Israeli yatishia kuharibu mfumo wa ulinzi anga wa Syria

Ndege nne za kijeshi za Israeli zilifanya mashambulizi kadhaa katika maeneo tofauti ndani ya Syria na Syria ulitumia makombora kujihami kuzishambulia ndege hizo. JACK GUEZ/AFP/Getty Images

WAZIRI wa Ulinzi wa Israel ametishia kuharibu mfumo wa ulinzi wa anga iwapo mfumo huo utatumiwa tena kuzishambulia ndege za kivita za nchi hiyo.

Jeshi la Israel lilisema kwamba lilitungua moja na roketi kadhaa zilizorushwa na Syria ili kuangusha ndege za Israeli wiki iliyopita, katika makabiliano makali zaidi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni baina ya maadui hao jirani.

Maafisa wa Jeshi la anga walisema kwamba ndege nne za kivita za Israel zilikuwa kwenye misheni ya kuharibu msafara wa magari yaliyobeba silaha zilizokuwa zinapelekwa kwa kundi la Hezbollah na kwamba zilishambuliwa na makombora kutoka ardhini, na moja ya makombora hayo liliangushwa na mfumo wa ulinzi angani wa Israel unaofahamika kama “Arrow.”

“Iwapo Wasyria watatumia mfumo wao wa ulinzi dhidi ya ndege zetu tena, tutaiharibu mifumo hiyo bila kusita,” Avigdor Lieberman alisema, matamshi ambayo yalitangazwa na redio ya nchi hiyo.

Damascus ilidai kwamba ilifanikiwa kutungua ndege moja katika eneo linalomilikiwa na Israel na ndege nyingine ilipigwa japo haikuanguka – madai ambayo yanakataliwa na jeshi la Israel, likisema kwamba hakuna ndege iliyopigwa.

Israel ilifanya mashambulizi karibu na eneo la Palmyra kusaidia “Kundi la kigaidi la ISIS na katika jitihada ya kuinua morali ya kundi hilo na kutoa mawazo yake kwenye ushindi ambao jeshi la Syria limekuwa likipata dhidi ya kundi hilo,” taarifa ya jeshi la Syria kwa vyombo vya habari ilisema.

Mashambulizi mengi ya anga ambayo Israel imekuwa ikiyafanya katika eneo linalomilikiwa na Syria katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakilenga kuzuia silaha zinazopelekwa kwa kundi la Hezbollah, ambalo hupigana kwa kushirikiana na serikali ya Rais Bashar al-Assad dhidi ya makundi ya waasi.

Wakati Jeshi la Ulinzi la Israel halisemi lolote juu ya nia hasa ya operesheni zake, Hezbollah, kama ilivyo Iran, imeapa kuliharibu taifa hilo la Kijahudi.

Katika matamshi yasiyo ya kawaida juu ya operesheni hiyo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema, “Sera yetu haibadiliki. Tunapogundua juu ya jaribio la kupeleka silaha za kisasa kwa Hezbollah, na tunazo taarifa za kiitelijensia na uwezo wa kuzifanyia kazi, tunafanya hivyo. Hivyo ndivyo ilivyo.”

Kwa kiasi kikubwa Israel haijaathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, isipokuwa tu kwa kiasi kidogo cha mashambulizi kutoka upande wa Syria, ambayo imekuwa ikijibu.

Anga katika Syria zimejaa shughuli za kijeshi, huku ndege za Urusi na zile za Syria zimekuwa zikisaidia majeshi ya serikali kupambana na waasi, huku zile za Marekani zikifanya mashambulizi dhidi ya kundi la ISIS na al-Qaeda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *