Makala
Mraba wa Maggid
Hivi Mugabe nae ni chaguo la Mungu?
Maggid Mjengwa
Toleo la 036
2 Jul 2008

KUNA wakati dikteta  Mobutu Seseseko wa iliyokuwa Zaire ya zamani alipata kumfokea Waziri wake wa Habari na Utangazaji.

Kisa?  Waziri yule aliruhusu televisheni ya taifa kurusha mkanda ulioonyesha tukio la kukamatwa na kupigwa risasi kwa dikteta Nikolai Ceausescu wa Romania mwishoni mwa miaka ya 80.

Tukio la Ceausescu kukamatwa na kupigwa risasi lilionyeshwa dunia nzima. Waziri yule wa Mobutu hakuona sababu ya kuwaficha watu wa Zaire kuliona, maana ule ulikuwa ni ukweli wa hali halisi, kuwa wananchi waliokuwa wakikandamizwa wamesimama na kufanya mapinduzi.

Lakini kwa Mobutu, dikteta Ceausescu hakutofautiana  sana na yeye ( Mobutu), hivyo aliingiwa na hofu kuwa kwa Wazaire kuliona tukio lile, lingewaamshia ari ya kutaka kupambana na utawala wake.

Kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, serikali na vyama tawala vina vyombo vyake vya mawasiliano ikiwamo redio na televisheni na magazeti. Katika nchi nyingi za Kiafrika, hata kama huitwa ni vyombo vya umma vya mawasiliano, vyombo hivyo huwa na jukumu la kwanza la kulinda maslahi ya watawala.

Waziri yule wa habari wa Mobutu alimtangulia bosi wake katika kusoma alama za nyakati, akaruhusu taarifa ile ya kukamatwa na kupigwa risasi kwa Ceausescu irushwe hewani ingawa haikulinda maslahi ya bosi wake. Ni  Mobutu aliyeshindwa kusoma alama za nyakati, na zaidi, alikiogopa kivuli chake mwenyewe.

Katika nchi zetu hizi za Kiafrika, hadi hii leo bado tuna viongozi wenye hulka za akina Mobutu. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ni mfano mmojawapo.  Kuna mengi yanayofanana kati ya Mugabe na Mobutu.

Itakumbukwa kwamba alipoingia madarakani, Jenerali Mobutu alianza kudhibiti vyombo vya habari, wasomi na waandishi wa vitabu.

Mugabe yeye hakuanza kama Mobutu, bali anamalizia maisha yake ya kiungozi kama Mobutu. Ni katika Zimbabwe ya sasa ambapo hali ni mbaya kuliko katika Zaire ya Mobutu. Mugabe amevidhibiti vyombo vya habari na anawaandama wote wenye kupingana nae.

Kuna Wazimbabwe waliopoteza maisha yao kwa kupingana na Mugabe, kuna wengi pia walioikimbia nchi yao.

Mugabe, kama ilivyokuwa kwa Mobutu, naye  anataka na anapenda Wazimbabwe wamuimbe yeye na wampigie makofi hata kwa kauli za kipumbavu. Mugabe anashindwa kuelewa kuwa unaweza kumpeleka punda mtoni, lakini kamwe huwezi kumlazimisha kuyanywa maji.

Kwamba unaweza kumlazimisha mwanadamu kukupigia makofi, lakini kamwe si kutabasamu. Hilo la mwisho hutoka moyoni.

Ni majuzi tu Mugabe na kundi lake wameshiriki kuendesha uchaguzi wa kihuni huku mpinzani wake akichukua hatua za busara za kujitoa. Kuna kila dalili kuwa mwanzo wa mwisho wa Mugabe umefikia. Mugabe amewatumbukiza Wazimbabwe kwenye shimo refu na lenye giza nene.

Hakika Mugabe amewapeleka Wazimbabwe wengi motoni wangali bado duniani.  Ndipo hapa tunajiuliza busara za kutamka kuwa mtawala ni chaguo la Mungu! Hivi Mugabe nae ni chaguo la Mungu? Mobutu na  Idi Amin nao walikuwa chaguo la Mungu? Huenda huku ni kujitafutia dhambi kwa kumsingizia Mungu kwa asiyostahili nayo.

Hakika Zimbabwe ni mfano wa kutia majonzi. Nilibahatika kufika Zimbabwe kwa mara ya kwanza mwezi Desemba mwaka 1987. Ni miaka 21 iliyopita. Niliyoiona wakati huo ni nchi iliyoonyesha dalili zote za kunawiri kiuchumi.

Niliiona Zimbabwe yenye umri wa miaka saba tangu ipate uhuru wake. Kama ni mtoto, basi ulikuwa ni umri wa kwenda shule. Ndio, nchi ilinawiri. Kwa dola moja ya Zimbabwe mfukoni niliweza kula mlo mmoja wa mchana na chenji ikabaki.Leo Zimbabwe kuna noti moja ya dola milioni kumi!

Miaka 21 iliyopita sikuishia Harare tu, nilifika mji wa Bulawayo pia katika Zimbabwe hiyo hiyo. Huko  nikaona dalili hizo hizo za matumaini. Nikaenda hadi vijijini, sehemu za Mberengwa karibu na mpaka wa Msumbiji. Huko nikaona pia dalili za matumaini.

Watoto walikwenda kwenye shule zenye kutoa elimu bora kuanzia ngazi ya msingi. Huduma za afya nazo zilikuwa bora. Kwa wakati huo, Mugabe na chama chake ZANU walijitahidi kuhakikisha Wazimbabwe wanapata elimu bora na huduma nyingine kama vile afya.

Miaka kumi baadae, mwaka 1997 nikafika tena Zimbabwe. Nikaanza kuona dalili za treni inayoacha njia. Niliyaona hayo Harare, Bulawayo na kule Nyanga, mbali sana na mjini. Ikawa ni tofauti kubwa sana na Zimbabwe ya mwaka 1987.

Kinachomtokea Mugabe leo ni kile alichokipanda mwenyewe lakini anaogopa mavuno yake. Watoto wale niliowaona kule kijijini Mberengwa miaka 21 iliyopita ndio "wanaomsumbua" Mugabe sasa. Wamepata elimu bora, sasa wanayaona mapungufu pia.

Wanataka kushiriki siasa za nchi yao kupitia vyama vingi. Mugabe ameshindwa kusoma alama za nyakati. Wengi wa vijana wale aliowasomesha wakaja kuwa manesi bora barani Afrika, walimu bora pia. Leo wengi wao wamekimbilia Ughaibuni,  Mugabe hawataki tena.

Kwa Mugabe, hao "wameelimika sana!" Lakini, waliokimbia Zimbabwe nao wanawaamsha wenzao walio nyumbani, vuguvugu la kutaka mabadiliko linaendelea.

Mugabe nae anakikimbia kivuli chake. Hata kama amedhamiria kufia madarakani, kifo chake kitabaki kuwa ni cha aibu.

Mugabe wa sasa anarudisha nyumba mshale wa saa ya kuelekea kwenye maendeleo ya Zimbabwe na watu wake. Huu ni wakati wa Wazimbabwe kuongeza ari ya mapambano yao dhidi ya utawala dhalimu wa Mugabe na kundi lake. Ni wakati wa kufanya mabadiliko hata kama ni kwa kumwaga damu.

Somo kubwa tunalojifunza hapa, ni namna gani mtu mmoja au kikundi cha watu kinavyoweza kuiingiza nchi shimoni kwa sababu za kifisadi.

Ni imani yetu, kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho. Huu ni mwanzo wa mwisho wa Mugabe. Huu si mwisho wa mwanzo wa Zimbabwe. Mungu Ibariki Afrika.  

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Maggid Mjengwa
mjengwamaggid@gmail.com
+255-754678252, +255-712956131
http://mjengwa.blogspot.com

Maggid Mjengwa pia ni Mwandishi wa Kitabu; "Maisha Ya Barack Obama, alikotoka, aliko na anakokwenda". Kinapatikana mitaani.

Toa maoni yako