Hongera Nape, lakini usiishie kwenye bendera

MICHEZO nchini Tanzania iko 'hoi bin taaban' na inapumulia mashine. Yote iko katika hali hiyo. Si soka, si riadha, si ngumi, michezo yote hoi.

Hakuna mchezo unaoweza kusimama juu ya mchezo mwingine kujisifu unafanya vizuri. Michezo yote iko kwenye sura ya simanzi.

Hali ya michezo kuwa hivi imefanya hata mashabiki wa michezo wenyewe kukata tamaa na michezo wanayoipenda hasa linapokuja suala la ushiriki nje ya nchi.

Ni soka pekee ambako mashabiki bado wana imani na kujaa kwa wingi uwanjani, lakini nako hakuna lolote la maana linalowafanya mashabiki wa mchezo huo kuwa na imani ya kupata wanachokitaka wanapozitazama timu zao.

Ndiyo,  kama nchi katika michezo tumekwama na hakuna wa kutukwamua zaidi ya kujikwamua sisi wenyewe. Kazi kubwa inatakiwa ifanyike kwenye michezo yote ili yale mafanikio wanayoyaota Watanzania wengi siku moja yawe ya kweli.

Kazi ya kuiinua michezo si kazi rahisi kama kuchukua kipande cha mkate na kukipaka siagi kisha kukipeleka kinywani, hii ni kazi inayomuhitaji kila mmoja kwenye nafasi yake ajitoe na awe na uzalendo.

 

Hii si kazi ya vyama vya michezo, viongozi wa vyama hivyo na wadau, hili ni jukumu la kila Mtanzania anayeguswa na michezo kushindwa kusonga mbele.

Licha ya kila mmoja kujitoa kwenye nafasi yake, lakini somo la uzalendo ndilo kuu linalotakiwa kuingia vifuani mwa watu watakaojitoa kuipigania michezo ambayo awali ilikuwa ikifanya vyema.

Tuna maswali kadhaa ya kujiuliza kabla ya kufanya lolote lile linalohusu anguko la michezo yetu kuanzia ngazi za wilaya, tarafa, mkoa mpaka taifa.

Kama tuliweza kufuzu Mataifa Afrika ya timu nane mwaka 1980, tunashindwaje kufuzu wakati huu ambao kuna zaidi ya nafasi ya timu 15 zinazoshiriki? Tunatakiwa kujiuliza maswali ya namna hii wapi tulipokosea.

Ilikuwaje tuwahi kuzalisha wanariadha mahiri, mabondia mahiri, tushindwe wakati huu ambao dunia imekuwa ya utandawazi?

 

Haya ndiyo maswali tunayotakiwa kujiuliza ili tukishapata majibu iwe rahisi kujitibu na kurudisha hadhi ya michezo ndani na nje.

Muda wa kunyoosheana vidole na kutupiana lawama umeshapita na hauko tena.

Huu ni muda wa kuijenga upya michezo ili kutoa ajira nyingi kwa vijana wenye vipaji kuweza kujiajiri kupitia vipaji vyao. Uendeshaji wa sasa wa michezo ni kama michezo yenyewe iko rehani.

Licha ya yote hayo uliyoyasoma juu na kuzalisha lundo la maswali kwenye bongo lako, michezo yetu inahitaji nguvu kubwa ya serikali ili iweze kukua vyema si vinginevyo.

Nguvu ya serikali ndiyo nyota wa mchezo kwenye uinuaji wa michezo nchini. Serikali ikitaka baada ya miaka mitano kutoka sasa Tanzania iende kushinda medali mbalimbali katika michuano yake inawezekana.

Hakuna nchi iliyopiga hatua katika michezo yake kama nyuma hakuna mkono wa serikali. Hata Wakenya walioshinda medali katika riadha mwaka jana kwenye michuano ya Olimpiki nchini Brazil, kulikuwa na nguvu kubwa ya serikali yao na makamu wao wa rais ndiye alikuwa mkuu wa msafara. Unadhani zile medali zilikuja kama bahati? Hapana! Walizitaka na wamezipata.

Kama kila chama kikijitahidi kuipeleka mbele michezo na serikali ikaipa kisogo michezo yenyewe hakuna kinachoweza kubadilika zaidi ya kila siku tutakuwa tukikutana hapa katika kurasa za namna hii na kutaja majina ya waziwazi kuwa kiongozi wa chama fulani anaiangusha taasisi yake. Serikali ndiyo mhimili mkubwa katika hili na hakuna mwingine anayeweza kuisaidia michezo.

Mkono wa serikali unahitajika viwanjani ili kubadili sura nzima ya michezo inayoonekana kulegalega wakati huu.

Vyama peke yake bila mkono wa serikali haviwezi kubadili lolote michezoni.

Ataingia kiongozi huyu na nahau zake nyingi za hapa na pale, ataondoka kiongozi huyo na kuja kiongozi mwingine naye atakuwa kama hivyo, lakini kama hakuna nguvu ya serikali ni wazi tunatwanga maji kwenye kinu bila kujijua.

Katikati ya wiki iliyopita Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alikabidhi bendera ya Tanzania kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnum’ aliyekwenda kutumbuiza nayo kwenye ufunguzi wa fainali za Mataifa Afrika nchini Gabon.

Huu ulikuwa ushindi na mwanzo mzuri kwa michezo kutupiwa macho na serikali.

Kitendo cha Nnauye ni cha kupongezwa kwa wanamichezo. Lakini kutoa bendera na nasaha pekee haitoshi kuinua michezo.

Nnauye ameonyesha ni mtu ambaye alikuwa akisubiliwa muda mrefu nchini.

Watu wa michezo tulimkosa miaka mingi mwanadamu wa aina hii. Huyu ni mtu aliyehitajika miaka mingi kuja kuijengea misingi na mwanzo mzuri michezo yetu.

Kitendo chake cha kusimama mbele ya vyombo vya habari na kumkabidhi bendera Diamond Platnumz, kinaonyesha wazi serikali ya awamu hii inaipa kipaumbele michezo.

Lakini nguvu na Nnuye haitakiwi kuishia kwenye utoaji wa bendera na kumsubili Mtanzania arejee na tuzo na kupiga naye picha kisha kumpongeza, nguvu hii anatakiwa kuisambaza kuanzia chini kwenye michezo yote.

Kasi hii aliyonayo na wadhifa wake siku moja ataitoa hapa ilipo michezo yetu na ikaelekea kwenye kilele cha mafanikio na kurudisha ajira kwa vijana waishio mtaani wakati wana vipaji.

Nnauye iamshe michezo yetu na kurudisha sura za furaha na kutoa sura za huzuni kwenye mapaji yetu.

Michezo yetu ina changamoto nyingi zaidi ya ukabidhiwaji bendera, lakini kwa mwanzo huu si vibaya tukianza kujipongeza kumpata mtu aina ya Nnauye. Maana michezo ilikosa dira, lakini mpaka kufikia 2020 kuna kitu kitakuja kutokea. Kila la kheri Nnauye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *