
HALI ya vitisho imeendelea dhidi ya baadhi ya viongozi wa dini nchini, ambao wamejitokeza kufichua siri za magenge yasiyo na maadili kitaifa yanayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya baadhi ya viongozi na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, Raia Mwema, imeelezwa.
Mmoja wa viongozi hao wa dini ni Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ambaye wiki iliyopita, aliwaeleza vijana wa kanisa hilo aliokutana nao jijini Dar es Salaam kuwa, naye amekuwa akifanyiwa njama za kunyamazishwa ili asiharibu maslahi ya genge la wafanyabiashara ya dawa za kulevya.
Katika hali isiyo ya kawaida, Kardinali Pengo aliwaeleza vijana wa kanisa hilo katika misa maalumu ya ufukweni inayowakutanisha vijana kila mwaka jijini Dar es Salaam kuwa kumekuwa na kundi la watu wanaoamini anaharibu mwenendo wa mipango yao katika biashara kulevya.
Kutokana na hali hiyo, Pengo aliwaonya vijana kutoendelea kutumika kama ambavyo baadhi yao wamekuwa wakitumika kwa muda mrefu katika biashara hiyo. Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya wahusika wa genge hilo ambalo ameeleza kuwa wamekuwa na mipango ya kumnyamazisha.
Kwa mujibu wa Pengo, stahili wanayotumia kutaka kumnyamazisha ni pamoja na kutaja jina lake katika orodha ya wafanyabiashara ya dawa za kulevya, hali ambayo amesema haitamnyamazisha na badala yake ataendelea kuzungumza kufichua ukweli kuhusu wahusika katika biashara hiyo haramu.
Aliwataka vijana kutukubali kutumika kwa manufaa ya baadhi ya watu hao wachache ambao kwa sasa wameonyesha mwenendo wa kuchukizwa na watu wengine wanaowakosoa.
“Ninyi vijana msikubali kutishwa,” alieleza Kardinali Pengo na kuweka bayana kuwa watenda maovu wakiwamo wanaouza dawa za kulevya wako radhi kuwatumia vijana kufanikisha malengo yao huku wakiwa tayari kuwatishia viongozi wa dini wanapojaribu kukemea uovu wao huo.
Aliwahimiza vijana kupingana na magenge wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya akisema; “Mnao uwezo wa kuwa askari kupigana nao, silaha yenu si bunduki bali ni ukweli.”
Kauli hiyo ya Kardinali Pengo imekuja miezi kadhaa baada ya kuwapo kwa malumbano kati ya baadhi ya viongozi wa dini na Serikali, kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete, alipowaomba viongozi wa dini kusaidi vita dhidi ya dawa za kulevya.
Katika mwendelezo wa kauli hiyo ya Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, aliwahi kuwaonyesha wabunge picha za video zinazoonyesha baadhi ya wahusika wa dawa za kulevya, wakiwamo baadhi ya viongozi wa dini wa baadhi ya makanisa yasiyo maarufu nchini.
Katika hatua nyingine Padre wa Kanisa Katoliki nchini, Baptist Mapunda, wa Parokia ya Manzese Dar es Salaama, amezungumza na gazeti hili na kumtahadharisha Rais Jakaya Kikwete, kuchukua hatua za haraka kunusuru amani ya nchi iliyopo shakani kutokana na sababu mbalimbali.
“Katika kipindi hiki tatizo la udini limezidi kuwa kubwa sana, kuna makundi yameibuka kutukana dini nyingine hadharani, kauli za kutishia amani za wanasiasa, polisi kupiga raia, ubambikizaji kesi, wananchi kuchukua sheria mkononi, hivi vyote ni viashiria hatari sana kwa amani ya nchi, ninapata shaka,” alisema Padri Mapunda.
Katika kile kinachoonyesha kuwa hali ya kutiliana shaka baina ya viongozi wa dini na viongozi wa serikali, hivi karibuni Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela, aliwataka viongozi wa dini kuendelea kukosoa Serikali katika hali ya staha.
Maoni ya Wasomaji
Namuunga mkono Padre Mapunda
Namuunga mkono Padre Mapunda kwa alichokisema. Hadi sasa, kuna tatizo kubwa la udini linaloendelea, na kuna mikakati mizito inasukwa sehemu za kuabudia. Mbaya zaidi viongozi wa serikali wanatumia rungu hilo kama mwanya wa kuendelea kubaki madarakani. Kwa sasa viongozi wa dini wanatumiwa kama chambo kuwawezesha watawala waendelee kuwa madarakani. Hata suala la urais kwa sasa unaamuliwa kwa misingi ya dini, na kama hamuamini, fuatilieni matamko ya waislam wa Mwanza. Mi naamini, kwa taifa hili hatutapata kupona hadi hapo viongozi wa dini za kikristo na wale wa kiislam watakapokubali kukaa meza moja na kumaliza tofauti za dini zao, hasa zile zenye mwelekeo wa kisiasa. Matatizo ya nchi hii yangeweza kutatuliwa kama viongozi wa dini wasingetanguliza maslahi ya dini zao. Wakumbuke kuwa serikali inatumia ule ule mfumo wa Kikoloni wa Divide and Rule (D & R) na kwa kiasi kikubwa wanafanikiwa sana hapa tanzania. Chonde chonde viongozi wetu wa dini, jaribuni kukaa meza moja kwa majadiliano yatakayozaa muafaka wa dini zote. Naam na Mungu tunayemwabudu awatangulie katika hilo.
kwa mtazamo wangu mimi naona
kwa mtazamo wangu mimi naona viongozi wa dini kazi yenu ni kufichua maovu ndani ya jamii especially serikari viongozi wa dini msiogope songa mbele mungu yuko nyuma yenu muokoe taifa letu.