Karamagi ahoji nisaidie nini?

MMOJA wa vigogo waliotajwa na Rais John Magufuli kuwa anatakiwa kuhojiwa na vyombo vya dola kuhusu mikataba ya madini, Naziri Karamagi, ameibuka na kudai kwamba hadi sasa hajui anatafutwa asaidie kitu gani kwenye sakata hilo.

Katika mazungumzo yake na Raia Mwema, Jumanne wiki hii, Karamagi alisema taarifa za kutakiwa kuhojiwa na vyombo vya dola kuhusu ushiriki wake katika inayodaiwa kuwa hasara ambayo Tanzania imepata katika sekta ya madini, amezipata kupitia magazeti na mitandao ya kijamii na hajui zaidi ya hapo.

“Nashukuru sana kwa kunitafuta. Habari na mimi nimezipata kwenye magazeti na mitandaoni na sijajua hasa ni kitu gani nahitajika kumsaidia Rais kufikia azma yake ya kurekebisha sekta ya madini. Nikishakujua hilo, mimi mwenyewe nitakutafuta,” alisema Karamagi.

Karamagi alikuwa waziri wa Nishati na Madini wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na ndiye aliyekuwa waziri wakati serikali ikiingia mkataba mpya wa mgodi wa Buzwagi ulioleta matatizo bungeni katika wakati wake.

Katika hotuba yake ya Jumatatu wiki hii, baada ya kupokea Ripoti ya Kamati ya Makinikia II iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro, Rais John Magufuli, alimtaja hadharani Karamagi akidaiwa kuwa mmoja wa watu wanaotakiwa kuhojiwa na vyombo vya dola kutokana na uhusika wake huo.

Ripoti hiyo ya Makinikia, pamoja na mambo mengine, ilieleza matatizo chungu nzima ya sekta hiyo, ikiwamo kwamba Taifa limepoteza mapato ya takribani shilingi trilioni 108 katika kipindi cha kati ya mwaka 1998 hadi mwaka huu, kutokana na uzembe wa usimamizi wa sekta hiyo.

Karamagi alikuwa mmoja wa vigogo 10 waliotajwa na ripoti; wakiwamo mawaziri wengine waliopita wa wizara hiyo, waliowahi kuwa wanasheria na washauri wa kisheria wa serikali pamoja na watu waliowahi kuwa makamishina wa madini katika kipindi chote cha upotevu huo.

Hayo yakiendelea, juzi usiku, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alitoa taarifa kwamba watu wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo ya Profesa Osoro hawatatakiwa kusafiri kwenda nje ya nchi katika kipindi hiki ambacho vyombo vya dola vitaanza kazi zake.

Orodha hiyo ya vigogo inahusisha watu maarufu kama vile Andrew Chenge, William Ngeleja, Dk. Peter Kafumu, Julius Malaba, Sazi Salula, Paul Masanja, Maria Kejo na  Johnson Mwanyika.

Kulinganisha na Ripoti ya Makinikia I, katika ripoti ya Osoro jambo moja kubwa limeibuka ambalo linahusu uhalali wa Acacia kufanya biashara yake nchini ilhali ikidaiwa haijasajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara nchini (BRELA).

Mmoja wa wanasheria wabobezi katika eneo la madini nchini, Dk. Rugemeleza Nshalla, aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu kwamba Acacia wanafanya shughuli zao kupitia kampuni zilizosajiliwa hapa nchini.

Kwa mfano, alisema mgodi wa Bulyanhulu unaendeshwa na kampuni ya Bulyanhulu, ule wa Buzwagi unaendeshwa na kampuni ya Pangea wakati ule wa North Mara unaendeshwa na kampuni ya North Mara.

“Ni jambo la kawaida kwa kampuni hizo kuanzisha kampuni nyingi kwa ajili ya kurahisisha mambo yao. Unaweza kukuta Acacia haijasajiliwa lakini zile za ndani zimesajiliwa.

“Nisichokipenda mimi ni kwamba linapokuja suala kama la sasa, unakuta Acacia ndiyo inakuwa msemaji wa kampuni hizi za hapa. Sasa kama wanataka, si wasajili hapa na hiyo Acacia yao?” alihoji.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi, alisema ameisoma ripoti yote ya Osoro na akasema mambo ya msingi yanafahamika lakini suala la Acacia linaweza kupata maelezo ya kisheria.

“Ngoja nikwambie, kwenye biashara kuna jina la biashara na alama ya biashara. Acacia imesajiliwa huko ilikosajiliwa lakini inaweza kutumia hilo jina ambalo ni alama yake hapa bila kuathiri kampuni zinazofanya kazi zake hapa.

