Kibanda si wa kwanza, natamani awe wa mwisho

BAADA ya makala yangu ya wiki iliyopita, nimepokea vitisho vingi na laana kuwa ninachochea udini. Mmoja ameapa kuwa atanitafuta popote ili anifanye kama alivyofanywa Absalom Kibanda. Kosa langu kubwa, anadai nimezusha kwa kudai kuwa dini na kabila la Kibanda vimechangia kutekwa na kuumizwa kwake.

Nimeirudia mara nyingi makala ile na sikufanikiwa kuona nilipoteleza. Ni kweli Kibanda ni mwana habari, ni kweli Kibanda ni Mnyakyusa, na ni kweli Kibanda ni Mkristo. Hoja ya kwamba vigezo hivi vitatu vimechangia katika mateso yake na watu “wasiojulikana”, nimeieleza kwa kina katika makala ile japokuwa inahitaji msomaji atulie na kuiacha akili ifanye kazi kuliko jazba.

Asiyekubaliana nami kwa hoja niliyoijenga, anayo ruksa kutuhakikishia ni kwa nini Kibanda aliteswa na kuachiwa kilema cha kudumu. Wakati ambapo nauchukia udini na ukabila, nachukia kupita kiasi vitendo vya utekaji na uuaji wa watu wanaodhaniwa ni wapinzani wa mfumo dhaifu tuliouchagua wenyewe.

Vitendo vya kuteka, kutesa na hata kuua watu katika mazingira ya kutatanisha lazima vitafutiwe ufumbuzi na tafsiri kwa nini vinatokea na kukaliwa kimya na mamlaka husika. Wanaopingana nami watuambie sasa ikiwa Kibanda si mwana habari, si Mnyakyusa na si Mkristo. Wakimaliza, watueleze ni kwa nini walimfanyia hivyo au kwa nini alifanyiwa vitendo hivyo vya kinyama.

Uchochezi haufanywi na wanaoandika kuwa kuna udini, ukabila na uhasama kati ya watawala na wana habari. Uchochezi unafanywa kwanza na ndipo unaandikwa. Tukubaliane kimsingi hata kama inauma kuwa, “mjumbe hauawi”.

Tukumbushane machache kwa faida ya wanaojifanya kusahau. Utekaji na mauaji yanayofanywa kwa misingi ya uhalifu wa kawaida, huwa haichukui muda mrefu kubaini wahalifu hao. Tumewahi kuona wahalifu wakikamatwa ndani ya saa 24 tena wakati Jeshi la Polisi likiwa halina vifaa wala mitandao kama ilivyo sasa.

Hatujasahau mauaji ya wakili Kapinga yaliyotokea katika lango la kuingilia nyumbani kwake huko Mbezi. Wauaji hao walikamatwa na kufunguliwa mashtaka. Juzi juzi tumeona mauaji ya Kamanda Barlow huko Mwanza. Hata kama kulikuwa na harufu ya misigano ya kimaslahi ndani ya jeshi la polisi lakini haikuchukua muda wahusika (watuhumiwa) walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Vifo na utekaji nilivyovijadili katika makala iliyopita vimeendelea kubakia kitendawili huku vyombo vya usalama vikizua viroja vingine. Mauaji ya Profesa Juan Mwaikusa mpaka sasa umma haujui ni nini kilitokea. Vyombo vya dola vimeendelea kuzua kwenye mitandao ili kupoteza watu wasiunganishe tukio hilo na mengine yanayotokea. Utekaji na utesaji wa Dk. Steven Ulimboka mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani. Yule Mkenya aliyetambulishwa na Kamanda Kova ameyeyuka na dola ikafyata mkia baada ya kukosea mahesabu.

Mauaji ya mwandishi Daud Mwangosi na kiburi cha dola kuendelea kuwakingia kifua wauaji ni kumgeuza hayati Mwangosi kama jambazi aliyepigwa risasi akipambana na polisi. Aidha ni kuchora taswira kuwa mauaji yale yaliagizwa na dola na ndiyo maana wauaji hawachukuliwi hatua kwa sababu walitekeleza maelekezo rasmi ya mkuu wao. Mauaji ya kinyama ya namna hii ni kinyume kabisa cha haki za binadamu kwa sababu hayakuagizwa na mahakama. Kuua ni jinai hata kama imefanywa na dola.

