WENGI miongoni mwetu tunaijua hadithi ya meli kubwa iliyoitwa RMS Titanic, ambayo ilizama katika Bahari ya Atlantiki usiku wa tarehe 14/15 Aprili 1912 ikiwa katika safari yake ya kwanza kati ya Southampton na New York.
Hii ilikuwa ni meli ya abiria ya anasa iliyokuwa kubwa kuliko nyingine yo yote katika historia ya dunia hii, ikiwa na kila aina ya vivutio vya burudani vya kutosha kuwastarehesha abiria wakwasi walikouwa wamedhamiria kusafiri kwenda Marekani kwa staili ya pekee.
Aidha, watengenezaji wa meli hii, Hartland and Wolff wa bandari ya Belfast, Ireland, waliamini kwamba walikuwa wameunda meli isiyoweza kuzama. Wakatamba hivyo, na waliowasikiliza wakaamini hivyo. Imani hiyo ilizaa jeuri pia, kiasi kwamba hata ile kinga au hadhari inayohitajika kwa kawaida katika meli kama hiyo ikadharauliwa, na badala ya kuwa na mitumbwi ya kuokoa maisha kwa idadi ya kutosha ikafungwa mitumbwi ya kuweza kuokoa abiria 1,178 tu wakati idadi ya abiria ikiwa ni 2,223.
Meli iliyobashiriwa kwamba haingeweza kuzama ikazama, na katika kuzama huko wakaangamia abiria wapatao 1,517. Inaaminika kwamba laiti ingekuwapo mitumbwi ya kutosha hawa abiria wasingekufa, au wangekufa wachache sana.Hii ni simulizi inayojulikana kwa watu wengi. Hata wale wasiopenda kujisomea watakuwa wamepata fursa ya kuiona katika filamu ya sinema iliyoigizwa na Leo di Caprio.
Lakini iko hadithi nyingine, hadithi halisi, ambayo haijulikani kwa watu wengi. Mwaka 1898, ndiyo kusema miaka 14 kabla ya kuzama kwa Titanic, mwandishi Mmarekani, Morgan Robertson, alikuwa ameandika riwaya fupi kwa jina la Futility, ambayo ilihadithia kisa cha meli iliyoitwa Titan, iliyokuwa kubwa kuliko meli zote zilizokuwa zimeundwa hadi wakati huo, na ambayo ilielezwa kwamba haiwezi kuzama.
Kwa imani kwamba haiwezi kuzama, waendeshaji wa meli hiyo hawakuona sababu ya kuibebesha mzigo mkubwa wa mitumbwi ya kuokoa abiria bila sababu yo yote. Titan ilizama katika mazingira kama yale ya kuzama kwa Titanic miaka 14 baadaye. Idadi ya watu waliokufa katika meli ya hadithi haikupitana sana na wale waliokufa katika Titanic.
Katika hali ya kawaida watu hutaraji kwamba maisha halisi ndiyo chanzo cha sanaa, kwa maana kwamba riwaya nyingi, tamthilia, maigizo, filamu za sinema, nyimbo, mashairi, michongo, sanamu na kadhalika, huwa ni vielelezo vya kisanii vya maisha ya binadamu. Ni nadra sana kwa maisha ya binadamu kufuata vielelezo vya kisanii, kwa mfano kwa jamii kufanya mambo kwa jinsi ilivyoelekezwa katika wimbo, au filamu au riwaya. Hata wanapoelekea kufanya hivyo, huo unakuwa ni mzunguko mwingine kwa sababu kile kielelezo cha sanaa mwanzo wake yalikuwa ni maisha halisi.
Hii inaeleza nini kuhusu wajenzi wa Titanic, meli ya ukweli, na uhusiano wao na waundaji wa Titan, meli ya riwaya? Je, waundaji wa Titanic walikuwa wameisoma riwaya ya Robertson, ikawavutia kiasi cha kuamua kuona kama inawezekana kuunda meli kama ile halafu wakaifanya iwe haiwezekani kuzama? Kwamba waundaji wa Titanic walishawishika kufuata mfano wa riwaya na kughairi kuweka idadi mwafaka ya mitumbwi ili tu waone kama watu watakufa kweli, kama riwaya ilivyokuwa imeonyesha?
Kwamba, ilipoundwa Titanic waendeshaji wake waliamua kufuata hatua kwa hatua yale yote yaliyokuwa yameisababisha Titan kuzama, ikiwa ni pamoja na kufuata karibu njia ile ile kuelekea Marekani? Kwamba hii ilitokana na kujiamini kupita kiasi, jeuri iliyopindukia, ulevi wa kitaaluma uliokithiri au ujuha usioelezeka?
Katika nchi zetu nyingi za Afrika hivyo ndivyo tunavyoenenda; ni kama vile tumesoma riwaya ya maafa, tumeipenda na tunajaribu iwapo inawezekana kweli kupatwa na maafa kama hayo. Riwaya yenyewe si lazima iwe ya mtunzi mahiri mwenye maono makali, kwani maisha ya nchi zetu, hasa tunavyozitendea na kuwatendea wananchi wake, ni kama riwaya, na mafunzo yake maridhawa yangeweza kutuonya tufanye hadhari na mienendo yetu yasije yakatufika yaliyowafika wenzetu katika riwaya za kweli za maisha ya mataifa mengine.
Hivi ni nani anayeshindwa kuona kwamba katika nchi zote za Kiafrika ambamo wananchi wamenyimwa haki zao kumetokea machafuko? Ni mjinga gani asiyejua kwamba hata watu wangekuwa wametulia wanaelekeya kila wanapoelekezwa, mithili ya kondoo, hawatakubali kuwa hivyo daima, na kwamba siku moja watasema, Basi! Inatosha! Kifaya!
Ni watu wapuuzi tu ndio wanaoweza kuangalia mifano ya nchi ambako kumetokea maafa kwa sababu ya ama uroho wa watawala, ama ujinga wao, ama kutojali kwao, ama fedhuli yao, halafu wakashindwa kuelewa kwamba hayo yaliyotokea kwingine yanaweza kuwapata na wao, na kwamba hakuna nchi iliyokata bima ya kuiwezesha kuepukana na zahma kama hizo.
Bima pekee inayoweza kuikinga nchi na maafa ninayoyajadili ni kujenga misingi ya uongozi unaosimamia haki kwa wananchi wote, uongozi usiovumilia matendo ya uonevu, dhuluma, wizi na ubabaishaji wa aina yo yote, uongozi ambao nimesema, na sina shida kurudia tena, tumeshindwa kuujenga tangu alipotutoka Mwalimu Julius Nyerere.
Tukumbushane kidogo kuhusu historia yetu. Mwaka 1966 nilikuwa kidato cha nne, Bukoba, lakini nilikuwa mshririki katika mijadala iliyohusu Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na malumbano baina ya Rais Nyerere na uongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu, hususan viongozi wa National Union of Tanzania Students (NAUTS), akina Samuel Sitta, Onesforo Chawe na wengine. Nakumbuka vyema maswali na majibu yaliyofanyika baina ya Nyerere na viongozi wa NAUTS, mwezi Agosti, makao makuu ya TYL, Barabara ya Morogoro.
Nyere alijaribu kutuelewesha kwamba jeshi hilo lilikuwa linaanzishwa kwa maslahi ya vijana wenyewe, ili waweze kuandaliwa kwa ajili ya utumishi wa jamii zao, na kwamba katika hili hakukuwa na nia ya kuwakomoa vijana. Lakini, kwa sababu viongozi hao hawakuridhika na maelezo ya Mwalimu, miezi kama miwili baadaye, wakafanya maandamano makubwa jijini Dar es Salaam yaliyoishia Ikulu ambako Nyerere alikuwa akiwasubiri, akiwa amefanya mipango yote ya kuwafukuza chuoni na kuwarejesha makwao.
Hotuba yake (niliifuatilia nikiwa shuleni Bukoba) ilikuwa kali kuliko hotuba nyingine alizowahi kutoa, na akawakemea kweli kweli vijana wale kwa kutojali nchi yao.
Lakini pia alitamka jambo ambalo sitaweza kulisahau maisha yangu yote. Alisema, na nadhani nitakuwa namnukuu, “Everyone in this blessed country is demanding his pound of flesh, everyone, including me!” (Kila mmoja katika nchi hii anadai ratili yake ya nyama, pamoja na mimi). Kama nimekosea kwa kutokuwa na ufasaha wa nukuu, naomba radhi, lakini angalau maudhui yalikuwa ndiyo hayo. (Anayetaka kujua chimbuko la maneno hayo kuhusu ratili ya nyama asome Mabepari wa Venisi, tafsiri ya Mwalimu ya Merchant of Venice, ya Shakespeare).
Papo hapo Mwalimu akatangaza kwamba anachukua hatua ya kujinyima kama mfano, kwa kupunguza mshahara wake kwa asilimia 20. Ninaelezwa kwamba mshahara huo wa Mwalimu aliendelea nao hadi anastaafu mwaka 1985. Sijui kama ni kweli au la, lakini muhimu ni ile ishara aliyotoa kama kiongozi.
Leo hii madaktari na wauguzi wamegoma wakidai maslahi yao yaboreshwe ili wafanye kazi katika mazingira bora na salama zaidi, wanatishiwa kufukuzwa, papo hapo tunapata taarifa kwamba wabunge wameanza kulipwa posho zilizokuwa zikilalamikiwa na waanchi wengi.
Inawezekana kabisa kwamba madaktari wamezidisha chumvi katika madai yao, sijui. Ninachojua ni kwamba wanafanya kazi muhimu kwa masiha yangu na wanajamii wengine wengi kuliko kazi inayofanywa na wabunge, hasa wabunge wa aina fulani ninayoiona mimi. Inaingiaje katika mantiki kwamba wakati tunawatisha madaktari kwamba tutawafukuza, wakati huo huo tunawalipa wabunge posho za kufanya kazi waliyoiomba?
Kama tunasema tutamuenzi Baba wa Taifa, hebu basi tumuenzi katika jambo hili tulilo nalo. Tukubali kwamba baadhi ya madai ya madaktari yanaweza kuwa ya msingi, lakini si yote. Waelezwe kwamba hata kama ni haki yao lakini madai hayo hayatekelezeki kwa sababu Serikali haina uwezo huo.
Papo hapo, Serikali ifanye kazi ya kuonyesha kwamba ni Serikali isiyokuwa na uwezo, kwa kukomesha matendo yote yanayoashiria ni Serikali nono iliyovimbiwa, ikiwa ni pamoja na kukomesha mara moja posho zisizo na maelezo za wabunge; magari-viwanda yanayowabeba watendaji wa serikali; tiketi za daraja la kwanza kwa mawaziri; posho mbili mbili wanazolipwa mawaziri wakisafiri nje na ndani ya nchi… na kadhalika. Kwa ufupi, maofisa wa Serikali waache kuwaibia wananchi wao, matajiri wao.
Kwa waanchi wanaowaangalia wakuu wa Serikali wanawaona kama vioja. Inawezekana vipi kusema huwezi kuwalipa watu wanaofanyakazi usiku na mchana na kisha ukawalipa wengine posho ambazo hazina kichwa wala miguu.
Inaelekea tunataka kuiga zile riwaya tulizozisoma tukiwa mbali, kwa sababu zilitokea katika nchi zilizo mbali nasi, lakini tujue kwamba hizi hazikuwa riwaya bali maafa halisi yaliyowapata wenzetu. Hatuna sababu ya kufanya kama wale majuha waliounda Titanic baada ya hadhari iliyotokana na riwaya ya Titan.
Maoni ya Wasomaji
Ni kweli serikali yetu
Ni kweli serikali yetu imevimbiwa sana na imeshaanza kujitapikia kwa kuonyesha dharau kwa madaktari wetu na kutojali gharama ambazo zimetumika kuwasomesha hawa madaktari. Viongozi wa serikali hawatumii huduma za hospitali zetu - wao na ndugu zao - wanapelekwa nje kwa gharama za walipa kodi kutibiwa magonjwa yanayotibika hapa nchini, ndio maana hawajali kuboresha sekta nzima ya afya.
Ila serikali ione aibu basi
Ila serikali ione aibu basi,siyo madaktari tu hata manesi,wakunga na wauguzi wengine.Hawa watu wanafanya kazi ngumu na ya hatari kwelikweli.wanaokoa maisha ya nguvu kazi ya nchi.
Hao wabunge wana matatizo,na hao wabunge waliokuwa na kiherehere cha posho tumewaona tunawasubiri 2015
Pinda,Makinda wanatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kupotosha wananchi(kuvujisha siri za serikali?)