“Kwa mfano, watu wengi wanajua kwamba Vodacom ndiyo inamiliki M-Pesa lakini ukweli ni kwamba huduma za M-Pesa zinaendeshwa chini ya kampuni tofauti kabisa inayojulikana kama M-Pesa Limited. Nadhani hata Azam inaweza kuwa mfano mzuri,” alisema.

Kwa upande wake, waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, ametia mkono katika suala hilo akisema kinachotakiwa sasa ni kuyaweka mambo ya rasilimali chini ya ulinzi wa Katiba.

“Ni wajibu wa kila mtu kulinda mali za umma. Baada ya kamati hizi mbili, matatizo yote yanaonekana wazi wazi na hasa katika suala la mikataba na si mikataba tu ya dhahabu bali maliasili yetu yote.

“Kuna udhaifu katika mikataba na usimamizi wa mikataba. Kwenye hili suala tunapambana na watu wazito lakini ni pia hili ni suala la kitaifa. Pamoja na matatizo ya miaka ya nyuma tukubali kwamba ni suala la ulinzi wa rasilimali za nchi ni letu sote. Tuungane.”

Warioba pia alizungumzia tatizo la maadili ambalo vile vile lilijitokeza katika maoni ya wananchi wa Tanzania wakati wa ukusanyaji maoni yao kwa ajili ya mchakato wa kuandika Katiba Mpya chini ya usimamizi wa Tume ya Katiba aliyoiongoza akiwa mwenyekiti.

Kuhusu maadili alisema; “Tatizo la maadili ni kubwa sana. Hili suala lilizungumzwa na wananchi, kubadili sheria pekee hakutoshi kinachotakiwa kufanywa sasa ni kuhakikisha suala la misingi ya kulinda rasimali na maadili iwekwe kwenye katiba ya nchi, liwe suala la kikatiba.

Hisa za Acacia

Wakati sakata la makinikia likiendelea, hisa za kampuni hiyo zimekuwa zikiporomoka katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kutoka kiwango cha juu cha shilingi 13,000 miezi michache iliyopita hadi wastani wa shilingi 8,000 kufikia jana.

Hata hivyo, wakati ripoti ya kwanza ya makinikia iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ilipokabidhiwa kwa Rais Magufuli mwezi uliopita, thamani ya hisa za Acacia zilishuka kwa asilimia 40 lakini baada ya ripoti ya Profesa Osoro, hisa zimeporomoka kwa asilimia 13 tu.

Wakati wa shughuli za ununuaji na uuzaji wa hisa zilizofanyika DSE jana asubuhi hadi mchana, bei ya kufungua soko ilikuwa pauni 264 kwa hisa lakini mpaka soko linafungwa bei ilikuwa pauni 261.

Mwisho wa yote ni nini?

Raia Mwema limezungumza na mmoja wa wabobezi wakubwa katika sekta ya madini ambaye aliwahi kushiriki katika mojawapo ya tume zilizoundwa katika miaka ya nyuma ambaye alisema jambo hili linapaswa kuchukuliwa kwa umakini.

Alisema njia pekee ya jambo hili kumalizika kwa usalama ni kwa serikali na Acacia kushirikiana katika kujenga mtambo wa uchenjuaji wa madini hapa nchini na kuziba upungufu uliokuwepo huko nyuma.

“Mwisho wa hili ni nini? Ipo hatari ya marais wastaafu kuletwa mahakamani kutoa ushahidi. Sasa marais wastaafu wakiitwa na kuzungumza mwisho wake ni nini? Mimi naunga mkono juhudi za Rais lakini lazima tuangalie mwisho wa haya.

“ Ni lazima itafutwe kitu kinaitwa win-win situation. Wawekezaji waone wametendewa haki na serikali pamoja na Rais Magufuli ni lazima nao waone juhudi zao zimezaa matunda. Ikipatikana win-win mapema, itaepusha mengi,” alisema.

Mapendekezo ya Kamati ya Makinikia II

Jambo jingine katika hitimisho la sakata hili ni mapendekezo ya kamati ya makinikia II. Mapendekezo hayo ni pamoja na serikali, kupitia BRELA ichukue hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Acacia Mining Plc ambayo imekuwa inaendesha shughuli zake nchini kinyume na matakwa ya sheria. 

Serikali idai kodi na mrahaba kutoka kwa makampuni yote ya madini ambayo yamekwepa kulipa kodi na mrahaba stahiki kwa mujibu wa sheria. 

Serikali iendelee kuzuia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi mpaka hapo kampuni za madini yanayodaiwa zitakapolipa kodi, mrahaba na tozo stahiki kwa mujibu wa sheria. 

Serikali ianzishe utaratibu utakowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia (smelter) ili kuondoa upotevu wa mapato na kutengeneza ajira kwa watanzania. 

Serikali ifanye uchunguzi  na kuchukua hatua za kisheria  dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria wakuu wa serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba, na makamishna wa madini, wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini na watumishi wengine wa serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia (Freight Forwarders (T) Ltd na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.  

Serikali ifute utaratibu wa kupokea malipo ya mrahaba ya asilimia na kusubiri malipo ya asilimia 10 kulipwa baadaye wakati kampuni hizo za madini huuza madini hayo na kupewa  fedha taslimu kwa mkupuo. 

Serikali ifanye uchunguzi kuhusu mwenendo wa watumishi wa idara ya walipakodi wakubwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kushughulikia madai ya kodi ambayo Mabaraza ya Rufani ya Kodi na Mahakama zimekwisha yatolea uamuzi na vilevile ichunguze mienendo ya watumishi wa mabaraza ya kodi kwa kutotolea uamuzi kesi za kodi kwa muda mrefu kuhusu mashauri yaliyochukua muda mrefu kukamilika katika vyombo hivyo. 

Benki Kuu ya Tanzania ifuatilie malipo ya fedha za kigeni yanayotokana na mrahaba kwa mauzo ya madini.   

Serikali ianzishe utaratibu wa kulinda maeneo ya migodi na viwanja vya ndege vilivyop migodini ili kudhibiti vitendo vya hujuma vinavyoweza kuwa vinafanywa na kampuni za migodi ikiwemo utoroshaji wa madini. 

Sheria iongeze kiwango cha adhabu zilizoainishwa kwa makosa ya ukiukwaji wa Sheria ya Madini na Sheria za Kodi. 

Serikali kupitia wataalamu wabobezi katika majadiliano na mikataba (expert in negotiation and contract) wapitie mikataba yote mikubwa ya uchimbaji madini (review) na kufanya majadiliano na kampuni za madini ili kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija kwa taifa na badala yake kuweka masharti yenye tija kwa pande zote mbili kwa kuzingatia maslahi ya nchi; 

Sheria iweke kiwango maalumu cha asilimia ya hisa ambazo zitamilikiwa na serikali katika kampuni zote za madini nchini. Aidha, sheria ielekeze serikali kufanya majadilaino ili kuwezesha kununua hisa katika kampuni za uchimbaji madini ili kuiwezesha kupata mapato zaidi na ushiriki katika uamuzi mbalimbali muhimu kwenye biashara ya madini. 

Serikali iunde chombo cha kusimamia biashara ya usafirishaji bidhaa nje ya nchi kupitia bandari kama ilivyokuwa shirika la NASACO ili kudhibiti biashara haramu na kuondoa mianya ya ukwepaji kodi.  

Sheria itamke bayana kuwa madini ni mali asili ya Watanzania na iwekwe chini ya udhamini na uangalizi wa Rais kwa manufaa ya Watanzania.        

Sheria itamke bayana kuwa mikataba yoyote ya uchimbaji mkubwa wa madini (Mining Development Agreement) isiwe ya siri na lazima iridhiwe na Bunge kabla ya kuanza kutekelezwa. 

Sheria itoe masharti ya wazi ya kuzingatiwa na iondoe uhuru wa mamlaka ya (discretionary powers) Waziri wa Nishati na Madini, kamishna wa madini na maafisa madini wa kanda katika utoaji wa leseni za uchimbaji madini.  

Sheria ya madini iweke masharti kwamba mwombaji wa leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini lazima aoneshe mchanganuo wa kina kuhusu namna mafunzo kwa wazawa yatakavyotolewa kwa lengo la ajira kama wataalamu na kuchukua nafasi za uendeshaji wa migodi husika na kupunguza au kuondoa kabisa wataalamu kutoka nje ya nchi.  

Sheria ielekeze kampuni za madini kuweka fedha zinazotokana na mauzo ya madini katika benki zilizopo nchini ili kuimarisha uchumi wa nchi na kuondoa mianya ya ukwepaji wa kodi na tozo mbalimbali. 

Serikali ipitie na kufanya marekebisho au kufuta na kubadili kabisa Sheria ya Madini na Sheria za Kodi ili kuondoa pamoja mambo mengine, masharti yote yasiyokuwa na manufaa kwa taifa ikiwa ni pamoja na masharti yaliyomo kwenye kifungu thabiti (stability provision). 

Serikali igharimie na kutoa mafunzo kwa watumishi wa serikali ili kuwapatia uelewa na weledi katika nyanja ya majadiliano na uendeshaji wa mashauri yatokanayo na mikataba ikiwemo ya mikataba ya madini (skills in negotiation and arbitration). 

Serikali kupitia kamishna wa madini iwe inafanya ukaguzi wa mara kwa mara  kwa kampuni za madini ili kujihakikishia uzingatiaji au ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji na kuchukua  hatua ipasavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *