MIEZI michache iliyopita nilikutana jijini Nairobi na waziri mmoja wa zamani aliyetumika kwa muda mrefu katika serikali za Mwalimu Julius Nyerere na waliomfuatia. Siku hizi anajituma mwenyewe na hali yake alhamdulillahi si mbaya. Kwa hakika, mwanaharakati huyo wa zamani wa TANU ameinuka sana katika maisha kwa bidii yake ya kazi.
Nilimpongeza kwa hilo, kisha nikamwambia nilikuwa na swali la kumuuliza: “Akitokea ghafla Mwalimu na akayaona unayoyafanya unadhani atakwambia nini?”
“Duh,” alijibu. Halafu akacheka na kusema; “Swali zuri,” akacheka tena. Niliona kama nilimweka pabaya; mara akayazoazoa mawazo yake na kuniambia “lakini Mwalimu mwishowe alitambua kwamba sera zake (za kiuchumi) hazikufanikiwa.”
Mheshimiwa huyu ni miongoni mwa wale waliokuwa wakiaminiwa na Mwalimu kwa msimamo wao wa kiitikadi.
Wakati wa enzi ya Nyerere viongozi wa sampuli hiyo wakipigiwa mfano kuwa ni viongozi ‘waso ila, waso waa.’ Walionekana kuwa wajamaa waliokamilika. Ujamaa wao uliandamana na hisia za kizalendo na za uongozi wenye maadili.
Nilikutana na mheshimiwa huyo kwenye mkutano uliokuwa ukilijadili suala nyeti la wageni kumiliki ardhi, hasa za kilimo, barani Afrika. Siku hizi anamiliki kampuni yenye kuwavutia wawekezaji wa kigeni kuja Afrika kununua maelfu ya maekari ya ardhi kwa ajili ya kilimo, kilimo ambacho mazao yake aghalabu hupelekwa nchi watokazo hao wawekezaji.
Aliongea kwa fasaha mkutanoni akieleza jinsi kampuni yake inavyowaalika hao wawekezaji wa nje. Sitomtaja jina kwa sababu nikimnyoshea yeye kidole inaweza kuonekana kama ninamuonea. Kwanza, kwa vile sina ushahidi ya kuwa amekiuka sheria au ikiwa amepata mali yake kwa njia za haramu. Pili, kwa sababu kuna waheshimiwa wengi wengine wanaostahiki hasa kunyoshewa vidole kwa vile wanajulikana kuwa wamejipatia mali ama kwa kukiuka sheria au kwa kuzipinda sheria ili zihalalishe wizi wao wa mali za umma.
Kwa vile hakuna takwimu kamili na za kuaminika kuhusu viwango vya rushwa na ufisadi nchini hakuna ajuaye kwa uhakika kiwango halisi cha gharama ambayo Tanzania inalazimika kulipa kutokana na vitendo hivyo vya ufisadi na vya ulaji rushwa kwa jumla. Tunaweza kukisia tu kwamba kila mwaka mabilioni ya shilingi yanatoka kwenye mfuko wa hazina ya Serikali na kuingia kwa magendo katika mifuko binafsi ya mafisadi. Zote hizo ni fedha za umma.
Isitoshe kuna mzigo mwingine ambao wananchi wanabidi waubebe ili mambo yao yawaendee, ili kwa mfano waweze kupata huduma ambazo ni haki yao kuzipata bila ya kumlishia yoyote. Lakini kwa uoza wa mfumo uliopo hawawezi kuzipata bila ya kulishia.
Ndio maana ikawa rahisi kuzitambua zile wizara na idara zenye mlo, yaani taasisi ambazo wenye dhamana nazo wanatumia madaraka yao kujinufaisha. Hilo si geni na lilikuwako hata wakati Nyerere alipokuwa madarakani. Lakini kuna kuzidiana.
Wakati wa Nyerere lishialishia ilikuwa zaidi katika ngazi za chini za uongozi na viwango vya rushwa havikuwa vikubwa hivyo. Vigogo havikuweza kujiingiza kadamnasi katika vitendo vya ufisadi. Vikimwogopa Nyerere. Havikuthubutu kumchezea.
Nyerere alikuwa mkali na alipitisha sheria ya mtu yoyote aliyepatikana na hatia ya kula au kulisha rushwa afungwe na halafu atandikwe viboko 24. “Viboko 12 apigwe akiingia gerezani na 12 akitoka, akamuonyeshe mkewe,” alisema Nyerere.
Pengine hiyo ilikuwa hukumu ya kimabavu lakini hukumu kama hiyo inaashiria ujasiri wa kiongozi na Serikali yake kupambana na rushwa. Daima ujasiri katika uongozi wa nchi huwa unaanzia juu. Pindi kiongozi akishindwa kuwa na ujasiri mapambano kama hayo hayawezi kufanikiwa. Tabasamu za jukwaani wakati wa kuzungumzia masuala mazito ya ufisadi huchukuliwa na wanamtandao wa rushwa kuwa ni mzaha au kwa lugha ya kileo usanii tu.
Nchini Tanzania inaonyesha kwamba mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa jumla yanaelekea kugonga mwamba. Raia wangali wanajiuliza lini ahadi zinazotolewa na wenye kuiendesha nchi zitatimizwa?
Rushwa, kwa kweli, ilianza kutanda kwa mapana na marefu katika awamu ya pili. Pale Rais Ali Hassan Mwinyi ‘alipoufungua’ uchumi, wahujumu uchumi waliutafsiri vibaya msemo wake wa ‘rukhsa’ na kuufanya uwe ruhusa ya kukiuka uadilifu. Rushwa ikashamiri na ufisadi ukaota mizizi.
Hali ilikuwa mbaya kiasi cha kumfanya Nyerere asiweze kuivumilia na akaona kheri aukosoe utawala wa mrithi wake bila ya kificho kwa kushindwa kupambana na rushwa. Akafika hadi ya kumpiga Mwinyi vijembe hadharani. Wafadhili nao walipoona mambo yanazidi kwenda kombo wakazuia kutoa misaada mwezi Novemba mwaka 1994. Ingawa kuna wakubwa waliojitajirisha wakati wa utawala wa Mwinyi, yeye mwenyewe hakuwa na dosari hilo.
Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa ndiyo iliyofurutu ada. Hilo lilikuwa jambo la kushangaza kwa sababu alipoanza kuushika usukani wa taifa Mkapa aliwapa wengi matumaini. Alimteua Waziri Mkuu (mstaafu), Joseph Warioba aongoze tume ya kutathmini hali ya rushwa nchini na sababu zake.
Tume hiyo, iliyoanza kazi Januari 26 mwaka 1996 hadi Aprili 24 mwaka huo huo, ilitoa mapendekezo yaliyozigusa sekta zote zenye mizizi ya rushwa.
La ajabu ni kwamba mengi ya mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo hayakufanyiwa kazi na mengine hayakufanyiwa kazi vya kutosha. La kusikitisha ni kwamba wakubwa hawakuguswa. Badala yake vigogo wengi walimaliza muda wakichukuwa chao mapema.
Mali nyingi za Serikali, kuanzia majumba, mashirika ya umma mpaka migodi ikauzwa kwa bei za kutupwa na wanunuzi walikuwa baadhi ya wakubwa akiwemo Rais mwenyewe. Asiyewahi kupata chake alionekana kuwa alizubaa au kama wasemavyo mitaani, bwege.
Ikaingia Awamu ya Nne kwa kishindo kikubwa lakini katika kupambana na rushwa na ufisadi kishindo hicho kilikuwa cha kelele tupu. Kashfa za ufisadi zenye kuwagusa wakubwa zilizidi kuibuka na ilikuwa taabu kuzificha au kuzigubika.
Mapambano dhidi ya rushwa bado yanaelekea kugonga mwamba. Kiroja cha mambo ni kwamba wakuu wa awamu hii nao mpaka sasa wanauimba wimbo ule ule wa awamu iliyotangulia.
Kwa mwendo huu inaelekea kwamba hali itaendelea kuwa vivi hivi mpaka atapopatikana Sokoine wa pili, kiongozi atayefanana na Marehemu Edward Moringe Sokoine kwa nia, ujasiri, vitendo na uadilifu.
Kiongozi wa aina hiyo ni yule ambaye ukimuangalia utajua kweli huyu ana uchungu na taifa lake na watu wake. Kiongozi wa aina hiyo atasaidiwa na sheria na uhuru wa Mahakama katika mfumo wa utawala bora utaohakikisha kwamba wananchi wote ni sawa mbele ya sheria. Hivi sasa vyombo vya sheria haviaminiki kwa vile vinaonekana kwamba navyo vimeambukizwa ugonjwa wa rushwa.