Hata zile tuhuma nyingine mbili nilizozungumzia zinazowahusu mawaziri waandamizi wawili katika serikali hii, inapaswa tukumbuke mambo makuu mawili. Kwanza, Dk. Harrison Mwakyembe kwa mkono wake aliandika taarifa ndefu akivituhumu vyombo vya dola kwa kupanga njama za kummaliza kwa njia mbalimbali. Alidai zilitumika ajali, sumu na hata kikosi maalumu kilichoagizwa ili kukamilisha kazi hiyo. Namba za magari zilitajwa na taarifa ile ilikabidhiwa polisi. Hata watu waliomfikia na kumwonya aliwataja.

Ugonjwa wake ulibaki ni kitendawili, huku serikali ikishindwa kukanusha alichokisema Dk. Mwakyembe. Makala moja ilichambua wakati ule kuwa tuhuma za kumpa sumu Dk. Mwakyembe “Ziwe za kweli au za uwongo ni hatari tupu”. Kwa Dk. Mwakyembe kuzua tuhuma nzito kama zile dhidi ya vyombo vya dola ilitosha yeye achukuliwe hatua kali. Badala yake alipandishwa cheo.

Kama alichosema ulikuwa ni ukweli, ilitosha kupangua safu zote za vyombo vya usalama kwa sababu kilichokuwa kinapangwa kufanyika ni hatari kwa dola nzima na hasa kama hakikuwa na kibali cha mkuu wa dola. Wana usalama wakiachwa kuzoea kupanga njama za namna hiyo, kuna siku wanaweza kupanga njama dhidi ya roho ya taifa. Kilichoandikwa kitadumu, ipo siku maandishi ya Dk. Mwakyembe yataturudia maadam tunayo katika nyaraka za kumbukumbu.

Pili, Rais Jakaya Kikwete kwa nyakati mbili tofauti ametamka maneno yanayoashiria hatari ya “ugaidi baridi” na hatari ya kulipa visasi. Mara ya kwanza alikuwa anahutubia taifa mbele ya televisheni alipodai wanasiasa hawaaminiani tena kiasi cha kutoachiana glasi za maji wanapokaa pamoja kwa hofu ya kuwekeana sumu.

Mara ya pili alikuwa anahutubia kikao cha UVCCM mjini Dodoma aliposema kuwa yeye alipochaguliwa aliwateua kuingia serikalini hata watu waliomfanyia mambo mabaya sana wakati wa kampeini au huko nyuma katika utumishi wa serikali. Aliyasema haya kuonyesha kuwa si vizuri kulipiza kisasi.

Kwa yote mawili ni vigumu kuthibitisha kuwa wanasiasa wote wawili niliowataja katika makala yangu kuwa wako salama. Namaanisha ikiwa wakati wote walifanikiwa kutoacha glasi zao zikiwa na ulinzi, na kwamba hawakuwekewa sumu! Tamko la Rais linaonyesha kuwa mchezo huo upo ila hatujui waathirika ni wangapi.

Aidha, hatujui ikiwa yeye binafsi alisamehe kabisa waliomkosea huko nyuma, na ikiwa kwa kufanya hivyo, basi na wasaidizi wake walisamehe vivyo hivyo. Nasema haya kwa kuwa tunaanza kupata picha kuwa hata kama Rais mwenyewe hajaruhusu jambo fulani kuhusu wanaodhaniwa kuwa ni maadui wake au maadui wa chama chake, kuna tabia ya wasaidizi wake kufanya maamuzi ya hatari hata ya kutoa roho za watu ili kumfurahisha Bwana Mkubwa.

Kwa yote niliyosema hapo juu, na kwa kuwa mpaka sasa waliompiga risasi Padre Mkenda hawajapatikana; waliomuua Padre Evaristus Mushi hawajapatikana; waliochoma makanisa hawajapatikana na waliomteka Kibanda bado hawajapatikana, ni ruksa kwa wazalendo wa nchi hii kupiga ramli ili kupata tafsiri ya matukio haya.

Wanaofanya hivyo wanafanya hivyo kwa misukumo ya kidini, kikabila, kisiasa, kishirikina, au kimkakati wa kufunika udhaifu wa dola? Kuna uvumi wa muda mrefu umekuwa ukienezwa  kuwa hata baadhi ya wanasiasa fulani wanaoonekana ni miiba kwa utawala huu, ni “marehemu wanaotembea” kwa sababu “wameshatengenezwa tayari” na wana usalama na kuwa hawatafika mwaka 2015. Ushabiki huu wa hatari juu ya roho za watu hauwezi kuachwa uendelee bila kuchambuliwa kwa hofu ya kuwa ukichambuliwa utaonekana ni uchochezi.

Absalom Kibanda si wa kwanza kufanyiwa mchezo huu mchafu, lakini tulio wengi tunatamani awe wa mwisho. Vitendo vya kuunda visingizio vya kutesa watu ili kufunika “mauaji” baridi yanayoendelea katika taifa letu havikubaliki hata kidogo. Yeyote anayeendelea kushabikia mambo haya, si hoja yeye ni nani katika utawala huu, lakini ajue anambusu chatu. Damu isiyo na hatia ina tabia ya kuwarudi watawala baada ya kutoka madarakani.

One thought on “Kibanda si wa kwanza, natamani awe wa mwisho”

  1. Kanyambala says:

    Tumefika mahali ambapo vyombo vyenye jukumu la kulinda amani ya Taifa letu, si tena vyombo vya kuaminika. Mwakyembe alitaja watu anaowashuku kuwa wanamfuatilia ili kumdhuru hata kabla ya madhara yenyewe kumpata. Steven Ulimboka alitaja mtu anayemshuku kuhusika na kuteswa kwake, kama alivyosema Kibanda. Na wote waliohusika wameonekana kuwa na uhusiano, kwa namna moja au nyingine, na vyombo vya dola. Watu wenye makoti waliomteka Kibanda wanashabihiana na watu wenye makoti waliomvamia na kumuua Jwani Mwaikusa. Mwangosi, mchana kweupe, aliuawa kwa mikono ya askari wa Jeshi letu tukufu la Polisi, katikati ya kundi la askari wenye silaha. Sasa kwa nini watu wasiseme kwamba vyombo hivi vinahusika? Ni kweli hakuna uhakika kwamba kushambuliwa kwao ni kwa sababu ya kabila lao, lakini cha msingi hapa ni kuhusishwa kwa vyombo vya dola kuangamiza utu wa mtu asiye na hatia. Lazima tupate hofu na wasiwasi kuwa, wakati Usalama wa Taifa wanashutumiwa kuwa legelege katika kutimiza, au kujua wajibu wao kwa Taifa, wanahusishwa pia na ubaya huu unaofanyika. Tunajiuliza, kuna nini nyuma ya pazia? Mipaka yetu iko wazi kama nyumba isiyo na mwenyewe, huku wavamizi wakivamia wanavyopenda. Wasomali na Wahabeshi hawaishi kujipenyeza, kila kukicha, mpaka kwa neema ya Mungu tu ndiyo wanakamatwa. Wanyama wanatoroshwa na misitu inaangamia tukiangalia. Hivi ni kweli hakuna vyombo vinavyohusika na haya? Wananchi wamefika mahali lazima wajiulize, TISS ipo?  POLISI, wapo? Uhamiaji, je? JWTZ, wako wapi? Haya yanayotokea, yanaweza kuonekana ni madogo, lakini kidogo huwa kikubwa kikilelewa. Kama leo Madaktari, Wanahabari, Makasisi, Masheikh, Majaji na hata Mawaziri, wanaweza kufanyiwa haya, nani atabaki? Kuna kipindi nilikuwa najiuliza sana sababu ya Rais wetu kuvaa kinga ya risasi kifuani wakati nchi ina amani, lakini sasa naanza kuwaza vingine kabisa, hana budi kutoisahau! Tuna-e-le-kea wapi! Usalama wa raia ni haki ya msingi ya kila mmoja wetu, na vyombo hivi vya dola ndio wajibu wake kuhakikisha unakuwepo, siyo kutumika kinyume cha hapo!  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *