Kama serikali haihitaji mabadiliko, ituambie inachokihitaji

MOHAMED Kiganja ameyaweka kiganjani mwake mabadiliko ya kiuendeshaji yanayotaka kufanywa na klabu za soka za Simba na Yanga. Kiganja ndiye Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

Tangu lijitokeze suala la mabadiliko ya kiundeshaji kwa klabu hizo kongwe, Kiganja amekuwa akipinga mabadiliko hayo ya kiuendeshaji bila ya kutoa sababu za msingi na nini kifanyike.

Maisha ya kupinga kila kitu bila kuja na kitu mbadala yameshapitwa na wakati. Ni wakati wa Kiganja kuja na mpango mwingine tofauti na huu wa mabadiliko ili klabu hizi ziondoke kwenye dimbwi hili la umasikini uliopitliza na kuacha kutegemea kuishi kupitia mifuko ya wahisani wanaojitolea.

Simba, Yanga zimeishi maisha ya kutegemea mifuko ya wahisani kwa muda mrefu bila ya wahisani wenyewe kunufaika na kile wanachokitoa.

Nani anayetaka kutoa fedha au rasilimali zake na hajui atazirudisha vipi? Ni muda wa Kiganja kujiuliza swali hili kabla ya kufanya lolote lile.

Uzuri wa mfumo huu wawekezaji wenyewe wameshameweka wazi mchanganuo wa mambo yatakavyokuwa, huu wasiwasi wa serikali unatokea wapi?

Moja ya kauli ya kusikitisha kuwahi kutolewa na Kiganja ni ile ya kusema eti wawekezaji Yusuf Manji (Yanga) na Mohamed Dewji (Simba) wakaanzishe klabu zao na kuachana na klabu hizi za wanachama.

Hii ni moja ya hoja nyepesi iliyotolewa na serikali juu ya mabadiliko hayo ya kiuendeshaji yanayotakiwa kufanywa ndani ya timu hizi na serikali haionyeshi kuafiki walichokiafiki wanachama wa timu hizo. Hapa Kiganja aliushangaza umma.

Kauli za Kiganja moja kwa moja zinaonyesha serikali haiungi mkono suala hili. Wawekezaji wameona fursa na wanataka kuitumia na kwa kuwekeza sehemu inayotazamwa na kila mmoja ili kile wanachokiwekeza kiweze kuwafaidisha wao na sehemu wanayowekeza.

Leo hii kuwaambia waachane na timu hii na wakaanzishe timu zao ni kuonyesha jinsi gani mpira wetu bado ulivyo wa katika hali ya ujamaa.

Maisha ya ujamaa ndiyo yametufikisha hapa tulipo. Serikali ina nguvu ya kuzuia kila kitu na hakuna anayeweza kusimama juu yake, lakini hapa ingetakwa kujenga hoja ambayo ingewafanya hata wanaotaka mabadiliko kujifikirisha upya juu ya suala hili wanaloliamini wakati huu.

Wanachama ndiyo watu wa mwisho kuamua lolote lile ndani ya klabu hizi. Wao wana mamlaka ya kusema jambo fulani lifanyike na likafanyika bila kikwazo chochote kile. Inakuwaje wanachama wanaunga mkono mabadiliko lakini serikali inatia ugumu?

Si vibaya tukimtaja Kiganja kama mmoja ya watu wanaochelewesha mabadiliko katika soka, huku akishindwa kutoa hoja za kujenga na badala yake anaamini kile anachokisimamia.

Moja ya sera kuu ya serikali ya awamu ya tano ni kuwa na Serikali ya Viwanda. Ukishaona hili moja kwa moja unaona jambo la uwekezaji linapewa umuhimu mkubwa.

Inakuwaje watu wamewekeza kwenye viwanja na sehemu mbalimbali na hakuna matatizo kila kitu kinakwenda kwenye mstari, lakini uwekezaji katika soka unaonekana tatizo na wawekezaji wanaambiwa waende kuanzisha klabu zao kama ilivyo kwa Azam FC?

Wafanyabiashara wakubwa wana muono wa tofauti kwenye biashara wanazozisimamia. Kama wamiliki wa Azam waliona wanaweza kuwekeza kwa kuanzisha timu yao sio dhambi kwa wafanyabiashara wengine kuwekeza kwenye timu zenye majina makubwa na hiki ni kitu rahisi kukielewa katika biashara ya kileo.

Manji na Dewji wanajua tayari timu hizo zina mtaji wa rasilimali watu na wao wanaweka fedha ili maendeleo na mgawanyo uanzie hapo. Nadhani Kiganja alipaswa kusimamia hilo na kuangalia mchakato kama ni halali, mgawanyo wanauonaje kama serikali na sio kuzuia au kutoa hoja nyepesi ya kila mwekezaji aanzishe klabu yake.

Kuanzisha timu na timu ikaja kusimama kama zilivyo Simba na Yanga si jambo dogo hata kidogo. Simba na Yanga tunaziona sasa hazijaja tu kama mvua ya vuli. Zilitengeneza na kufikia hivi, inakuwaje mwekezaji anaambiwa akaanzishe timu yake na kuwekeza huko na si huku?

Kuna faida nzuri inapatikana kuwekeza ndani ya timu hizi ambazo baada ya muda mfupi kila upande utapata faida na wawezekezaji wanalipenda hili na si vinginevyo.

Kama serikali hawaoni mpango huu wa uwekezaji ni mpango wa maana na wenye kuleta manufaa makubwa huko tunakokwenda, si vibaya wakaitisha mkutano na kutoa mapendekezo yao kuwa hawautaki mfumo wa mabadiliko na watuambie wanataka klabu hizi ziendeshwe kwa mfumo upi wanaotaka wao.

Ukimya wao na matamko yao unafanya kila mmoja ndani ya timu hizo kuwaona wao ndiyo wakwamishaji wakuu wa mchezo wa soka nchini.


0746-594360

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *