- Bunge linapogeuka tingatinga la kubomoa mafao ya pamoja…
KATIKA makala yangu ya mwisho tuliona kwamba nyaraka rasmi za CCM zinaeleza kuwa utawala wa sheria ni utawala unaohakikisha kwamba haki zote za binadamu katika dola zimeingizwa katika zizi la sheria za bunge. Zizi hili huwa chini ya ulinzi wa majaji na mahakimu, na hivyo kuhakikisha kwamba watawala na watawaliwa wanaishi chini ya paa moja la nyumba ya sheria bila kuacha mianya yoyote ya udikteta.
Lakini siyo kila sheria itakayotungwa na bunge inafaa kwa sababu tu imetungwa na bunge. Kuna sheria bora na sheria mbaya. Kwa hiyo, swali lililo mbele yetu leo ni hili: Kwa kuziangalia sheria zinazotungwa na bunge, tunaweza kutumia mizani gani ili kutofautisha kati ya sheria bora na sheria mbaya?
Kwa mfano, ukiiangalia sheria kama vile sheria ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma ambayo inaelekeza asasi zote ambazo ni mafao ya pamoja katika taifa zibinafsishwe, unaweza kutumia mizani gani ili kujua kama ni sheria bora au sheria mbaya? Hili ndilo suala ninalopenda tulijadili leo.
Katika medani za kisiasa nchini kuna majibu tofauti kwa swali hili kulingana na mwegemeo wa mawazo (school of thought) wa mtoa jibu.
Katika kulijibu swali hilo, upembuzi wangu unalalia kwenye mwegemeo wa mawazo unaosisitiza kwamba uzito wa ubora wa sheria za dola yafaa upimwe kwa kutumia mizani ya sheria ya maadili asilia, mizani ambayo hutumia “mafao ya binadamu” kama mawe kwa ajili ya kupimia uzito wa ubora huo.
Tutayachunguza maudhui ya sheria hii kwa kuanzia na jawabu kwa swali lifuatalo: Mafao ya binadamu ni kitu cha aina gani? Ni rahisi kuelewa maana ya maneno “mafao ya binadamu” kama mtu tayari anaelewa maana ya “haki za binadamu”. Kwa hiyo tuanzie hapo.
Kama tulivyokwishakuona huko nyuma, ikiwa mtu aitwaye “A” anayo haki ya kudai kitu kiitwacho “B” kutoka kwa mtu aitwaye “C” ambapo ndugu “C” anao wajibu wa kutimiza madai kwa sababu ya maelezo ambayo hapa tuyaite “D”, basi ndugu “A” huitwa mdai, kitu “B” huitwa madai, ndugu “C” huitwa mdaiwa kwa maana ya mtu aliye na wajibu wa kutimiza madai, na maelezo “D” huitwa sababu inayoeleza uhalali wa madai haya, ambapo kitu kinachodaiwa huitwa “fao” la mdai tajwa, neno ambalo wingi wake ni “mafao”.
Kwa msingi huu, mali, uhuru, uhai, afya njema ni mafao ya binadamu. Kadhalika, maarifa, michezo, mazoezi ya viungo, amani, ibada, ndoa, familia, kazi, urembo na mengine yanayofanana na hayo, ni mafao ya binadamu.
Katika orodha hii baadhi ya mafao ni mafao binafsi. Mfano wa fao binafsi ni mali kama vile gari. Lakini mafao mengine ni mafao ya pamoja. Mfano wa fao la pamoja ni barabara ya lami tunakopitia sote kila siku iwe ni kwa miguu au baiskeli au gari.
Na utafiti mdogo utathibitisha kauli kwamba kila kitendo cha binadamu ni mkakati wa kufukuzia kitu fulani ambapo kitu kinachofukuziwa, kwa mtazamo wa mfukuzaji, ni mafao ya binadamu.
Yaani, hakuna mtu mwenye akili timamu atafukuzia kitu anachoona hakimfai. Hata mtu anayekunywa sumu kwa lengo la kujiua anakuwa ameona kwamba sumu hiyo na kifo kitakachotokana na sumu huyo ni mafao kwake!
