,146 hadi pointi 2,192 wiki jana za wiki ya awali kutokana na kupungua kwa bei ya hisa mbalimbali zilizopo sokoni.

Kiashiria cha kampuni za ndani (TSI) wiki jana pia kilipungua kwa pointi 170 kutoka pointi 3,550 had pointi 3,380 kutokana na kupungua kwa bei ya hisa za baadhi ya kampuni nne za ndani.

Sekta ya viwanda (IA) nayo ilipungua kwa pointi 313 kutoka pointi 4,508 hadi pointi 4,194 za wiki jana nah ii ilitokana na kupungua kwa bei ya hisa za Kampuni ya Bia (TBL) kwa asilimia 10.5.

Kwa upande wa sekta ya huduma za kifedha na benki (BI), kiashiria chake kimeshuka kwa pointi mbili kutokana na kupungua kwa hisa ya DSE kwa asilimia 1.9 huku kile cha huduma (CS) nacho kikipungua kwa pointi 20 kutokana na kushuka kwa bei ya hisa za Swissport, ambayo imeongoza kwa biashara ya wiki jana.

Wakati huohuo, mauzo ya hati fungani kwenye soko la hisa yalishuka kjwa asilimia 67 kutoka hati fungani zenye thamani ya shilingi 24.2 bilioni hadi kufikia shilingi bilioni nane za wiki jana.

Kwa mujibu wa Mususa, hati fungani nne za serikali zenye thamani ya shilingi bilioni 8 ziliuzwa na kununuliwa katika wiki iliyoishia Februari 3 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *