- Ni muumini wa siasa za kunganisha wananchi, achukia majungu
- Avihamasisha vyombo vya habari kuibua maovu
- Amtaka Mkurugenzi Mbeya, asibabaike na wezi, atamlinda
KUWASILI kwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Mbeya, Abass Kandoro, kumefungua ukurasa mpya unaotoa matumaini kwa wakazi wake na kufunga ukurasa wa siasa za kibabe, majungu na vitisho zilizodumu kwa takribani miaka mitano.
Tofauti za kiutawala kwa vipindi hivi viwili zimejibainisha katika utendaji wa Kandoro tangu alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kuongoza mkoa huu pamoja na tukio la juma lililopita katika hafla ya kumkaribisha na kumuaga mtangulizi wake, John Mwakipesile, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo ya kumuaga, Mwakipesile alidhihirisha hasira zake dhidi ya baadhi ya wanahabari mkoa hapa, hususan wanaoandikia magazeti.
“Wale ambao walinichukia na walionyesha chuki zao openly walinisaidia sana, wengine niliambiwa waliapa kutoandika mazuri yangu, waliapa kuniandika vibaya, walinisaidia sana kuchapa kazi na wao kuonekana wapumbavu, sina chuki nao,” alisema Mwakipesile na kuongeza, “Sasa mabadiliko yamepatikana na mabadiliko yoyote yanazaa hisia za woga na hofu, lakini mabadiliko yanaleta fursa mpya.”
Utawala wa Mwakipesile uliwagawa waandishi wa habari katika makundi mawili. Kwanza, ni kundi la wateule wachache na pili ni kundi alilolibanisha mwenyewe kuwa halimpendi na kutotaka kufanya nalo kazi.
Kandoro na vyombo vya habari
Mwakipesile akiwagawa wanahabari hao, Kandoro kwa upande wake ameeleza mtazamo wake wenye muelekeo wa kuwaunganisha watu na si kuwagawa.
Akizungumza mara baada ya mtangulizi wake, Kandoro aliweka bayana imani yake kwa wanahabari akisema; “Ninachowapenda waandishi wa habari huwa hawapendi kumsingizia mtu, bali hutoa habari zenye changamoto kwa viongozi kuzifanyia kazi.”
Katika kuthibitisha kauli yake hiyo, Kandoro amepanga kwenda Lupa kufuatilia kiini cha tatizo la maji kama lilivyoibuliwa na wanahabari mkoani hapa, walipoweka kambi ya siku mbili katika Wilaya ya Chunya, juma lililopita.
Tatizo la maji linalowakabili wananchi wa Lupa linatokana na visima vilivyochimbwa na serikali kutotoa maji, lakini kinachoshangaza zaidi ni pale visima vilivyochimbwa na watu binafsi kutoa maji na wananchi hutozwa kati ya Sh 200 hadi 500 kwa chombo (dumu) cha lita 20.
Mtindo anaoutumia Kandoro kufuatilia changamoto zinazoibuliwa na wanahabari unaonekana kuwahamasisha zaidi kuingia vijijini kuendelea kuibua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kauli ya Kandoro na hatua yake kufuatilia changamoto zinazoibuliwa na wanahabari inathibitisha kile alichokifanya mara baada ya kuwasili mkoani hapa, ambapo alitembelea ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya (MBPC) mapema mwezi huu, ziara iliyoashiria utayari wake katika kushirikiana na wanahabari wote habari bila ubaguzi.
Kandoro anakuwa Mkuu wa Mkoa huo wa kwanza kufanya ziara ya utambulisho kwa wanahabari mkoani hapa, hatua inayotafsiriwa na wanahabari kuwa ni mwisho wa uhasama uliotokana na majungu yaliyotawala utawala uliopita kati ya uongozi wa mkoa dhidi ya wanahabari pamoja na wabunge wa mkoa huo.
Miongoni mwa watu waliokumbana na rungu la Kandoro mkoani humo ni wale wanaoishi kwa majungu ambapo amewatumia salamu rasmi kwamba hapendi majungu na kubainisha kuwa humkosesha raha.
“Mtu akija ofisini kwangu kuleta majungu sitaweza kumsikiliza lakini siwezi kumfukuza kwa sababu nitamwonea aibu, ila nitamhurumia kwa kupoteza muda wake kwani sitofanyia kazi majungu,” alisema Kandoro akipeleka salamu za wazi kwa wapika majungu mkoani humo.
Msimamo wake kuhusu majungu aliutoa pia katika kikao chake na wazee wa mkoa huo wakiwemo viongozi wa kijadi, machifu, ambapo aliwaeleza kuwa sifa ya msingi ya kiongozi ni kuwaunganisha watu wake.
“Sifa kubwa ya kiongozi ni kuwaunganisha, sio kutenganisha watu, ukiona kiongozi anatenganisha watu huyo sio kiongozi ni mbabaishaji,” alisema Kandoro.
Mkurugenzi wa Jiji Mbeya apewa meno
Katika hatua nyingine, Kandoro amewataka viongozi wa Jiji la Mbeya kutotegemea hisani hisani kutoka kwake na kwamba wasahau kufanikisha njama zao za kumng’oa Mkurugenzi wa Jiji hilo, Juma Iddi.
Kandoro alitoa msimamo huo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kilichokuwa kikijadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Kwa mujibu wa Kandoro, anazo taarifa kuhusu njama za kumng’oa Mkurugezi huyo, ambaye kwa watendaji hao amewazibia mianya ya wizi wa fedha.
Mkurugenzi huyo aliwasili kuanza majukumu yake hayo mkoani Mbeya, Oktoba, mwaka jana na kati ya mafanikio yake ni kupandisha makusanyo ya fedha, kutoka chini ya Sh. bilioni mbili kwa mwaka wa fedha uliokwisha, hadi Sh. zaidi ya bilioni saba, kufikia Juni mwaka huu.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/2012, Jiji la Mbeya limepanga kukusanya zaidi ya Sh. bilioni 11, ufanisi ambao umempa sifa mkurugenzi huyo.
Kutokana na ufanisi wa mkurugenzi huyo, wakazi wengi mjini hapa wamewekeza matumaini yao kwake, tofauti na awali ambapo matumaini hayo yaliwekezwa zaidi kwa mbunge.
Kutokana na wizi mkubwa wa mapato uliokuwapo awali kiasi cha Halmashauri ya Jiji kupachikwa jina la “shamba la bibi,” miradi mingi ya maendeleo utekelezaji wake haukuwa wa kuridhisha hadi Jiji kupewa hati yenye mashaka kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
“Idd umefanya kazi kubwa ya kuziba mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma lakini kazi hiyo ina lawama nataka uendelee na moto huo huo, usiogope hizo lawama na sisi tutakulinda kwa ajili ya maslahi ya wananchi,” alisema Kandoro akimhakikisha usalama wake mkurugenzi huyo.
“Kama kuna mtu mwenye mpango wa kumpiga vita mkurugenzi huyu kwa sababu ya kazi yake ya kuziba mianya ya ubadhirifu wa fedha namuamuru aache mara moja kwani sisi tutamlinda na hatutakubaliana na vita hiyo,”alisema Kandoro.
Katika siku za hivi karibuni kundi linaloaminika kuhusika na wizi wa mapato ya Jiji la Mbeya limeanzisha vita ya chini chini dhidi ya Mkurugenzi huyo likidai kuwa anaendesha Jiji kutokea msikitini, madai ambayo tayari yamebezwa na wananchi wanaoamini kuwa ni vita inayotokana na Mkurugenzi huyo kuwadhibiti wezi wa fedha zao.
Pamoja na wizi wa fedha za jiji, uongozi wa jiji hilo uliokuwepo kabla ya Iddi ulibariki kuvuruga mipango ya matumizi ya ardhi jijini humo likiwepo eneo la Iwambi lililopangwa uwe mji mpya (satellite town) ya jiji.
Hata hivyo taarifa za ndani ya idara hiyo ya ardhi zinabainisha kuwa viongozi walitanguliza maslahi binafsi na kuvuruga mpango huo, viwanja vikagawiwa kwa shinikizo, wengi wao wakijilimbikizia zaidi ya kiwanja kimoja. Kutokana uvurugaji huo, baadhi ya watu wanadhihaki wakiita “satellite squatter.”
Maeneo mbalimbali ya jiji yamegawiwa kiholela yakiwamo maeneo yenye makorongo ambayo awali yaliachwa wazi. Eneo jingine linaloendelea kumegwa kiholela ni lile lililotengwa kwa ajili ya kujengwa Ikulu ndogo ya mkoa.
Baadhi ya wakazi jirani na eneo hilo maarufu kwa jina la Ikulu wameonyesha hofu yao kwamba eneo hilo litavamiwa lote ndani ya muda mfupi ujao kutokana na hatua ya kuendelea kumegwa na kutumiwa kinyume cha mipango ya awali.
Kandoro ameanza kazi mkoani hapa akitumia mtindo wa uongozi unaounganisha watu, kupiga vita majungu, kusimamia utii wa sheria na kusimamia utamaduni wa watu kufanya kazi halali. Katika siku zake za awali kiuongozi, Kandoro amekwishatoa matumaini mapya kwa wakazi wa Mbeya.
Toa maoni yako