Habari
Jiji la Mbeya sasa barabara za lami kila kona
Felix Mwakyembe
Mbeya
Toleo la 274
26 Dec 2012
Jiji la Mbeya
  • Wananchi wafarijika, waendelea kuimwagia sifa Serikali ya JK

NDOTO ya wakazi wa Jiji la Mbeya kuona mabadiliko na maboresho muhimu katika sekta ya miundombinu, hatimaye imetimia baada ya kukamilika kwa moja ya barabara zinazoendelea kujengwa hivi sasa jijini humo.

Barabara hiyo muhimu iliyokamilika hivi karibuni, ni ile ya Airport- Samora, inayohudumia wakazi wa eneo la Iyela, au Airport, kama linavyofahamika kwa walio wengi, ambayo imekamilika kwa kiwango cha lami.

Hata hivyo, pamoja na barabara hiyo kukamilika na hivyo kurahisisha mawasiliano ya usafiri baina ya maeneo hayo, hofu iliyowajaa wananchi hao ni juu ya ajali. “Na sisi sasa tumekuwa watu baada ya kuletewa barabara ya lami. Kwa kweli ni kama ninaota vile, itasaidia kusafirisha mazao yetu kutoka mashambani. Sisi ndio tunalisha jiji la Mbeya kwa mboga mboga mboga na matunda,” anasema mkazi wa Swaya baada ya barabara hiyo kuwekwa tabaka la lami Jumamosi ya wiki iliyopita.

Kijiji cha Swaya kipo nje kidogo ya jiji la Mbeya, na ni maarufu kwa kilimo cha mboga mboga, soko lao kuu likiwa katikati ya jiji, na hivyo kwa wananchi wa eneo hilo kwao umuhimu wake ni usafirishaji wa mazao yao kwa urahisi na haraka zaidi.

Mbali ya usafirishaji wa mazao ya chakula kutoka kijiji cha Swaya, kukamilika kwa barabara hiyo ni faraja kubwa kwa wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari Samora ambao walikuwa wanalazimika kutembea kwa miguu kwa takriban kilometa mbili kwa siku kutokana na kukosekana kwa usafiri kati ya kituo cha Mafiat na shuleni hapo ambako barabara hiyo mpya inaishia.

Barabara hiyo ya kilometa 1.24, inayojulikana kwa jina la Airport- Samora road, ni sehemu ya barabara zenye urefu wa kilometa 28 zilizomo katika mpango wa ujenzi wa barabara za jiji hilo kwa kiwango cha lami ulioanza Novemba mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.

Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Techniplan SpA- Itali, M. Haq, anasema ameridhika na kiwango cha ubora wa kazi kilichoonyeshwa na kampuni inayojenga barabara hiyo ya CICO China.

Anasema kiwango cha ubora na ufanisi wa kazi walichokionyesha mafundi katika ujenzi wa barabara hiyo kinampa matumaini ya kazi kukamilika kwa wakati uliopangwa na kwa ubora waliokubaliana kwenye mkataba.

Mtazamo wa mtaalamu huyo unafanana na wa wananchi wa jiji la Mbeya ambao walieleza wazi kuridhika kwao na ubora wa barabara hiyo kwa kuiangalia tu, huku baadhi ya wahandisi kutoka miji mbalimbali iliyomo kwenye mradi huo nchini, wakibainisha kuwa kiwango hicho kinathibitisha udhibiti katika zabuni kwa baadhi ya wahusika kujiwekea kamisheni maarufu kama ‘ten percent.’

“Hapa hakuna ‘ten percent,’ ndiyo maana hata Rais wa kampuni amekuja, tena na mke wake, ukijumlisha ‘ten percent’ wanazodaiwa makandarasi, si chini ya asilimia 40 ya malipo yote ya kazi, ndiyo maana hulazimika kuchakachua," anasema Mhandisi mmoja kutoka moja ya majiji ya hapa nchini.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Elimu), Jumanne Sagini, Halmashauri za Majiji yote nchini, Halmashauri za Manispaa saba na Mamlaka ya Makao Makuu Dodoma (CDA), zinanufaika na mpango wa uboreshaji wa miji nchini unaotekelezwa kwa fedha kutoka Benki Kuu ya Dunia (WB).

Kwa mujibu wa Sagini, mpango huo unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 200, unahusu ujenzi wa miundombinu ya barabara, masoko, madampo, vituo vya mabasi, mifereji na uboreshaji mazingira. Anasema pamoja na mambo mengine, kwamba utekelezaji wa miradi hiyo inatofautiana kutegemeana na mahitaji ya kila jiji na manispaa.

Barabara hizo ni faraja kubwa kwa wakazi wa Jiji la Mbeya na mkoa huo kwa ujumla, ambapo sasa wanafunga mwaka huu wa 2012 wakiwa na miradi mikubwa mitatu ya kujivunia, kwa maana ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Soko la Mwanjelwa na barabara za lami zinazoendelea kujengwa ndani ya jiji.

Kukamilika kwa barabara hiyo ya Airport-Samora, kunafufua matumaini ya wakazi wa jiji hilo ambao awali walikata tamaa, kiasi kwamba haikuwa ajabu kuwakuta kwenye vijiwe wakihoji uhalali wa mji wao kupewa hadhi ya jiji, sababu kuu ikiwa ni kutoona mambo yakienda vema kama walivyotarajia, na hasa pale walipolinganisha na miaka ya kabla ya kupandishwa hadhi. Ni kwa msingi, baadhi ya wananchi hao katika vijiwe vyao, hawakosi kuimwagia sifa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kazi nzuri za maendeleo inazozitekeleza katika mkoa wa Mbeya, na hasa uboreshaji wa miundombinu ya barabara za jiji hilo.

Uwanja wa Ndege Songwe pamoja na Soko la Mwanjelwa, vinatarajiwa kuzinduliwa wakati wowote kuanzia sasa, wakati ujenzi wa barabara za lami jijini humo utakuwa ukiendelea lakini baadhi yake zitakuwa zimekamilika tayari kufikia Juni mwakani, zikiwa na urefu wa kilometa 28.

Tangu Desemba 13 mwaka huu, Uwanja wa Ndege wa Songwe ulianza kutumika, na kwa mujibu wa Meneja wa Uwanja huo, Valentino Kadeha, kinachosubiriwa ni uzinduzi rasmi tu unaotarajiwa kufanywa na Rais Kikwete.

Hata hivyo, ujenzi ni jambo moja tu katika kuimarisha miundombinu ya barabara jijini humu, la msingi ni utunzaji wake, jambo ambalo kwa uzoefu ni tatizo kubwa sana, si kwa Jiji la Mbeya pekee bali kwa taifa zima.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Juma Iddi, maandalizi yamefanyika kuhusu matunzo ya barabara hizo, ikiwamo kukutana na viongozi wa kata na mitaa na kuwaeleza wajibu wao katika kusimamia matunzo ya barabara hizo, ikiwamo utupaji taka ovyo, ambapo jiji litahakikisha takataka hazikai kwenye ‘maguba’ yaliyoko kwenye barabara, na kwamba hata wananchi nao wameelimishwa tayari.

“Wananchi lazima wafahamu kwamba fedha hizi (zinazotumika kuboresha miundombinu ya jiji la Mbeya) ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, kwa hiyo tutakuja kuzilipa,” anasema Iddi.

Katika hili la kutunza miundombinu ya huduma za jamii, Kaimu Katibu Mkuu, Sagini, anazichagiza mamlaka za serikali za mitaa nchini kusimamia sheria ndogo ndogo zilizopo kuhusu usafi wa mazingira ili kulinda barabara nchini ambazo anasema huigharimu nchi fedha nyingi.

Pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara, mpango huo wa uboreshaji Jiji la Mbeya (face lifting) unahusu pia ujezi wa kituo kikuu cha magari ya abiria na mizigo eneo la Nane Nane, taa za barabarani na shimo la takataka (land fill).

Barabara zinazojengwa kwa fedha kutoka Benki ya Dunia zimegawanywa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza itahusu kilometa 13.2 kwa barabara inayoanzia Sae kupitia kituo cha umeme cha TANESCO hadi Chuo Kikuu cha Theofilo Kisanji (TEKU) pamoja na barabara ya Airport kupitia Jacaranda hadi kituo cha mafuta cha Bhanji, eneo la Forest.

Barabara nyingine kwenye awamu hiyo ni ile ya Kamishina Road ambayo inanzia kwenye Mnara wa Uhuru kuelekea Weru Garden hadi Uzunguni, barabara ya Block T inayoanzia Kabwe kuelekea Kanisa la KKKT Luanda hadi SIDO na kituo cha mafuta cha Oil Com Soweto, na ile ya kuanzia Sea (TANESCO) hadi Zahanati ya Ituha.

Ujenzi wa barabara hizo utahusu pia mifereji ya maji na madaraja madogo aina ya makarafati, ununuzi wa magari mawili kwa ajili ya usimamizi wa barabara, mtambo mmoja wa kushindilia na mwingine wa kuchota mchanga na mawe unaofahamika zaidi kama kijiko.

Awamu ya pili ya mpango huo itakuwa na kilometa 14.6 na itahusu barabara ya pili eneo la Sokomatola pamoja na kituo chake cha mabasi, barabara inayoanzia CCM Ilomba kuelekea VETA hadi Machinjioni, kabla ya kukutana na ile itokayo Ilemi na kuelekea hadi Makasini eneo la Uyole na barabara ya Hospitali ya Mkoa inayoanzia Ndiyo Mini Super Market.

Nyingine katika awamu hiyo ya pili ni pamoja na ile inayoanzia Forest Mpya ambayo itaungana na ile ya Airport hadi Sae, barabara ya Igawilo inayoanzia barabara kuu ya Mbeya- Tukuyu kuelekea Kituo cha Afya Igawilo hadi Shule ya Sekondari Igawilo.

Ni katika awamu hiyo ya pili, ambapo kitajengwa Kituo Kikuu cha Magari ya Abiria na Mizigo katika eneo la Nane Nane, shimo la taka kwa maana ya dampo litachimbwa, ununuzi wa mizani ya kupimia uzito kwenye shimo la taka, magari matatu ya taka (side loaders), magari manne ya kuzolea taka (skip master), makontena 109 ya kubebea taka (skip bucket) magari matatu madogo na vikusanya taka 200.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, katika fungu la awamu ya pili watapiga pia picha za makazi ya jiji (satellite image) ambayo itasaidia kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo, na zaidi yatatolewa mafunzo kwa watendaji kuhusu ukusanyaji wa mapato, na kuweka mfumo wa kompyuta wa uendeshaji kazi za halmashauri ya Jiji hilo.

Katika mpango huo kabambe wa uboreshaji wa miundombinu ya barabara, Jiji la Mbeya halitegemei fedha hizo pekee kutoka Benki ya Dunia, bali litajenga kilometa nane kwa kiwango cha lami likitumia fedha kutoka vyanzo vyake vya mapato.

Barabara hizo ni pamoja na ile ya Kambarage inayoanzia Hospitali ya K’s hadi Hospitali ya Wazazi ya Meta na kituo kidogo cha mabasi cha Meta, barabara ya Maktaba ya Mkoa, barabara zote zinazozunguka City Park, barabara za Sokomatola zikiwamo ya TANU, barabara ya tatu na nne, wageni street na Nonde street, maegesho ya magari mkabala na Hoteli ya Sombrero na eneo ilipokuwa City Pub na vituo vidogo vya mabasi vinane.

Kwa kutumia fedha zake, jiji la Mbeya litajenga kilometa kumi za barabara kwa kiwango cha changarawe ambazo hapo mwakani zitawekwa lami, ambapo zitakuwa ndio mwanzo wa mpango wake endelevu wa kujenga kilometa kumi za barabara kwa kiwango cha lami kila mwaka.

Miongoni mwa kero za muda mrefu katika Jiji la Mbeya, ni pamoja na kukosekana kwa taa za barabarani ambapo pamoja na kelele za muda mrefu za wananchi ziliwekwa kwenye barabara moja tu itokayo Mafiat kuingia katikati ya jiji. Hata hivyo, kero hiyo itabakia kuwa historia, kwa kuwa tayari mradi wa uwekaji taa kwenye barabara kuu ya Tanzania- Zambia umekamilika na taa kuwashwa.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Felix Mwakyembe
fkyembe@gmail.com
+255-713290487

Toa maoni yako