Tukumbuke kwamba changamoto kubwa kwa kiongozi ni kuinua hali za maisha ya watu na katika nchi kama za kwetu hilo haliwezekani bila ya kuishinda rushwa. Jitihada za kuupunguza ufukara katika jamii hazitoweza kamwe kufaulu endapo rushwa inaachiwa iendelee kustawi.
Wala hakuna Serikali itayoweza kuchukua hatua za maana za kuweza kunyanyua hali za wananchi endapo Serikali hiyo inafanya kazi zake katika mazingira yanayovumilia na kupalilia ufisadi. Ni jambo la kuhuzunisha kuona kwamba siku hizi serikalini kunaonekana kuwa ni mahala pa kujitajirisha.
Huna haja ya kutazama mbali. Linganisha tu maisha ya mtu aliyekuwa waziri kwa muda wa miaka mitano na ya mfanyakazi wa Serikali aliyelitumikia taifa kwa miaka 25. Bado kuna wanaoumia na wenye machungu na hali ya rushwa akiwemo Warioba, lakini kilio chao bado hakijapata wa kukisikiliza.
Hivi sasa Zanzibar kuna matumaini ya kuanza kuchukuliwa hatua za kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kwa jumla. Tayari Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekwishaandaa Muswada wa Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar.
Muswada huo umefikishwa kwenye kikao cha sasa cha Baraza la Wawakilishi na unafafanua hatua kadha wa kadha zitazochukuliwa kupambana na wenye kuhusika na rushwa pamoja na wenye kuhujumu uchumi na mafisadi wengine wa kisiasa.
Mafanikio hayo lakini sina budi kusema yatategemea ari na uadilifu. La sivyo itakuwa ni kazi bure. Itakuwa ni kuigiza tume na juhudi nyingine zilizochukuliwa Bara ambazo ziliishia kuwa butu bila ya makali yoyote.
Maoni ya Wasomaji
mh ufisadi tanzania hauwezi
mh ufisadi tanzania hauwezi kuondoka kwa vile ni sehemu ya mfumo (system) kwa hiyo hata huyo bwana mkubwa kutokana na mfumo na yeye hawezi kutoka ama kwa kufanya ufisadi au kuwavumilia mafisadi.
Rudia kauli ya lowasa NEC CCM Dodoma, alisema hata wewe rais unajua kuwa mkataba wa richmond nilitaka kuuvunja lakini ukaniambia kuwa nisubiri nisikilize ushauri wa makatibu wakuu. kwa hiyo hapa inaonesha wote wamo.
kwa Zanzibar nako pia mfumo ni huo huo wa CCM kwa hiyo hali bado itakua hivyo labda BARAZA LA WAWAKILISHI lisiwe lelemama kama juzi lilivyotishia kuipigia serikali kura ya kutokua na iman (NO CONFIDENCE VOTE) kuhusu Tanganyika kuongeza eneo la bahari kiujanjaujanja kama walivyozoea.
Mimi ni Mzanzibar ninaependa serikali tatu, na kama watanganyika wakikataa basi nategemea mjadala ujao wazanzibar tunaweza hata kuuvunja muungano kwa vile sasa tuna umoja na pia tumefahamu athari za muungano.
Tatizo sugu la rushwa ni
Tatizo sugu la rushwa ni kubwa mno na haliwezi kumalizwa kwa siasa hizi za ahadi hewa na kuwakumbatia viongozi wabovu na wasiojali kabisa wananchi wa Tanzania.
Muswada wa kutenganisha biashara na siasa mpaka leo ni kitendawili na haujapelekwa hata Bungeni kulikoni wanaogopa nini au tusubiri Katiba Mpya ndio tuweke kipengele hicho kwamba ni marufuku kiongozi wa umma kutumikia wananchi na halafu kufanya shughuli nyingine za kibiashara mbali na siasa !
Acheni Mwalimu Nyerere aitwe Mwalimu hakuna kama yeye enzi hizi na kama yupo ajitokeza hadharani na kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi na kiuchumi.
Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika !!
Zumbe,Dar es salaam,Tanzania.