Makala
JK: CCM kujivua gamba pekee hakutoshi
Mkweli Ukweli
Toleo la 222
18 Jan 2012

MIAKA mitatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa kwanza mara baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995, nikiwa na fikra nzito juu ya hali itakayokikabili Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya mfumo huo, niliwahi kuandika makala kwa ajili ya kuchapishwa kwenye gazeti la Daily News.

Mhariri wa gazeti hilo kwa wakati huo, baada ya kuipitia makala hiyo, aliniambia kuwa ilimwia vigumu kwake kuamua makala hiyo ichapishwe kutokana na yale yaliyokuwamo ndani yake, kwani kama angeamua vinginevyo, lazima wakubwa wake kikazi wangetaka kumjua mwandishi wa makala hiyo.

Wakati huo ningali bado mtumishi wa Serikali, nilikuwa nikichangia kwa kuandika makala katika gazeti la Daily News kama concerned citizen (raia mwenye kujali) bila kutaja jina langu.

Hivyo kama angeruhusu makala hiyo ichapishwe na wakubwa zake wakataka kujua mwandishi ni nani, angelazimika kunitaja. Baada ya wote wawili kutafakari kwa makini woga huo, kwa kuzingatia athari zake kwangu nikiwa bado mtumishi wa Serikali na kutomweka matatani kikazi mhariri wa gazeti hilo, tulikubaliana kuwa isichapishwe.

Katika makala hiyo nilizungumzia mambo matatu ya msingi yakihusu ulazima wa chama tawala CCM, kujibadili kimfumo ili hapo baadaye kiweze kujiendesha bila kukabiliwa na misukosuko mikubwa ya kifedha na kisiasa katika mfumo wa vyama vingi.

Kati ya mambo hayo matatu niliyoyataja, mojawapo likiwa ni ulazima wa CCM kuondokana na mfumo wa kuwa na watumishi wengi walioajiriwa. Hili niligusia kwa kuamini kwamba chama hicho hakitakuwa tena na uwezo wa kujipatia mapato kwa kuitumia dola kwa njia moja au nyingine, kama ilivyokuwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Kwa mtazamo huo, maoni yangu yakiwa kwamba CCM ibaki na watumishi wachache wa kulipwa mshahara na kazi zake nyingi ziwe mikononi mwa wanachama wake kwa msingi wa kujitolea.

Jambo la pili nililozungumzia katika makala hiyo kwa kujua kwamba bado chama kitahitaji fedha hata kama kitapunguza idadi ya watumishi wa kulipwa kwa kiasi kikubwa, ni chama hicho kuwa na mikakati ya miradi mbalimbali ya kibiashara.

Lakini nikatahadharisha kwamba miradi hiyo isiwe ya mfumo wa biashara kama zile zilizoendeshwa chini ya shirika lake la kiuchumi lililokufa la SUKITA.

Hivyo kwa mtazamo huo, nilikuwa na maoni kwamba CCM ingeweza kuwekeza katika ujenzi wa majengo kwani ilikuwa na viwanja au aridhi ya kutosha kukidhi mahitaji hayo nchi nzima.

Jambo la tatu nililolisema ni kukitahadharisha chama hiki kikongwe tawala kuwa kama hakitachukua hatua hizo, kitatumbukia katika dimbwi la kuwategemea wafanyabiashara zaidi kuliko siku za nyuma ili kiweze kujiendesha.

Na matokeo yake yatakuwa CCM kulazimika kuwakumbatia wafadhili wake hao na hatimaye kujikabidhi mikononi mwao.

Yote hayo niliyotabiri takriban miaka 26 sasa ndiyo yanayojidhihirisha kwa upande wa chama hiki kikongwe nchini.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya nilipoandika makala hiyo, onyo alilotoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mara tu baada ya kung’atuka kwake, halikunijia akilini wakati huo.

Naamini baadhi ya wasomaji wa makala hii mtakumbuka kwamba Mwalimu, alipofanya ziara yake nchi nzima kuwashukuru na kuwaaga Watanzania baada ya kuachia ngazi ya kuliongoza taifa hili mwaka 1985, alijionea mengi yanayowakabili wananchi.

Kati ya yale aliyoyaona ni kuhusu chama tawala kutokuwa karibu na wananchi. Na baada ya ziara hiyo akatamka wazi kuwa hakujua jinsi CCM ilivyokuwa mbali kiasi hicho na wananchi.

Alipoulizwa na waandishi wa habari ilikuwaje ashangae wakati yeye ndiye alikuwa akikiongoza, alijibu kuwa ziara yake hiyo akiwa sio Rais tena, ndiyo ilimpa fursa ya kuilewa hali hiyo.

Ningekumbuka kushangaa huko kwa Baba wa Taifa wakati naandika makala ya kuihadharisha CCM juu ya ulazima wa kujiunda upya, nisingekosa kunukuu kushitushwa huko kwa Mwalimu Nyerere kutokana na ziara yake hiyo ndefu ya nchi nzima na ya mwisho wakati wa uhai wake baada ya kung’atuka.

Kwa bahati mbaya, kuwa mbali na wananchi kwa CCM kulikomshitua Baba wa Taifa, hakukufanyiwa tathmini wala kuonwa kuwa ni suala la lazima kushughulikiwa wakati wa kipindi kizima cha Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, akiwa Rais wa Jumhuri ya Muungano na pia Mwenyekiti wa CCM.

Horace Kolimba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM wakati wa uongozi Mwinyi, kabla ya kukutwa na mauti huko Dodoma, aliigusia hali hiyo iliyoonwa na Baba wa Taifa pale alipotamka kuwa CCM “imepoteza dira.” Lakini pia naye hakueleweka kwa wana CCM wenzake.

Benjamin Mkapa naye katika kipindi chake cha urais, hakuwa na muda wa kushughulikia masuala ya chama chake cha CCM akiwa kama Mwenyekiti. Mkapa ajenda yake kuu katika kipindi cha utawala wake, ilikuwa kufufua uchumi kwa kuuza mashirika ya umma na hatimaye yeye mwenyewe kujiuzia Mgodi wa Kiwira uliopo mkoani Mbeya.

Kutokana na vipindi viwili vya uongozi wa marais hawa wawili wastaafu (Mwinyi na Mkapa) kuiacha CCM kuendelea kuwa mbali na wananchi na bila uongozi wenye dira, matokeo yake yakawa chama hiki tawala na kikongwe, kuvamiwa na wafanyabiashara wajanja wachache walioiona CCM kuwa ni kichaka cha kujineemesha na kuficha maovu yao.

Hali hii ya kutisha ya CCM kuwa mbali na wananchi na kupoteza dira kama walivyoieleza Mwalimu na Kolimba, ndiyo ambayo leo inakisumbua Chama cha Mapinduzi.

Hali hii ndiyo inayomlazimu Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM wa sasa ambaye pia ni Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, alazimike kuchukua hatua za chama hiki tawala “kijivua gamba.”

Gamba hili ni la CCM kutekwa na wafanyabiashara waroho kwa kipindi cha miaka ziadi ya 20, tangu kutangazwa kwa Azimio la Zanzibar la mwaka 1986, kwa Tanzania kuachana na mfumo wa kiuchumu wa kijamaa.

Kama inavyoonekana katika makala hii, hatua za Kikwete anazozichukua kuivua gamba CCM hazitoshi. Itambidi aende mbali zaidi na kubadili mfumo mzima wa uendeshaji siasa za CCM.

Akiwa Mwenyekiti wa CCM, asiishie kwenye hatua ya kuwaondoa mafisadi na viongozi wabovu tu ndani ya chama tawala. Akiwa tegemeo la wana CCM kuwa ndiye wa kukinusuru chama chao, ni lazima aende mbali zaidi kwa kubadili mfumo mzima wa chama kuendesha shughuli zake za kisiasa kama nilivyodhamiria kuishauri CCM, katika makala yangu ambayo mhariri wa Daily News alisita kuichapisha.

Watanzania kwa ujumla wetu, hatuna budi kuzingatia ukweli kwamba Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi na si ya wafanyabiashara wachache wanaotaka kujitajirisha na kuficha madhambi yao ndani ya vyama vya siasa.

Chama chochote cha kisiasa ambacho kitapuuza ukweli huu, iwe CCM au chama kingine chochote kile kitakuwa kimejitenga na Watanzania.

Kwa maana hiyo, ukweli huu na hadhari hii sio tu ya kuzingatiwa na CCM, bali hata na vyama vyote vya kisiasa vinavyopigania kutaka kuchukua uongozi wa kutawala Tanzania.

Na ujumbe unaotolewa wakati huu na akina Nape Nnauye na wenzake kwa wanachama wenzao wa CCM, unawalenga wafanyabiashara wa aina hiyo kutokana na kuzingatia kwao ukweli huu.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Mkweli Ukweli
ukweliniukweli@yahoo.com

Toa maoni yako