Hisa za Vodacom mtihani

HISA za awali za kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom ambazo huenda zikaanza kuuzwa kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mapema mwakani, zitakuwa ‘mtihani’ kwa Watanzania.

Tahadhari hiyo imetolewa na washauri wa uwekezaji ambao wanaamini kwamba huenda Watanzania wasiweze kuzinunua zote kutokana kutokuwa na ukwasi wa kutosha.

Kampuni hiyo ambayo inaongoza kwa wingi wa wateja miongoni mwa kampuni za simu nchini, imetangaza kuwa itauza hisa zake asilimia 25, zenye thamani ya shilingi bilioni 500.

Washauri wa biashara waliozungumza na Raia Mwema mwishoni mwa wiki jana wamebainisha kwamba kiwango cha fedha zinazotarajiwa kukusanywa ni kikubwa mno, ukilinganisha na uwezo wa kifedha wa wawekezaji wengi wa ndani.

Katika kipindi cha miezi ya Januari na Februari, hali ya ukwasi kwenye soko la hisa huwa sio nzuri, kwani wawekezaji wengi wakiwemo watu binafsi na kampuni huwa wanakabiliana na majukumu yenye matumizi makubwa ya fedha ikiwemo malipo ya ada, madai ya kodi na gawio kwa wanahisa wake.

Wawekezaji wakubwa wa ndani katika soko la hisa ni kampuni binafsi, mifuko ya hifadhi za jamii, mashirika ya bima, benki za biashara pamoja na watu binafsi.

Imebainika kwamba kiasi cha fedha kinachopangwa kupatikana kutokana na mauzo ya hisa hizo kitakuwa ni kikubwa kuliko hisa nyingine za awali ambazo zimeshawahi kuuzwa kwenye soko tangu lianzishwe mwaka 1998.

Mshauri mmoja wa biashara kwenye soko la hisa ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kwamba pamoja na kuja kuondoa kiu kubwa kwa wawekezaji, uwezo wa soko hilo bado ni mdogo, hasa wawekezaji wa ndani.

DSE hivi sasa ina kampuni 25 zilizoorodheshwa ambapo kampuni za ndani ni 18 na zile zilizoorodheshwa kutoka masoko ya kigeni yakiwemo Nairobi na London ni saba. Kampuni za Acacia, EABL na TBL ndizo zinazoongoza kwa mitaji mikubwa kwenye soko hilo.

Kwa miaka mingi, wawekezaji wa soko la hisa wamekuwa wakilalamika kwamba wanakosa nafasi ya kuwekeza fedha zao kutokana na kutokuwepo na bidhaa za kutosha (kampuni).

“Tunajionea kuwa uuzwaji wa hisa za Vodacom umeangalia kiu ya wawekezaji lakini naona kiwango ni kikubwa sana ikilinganishwa na uwezo wa wawekezaji. Suala hapa ni namna Watanzania watakavyochangamkia hisa hizo na kuzimaliza zote,” alisema mtaalamu huyo

Hata hivyo, kwa kuwa soko la mitaji tayari limekwishafunguliwa kwa wawekezaji kutoka nje na wa ndani, kuna uwezekano mkubwa kwamba wawekezaji kutoka nje ndio watakaonufaika na fursa hii.

“Unaweza kuwa na hamu kubwa ya chakula, lakini inaweza kutokea pale utakapoletewa chakula hicho na ukashindwa kukila,” alisema mtaalamu huyo.

Alisema kukusanya shilingi bilioni 500 kutoka katika uuzwaji wa hisa za Vodacom Tanzania Ltd Plc itakuwa ngumu kwa wawekezaji wa ndani, hasa kipindi cha Januari.

Inatarajiwa kwamba hisa za Vodacom zitaanza kuuzwa sokoni kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwakani na malengo yake makubwa yalikuwa ni kuwaingiza Watanzania kwenye mfumo rasmi wa umiliki wa uchumi.

Uuzaji wa hisa za awali wa Vodacom Tanzania Limited Plc ni moja ya utekelezaji wa Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Mwaka 2010 ambayo inaagiza kampuni zote za simu za mikononi kuuza hisa zao kwa umma ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Dalali mwingine wa soko la hisa ambaye pia hakutaka kutajwa jina amebainisha kwamba Soko la Hisa la Dar es Salaam bado linakabiliwa na changamoto nyingi ya ukosefu wa bidhaa, lakini ujio wa Vodacom ni mtihani.

“Sidhani kama shilingi bilioni 500 ni saizi ya soko letu la hisa. Lakini ngoja tuone mpaka mwisho,” alisema kwenye mazungumzo na Raia Mwema.

Dalali huyo anaamini kwamba Watanzania wachache tu ndio watapata nafasi ya kununua hisa hizo na idadi kubwa ya hisa huenda ikachukuliwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

“Najua wawekezaji kutoka nje wamezipania sana hisa za Vodacom na pale ambapo zinaorodheshwa wengi wao watauza na fedha zinaenda nje ya nchi.  Bila kuwa na usaidizi wa wawekezaji kutoka nje ya nchi, toleo hili la hisa za awali za Vodacom litakuwa mtihani mkubwa kwa Watanzania kwani hiyo ni nafasi ya pekee ya kuwawezesha kiuchumi,” alisema

Kampuni hiyo tayari imekwishapeleka rasimu ya waraka wa matarajio (Prospectus) na maombi kwenye Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMSA), ambayo ndiyo mamlaka inayosimamia masoko ya mitaji nchini.

Akizungumza baada ya kuwasilisha rasimu ya waraka wa matarajio na maombi kwa CMSA, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao, alisema kwamba anatarajia mafanikio makubwa katika mchakato huo.

Mamlaka ya Mitaji na Masoko (CMSA) imethibitisha kupokea rasimu ya waraka wa matarajio pamoja na maombi rasmi ya uuzaji wa hisa na kusema kwamba yatapitiwa kabla ya kupitishwa.

Akiwasilisha muswada wa fedha kwa mwaka wa fedha 2016/17 Juni mwaka huu, mjini Dodoma, Waziri wa Fedha Dk Phillip Mpango alibainisha kwamba sheria inazitaka kampuni zote za simu za mkononi kuuza hisa hizo kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Tanzania ina jumla ya kampuni nane za simu za mikononi ambazo zote kwa pamoja, kabla ya Desemba 31 mwaka huu zinatakiwa kukamilisha mpango wa kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwa umma.

Vyanzo ndani ya sekta ya mawasilino vimebainisha kwamba kampuni zote huenda zikamaliza taratibu za kuuza hisa zao katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka kesho.

Hata hivyo, haijajulikana ni hatua gani itachukuliwa kwa kampuni ambayo itashindwa kufanya mchakato wa kuuza hisa zake kabla ya kipindi kilichopangwa.

Uchambuzi uliofanyika hivi karibuni umebainisha kwamba huenda hisa hizo zisifanikiwe kuuzwa zote kwani dalili zinaonyesha kwamba kipaumbele kitatolewa kwa Watanzania.

4 thoughts on “Hisa za Vodacom mtihani”

 1. Valence Myovella says:

  How much is it sold per one share?

  1. Raia Mwema says:

   TZS 850 per share!

 2. evodia says:

  Minimum amount required  for shares is?

  1. Raia Mwema says:

   Minimum amount of shares is 100.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *