KUNA watu kati yetu wakisikia “serikali imesema” basi wanabingilika chini na kujiachia wakiwa tayari kuitikia “ndio mzee”.
Watu hawa kati yetu wanaposikia kauli kuwa “serikali imesema” basi wanapoteza uwezo wao waliojaliwa na Mwenyezi Mungu kuhoji na huwa wapesi kukubali. Katika demokrasia yetu changa tuna kazi kubwa sana ya kuwafungua wananchi wetu waweze kuelewa kuwa hakuna serikali duniani ambayo ina tabia ya kusema kweli, kuwa adilifu na ya uwazi. Serikali hiyo haipo. Serikali zote duniani zina tabia ya kujifichaficha, kudanganya na wakati mwingine kulazimisha.
Kwa wale wanaoamini kuwa serikali haipaswi kupingwa au kuhojiwa ni vigumu kwao kuweza kuuona uovu wa serikali hadi ikiwa imechelewa sana.
Historia ina mifano mingi ya ukimya wa watu pale ambapo serikali zao zilipoanza kupanua mbawa zake na kuchanua kucha zake kali zilichongwa zikachongeka.
Ujerumani iliona dalili zote za kuinuka kwa Hitler lakini watu wengi hawakuamini kuwa angeweza kufanya aliyoyafanya. Taarifa zake kwenye vyombo vya habari katika kuhalalisha kwanini Wayahudi waangamizwe na kuondolewa zilipokewa na wengine kama utani.
Kuinuka kwa watawala wengine wenye mrengo wa kidikteta katika historia kumekuwa hivyo hivyo. Wengi wao wametumia karata ya uzalendo kwa nchi na kuweza kuwahadaa wananchi wao kuwa mambo yale ambayo serikali inafanya ni kwa ajili yao. Na bahati mbaya serikali zote zina watetezi wake. Na mara zote watetezi wale wa serikali ni wale ambao upande mmoja ni wanufaika wa moja kwa moja wa serikali hiyo na upande mwingine ni wale ambao huamini kirahisi kila neno “serikali” linapotajwa.
Serikali ni binadamu
Mara nyingi watu husahau kuwa serikali ni binadamu kama sisi. Hakuna serikali inayoendeshwa na mashine au maroboti. Kwa vile serikali huongozwa na binadamu basi serikali ina tabia zile zile za kibinadamu. Serikali hudanganya, serikali hukandamiza, serikali hudhulumu na wakati mwingine serikali au kwa jina la serikali watu wamepoteza maisha yao. Kwa vile serikali ni binadamu wenzetu ni muhimu kwa mtu mwenye akili timamu (au anayejidhania ana akili timamu au ana masalio ya akili timamu) kushuku kauli na matendo ya serikali.
Wananchi wanapopoteza uwezo wa kuishuku serikali yao wanajiweka katika mazingira ya kufanyiwa lolote, wakati wowote, mahali popote na yeyote kwa jina la serikali.
Matokeo yake maofisa wa “serikali” wanaweza kuja ofisini au nyumbani kwa mtu na kumwambia “serikali inataka” jambo hili au lile na mtu yule kwa vile akisikia “serikali” basi anaamini kuwa kuna lengo zuri hujikuta akiuza utu wake, hadhi zao na hata vyeo vyao kwa sababu walighilibiwa na maofisa wa serikali.
Serikali hubanwa na Katiba na sheria
Ni kutokana na kujua hulka hiyo ya serikali ambayo ni ya kibinadamu, jamii za watu zikaamua kujitungua Katiba na sheria mbalimbbali ili kudhibiti serikali. Ndugu zangu, serikali inaweza kufanya yale tu ambayo inaruhusiwa kufanya ndani ya Katiba. Serikali haiwezi na haipaswi kufanya jambo lolote lililo nje ya yale ambayo imepewa kwenye Katiba.
Nakumbuka miaka michache nyuma Rais Jakaya Kikwete alitamba bungeni kuwa anayo madaraka ya kuweza kuamuru “Dk. Slaa akamatwe na akakamatwa” na kauli hiyo kwa masikitiko makubwa ilipokewa na baadhi ya watu kuwa ni ya kweli. Naamini nilikuwa mtu pekee niliyepinga wazi kauli hiyo ya Kikwete na kumkatalia kuwa hana madaraka hayo.
Nilisema wakati ule kuwa “Rais anayo madaraka yale tu ambayo tumempa kwa Katiba.” Inashangazwa watu wetu wasomi na wanasheria hawakuona the fallacy katika hoja ile ya Kikwete.
Matokeo yake ni kweli kuna polisi wanaamini kwa vile wao ni polisi basi wanaweza kufanya lolote kwa yeyote na wakati wowote; wapo maofisa wa usalama wanaamini wanaweza kufanya lolote kwa yeyote; wapo mawaziri wanaoamini kwa vile ni mawaziri wanaweza kufanya lolote kwa yeyote na wakati wowote; na wapo viongozi ambao wanaamini hivyo hivyo.
Hawa, wanaposimama kuzungumza wanajiona ni miungu watu! Kwa jina la serikali kila goti linatakiwa kupigwa na kila ulimi ukiri!
Inanikumbusha ile sanamu ya serikali ya Mfalme Nebukadneza wa Uajemi (Persia) ya kale ambapo mawaziri, maliwali, wasomi na wanasiasa walijikuta wanalazimika kuipigia magoti isipokuwa wale vijana wa Kiebrania waliokuwa marafiki wa Nabii Daniel.
Isikilize serikali, kisha ihoji
Katika demokrasia wananchi ndio msingi wa madaraka yote. Hivyo, wananchi wanayo haki na wajibu wa kikatiba kuihoji serikali yao na kuhoji watumishi mbalimbali wa serikali hiyo.
Wananchi wanatakiwa kuwa na uwezo wa kumhoji kiongozi yeyote. Hili mara nyingi linatakiwa kufanywa na wabunge bungeni kama wawakilishi wa wananchi na nje ya Bunge wananchi wenyewe. Chombo kingine kinachotakiwa kufanya kazi hii ya kuiohoji serikali ni vyombo vya habari. Vyombo vya habari vinalo jukumu la kuwa vinaishuku serikali wakati wowote.
Vyombo huru vya habari havitakiwi kamwe kuwa vipaza sauti vya serikali. Vyombo vya habari vinatakiwa kuwa sauti, midomo na masikio ya wananchi. Vinatakiwa kuuliza maswali ambayo wananchi wangeuliza na kudai maelezo ambayo wananchi wangetaka kupatiwa.
Kwa mfano, mara kwa mara napata taarifa za habari kutoka Ikulu au Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini mara zote nimekataa kurusha kama zilivyo kwa sababu mimi si mpashaji habari wa Ikulu au Ofisi ya Waziri Mkuu. Ofisi hizo zinatoa taarifa ambayo wanataka tuipeleke kwa wananchi lakini hawatoi nafasi ya kujibu maswali yetu kuhusu taarifa hiyo kabla hatujairusha.
Nimeona mara nyingi magazeti na vyombo vya habari vingi vimekuwa kama kasuku kuwa wakipata barua pepe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu au Ikulu basi wanairusha jinsi ilivyo. Kwanini? Kwa sababu wanaamini Serikali inasema kweli! Kwa kufanya hivyo vyombo hivyo vya habari vinapoteza nafasi ya kuhoji taarifa ya Serikali. Hii ndiyo sababu kwa nchi kama Marekani kila siku majira ya saa saba za mchana Mwandishi wa Habari wa Ikulu hukutana na waandishi wa habari na kuwapa taarifa mbalimbali kisha kupokea maswali yao ili kuhakikisha kuwa habari inayoandikwa ina kina kinachostahili.
Bahati mbaya sana kwa Tanzania waandishi wa habari wa Ikulu na Ofisi ya Waziri Mkuu na hata wale wa taasisi nyingine za umma, hawana uwezo wa kusimama mbele ya waandishi wenzao kujibu maswali ya taarifa wanazotoa kwa barua pepe! Lakini ni jukumu la wahariri kuweka mgomo wa kupokea habari hizo isipokuwa kama nafasi ya kuhoji walioleta taarifa hizo inatolewa.
Hivyo basi, tunapoendelea kujenga demokrasia yetu changa ni jukumu letu kama Watanzania kuwa makini na kauli na vitendo vya Serikali. Unaposikia wakati wowote kuwa “serikali imesema” au “serikali imetoa taarifa” mwitikio wako wa kwanza lazima uwe “je inasema kweli”, “ni kitu gani kimepotoshwa”, “ ni maneno gani yamepindishwa”n.k Ukiona akili yako haijashawishika usiamini wala kukubali kirahisi.
Tusipofanya hivyo kama mtu mmoja mmoja au kama taifa basi tunaipa Serikali kibali cha kusema lolote, kufanya lolote, kwa yeyote, wakati wowote na mahali popote! Tunaipa Serikali haki ya kuwa mbabe juu ya wananchi. Na tukiendelea hivyo, tutajikuta tunaishi kwenye utawala wa kidiktea ambao sisi wenyewe tumeukumbatia na kuukubali kwa sababu hatukuthubutu kuuhoji au kuupinga.
Toa maoni yako