Na baada ya kueleza maana ya “mafao ya binadamu” sasa tunaweza kutumia maarifa hayo kujibu swali hili hapa: Sheria ya maadili asilia ni kitu cha aina gani na inatuelekeza nini?
Kwa ufupi, sheria ya maadili asilia ni sheria ambayo hutumika kama mizani ya kupimia kilo za uzito wa uadilifu katika matendo ya binadamu kwa kutumia “mafao ya binadamu” kama mawe ya kupimia uzito huo katika mizani hiyo.
Katika mizani ya sheria ya maadili asilia, kitendo chochote chenye uzito unaobetua jiwe lolote la “mafao ya binadamu” huitwa kitendo kibaya kimaadili wakati kitendo chochote chenye uzito unaoheshimu “mafao ya binadamu” huitwa kitendo kizuri kimaadili.
Kwa mfano, kuvuruga ibada, kumwua mtu asiye na hatia, kuzini, kuiba, na kudanganya, ni matendo mabaya kimaadili, lakini siyo kwa sababu misahafu inayakataza. Misahafu inayakataza kwa sababu ni matendo mabaya kimaadili.
Na ubaya wake unatokana na ukweli kwamba ibada, uhai, uaminifu katika ndoa, mali inayomilikiwa kihalali, na ukweli, ni baadhi ya mafao ya binadamu. Kuhujumu mafao haya na mafao yanayofanana na haya ni makosa kwa mujibu wa mizani ya sheria ya maadili asilia.
Kwa ujumla, sheria ya maadili asilia inaelekeza kwamba katika matendo yote yanayofanywa kwa makusudi, kila binadamu anao wajibu wa kuchagua matendo mema na kuepuka matendo mabaya.
Na matendo mema ni matendo yote ambayo yanaheshimu seti nzima ya mafao ya binadamu na matendo mabaya ni matendo ambayo yanahujumu seti nzima ya mafao ya binadamu kwa namna moja au nyingine.
Hata hivyo, maelekezo haya hapo juu yanazalisha swali jingine muhimu. Na swali lenyewe ni hili: Kanuni za maadili asilia kama vile usiue, usizini, usiibe, na usidanganye husanifiwaje kwa kutumia sheria ya maadili asilia?
Jambo hili ni rahisi sana kuonyesha kwa kutumia mbinu za kawaida za usanifu wa hoja zenye kiima na kiarifa (premises and conclusions). Kwa kuanzia na sheria ya maadili asilia iliyotajwa hapo juu, mchujo wa kiakili utaonyesha kirahisi kwamba hoja ifuatayo ni sahihi:
Matendo yote yanayofanywa kwa makusudi na yakahujumu mafao ya binadamu, ni matendo mabaya kimaadili; Tunao wajibu wa kimaadili kuyaepuka matendo mabaya; Kitendo “X” ni kitendo kinachohujumu mafao ya binadamu yaitwayo “Y”; Hivyo tunao wajibu wa kimaadili kukiepuka kitendo “X”.
Katika mtiririko huo hapo juu, kazi inayokuwa imebaki ni kutafsiri kitendo husika (X) na kukihusianisha na mafao husika (Y). Tuchukue mfano wa kitendo cha kuiba ambacho uchanganuzi wake wa kimaadili utakuwa kama ifuatavyo:
Matendo yote yanayohujumu mafao ya binadamu ni matendo mabaya kimaadili; Tunao wajibu wa kimaadili kuyaepuka matendo mabaya; Kitendo cha “kuiba” ni kitendo kinachohujumu mafao ya binadamu yaitwayo “mali ya jirani”; Hivyo tunao wajibu wa kimaadili kukiepuka kitendo cha “kuiba”.
Na mantiki hii inaweza kutumiwa kwa kila kitendo cha binadamu kinachoweza kufikirika kuanzia kuua, kuzini, kudanganya, na kadhalika.
Maelezo yote mpaka hapa hayana tatizo kubwa. Lakini je, sheria za bunge, kama zile sheria zinazokataza utapeli, husanifiwaje kwa kutumia kanuni za maadili asilia kama vile kanuni inayokataza wizi?
Yaani, tukisha kujua kwamba kuna kanuni ya maadili asilia inayotukataza kuiba, tunawezaje kufahamu pia kwamba kanuni hii inatukataza kufanya utapeli na hivyo kutunga sheria bungeni inayokataza utapeli?
Swali hili nalo ni rahisi kujibiwa kwa kutumia mbinu zile zile za usanifu wa hoja zenye kiima na kiarifa, ambapo tunaweza kuonyesha jinsi wabunge wanavyotumia kanuni ya maadili asilia dhidi ya wizi kutunga sheria dhidi ya utapeli kama ifuatavyo:
Matendo yote yanayohujumu mafao ya binadamu ni matendo mabaya kimaadili; Tunao wajibu wa kimaadili kuyaepuka matendo mabaya; Kitendo cha “kuiba” ni kitendo kinachohujumu mafao ya binadamu yaitwayo “mali ya jirani”; Hivyo, tunao wajibu wa kimadili kukiepuka kitendo cha “kuiba”; Kitendo chochote cha kitapeli ni kitendo chenye mnasaba na kitendo cha kuiba; Hivyo, tunao wajibu wa kimadili kukiepuka kitendo chochote cha kitapeli.
Hivi ndivyo sheria zote za bunge zinavyotungwa kuanzia katika sheria ya maadili asilia, kupitia katika kanuni asilia za maadili ambazo zinaweza kujulikana kwa kila mtu, hadi kwenye kanuni maalum ambazo lazima zigunduliwe baada ya mchujo timamu wa kiakili, kama sentensi mbili za mwisho katika hoja hiyo hapo juu zinavyoonyesha.
Siyo kila mtu anaweza kuona kirahisi kwamba “kitendo chochote cha kitapeli ni kitendo chenye mnasaba na kitendo cha kuiba.” Na hii maana yake ni kwamba bungeni siyo mahali pa kupeleka waimba pambio au waimba taarabu au wacheza twisti. Kule wanahitajika watu wanaoweza kufanya michujo timamu ya kiakili, na hivyo kututungia sheria bora.
Baada ya kuyasema hayo yote sasa turejee kwenye swali muhimu la mwisho: Binadamu huwezaje kutambua kwamba anawajibika kufanya matendo mema na kuepuka matendo mabaya?
Jibu la haraka ni kwamba sheria ya maadili asilia ya binadamu “imeandikwa” katika kuta za ubongo wa kila binadamu. Jambo hili linathibitishwa na hubahisia (inclinations) alizo nazo kila binadamu tangu kuzaliwa.
Kutokana na hubahisia hizi, binadamu hutambua kwamba anao wajibu wa kuheshimu uhai; wajibu wa kujenga mahusiano ya kingono na binadamu mwenye jinsia ngeli tofauti na yeye; na wajibu wa kuupiga vita ujinga, kufanya ibada, na kufanya urafiki na majirani.
Yaani, uhai, watoto, maarifa, ibada, na urafiki ni baadhi ya mafao ya binadamu ambayo kila binadamu hujikuta akiyafukuzia kutokana na msukumo wa hubahisia alizo nazo mwilini mwake, lakini bila kufundishwa na yeyote.
Haya mafao ya binadamu huwa ni kituotamati (telos) au tuseme “telosia” ya mshale wa hubahisia ambao huchomoza kuanzia katika kitako cha akili ya kila binadamu. Matendo yote ya binadamu hujielekeza katika telosia hizi kwa sababu zina mvuto kwa binadamu.
Na chochote kinachokuvutia utakipenda, utakiheshimu na utakilinda. Hivyo ndivyo kanuni zote za maadili asilia kama vile usiue, usiibe, usizini, usidanganye, na zingine zinavyogunduliwa na binadamu!
Sheria za bunge zinazopingana na kanuni hizi za maadili asilia ni sheria uchwara, kwa sababu hubomoa hekalu la mafao ya pamoja katika taifa.
Ni maoni yangu kwamba, kutokana na yote yaliyojadiliwa katika kujibu maswali haya, changamoto moja imeibuka: Ni sifa gani anapaswa kuwa nazo mbunge wa Tanzania pale bungeni Dodoma ili hekalu la mafao ya pamoja katika taifa lisiendelee kubomolewa kwa msaada wa sheria za bunge? Sote tunawajibika kulijibu swali hili.
Inaendelea
Toa maoni yako