Kama mnataka ‘Ukawa’, wakati ni huu

MWAKA 1995, Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi. Wakati huo, ‘kizazi cha dhahabu’ cha upinzani kilikuwa tayari kwa mapambano.

Nakiita kizazi cha dhahabu kwa sababu naamini wengi wa waliokuwa vinara wake walikuwa watu ambao ama walikuwa wamepigania upinzani kwa zaidi ya miongo mitatu na wengine waliingia upinzani na kupoteza vingi; ajira zao, marafiki na vipato.

Hapa kuna majina mengi, Chifu Abdallah Fundikira, Abdulrahman Babu, Mabere Marando, Profesa Mwesiga Baregu, Ndimara Tegambwage, Edwin Mtei, Bob Makani na vijana kama akina James Mbatia.

Profesa Ibrahim Lipumba alipata kunisimulia kwamba mtu aliyekuwa mpambe wake wakati akioa (mtu maarufu ambaye sitamtaja jina), alivunja naye urafiki mara baada ya kufahamu kuwa amejiunga na CUF.

Hizi ndizo nyakati ninazozizungumza. Vigogo hawa wakawa wamejiandaa vema kwa ajili ya uchaguzi huo wa aina yake. Kukatokea mgogoro ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mmoja wa wanasiasa maarufu wa wakati huo, Augustino Mrema, akajiuzulu uwaziri na kisha akahamia upinzani.

Pamoja na upinzani kuwa na vinara wote hao, hatimaye  Mrema aliyehama kutoka CCM akapitishwa kuwa mgombea wa chama cha NCCR Mageuzi. Mwisho wa uchaguzi, Mrema alishindwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa.

Ukiongea na vinara wa upinzani, watakwambia Mrema alisaidia wao kupata kura nyingi kuliko kama wangemsimamisha mgombea mwingine yeyote.

Miaka 20 baadaye, yaani mwaka 2015, upinzani ulikuwa na nguvu baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010. Mara hii, upinzani haukuwa na wabobezi wengi kama ilivyokuwa mwaka 1995 lakini uliungwa mkono na kundi kubwa la watu nje kuliko ilivyokuwa nyuma.

Wengi walitaraji pengine mgombea wa upinzani angekuwa Profesa Lipumba au Dk. Wilbrod Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema. Hata hivyo, ukatokea mgogoro mwingine CCM na Edward Lowassa akakihama chama hicho na kuhamia upinzani.

Huyo ndiye baadaye, kama ilivyokuwa kwa Mrema mwaka 1995, akaja kuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichobeba bendera ya umoja wa vyama vya upinzani.

Ukizungumza na vinara wa siasa za upinzani hivi sasa, watasema Lowassa aliwasaidia kupata kura nyingi na wabunge wengi kuliko kama wangemsimamisha mtu mwingine. Hoja hii inaweza kuwa kweli. Lakini, inaweza kuwa kweli tu kama kungekuwa na ulinganifu wa endapo ingemsimamisha mtu kama Dk. Slaa.

Uzoefu katika nchi tofauti unaonyesha kwamba vyama vilivyodumu madarakani kwa muda mrefu huwa vinaondolewa tu na mtu ambaye hana uhusiano kabisa na wale waliokuwa madarakani muda mrefu.

Labda nichukue mfano wa Zambia. UNIP ya mzee Kenneth Kaunda ilikuwa imekaa madarakani kwa takribani miaka 30. Aliyekuja kumshinda Kaunda alikuwa ni Frederick Chiluba aliyekuwa kiongozi wa Vyama vya Wafanyakazi.

Kwa Tanzania, simuoni mtu wa aina ya Chiluba kwa sababu vyama vya wafanyakazi havina tena nguvu ile iliyokuwa navyo huko nyuma. Kimsingi, kama utaniuliza mimi, nadhani vyama hivyo vilikuwa na nguvu zaidi wakati wa ukoloni kuliko baada ya Tanganyika huru na Tanzania baadaye.

Ambacho vyama vya upinzani vya Tanzania vinahitaji ni kuwa na umoja na kusimamisha mgombea mmoja mwenye nguvu anayekubalika na wote. Mgombea huyo anatakiwa kutafutwa na kupatikana sasa na si katika mwaka wa uchaguzi.

Kwa sababu upinzani wa Tanzania umeshaonja matunda ya muungano uliopewa jina la Ukawa mwaka 2015, ni wazi kazi ya kutengeneza muungano makini zaidi na imara zaidi ni rahisi kuliko ilivyokuwa kabla ya kuelekea mwaka 2015.

Kama itatokea CCM wakagombana wenyewe wakati huo, watakaotaka kuhamia upinzani watafanya hivyo wakijua fika kwamba wanakwenda kuongeza nguvu tu na si kuwa wagombea.

Ni aibu kwamba kwa miaka zaidi ya 25, upinzani umeshindwa kutengeneza mgombea mmoja wa kutoka miongoni mwao mwenye ubavu wa kushindana na CCM. Nguvu ya upinzani inatakiwa kuwa kwenye umoja wao na tamaa ya wananchi kwenye kutaka mabadiliko na si kwenye kuvizia “wahamiaji” kutoka chama tawala.

Hivi sasa, upinzani una vijana makini ambao hawana mawaa au uhusiano wowote na CCM kwenye maisha yao. Huko nje, kuna kundi kubwa la vijana walio tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayepitishwa na upinzani ulio makini.

Na mbeba bendera huyo anatakiwa kuwa makini na kujulikana na wote. Ikiwezekana, huyo ndiye azunguke nchini kuomba kura wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019. Watu wakimwona, wajue kwamba huyu ndiye.

Hili linawezekana tu kama juhudi za kutengeneza umoja huo wa vyama vya upinzani zikianza sasa. Kama upinzani watataka kutengeneza Ukawa nyingine mwaka 2020 kwa kutaraji kwamba kuna kigogo atahama kutoka CCM wakati huo; watakuwa wanafanya kazi ileile ya kutwanga maji kwenye kinu.

Wakati ni huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *