Je, Magufuli ataweza kutawala kwa ujasiri bila kuitwa dikteta? (3)

“Taratibu za uhuru wa mtu kutoa maoni juu ya mabadiliko ama ya sheria iliyopo au ya Katiba au juu ya uendeshaji na usimamizi wa serikali wakati anafuata sheria zilizopo lazima ziruhusiwe katika mfumo wowote unaoitwa wa kidemokrasia.

“Kwa kweli sifa moja ya demokrasia ya kweli ni kwamba inawapa wachache nafasi ya kisheria ya kujaribu kuwashawishi (wale) wengi waone ubora wa maoni yao.

“Ni demokrasia gani hiyo inayozuia wananchi kuihoji (Serikali) na Katiba yake, au sheria nyingine yoyote ya nchi na utawala?.  Demokrasia ikichukua sura ya udikteta, udikteta wenyewe utakuwa na sura gani?”  (Mwalimu Julius K. Nyerere).

KATIKA sehemu ya kwanza na ya pili ya makala haya, tuliona chimbuko na jinsi itikadi ya kiharakati ya maendeleo, kwa maana ya ajenda ya maendeleo kwa shuruti na juu ya vitu vingine vyote, ilivyochukua kiti cha mbele katika maisha ya wananchi kwa gharama ya uhuru wa raia, haki za binadamu na haki za mtu mmojammoja na za kivikundi kwa kauli mbiu ya “Maendeleo” tangu na baada ya uhuru.

Tuliona jinsi viongozi walivyotifua na kutibua demokrasia ya kweli kwa nguvu turufu ya kauli mbiu zao, kuanzia na Mwalimu Nyerere (1961 – 1985) kwa kauli mbiu ya “Uhuru na Kazi”, kisha “Uhuru ni Kazi”, Marais Ali Hassan Mwinyi (1985 – 1995); Benjamin William Mkapa (1995 – 2005) na Jakaya Mrisho Kikwete (2005 – 2015) ambao, japo waliingia na misemo yao ya kuongoza nchi kama vile, “Kila Kitabu na Zama Zake”, “Uwazi na Ukweli” na “Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya” (ANGUKA), kwa mfululizo huo; misemo ambayo, kwa maoni yangu haikuwakilisha kauli mbiu za maendeleo ya uchumi kwa maana halisi ya “ideology of developmentalism”, bali vilikuwa vibwagizo tu vya kutambulisha “awamu” za utawala wao, kila mmoja kwa mwondoko wa mdundo wa ngoma yake.

Tuliona pia kuingia kwa utawala wa awamu ya tano, chini ya John Pombe Magufuli (JPM) kwa kauli mbiu ya “Hapa Kazi tu”, kwa nahau na kwa misingi karibu sawa na ya awamu ya Mwalimu Nyerere kuashiria kurejea kwa itikadi ya maendeleo, lakini safari hii bila kufafanua dira wala itikadi ya uchumi kama ilivyokuwa kwa “Ujamaa na Kujitegemea” ya Serikali ya Rais huyo wa Kwanza.

Chini ya “Ideology of Developmentalism”, kama tulivyoona, mara nyingi demokrasia makini hutundikwa mtini kwa kisingizio cha “Maslahi ya Umma/Nchi” kwa njia ya Katiba kandamizi, jambo ambalo “awamu” ya kwanza ilikwepa kufungwa nira na udikteta huo wa kikatiba kwa mafanikio makubwa kijamii na kiuchumi. Lakini awamu za pili, tatu na ya nne, licha ya kutawala chini ya Katiba kandamizi, ziliendesha nchi bila itikadi ya uchumi wa ndani kiasi kwamba uchumi uliparanganyika na maovu ya kijamii kutamba.

Milango ya udhaifu huo ilifunguliwa hadi bawaba ya mwisho kwa serikali ya awamu ya pili kwa kuruhusu sera za IMF na Benki ya Dunia (WB) kutawala kwa njia ya programu za kurekebisha uchumi zilizozaa sera za soko huria, uwekezaji na ubinafsishaji usiojali na kuzikwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1992.

Matokeo yake yalikuwa ni nchi na uchumi wake kutekwa nyara na ubeberu wa kimataifa na ukoloni mamboleo kutamalaki chini ya sera za kimumiani za IMF na Benki ya Dunia. Na ili kujikomboa kutoka hapo tulipofikia, kunahitaji ukombozi wa pili kwa nguvu ya ziada, ikiwezekana kwa njia ya “kutumbua majipu” na kuvunja minyororo ya uchumi tegemezi na utandawazi wenye kuzaa ukoloni mamboleo. Je, JPM ataweza kuongoza vita hiyo bila kuitwa dikteta?.  Sasa endelea…

Ni wakati wa utawala wa Mkapa, Tanzania iligeuka “kivutio” cha “wawekezaji” mumiani; uporaji wa rasilimali za Taifa ukakithiri, rushwa, ufisadi na kutowajibika miongoni mwa viongozi vikatia fora na kwa nchi kutekwa na ubepari wa kimataifa.

Rais wa Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, aliingia madarakani (2005) wakati tayari nchi ikiwa imeparanganyika asilimia 99, kiuchumi na kijamii; wala kauli mbiu yake ya ANGUKA haikubadili chochote; naye akabaki akiangalia nchi ikitafunwa na nyang’au wa kimataifa kwa kushirikiana na mawakala wao wa ndani ya nchi, kila mmoja kadri ya ukali wa meno yake.

”ANGUKA”, ambayo haikuwa kauli mbiu wala itikadi ya maendeleo, ilishuhudia nchi ikilemewa mzigo wa maovu ya kijamii na kuanguka kwa uzito wake; huku rushwa, ufisadi, uonevu na kuibuka kwa matabaka kwa misingi ya kiuchumi, kijamii na kidini yakimea hima kama magugu kwenye shamba lenye rutuba lililotelekezwa. 

Nchi iligeuka “shamba la bibi”; sauti zikasikika, “wako wapi viongozi wanaojali?. Ziko wapi haki za wanyonge mbele ya wenye mitaji”, zilihoji kwa ghadhabu katika nchi ambayo fedha sasa ilinunua madaraka na madaraka yalipora utajiri.

Lakini pamoja na yote hayo, Rais Kikwete, kama walivyokuwa Mkapa na Mwinyi, hakuonesha ubabe chini ya Katiba, huenda kwa sababu, yeye na wawili hao waliomtangulia, hawakuwa na ajenda wala kauli mbiu makini juu ya maendeleo; na kwa uliberali wao huo usio na mipaka, nchi iliingia kwenye mitafaruku kwa kukosa dira ya maendeleo.

“Hapa Kazi tu”, ni kauli mbiu ya maendeleo ya Rais Magufuli tangu aliposhika kiti cha urais mwaka 2015 na kuinua nyoyo za watu kwa matumaini ya “Ukombozi” wa Pili tangu Mwalimu.

Siku zote, kwenye hali ngumu na mitafaruku, watu wana tabia ya kutegemea viongozi wenye nguvu kutatua matatizo yao kwa kuvunja minyororo iliyobana. JPM alikonga roho za wengi alipoonesha kukerwa na kuapa kuivunjilia mbali minyororo hiyo na mfumo wa ubeberu wa kimataifa ulioikaba koo nchi. Kwa madhila hayo, hakuwa na silaha nyingine mbali na kutumia vifungu vya katiba iliyopo vinavyomfanya atende kidikteta kuliokoa taifa.

Kama tulivyoona JPM na Mwalimu Nyerere, wanaunganishwa na kauli mbiu ya “Kazi” kama msingi wa maendeleo. Lakini tofauti na Mwalimu, yeye anaonekana kufurahia mno madaraka makubwa  chini ya Katiba ambayo Mwalimu aliyachukia na ambayo licha ya kuwa nayo, aliongoza nchi kwa hekima, amani na utulivu kwa kuchanganya na akili zake.

JPM na Mwalimu Nyerere wanashabihiana pia itikadi ya harakati za maendeleo, itikadi ambayo isipotekelezwa kwa busara na hekima kubwa, inaweza kuzua udikteta. Tena, tofauti na Mwalimu chini ya Katiba kandamizi, JPM anaelekea kutekwa zaidi na matarajio ya itikadi kwa gharama ya na dhidi ya haki za mtu mmoja mmoja, uhuru wa mawazo, uhuru wa kujieleza na kusikilizwa – kuashiria kuzaliwa kwa  utamaduni mpya toka uhuru wa nchi hii utamaduni wa matumizi ya vyombo vya dola hadharani hata pale pasipostahili.

Hivi leo, ni fasheni kwa watawala, kuanzia Rais, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuzungukwa na “askari” na wana usalama kwa gharama, wenye silaha za moto kila waendako kwa matumizi mabaya ya madaraka, yakiwamo kuwapa amri kukamata na kuweka ndani watu wanaotoa mawazo “kinzani” wasiyotaka kusikia. Wamekosa subira na usikivu, bali majibu yao ni kwa njia ya “kuweka watu ndani” na “kutumbua majipu”.

Fasheni ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuvamia taasisi za habari (Makonda dhidi ya TV Clouds), au kutia ndani waandishi wa habari kwa kuandika ukweli mchungu unaouma, na matumizi ya Kamati za Ulinzi na Usalama hata kwa masuala ya kawaida kana kwamba nchi iko katika hali ya vita na adui wa nje, ni ishara ama ya kujikweza kwa watawala kama tabaka maalumu tofauti na wananchi ili waogopwe (kuwa wao sio watu wa “kuchezewa”) mithili ya enzi za ukoloni; au ni udhaifu kiuongozi na “uvivu” wa kuelezea mambo mpaka wananchi wakaelewa.

Yote haya yasipodhibitiwa, yanaweza kupelekea serikali kudhibiti kila hatua ya maisha ya mwananchi, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kidini na kwa serikali kutowajibika kwa wananchi (wenye hofu) kwa vitendo vyake na kwa majukumu inayopaswa kutekeleza.

Hatuna sababu za msingi za kujenga utamaduni wa hofu na kuogofya miongoni mwa wananchi mithili ya enzi za utawala katili wa Wayunani wa kale kufikia raia kusema:  “Nawaogopa Wayunani (watawala) hata ninapobeba zawadi kuwapelekea”.

Sote tunaelewa uzalendo wa Rais JPM kwa nchi yake na nia yake njema ya kuona taifa letu linastawi kwa manufaa ya wananchi. Huu ni mfanano thabiti wa uzalendo wake na Baba wa Taifa, ambaye pia ndiye mwasisi wa “amani na utulivu” tunaojivunia. 

Lakini tofauti na Mwalimu ambaye hakupenda kutumia sana vyombo vya dola katika kusukuma mambo ya kiutawala; pengine ni vyema pia Magufuli, akashauriwa na kukubali kwamba, uwezo wa Rais wa kutenda kazi bila kulazimika kupokea ushauri, tangu kale, haujumuishi kutenda nje ya mipaka ya Katiba ya nchi pamoja na Sheria zilizotungwa.

Mapungufu yanayojitokeza, yenye kuathiri demokrasia na utawala bora, na Rais kuyabariki, huenda yanatokana na ushauri hafifu anaopata kutoka kwa baadhi ya wasaidizi wake wasio na ujuzi na umahiri katika mambo ya Uongozi wa Nchi na Usimamizi wa Serikali (Statecraft) kutokana na yeye kuamua mwanzo mpya na “damu mpya” hata katika maeneo nyeti yanayotaka “hekima ya utu uzima”.

Alipobaini kwamba nchi haikuwa na watumishi mahiri, wenye taaluma ya uongozi wa Serikali mwanzoni mwa uhuru (1961), Mwalimu hakusita kuomba msaada kutoka kwa Waingereza ili kuimarisha ofisi yake na kwa ushauri juu ya mambo ya nchi.  Aliletewa Mama Joan Wickens ambaye alifurahia kazi zake kwa miongo mingi baada ya Uhuru. 

Kwa hili, JPM asilifumbie macho wala kulionea haya.  Je, haikusemwa tangu kale kwamba, “yakupasa kwanza kutazama nyuma ili kwenda mbele kwa uhakika zaidi”? Au tunasahau kwamba “ngoma ya watoto haikeshi”?

2 thoughts on “Je, Magufuli ataweza kutawala kwa ujasiri bila kuitwa dikteta? (3)”

 1. Marco Mkalimoto says:

  Nakubaliana na Mzee wangu Mihangwa Joseph kuwa enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere hakutumia sana nguvu ya vyombo vya dola tofauti na ilivyo sasa.Kimsingi kumekuwa na matumizi mabaya ya Kamti za Ulinzi na Usalama katika Mikoa na Wilaya kwa "wakati fulani"lakini wakati mwingine zimetumika vibaya.

  Lakini kwa nchi ambayo watu walipora na kununua madaraka na madaraka kutumika kupora rasilimali za nchi hakuna namna nyingine ya kuwadhibiti hawa lazima nguvu za ziada zitumike kuondosha mfumo huo mbovu.Binafsi nakubaliana na hatua anazo chukua Rais Magufuli maana "washauri hawa ni akina nani" na kama walikuwepo awamu zilizopita hawakuona ufisadi na rushwa iliyotamalaki?

  Katika nchi ambazo zimepiga hatua kama Singapore,India na Malysia utaona mondo waliouchukua kufikia maendeleo ulikuwa wa aina hii ya rais Magufuli.Katika safari ya maendeleo ukianza wimbo wa utawala bora mara mijadala isiyokuwa na ukomo huwezi kufika katika maendeleo ya kweli.Je nchi kama ya China ina Demokrasia?Na je tunaonaje hatua ya maendeleo iliyofikiwa?.Ipi njia sahihi

   

  Nakutakia kazi njema

  Marco Mkalimoto

 2. fifa symbol says:

  It’ѕ gret that you are getting thougɦts from
  this polst as well as frⲟm our argument made here.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *