NIMEAMBIWA kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halina mpango wa kumwongezea mkataba Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Borge Poulsen, mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa sasa kuifundisha timu hiyo mnamo Agosti mwaka huu.
Haijulikani bado ni nani anaweza akapewa nafasi hiyo baada yake. Hakuna mtu ambaye anaweza kwa uhakika kabisa kutangaza ni makocha wangapi wanaweza wakavaa viatu vya raia huyo wa Denmark.
Na hili ndilo tatizo letu la kwanza kama taifa wakati linapokuja suala la uteuzi wa kocha mpya wa ama vilabu au timu yetu (zetu) za taifa. Nimesema zetu kwa vile nimebaini tatizo hili lipo kwenye karibu michezo yetu yote.
Rais Jakaya Kikwete alimleta kocha kwa ajili ya mchezo wa netiboli na baadaye kocha huyo akaondoka pasipo kufanya chochote. Wakati nikiendesha kipindi cha luninga cha Spoti Kizaazaa, nilipata bahati ya kuzungumza na makocha wawili wa timu za taifa za michezo ya riadha na ngumi kutoka Cuba.
Primentel Hurtado wa ngumi na Andre Baro wa riadha. Wote hawa kuna kipindi huwa wanakaa muda mrefu bila ya kufanya kilichowaleta. Swali linakuja, kwa nini tulimleta Poulsen, Hurtado au Baro?
Nani alifanya upembuzi yakinifu na ikajulikana wazi pasipo shaka kwamba suluhisho ni Poulsen kwenye soka? Nani alifanya utafiti na akabaini kwamba suluhisho la Tanzania kwenye ngumi ni kumleta Hurtado wa Cuba?
Ndiyo hapa sasa linapokuja suala la uteuzi wa wiki hii wa Roy Hodgson kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya soka ya England.
Chama cha Soka cha England (FA), kimewashangaza wengi kwa kumteua Hodgson kuwa kocha ilhali wengi walidhani nafasi hiyo ingeenda kwa Harry Redknapp, kocha wa sasa wa Tottenham Hotspurs.
FA imetoa hoja tatu za kumteua Hodgson lakini kubwa zaidi ni namna atakavyosadia kuendesha kituo kipya cha soka cha taifa la Uingereza kilichopo Burton.
Chuo hicho kitakuwa na kazi ya kufundisha makocha wa baadaye wa Uingereza na kukuza vipaji vya vijana. Kinafanana sana na kile maarufu cha Clairefontaine cha Ufaransa au La Masia cha Barcelona. Waingereza wameweka matumaini makubwa sana kwenye kituo hiki.
Inaonekana Roy ana mawazo mapana zaidi ya kuendeleza kituo hiki kuliko Harry. Na ukweli kwamba amefundisha nchi nyingi za Ulaya kama vile Sweden, Finland, Uswisi na Italia, kumemwongezea pia maksi. Kwa hiyo uamuzi wa kumteua Hodgson, hata kama una wakosoaji kibao, una maelezo.
Ningetaraji hali kama hii wakati TFF au Serikali inapotaka kuleta makocha kutoka ughaibuni au hata hapa ndani kwenye timu zetu za taifa.
Kwamba, je, Poulsen akiondoka, taifa letu litahitaji kocha wa namna gani kumrithi? Kocha wa kutupeleka kwenye Kombe la Dunia mwaka 2014 au 2018? Kocha wa kutupeleka kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani au mwaka 2018?
Kocha mwenye historia ya kuzoa mataji au kukuza vipaji? Kocha mwenye historia ya kukuza maendeleo ya mchezo husika kwenye nchi alizowahi kwenda au kocha mbomoaji?
Je, tutahitaji kocha wa bei nafuu na mzuri au wa bei mbaya na mzuri? Tuna uwezo wa kumwezesha kupata yote anayohitaji ili kufanikisha kile kilichotufanya tumchague yeye?
Je, kuna miundombinu ya kutosha kumwezesha kocha huyo kufanya kazi tunayoitaka au miundombinu yetu itamfaa zaidi kocha X kuliko kocha Y? Je, kama kocha husika huleta matokeo mazuri baada ya miaka mitano, je tunaweza kumtetea hadi afikishe muda huo hata kama washabiki watakuwa hawamtaki?
Maana tunafahamu kwamba subra ni jambo adimu kwa mashabiki.
Si vizuri taifa letu kuleta au kupokea tu makocha kwa sababu wanalipiwa na mtu fulani. Si vizuri kupokea makocha kwa sababu wamepigiwa debe na mawakala wao. Taifa letu halifaidiki kwa chochote.
Ningependekeza kuwa kwa wakati huu ambapo inajulikana dhahiri kuwa Poulsen ataondoka, TFF ingefanya jambo la mbolea kama ingeanza kuandika muhtasari kuhusu ni aina gani ya kocha ambaye anafaa kuchukua mikoba ya Poulsen.
Wakishajua ni sifa zipi zinatakiwa, waangalie ni akina nani wenye sifa hizo ambao wako sokoni hivi sasa. Ni muhimu kuwa na majina walau matatu ili kupata chaguo zuri.
Baada ya kuwabaini kitakachofuata ni kuwapa kazi. Ni lazima waajiri hao wawaweke makocha hao kwenye madaraja. Kuwe na mwenye nafasi ya kwanza, wa pili na watatu.
Itasaidia zaidi kufanya kazi hiyo hivi sasa kwa vile kuna makocha wanaweza kuwa hawana kazi leo lakini wakapata kazi wiki ijayo. Iwapo nchi masikini kama Burkina Fasso inaweza kuajiri kocha mkubwa kama Paulo Duarte na Senegal wiki hii tu imempata Pierre Lenchantre, kocha maarufu tu duniani, nasi tunaweza kupata makocha wazuri tu tukitaka.
Cha msingi ni kujiandaa kupata kocha tunayemtaka. Nimetumia tu mfano wa TFF kwenye soka lakini lengo la makala hii ni kutaka vyama vyote husika vya michezo vijenge utamaduni wa kuleta makocha inaowahitaji na si kuletewa makocha.
Sisemi kwamba kwa utaratibu huu tutaanza kutwaa mataji lakini walau kuna mtu ataweza kutoa maelezo ya kwanini tumemleta kocha fulani na si kama ilivyo sasa ambapo inaonekana vyama vinaletewa tu makocha na watu.
Poulsen alikuwa miongoni mwa makocha wa timu ya taifa ya Denmark mwaka 1992 wakati walipotwaa Kombe la Ulaya. Baada ya hapo amefundisha timu mbili tatu za Asia. Swali linakuja, ni sifa zipi zilimpa nafasi ya kuja kuifundisha Taifa Stars?
Unaweza leo kumleta Jose Mourinho aje kuifundisha Stars na asipate mafanikio lakini Henri Kasperzcack wa Poland anaweza kuja na kuipa Stars mafanikio. Tatizo ni kufahamu una wachezaji wa aina gani na wanahitaji mwalimu wa namna gani na kwa muda gani.
Ni muhimu sana kwa taifa letu kuwa na utaratibu huu wa kujipanga kabla hatujakurupuka kuleta kocha mpya.
Maoni ya Wasomaji
nahisi aliyesema "...........
nahisi aliyesema "...................kichwa.......mwendawazimu" alikuwa sahihi kiasi flani.