TUPENDE tusipende, kifo ndio ufumbuzi murua wa matatizo yote duniani. Hakuna binadamu – hakuna tatizo
Jaji Warioba: Wanaharakati wanageuza mawazo yao juu ya Katiba mpya yaonekane ni ya wananchi
WIKI iliyopita katika gazeti hili tulichapisha sehemu ya kwanza ya mahojiano kati ya Mwandishi Wetu na Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba. Ifuatayo ni sehemu ya pili na ya mwisho ya mahojiano hayo kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa nchini.
Raia Mwema: Unachotaka kusema hapa ni kwamba nchi inapita katika kipindi kigumu kwa maana ya uchumi na siasa; lakini badala ya kukabili hali hiyo, hakuna kinachofanyika, kilichopo ni malumbano na mbio za kutafuta madaraka?
Jaji Warioba: Ndiyo. Tunachokiona sasa ni mbio za madaraka. Kwenye vyama sasa cha muhimu ni madaraka. Itikadi si muhimu, sera si muhimu, na ilani si muhimu. Hatuko pamoja. Tukizungumza kama nchi tunazungumza madaraka na tukizungumza kama vyama vya siasa tunazungumza madaraka.
Tuliamua wenyewe kuwa na demokrasia kwa maana ya vyama vingi. Huwezi kuwa unasema unaendesha demokrasia wakati ndani ya vyama vya siasa kwenyewe hakuna demokrasia. Ninavyoangalia, kama hatukushughulikia mambo haya vyema, kuja kufika mwaka 2015, tutakuwa na matatizo makubwa.
Raia Mwema: Zama hizi zina mifano ya nchi ambazo zinaunda ubia wa haraka haraka kati ya vyama vya siasa ambavyo havina cha kufanana kwa maana ya itikadi wala sera, ali mradi, vina nafasi ya kuunda serikali na kuchukua madaraka, hili linawezekana pia hapa?
Jaji Warioba: Zipo nchi nyingine kwa hamu hii ya kutaka madaraka, vyama vya siasa vyenye itikadi na sera tofauti kabisa huwa vinaunda kitu kinaitwa coalition.
Hiyo ni ili mradi tu watu wapate madaraka. Kama hatutabadilika, naiona hiyo ikitokea hapa. Kwa sababu hao wanakubaliana na wanasukumwa na jambo moja tu: madaraka.
Sasa katika mazingira haya, ambamo hali ya uchumi inaleta wasiwasi na hali ya siasa si nzuri, ukifikiria kwamba mwaka huu tunanza mchakato wa kuandaa katiba mpya, kazi hiyo haitakuwa rahisi katika mazingira haya. Ukiwa katika mazingira ya hali ngumu ya uchumi, yenye vurugu katika siasa, kuandaa katiba mpya, kunahitaji umakini wa hali ya juu kabisa.
Tumekubaliana kwamba tutakuwa na katiba mpya. Hili halinipi wasiwasi. Na tunakuwa na katiba mpya sasa hivi, kwa sababu ya utaratibu wa kutunga katiba. Mwaka 1962 tulipata katiba mpya kwa kubadili utaratibu tu. Bunge lile likajigeuza likawa Bunge la Katiba. Likapitisha Katiba ile ikawa ni Katiba ya Tanganyika wakati ule.
Ukiitazama ile Katiba, ukalinganisha na ile tuliyopatia Uhuru, utakuta sehemu nyingi zilibaki. Tulibadili katika sehemu ya utawala tu. Lakini mambo yale ya msingi yalibaki vilevile. Tukaendelea, tukawa tunaibadili Katiba kila mahitaji yalipojitokeza.
Wakati wa Muungano tukawa na Katiba ya muda, ikawa inafanyiwa mabadiliko, na yalifanyika mabadiliko mengi tu. Kwa sababu ni kawaida, kwa sheria yoyote, hata hii ya msingi, kufanyiwa mabadiliko.
Ilipofika mwaka 1977, hapo tukasema sasa tunahitaji katiba ya kudumu. Tuondokane na ile ya muda. Ikatengenezwa. Yalikuja mabadiliko makubwa tu, lakini pia kuna mambo ya msingi yalibaki, mengi tu, yaliyokuwa yemeanzia katika katiba zilizopita.
Mwaka 1984 tulifanya mabadiliko makubwa tu. Tukaweka muda wa ukomo wa urais, tukaingiza haki za binadamu, na haya yalikuwa ni mabadiliko makubwa tu, na tukapunguza kwa kiwango, madaraka ya rais.
Sasa tunakwenda kwenye Katiba mpya. Itakuwa ni Katiba mpya kwa maana kwamba tumebadili utaratibu. Nataraji yatakuja mabadiliko makubwa, lakini nataraji pia kwamba kuna mambo ya msingi yatabaki.
Kuna ambao wanafikiri kwamba katiba mpya itakuwa ni tafauti kabisa, kwamba itakuwa mpya kabisa. Vitu vipya kabisa. Hapana. Nadhani tutaendelea na utaratibu huu huu, kwamba kuna mihimili mitatu, sidhani kama kuna watu wanasema tuondoe mihimili ya sasa tuweke mingine.
Utakuwa na Serikali, Bunge na Mahakama. Utakuwa na Serikali za Mitaa, inawezekana tukaangalia kwamba tupeleke madaraka zaidi kwenye Serikali za Mitaa.
Tutaangalia kwenye mihimili hii mabadiliko yafanyike wapi, kama ni kwenye Serikali tutaangalia madaraka ya rais, wengine wanasema ni makubwa mno, labda tuyapunguze, na ukishakuyapunguza unayapeleka wapi kwenye mihimili mingine.
Tutaangalia Bunge, liwe la aina gani? Na tutaangalia aina za wabunge, ziwe ni zipi? Sasa tuna wabunge aina nyingi; wa kuchaguliwa, wa viti maalumu, wa kuteuliwa. Sijui kama tutabaki na hao hao au tutabadili, na wapatikanaje? Je, ni kwa kura hizi za kawaida zinazopigwa au tutawapata kwa uwiano?
Tume ya uchaguzi itakuwaje, ni kweli tutafanya mabadiliko, lakini ukweli pia ni kwamba vyombo hivi vitakuwa bado vipo. Inawezekana namna ya kufanya kazi zao ndiyo ikabadilika lakini madaraka yao yakabaki yale yale.
Itakuwa ni hivyo kwa Mahakama pia. Tunaweza kuangalia, je, Mahakama zetu zina uhuru wa kutosha? Tunahitaji kuziongezea uhuru? Kwa hiyo watu wasifikiri kuwa kila kitu kitakuja kipya. Hapana.
Raia Mwema: Tayari kuna lugha zinagongana, miongoni mwa vyama, wasomi na wanaharakati kuhusu Katiba hii. Katika hali hii hatuwezi kuishia kwenye Katiba ya maslahi ya makundi haya?
Jaji Warioba: Kwangu haya yote si muhimu sana. Cha muhimu ni namna ambavyo tutaendesha mchakato huu. Kwanza kumekuwa na mabishano ya muda mrefu tu ya sheria yenyewe ya kuanzisha mchakato. Nadhani mabishano haya yamekula muda wetu bila sababu. Hata hivyo, tutegemee kwamba sasa hilo limefika mwisho wake.
Sheria imepita, kulikuwa na makubaliano, wamezungumza, kwa hiyo, pengine wakienda tena bungeni wanaweza kufanya mabadiliko ambayo yataridhisha kila mtu ili tuanze mchakato.
Sasa katika mchakato, nadhani jukumu kubwa liko kwa viongozi, wasomi na wanaharakati. Hawa wakubali kwamba Katiba ni ya wananchi. Si ya makundi yao. Lakini dalili ninazoziona ni kama kila kikundi kinataka aina yake ya Katiba.
Kwamba wao wanaona hii ndiyo nzuri. Mimi nasema twende kwa wananchi. Tusiende na mawazo yetu, tukawashawishi wakubali mawazo yetu. Hapana. Twende kwa wananchi tuwasikilize. Tukiwasikiliza tutaelewa wanachotaka ni nini.
Na kubwa kwao ni mategemeo yao ya Tanzania wanayoitaka. Hili ndilo kubwa. Maana hapa tunabishana kwa mambo ambayo mimi naona kwamba tunaweza kukubaliana kwa urahisi kabisa. Mimi sioni kama kutakuwa na tatizo katika kukubaliana juu ya madaraka ya Serikali, madaraka ya rais, madaraka ya Bunge na madaraka ya Mahakama. Haya tunaweza kukubaliana.
Kubwa liwe ni katika hiyo Katiba tunayoitaka ya miaka 50 ijayo, je, tunataka Tanzania ya aina gani? Na umuhimu wake ni kwamba Katiba tuliyonayo sasa wananchi walikuwa wameshawishiwa wakijua Tanzania wanayoitaka ni ipi.
Msingi wa Katiba hii ya sasa, ulikuwa ni itikadi ya TANU, Afro na CCM. Sasa tumeingia kwenye vyama vingi vya siasa, sasa itikadi haiwezi tena kuwa msingi wa katiba, lazima tutafute muafaka wa kitaifa. Watu wanafikiri ukiwa na vipengele hivi, umeingiza madaraka, umeingiza mambo ya msingi, kwamba katiba hiyo sasa tayari.
Ukitazama Katiba ya sasa imetungwa juu ya misingi na inasema kwamba misingi mikubwa ambayo imewekwa katika Katiba hii, inasema: Sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Hii ndiyo misingi ya Katiba hii. Hapa unaweza pia kuongeza umoja.
Lakini inasema pia katika kujenga jamii hiyo lazima Serikali izingatie misingi ifuatayo: demokrasia, ujamaa na kutofungamana na dini yoyote. Hiyo ndiyo misingi, na hiyo ilitokana na itikadi ya TANU, Afro na CCM. Kwa hiyo kutekeleza Katiba hii kulifuata itikadi hiyo. Unaweza kuwa na vipengele vizuri sana, lakini watendaji wasipokuwa na maadili vipengele hivyo havina maana.
Kwa sababu ya itikadi hiyo ya TANU, Afro na CCM, wananchi walisema Tanzania wanayoitaka ni ya Ujamaa na Kujitegemea. Na mpaka leo, wengi wanafikiri ndiyo Tanzania wanayoitaka wakati mambo yamebadilika. Ujamaa haupo. Tunaweza kuwa na chama hapa kikaingia madarakani hata kama kinapingana na ujamaa. Lakini lazima kuwapo na misingi ya kitaifa ambayo ndiyo inayoongoza itikadi hizo.
Maadili, kwa mfano, yalitokana na itikadi ya TANU, Afro na CCM. Chukua Azimio la Arusha. Hili halikuwa sheria. Lakini lilisema kwamba kwa kuwa tumeamua kujenga Tanzania ya Ujamaa na Kujitegemea, na kuwa tunataka kuleta maendeleo ya nchi yetu kwa misingi hii, dira iliwekwa kwa mwelekeo kwamba ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Mimi kwangu bado haya ni ya msingi. Huwezi kuendelea bila haya. Ardhi tunayo na bado inatosha, watu tunao na wameongezeka. Matatizo yanakuja kwenye siasa safi na uongozi bora. Lakini hata katika uongozi bora tulikwishakusema kwamba tukitaka tusipate matatizo, tupige vita ujinga, umasikini na maradhi. Na haya bado yapo.
Ili tufaye hivyo, tukasema viongozi wote lazima wajue kwamba Tanzania tunayoitaka ni ya Ujamaa na Kujitegemea. Na kwa kuwa tuna ardhi, tuna watu, tunahitaji siasa safi na uongozi bora.
Wakatengeneza siasa, wakasema siasa ni Ujamaa na Kujitegemea. Uongozi bora wakauwekea masharti. Waliweza kumpima kiongozi yeyote kwa masharti yale. Walisema ukiwa kiongozi, usiwe na nyumba ya kupangisha, usiwe mjumbe wa bodi, usipokee mishahara miwili. Watu wa kawaida wanajua, wakiona mtu anafanya hayo, wanajua huyo si kiongozi.
Yale maadili hayakuwa sheria. Sheria imekuja kutungwa miaka ya 1990 wakati wa kuingia tena kwenye mfumo wa vyama vingi. Lakini hata pamoja na sheria hiyo, si rahisi wananchi kumpima kiongozi wao, maana mpaka ataje mali zake na huko anakotaja si rahisi wananchi kufika.
Kwa hiyo, katika Katiba inayokuja haya yatakuwa ya msingi. Tujue tunataka Tanzania ya aina gani. Na kwa maana hiyo, yeyote anayeingia kwenye uongozi ajue kuna miiko ya uongozi inayojulikana kwa wananchi. Hili litakuwa kubwa sijui litawekwa vipi kwenye Katiba.
Ili kupata maoni ya wananchi, italazimu kuwafuata wazungumze yanayowahusu. Ninachosema, ni kwamba sisi viongozi, wasomi na wanaharakati, tusije tukawapotosha wananchi.
Kuna arrogance (kiburi cha kujiona msomi, mkubwa) nchini, cha viongozi, cha wanaharakati na wanataaluma, ambao wanaona kwamba wananchi hawajui chochote. Eti ni lazima wananchi waelemishwe. Tena siku hizi eti kuna misamiati kama wananchi wangu, wapiga kura wangu. Hiki ni arrogance ambayo haitatufikisha kokote. Wananchi wanajua wanachotaka.
Tumezungumza hapa, kama ni matatizo kwenye kilimo, hakuna anayeweza kukueleza matatizo hayo vyema kama mkulima; hakuna anayeweza kukueleza matatizo ya kazi kama mfanyakazi. Na hali ni hiyo kwa mvuvi au mfugaji. Hawa wanajua. Tuwasikilize. Wanataka kilimo chao kiweje, ajira yao iweje, uvuvi wao uweje na ufugaji wao uweje. Baada ya hayo ndipo unaweza kujua Watanzania wanataka nini. Wanataka ardhi yao itumike vipi.
Kwangu mimi ile sehemu ya kwanza inayohusu misingi ndiyo iliyo kubwa. Huko ndiko tulikoanzia kama Taifa, tukaendeshwa na itikadi ambayo sasa haipo.
Pamoja na kwamba tuliongeza haki za binadamu humo, bado inalazimu kujenga taifa kwa msingi ambao wote tutaufuata. Na katika hilo tuwasikilize wananchi. Nashangaa kwamba sasa kila mtu amekuwa mwanaharakati. Anataka kwenda kumuelimisha mwananchi. Na nasikia kuna watu wanazunguka huko tayari. Wanachofanya ni kupeleka mawazo yao kule, yaonekane ni ya wananchi. Mkifanya hivyo mtakuwa na Katiba ambayo haitadumu kwa sababu itakuwa haikubeba msingi wa mawazo ya wananchi. Tusidharau wananchi.
Ukichukua tume zote za huko nyuma: ya Nyalali (Jaji Francis), Kissanga (Jaji Robert), ya Shivji (Profesa Issa), na Shivji alikwenda kwa wananchi kuhusu ardhi. Mawazo aliyapata kwa wananchi. Lakini linapokuja hili la katiba eti wanasema wananchi lazima waelimishwe. Mimi kiburi hiki kinanitisha.
Hata hivyo, hawa wanaosema wanataka kwenda kuwaelimisha wananchi hawanitishi. Nataraji tume itakayoundwa itaweka utaratibu ambao utawapa nafasi wananchi kuzungumza wanachokitaka, si walichopelekewa na wanaharakati. Tikapata mawazo ya wananchi tutatunga katiba itakayoweza kudumu. Wakati mwingine nawaza kwamba hata tusingehitaji tume kwa haya mengine.
Kama kweli tunaamua, tunaweza kuangalia madaraka ya rais, madaraka ya serikali au bunge liweje, tukakaa chini tukafanya. Lakini la msingi, hapa tupo katika mpito kutoka wananchi walikokuwa wanajua wanaelekea wapi, hiyo imebadilika, na hawaoni uongozi kama ule uliokuwa unawapeleka huko. Haupo.
Raia Mwema: Lakini watu wanasema kama Kenya wameweza, sisi tunashindwaje kuwa na katiba inayolinda maslahi ya wote?
Jaji Warioba: Nimesikia mifano. Wanazungumzia Kenya ilivyofanya. Ni kweli Kenya wamejitahidi. Lakini tusije tukachukua mfano wa Kenya. Walitaka Katiba ya kulinda haki za kila mtu na itakayoleta maendeleo. Wakaweka mambo mengi mle. Sasa hata kabla hawajaanza kuitekeleza sawasawa, tayari wapo wanaotaka mabadiliko.
Hawa wa hapa kwetu nao wanataka haya. Kila mtu anataka cha kwake kiingie. Katiba ni msingi. Haiwezi kubeba utashi wa kila mtu. Mkishaweka haya ya msingi, yakajulikana, haya mengine mnaweza kuyatungia sheria nyingine.
Zaidi ya hayo, napata wasiwasi, tunaingia mwaka 2012, tuna mchakato wa Katiba, lakini hali yetu ya uchumi inahitaji muda wetu mwingi na tafakuri yetu. Siasa nayo haionyeshi mwelekeo mzuri. Mwito wangu kwa wote ambao sasa ni kama wataalamu wa Katiba, ni kwamba kama tunataka katiba ya kweli, tuache wananchi watoe maoni yao.
Tusiende tukifikiri kwamba kila mmoja peke yake ndiye ana muarobaini wa suala hili. Maana madaraka haya, wakati mwingine, msuguano ulioko ni kama walioko katika madaraka hawakutaka mabadiliko, au kama ni mabadiliko basi madogo hivi.
Wale wanaotaka mabadiliko, si kwa msingi wa mabadiliko, bali kwa kutaka kuondoa hao walioko madarakani. Tusiende kwenye mabadiliko kwa kutafuta kubadili utawala, twende kwa kutafuta katiba itakayotuvusha miaka 50 ijayo.
Comments
ndugu mwandishi kuna makala
ndugu mwandishi kuna makala/interview yako kaatika toleo moja lililopita MZEE WARIOBA ALIDAI "SERIKALI 3 NI KUVUNJA MUUNGANO"
Kwa kweli nimesikitishwa sana na huyo mzee ambae mumekuwa mukimuona kuwa mzee wa busara. Sasa kama kweli anapenda demokrasia kwanini ALAZIMISHE WATU MFUMO ANAOUTAKA WA MUUNGANO?
Maana ya katiba mpya ni kuwapa wananchi uhuru wa kupata katiba waitakao na yeye amejidai hapo kuwa wanaharakati wawaache wananchi waseme wayatakayo, je huo si unafiki ndugu mwandishi?
Kwa kweli inabidi viongozi wasome alama za wakati, wazanzibar kwa sasa wameelimika na wameungana wakati wa kudanganywa umeisha/umepita.
Kama Warioba na wenzake wanataka serikali basi watoe maoni yao na wasiwalazimishe wengine wakubali mfumo ambao umekuwa ukiwanyonya miaka nenda miaka rudi na kuwarejesha nyuma kimaendeleo.
kama hamutaki serikali 3 basi wazanzibar wanajiandaa kuukataa muungano wa CHUMA ULETE.
NDUGU MWANDISHI NAOMBA UNIFIKISHIE UJUMBE HUU KWA WARIOBA.
Mzee WARIOBA tumechoka mfumo
Mzee WARIOBA tumechoka mfumo huu wa MUUNGANO wa serikali mbili kutokana na KUTUNYONYA na KUTUPOKONYA MAMLAKA NA RASILI MALI ZETU. Tuache tuamue hatma yetu. (wakati ni ukuta)
Bw JAJI WARIOBA wazanzibar
Bw JAJI WARIOBA wazanzibar tumechoshwa na muungano wa serikali mbili wenye lengo la KUZINYEMELEA RASILIMALI ZETU YAKIWEMO MAFUTA, Wakati wa nyeupe kuita nyeusi umepita, hiki ni kizazi kipya cha wazanzibar. (ZANZIBAR BILA TANGANYIKA INAWEZEKANA)
Mpendwa Zanzibar bila
Mpendwa Zanzibar bila Tanganyika haiwezekani! Huo ndio ukweli amini usiamini. Je visiwa vya Commoro vina uwezo kulika Tanzania? Ni lazima ujue kwamba Zanzibar ni kisiwa na watu wanapoongezeka nchi haiongezeki. Leo hii wako wapemba wengi sana Tanganyika. Wanafanya biashara zao bila wasiwasi wowote ni kwa sababu ya uimara wa Muungano. Wapo wengine wamekuwka wafugaji wakubwa kule Shinyanga na wanafanya hivyo kwa ajili ya uimara wa Muungano. Ikiwa mtajitenga na kuwa na Zanzibar yenu watanganyika watataka Wapemba wote warudi kwao. Na huko Zanzibar hakutakuwa na ardhi ya kuwatosha. Mtaenda wapi kuishi? Uwe mkweli ndugu kwa kuwaza kwa upana zaidi. Kwa kuwa Tanganyika ina ardhi kubwa watanzania wote tunafaidi hata sisi tunaotoka Zanzibar. Tena Zanzibar tuna matabaka mengi sana kuliko Tanganyika waarabu na watu weusi kwa kuzingatia Uunguja wangu na Upemba wako tutapambambana kugombea ardhi ndogo tuliyo nayo. Letu ni moja leo kwa kuwa tupo na watanganyika. Lakini watanganyika wakitoka hatutakuwa wamoja tena tutakuwa Waunguja na wapemba. Muungano pia umewasaidia wapemba wengi ambao ni wafanyabiashara kuwa na soko kubwa Tanganyika. Ndugu usiende kwa itikadi mbaya ya kutaka kuuvunja Muungano. Wewe unasema umeelimika aliyeelimika hana mawazo finyu kama ya kwako. Unatakiwa uwaze kwa upana zaidi mpendwa!
Add new comment