Makala
IGUNGA: Ubunge ni CCM, ‘ushindi’ ni CHADEMA!
Mayage S. Mayage
Toleo la 206
5 Oct 2011

UCHAGUZI mdogo wa Igunga umemalizika. Hatimaye Chama cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake, Dk Dalaly Peter Kafumu wameibuka washindi baada ya kujikusanyia kura 26,400 na hivyo kuwashinda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea wake Joseph Kashindye waliojikusanyia kura 23,260.

Nianze makala hii kwa kuipongeza CCM kwa ushindi huo ambao umekiwezesha kutetea jimbo hilo lililoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wake, Rostam Azizi aliyejiuzulu mwezi Julai mwaka huu.

Aidha, nichukue fursa hii kuipongeza CHADEMA kwa kujizolea kura nyingi kiasi hicho; ikijulikana kwamba chama hicho ni kipya kabisa katika siasa za Igunga.

Lakini pia nichukue nafasi hii kukipa pole Chama cha Wananchi (CUF) kwa mporomoko wa ghafla kutoka kura 11,000 mwaka jana hadi kura 2,000 tu.

Kwa ujumla pia nivishukuru  vyama vyote vilivyojitokeza kugombea kiti hicho kwa kuwa hiyo ndiyo kazi na wajibu wa kwanza wa kila chama cha siasa, na zaidi niwashukuru wagombea wote walioshindwa pamoja na vyama vyao kwa kuyakubali matokeo. Asiyekubali kushindwa siyo mshindani!

Baada ya utangulizi huo, nianze makala yangu ya leo kwa kuwakumbusha wasomaji wangu juu ya makala yangu ya wiki iliyopita iliyobeba kichwa  kilichosomeka: Niliyojifunza katika kampeni za Igunga. Katika makala hiyo, nilisema wazi kwamba, ingawa siyo nia yangu ya kukipigia debe CCM, lakini chama hicho ndicho kingeibuka mshindi wa uchaguzi mdogo huo wa Igunga.

Nilitoa sababu za msingi kwa nini chama hicho kitaibuka mshindi; ingawa pia nilitoa angalizo nikisema ushindi wenyewe huo hautapokelewa kwa mikono miwili na makundi yote ya wanachama, viongozi na wapenzi wa CCM.

Nilisema miongoni mwa sababu zitakazokifanya CCM kishinde ni kuwapo kwa chama hicho Igunga kabla na baada ya Uhuru, kwa maana ya TANU na baadaye CCM, pia kikijivunia mtandao mkubwa wa wanachama uliojengwa miaka mingi iliyopita. Aidha, nilisema mtaji wa madiwani wake wanaoshikilia kata 25 kati ya 26 za jimbo hilo, ungekiwezesha chama hicho kuwaachia kazi ya kampeni madiwani hao na kukiletea ushindi mkubwa.

Nikasema kwamba kama matokeo yangekuwa kinyume na ushindi, basi, tafsiri na ujumbe wa wazi kwa chama hicho ungekuwa kwamba madiwani wake na mtandao huo mkubwa wa wanachama wake wamekiasi kama alivyokiasi aliyekuwa mbunge kipenzi cha wana Igunga, Rostam, aliyeamua kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi wa kisiasa alizozipata kupitia chama hicho kwa maana ya ujumbe wa NEC Taifa na ubunge wa Igunga.

Kuhusu ushindi wa chama hicho kutoshangiliwa na viongozi na makada wake wote, niliweka wazi kwamba kampeni hizo za Igunga zimetoa somo kuu moja kwa baadhi ya makada wake; nini kuanzia sasa, na hasa baada ya uchaguzi huo wa Igunga wanatakiwa wakihubiri badala ya kuendelea na mahubiri ya falsafa ya kujivua gamba kwa kuwanyoshea vidole ‘mapacha watatu’ - Rostam, Edward Lowassa na Andrew Chenge.

Nilitaja baadhi ya majina ambayo, kwa nafasi zao na umuhimu wao ndani ya Chama ,walipaswa kushirikishwa uchaguzi huo lakini badala yake walipigwa marufuku na chama chao kukanyaga Igunga.

Wengi wa wasomaji wangu walielewa nilichokiandika, lakini pia wapo ambao hawakunielewa. Yote hayo ni sehemu ya mafanikio ya mwandishi!

Matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga yalitangazwa mchana wa Jumatatu. Binafsi sikupata bahati ya kwenda Igunga katika kipindi chote hicho cha kampeni. Lakini kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyokuwa na waandishi wake huko, nimejifunza mengi kuhusu Igunga na hali ya maisha ya wananchi wake.

Moja kubwa ambalo limeelezwa na karibu vyombo vyote vya habari nchini, ni umasikini wa wana Igunga pamoja na uduni wa huduma muhimu za jamii kama vile maji, afya na miundombinu ya barabara.

Mmoja wa wahariri aliyekuwapo huko, ametuambia wazi kupitia makala yake kwamba wananchi wa Igunga wanakunywa maji wanayoyapata kutoka kwenye mikondo ya maji. Anasema maji hayo wanayokunywa ndiyo yanayotumiwa na mbwa mwitu na fisi kunywa na kuogea usiku.

Lakini pia anasema kina mama wanatembea na ndoo na majembe kusaka maji porini, na wanapofika mahali penye dalili ya maji huanza kuchimbua na kupata maji hayo.

Binafsi, sina haja ya kutilia shaka taarifa ya mhariri wangu, Kulwa Karedia, katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti lake analolisimamia la Mtanzania Jumapili. Sina shaka na taarifa hiyo kwa sababu hicho alichokisema Karedia amekishuhudia kwa siku zote alizokaa Igunga kiasi cha kuwahurumia wananchi wa Igunga kwa mateso wanayoyapata kutokana na kero hiyo ya maji.

Tatizo nililoliona katika taarifa hiyo ya Karedia ni kutoshutumu wala kumtaja mhusika mkuu aliyesababisha madhira yote hayo ya wana Igunga, na badala yake akaelekezea shutuma zote kwa CCM na serikali yake; huku akikazia kuwaomba wana Igunga kutokichagua CCM wala mgombea wake kwa kuwa kwa miaka 50 ya Uhuru chama hicho na serikali hawajawafanyia chochote cha maana wana Igunga.

Ndugu zangu, sisi tulioko nje ya Igunga siku zote tumekuwa tukiaminishwa kwamba jimbo la Igunga ni paradiso na mfano wa maendeleo wa karibu majimbo yote nchini.

Siku zote tumekuwa tukihubiriwa na wanasiasa wa ndani ya CCM kwamba kabla ya mwaka 1994, jimbo la Igunga lilikuwa la mwisho kwa maendeleo, lakini baada ya mwaka huo kuwa chini ya mbunge Rostam Azizi limetoka kuwa jimbo na wilaya ya mwisho mkoani Tabora na kuwa jimbo na wilaya ya kwanza kwa maendeleo katika majimbo yote na wilaya zote za mkoa wa Tabora.

Hivyo ndivyo tumekuwa tukiambiwa. Hakuna mbunge wa jimbo lolote la Tabora aliyekanusha porojo hizo kuhusu paradiso ya Igunga wala hakuna mwana Igunga aliyekanusha na kusema huo ni uongo, tuna shida ya kila kitu na kila huduma hapa Igunga.

Hata CCM kilijua kwamba Igunga ni paradise, na ndiyo maana hata Mzee Benjamin Mkapa aliposimama kwa mara ya kwanza katika kampeni za uzinduzi wa kampeni za kumnadi Dk. Kafumu ile Jumamosi ya Septemba 10, aliwaomba wana Igunga wamchague mgombea wake huyo ili aendeleze mema na mazuri ya kimaendeleo aliyoyaacha mtangulizi wake, Rostam.

Karedia amekaa wiki tatu na nusu tu Igunga, sawa na takriban siku 27/28  na ameweza kushuhudia namna wana Igunga ‘walivyopigika’ kwa umasikini na maisha duni ya kulala bado kwenye nyumba za tembe.

Lakini hatuelezi kama mbunge aliyekuwapo, aliyeliongoza jimbo hilo kwa takriban miaka 18, sawa na karibu siku 6,588, aliwahi kuziona kero hizo na kufanya juhudi zozote za kuwaondelea madhira hayo wananchi hao wa Igunga.

Kwa mawazo yake, wajibu wa kuwaletea maji wana Igunga walau visima vifupi ni kazi ya CCM na serikali yake.

Mtu wa kwanza mwenye wajibu wa kuwaondolea kero ya maji na miundombinu mingine ya jamii, kama maji, afya, elimu na barabara za kuunganisha vijiji ni mbunge akisaidiana na Halmashauri yake.

Serikali Kuu inafanya yale makubwa ambayo kwa uwezo wa mbunge na uwezo wa Halmashauri hawawezi kuvifanya kutoka na ukubwa wa gharama zake. Ndiyo maana CCM katika Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu inaahidi ahadi ndo na kubwa kulingana na mahitaji ya jimbo na mkoa.

Siyo kila ahadi inayotangazwa na mgombea urais katika jimbo, kama kero hiyo ya maji, inatakiwa itekelezwa na Serikali Kuu; bali ahadi ile inakuwa mzigo kwa mbunge atakayechaguliwa pamoja na watendaji wa halmashauri husika.

Nawapongeza waandishi wote waliojaribu kwa jitihada zao binafsi kueleza juu ya ukweli halisi wa maisha ya wana Igunga - ukweli unaofuta porojo, propaganda na ghilba nyingine za kisiasa zilizokuwa zikituelekeza kwamba Igunga ni paradiso ya maendeleo mkoani Tabora.

Kwa kutupa ukweli huo, tunapata jibu sahihi la ni kwa nini CCM imekataliwa kwa kasi hiyo Igunga. Tunapata jibu ni kwa nini wana Igunga wameipokea ghafla CHADEMA na kukipigia kura zote hizo 23,260 ndani ya kampeni za muda mfupi ulio chini ya siku 30.

Ndugu zangu, wahenga walishasema tangu zamani. Mwenye shibe hamjui mwenye njaa. Rostam alipokuwa mbunge wa Igunga, matatizo ya wana Igunga hayakuonekana. Alipojing’atua katika siasa uchwara, miezi miwili tu iliyopita, Igunga inayo matatizo kibao.

Huu kama siyo upofu wa kisiasa ni nini? Kwani Rostam kaondoka na maji yake ya mabomba na visima? Kaondoka na barabara zake? Kaondoka na malambo yake ya maji?

Weledi wa mambo wanaposema biashara na siasa zitenganishwe, wana maanisha mfano wa jimbo la Igunga. Kumbe jimbo lilikuwa na matatizo kibao, lakini inapofika wakati wa uchaguzi tu mbunge wake anapita bila kupingwa kwa sababu ya ujanjaujanja tu!

Wanasiasa wote wa Tabora wakawa vipofu, wakawa hawaoni mateso hayo ya wana Igunga kama tulivyoelezwa na waandishi wetu waliokuwa huko kupitia habari na makala zao.

Labda nihitimishe makala hii kwa kuwauliza waandishi wetu waliokuwa Igunga, hivi kama Igunga ina matatizo lukuki namna hiyo kiasi cha kina mama na watoto wao kuhangaika na maji ya mitaro, huku wilaya hiyo hiyo ikitajwa kuwa paradiso ya mkoa mzima wa Tabora, na ndiyo inayoongoza kwa maendeleo kwa kila sekta kama tulivyoambiwa, na hayo majimbo mengine na wilaya nyingine ambazo sasa zimechukua nafasi ya Igunga ya mwaka 1994 zina hali gani?

Kwa nini CCM isitarajie matokeo mabaya zaidi siku zijazo? Nauliza hivyo; maana kwa hali ilivyojitokeza katika uchaguzi huo mdogo wa Igunga; japo ubunge umekwenda kwa CCM, lakini ushindi wa kweli umekwenda kwa CHADEMA.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Mayage S. Mayage
mayages@yahoo.com
+255-713670110

Toa maoni yako