Kampuni zaidi ya elfu 76 hatarini kufutwa, Tanesco na TBL ni miongoni – Brela

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ni miongoni mashirika ama kampuni zaidi ya 76,300 zilizoko hatarini kufutwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Utoaji Leseni Tanzania (BRELA).

Mashirika ama kampuni hizo zaidi ya 76,300, kwa mujibu wa taarifa ya Brela, yameshindwa kuwasilisha taarifa zao za mapato katika baadhi ya miaka ya uendeshaji, kinyume cha masharti ya Brela.

“Kampuni iliyosajiliwa nchini Tanzania ina wajibu wa kuwasilisha kwa Msajili wa Kampuni (BRELA) marejesho ya mwaka (annual returns), kila mwaka, yakiambatana na hesabu za kampuni zilizokaguliwa na kupitishwa na mkaguzi, chini ya vifungu 128(1) na 132(1) vya Sheria ya Kampuni (Sura 212).”

“ Aidha matawi ya kampuni za kigeni zilizoandikishwa nchini Tanzania pia yanapaswa kuwasilisha hesabu za mwaka (annual accounts) kila mwaka, chini ya kifungu 438(1) cha sheria hiyo.

“Kutokuwasilisha kwa taarifa na nyaraka hizo ni kosa kisheria ambalo linaweza kusababisha kampuni husika kufutwa, wamiliki na wakurugenzi wake kufikishwa mahakamani au vyote viwili kwa pamoja,” inaeleza taarifa ya BRELA iliyoko kwenye tovuti yake rasmi.

Kutokana na makosa hayo, kampuni na mashirika hayo yamepewa miezi mitatu kurekebisha kasoro hizo. Muda huo wa miezi mitatu unaanza Februari 8, mwaka huu (2017) na itakapofika Mei 8, mwaka huu, kampuni ama shirika lolote ambalo halitakuwa limekidhi masharti litachukuliwa hatua hizo za kisheria.

Mbali na Tanesco pamoja na TBL, kampuni ama mashirika mengine katika orodha hiyo ni pamoja na Mtibwa Sugar Estate Limited, Kilombero Sugar Company, Caltex Oil Tanzania Ltd na Unilever Tanzania Ltd.

Nyingine katika orodha hiyo ni pamoja na The Salvation Army Ltd, General Book Sellers Ltd, Shirika la Usafiri Dar e s Salaam Limited, The Dar es Salaam Printers Ltd, Tanganyika Packers Ltd, Mwanza Textile Company Limited, Tanganyika Motors Ltd na Kilimanjaro Timbers Company Limited. Katika orodha hiyo pia zimejumuishwa Ipinda Rice Mills (1992) Ltd, Mtwara Salt Works Ltd na Burka Coffee Estates Ltd.

                                                                                         

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *