Kampuni ya Bia Tanzania yashamiri kibiashara DSE

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo ni kampuni ya tatu kwa ukubwa wa mtaji kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) imeendelea kuongoza kwa idadi kubwa ya mauzo ya hisa tangia mwanzoni mwa mwaka huu.

Ripoti za soko DSE zimeonyesha kwamba, kampuni hiyo ambayo mwaka jana pia ilifanya vizuri, inayofanya biashara kubwa ya hisa ikilinganishwa na kampuni zote za ndani na nje ya nchi kwa wiki tatu mfululizo.

Katika kipindi hicho cha wiki tatu za mwanzo wa mwezi huu, hisa za TBL zimekuwa zikifanya biashara kwa asilimia zaidi ya 90 ya biashara ya jumla ya soko, hali ambayo ilichochea bei yake kuendelea kuwa imara.

Hata hivyo, pamoja na maendeleo hayo ya kibiashara, bei ya hisa za TBL zilipungua kuanzia mwanzoni mwa mwaka kwani wiki jana bei ya kufungia ilikuwa ni shilingi Tsh11,400 kwa hisa moja, kutoka shilingi Tsh12,000 za wiki iliyoishia Desemba 30, mwaka jana.

Katika kipindi cha wiki iliyopita, TBL iliongoza kwa biashara ya hisa kwa asilimia 79.7 ikifuatiwa na DSE kwa asilimia 11.7 na nafasi ya tatu ikashikiliwa na benki ya CRDB ambayo ilifanya biashara ya hisa kwa asilimia 7.3 ya biashara ya jumla ya soko.

Ripoti za DSE zimeonyesha kwamba, kati ya shilingi milioni 787 zilizopatikana kutokana na biashara ya hisa wiki iliyopita, mauzo na manunuzi ya hisa za TBL yalikuwa ni shilingi milioni 625.8, ambayo ni zaidi ya asilimia 90.

Biashara ya hisa ilichangamka siku za Jumatatu na Alhamisi za wiki jana  kwani zilichangia zaidi ya asilimia 80 ya mauzo yote ya soko kwa wiki iliyofanyiwa uchambuzi.

Hata hivyo, ripoti hizo zinaonyesha kwamba idadi ya hisa zilizokuwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa zilikuwa ni nyingi zaidi ya mahitaji ya kununua kutoka kwa wawekezaji mbalimbali wakiwemo wawekezaji wa ndani na wale kutoka nje ya nchi.

Katika kipindi cha wiki iliyopita, hisa nyingi zilizouzwa kwenye soko zilikuwa ni za wawekezaji kutoka nje ya nchi, na wanunuaji wengi wa hisa hizo pia walikuwa ni wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wawekezaji kutoka nje ya nchi, idadi ya wawekezaji wa ndani ilionekana kuongezeka wiki iliyopita, hasa siku za Jumatano na Ijumaa.

Katika siku hizo mbili za wiki, idadi ya hisa zilizokuwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa zilikuwa ni za wawekezaji wa ndani kwa asilimia 100 na asilimia kubwa ilinunuliwa na wawekezaji wa ndani ya nchi.

Kwa ujumla, bado idadi ya biashara ya hisa kwenye soko bado inachangiwa kwa kiasi kikubwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi kwani takwimu zimeonyesha kwamba bado wanashikilia soko kwa zaidi ya asilimia 90 kwa pande zote za kununua na kuuza.

Katika kipindi kuanzia Januari Mosi mwaka huu hadi Ijumaa iliyopita, kiasi cha shilingi bilioni 19.17 zilizopatikana kutokana na biashara ya hisa,  wawekezaji kutoka nje ya nchi walichangia kiasi cha shilingi bilioni 18.91.

Hali hii pia ilijionyesha kwenye robo ya mwisho ya mwaka jana ambapo kati ya shilingi bilioni 82.5 zilizopatikana kwenye mauzo na manunuzi ya hisa, wawekezaji kutoka nje ya nchi walichangia kiasi cha shilingi bilioni 78.4.

Kuwepo kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi inatokana na kuendelea kuimarika kwa thamani ya dola ya Marekani kwani wanaponunua hisa hupata hisa nyingi ikilinganishwa na kipindi ambacho fedha hiyo inaposhuka thamani yake.

Kwa mujibu wa ripoti za Benki kuu ya Tanzania (BoT) thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imefikia kiwango cha wastani cha Tsh2,260 mwanzoni mwa wiki hii, kutoka Tsh2,172 za mwishoni mwa mwezi Desemba, 2016.

Kwa mfano, mwekezaji mwenye dola 500 anayetaka kununua hisa za za kampuni yoyote kwa sasa ambapo thamani ya shilingi iko Tsh2,260, ana nafasi ya kupata hisa nyingi zaidi kuliko kipindi ambacho shilingi ilikuwa Tsh2,172.

Vilevile, pale thamani ya dola inaposhuka, wawekezaji wengi, hasa wale kutoka nje ya nchi huwa wanauza hisa zao kwa wingi kwani wanapobadilisha fedha wanazopata kuuza hisa zao kwenye dola, hupata ziada ya fedha.

Meneja wa bidhaa na masoko wa DSE Patrick Mususa alisema kwamba kwa ujumla mauzo ya hisa yalishuka wiki jana kwa asilimia 86 kutoka shilingi bilioni 5.5 za wiki ya awali hadi kufikia shilingi milioni 787 za wiki jana.

Idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa pia ilishuka kwa asilimia 15 hadi kufikia hisa 460,000 za wiki jana kutoka hisa 543,105 za wiki ya awali huku mtaji wa soko nao ukipungua hadi kufikia shilingi trilioni 18.7 wiki jana kutoka trilioni 19.1 za wiki ya awali.

Mususa alisema kwamba mtaji wa kampuni za ndani ulibaki kwenye kiwango kile kile cha shilingi trilioni 7.5 kutokana na kutokuwepo na mabadiliko yoyote ya hisa katika kipindi hicho.

Kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa katika soko (DSEI) kilipungua kwa pointi 51 kutokana na kupungua kwa bei ya hisa mbalimbali zilizopo sokoni na kiashiria cha kampuni za ndani kilibakia kwenye wastani wa awali wa Tsh3,550.

Kwa mujibu wa DSE, kiashiria cha sekta ya viwanda (IA) kilibakia palepale kwenye wastani wa Tsh4,508 wakati kile cha sekta ya huduma za kibenki na fedha (BI) nacho kikiwa hakikubadilika.

Ripoti za kila siku za soko zimeonyesha kwamba bado kuna idadi kubwa ya hisa zilizoko sokoni kwa ajili ya kuuzwa ikilinganishwa na mahitaji wa wawekezaji wanaotaka kununua.

Wawekezaji wanaouza hisa kwa wingi katika kipindi hiki kwa mujibu wa ripoti za DSE ni wale wa CRDB Bank, DCB Commercial Bank, DSE, NBM Bank, TBL, Swala, Mkombozi Commercial Bank, Mwalimu Bank na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC).

Hata hivyo, wawekezaji wengi katika soko bado wanapendelea zaidi hisa za CRDB, DSE, NMB, TBL, TOL Gases na Simba Cement. CRDB bado inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha hisa zinazopelekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa.

Raia Mwema imegundua kwamba, pamoja na kuanza kuchangamka kwa soko idadi ya hisa zinazonunuliwa kwenye soko  katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka ni chini ya asilimia 20 ya hisa zote zilizoko sokoni kwa ajili ya kuuzwa.

Pamoja na kuwepo na idadi ndogo ya wawekezaji, hasa wa ndani ya nchi, kumekuwepo na ongezeko la biashara ya hati fungani kwani kwa wiki jana ziliongezeka mara 90 ikilinganishwa na wiki ya awali.

Kuongezeka kwa kiu ya wawekezaji kwenye hati fungani inatokana na kuongezeka kwa viwango vya riba za mikopo hiyo ya serikali kutoka asilimia 17 za mwezi Desemba hadi asilimia 18 za wiki iliyopita.

Uchambuzi wa soko kwa mwaka 2016 uliofanywa na mtandao wa African- Markets umeonyesha kwamba kwa mwana jana hali ya soko haikuwa nzuri na kwa ujumla viashiria vyote vya soko havikubadilika.

“Mwaka 2016 ulikuwa mwaka wa misukusuko na mwaka wa kihistoria kwa DSE kwani ulikuwa ni mgumu kutengeneza pesa kwenye soko,” mtandao huo umesema kwenye ripoti zake.

Imeelezwa kwamba, katika kipindi cha mwaka jana, bei ya hisa za kampuni za ndani zilipungua na hatua hii ilisababisha kushuka kwa mtaji wa kampuni za ndani kwa shilingi trillion 1.3.

African-Markets imebainisha kwamba kwa mwaka huu, biashara ya soko kwa mwaka huu itategemea sana sera za kiuchumi za serikali lakini ongezeko la kampuni hasa za simu na mawasiliano zitaongeza mtaji na shughuli za kibiashara nah ii itaongeza mauzo na mapato kwa DSE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *