Tahariri
Maoni ya Mhariri
Kiini cha vurugu Zanzibar ni Udini si tu Muungano
John Bwire
Toleo la 241
30 May 2012

HATUWEZI kuamini kwamba kiini cha vurugu zilizotokea mwishoni mwa wiki hii, Unguja visiwani Zanzibar ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kimsingi, Muungano hauna umbile linaloweza kuonekana na kwa maana hiyo, Muungano hauwezi kushambuliwa kwa kuchomwa moto au kuupiga mawe. Muungano ni muundo wa kifikra na kisheria, unaotenganisha au kugawa mamlaka baina ya pande zilizoungana lakini katika taswira ya umoja.

Kwa hiyo basi, suluhu ya kutatua kero za Muungano au kujadili uwe katika muundo gani haitokani na vurugu za aina yoyote bali suluhu inapatikana kwa kushindana kwa hoja. Ni nguvu ya hoja ndiyo inayotibu kasoro zinazoweza kujionyesha katika Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar.

Na hata wito wa upande mmoja wa wananchi kutaka kujitenga na Muungano, unapaswa kusukumwa kwa nguvu ya hoja. Wito wa dhati wa kutaka kujitenga haupaswi kusukumwa kwa vitendo vya vurugu. Tena vurugu zenye mwegemeo wa kidini.

Ni kwa mtazamo huo, tunaamini kwamba vurugu za Zanzibar si ishara ya kero zinazotokana na Muungano. Kiini cha vurugu za Zanzibar ni watu wa dini moja kukosa uvumilivu kwa watu wa dini nyingine, ingawa dini yao wenyewe bila shaka hairuhusu uhalifu wa aina yoyote dhidi ya watu wengine.

Kwa hiyo, vurugu za Zanzibar kiini chake ni chuki binafsi ya watu fulani waliomo ndani ya kikundi kinachoitwa Uamsho. Ni chuki ya watu fulani ndani ya kikundi hicho ambayo haina utetezi wowote ndani ya dini ya wanakikundi.

Hata kama kwa bahati mbaya Zanzibar ikijitenga kama ambavyo ndoto za wafanya vurugu hao zitatimia, bado kwa matakwa ya busara visiwa hivyo vitahitaji kuendeshwa kwa kushirikisha watu wengine nje ya eneo hilo.

Na kwa kweli, watu hao wa nchi nyingine maana yake ni watu wa dini nyingine. Tumekwishakuona kwa mfano, nchi zenye viongozi wakuu wenye mwegemeo wa kidini zinavyoendesha uchumi wake kwa kushirikisha nchi zisizo za kidini.

Kwa vigezo vyote, vurugu za Zanzibar msingi wake ni ubaguzi wa kidini. Vigezo hivyo ni pamoja na hatua ya wafanya vurugu kuchoma makanisa. Kama kweli walilenga kufanya uharibifu usiojenga taswira ya ajenda yao ya siri ya ubaguzi kwa nini hawakuchoma nyumba za ibada za dini yao?

Ikumbukwe kuwa, hata kwa upande wa Tanzania Bara kuna maeneo yenye wakristo wengi na asilimia ndogo sana ya Waislamu. Lakini pamoja na tofauti hiyo, Wakristo walio wengi wameonyesha mfano mzuri wa kuvumilia na kuheshimu dini za wenzao kama ambavyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyotaka.

Na kwa hiyo, tungependa kwa upande wa Zanzibar kuendeleza moyo wa subira na uvumilivu kwa watu wa dini tofauti. Tungependa Wazanzibar wachache wenye ubaguzi wa kidini angalau kuheshimu mawazo ya Wazanzibar wenzao walio wengi ambao waliridhia Katiba mpya ya Zanzibar kutoifanya Zanzibar kuwa visiwa vyenye mlengo wa kidini.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
John Bwire
jbwire@raiamwema.co.tz

Maoni ya Wasomaji

Mwalimu Nyerere aliisha liona hili na Hakika dhambi ya kubaguana itaendelea kuitafuna Zanzibar hata nje ya muungano. Kudhani watakuwa na mafuta ni kiini macho kwa sababu yatachimbwa na wenye fedha. Nigeria wanazalisha sana mafuta lakini wana matumaini madogo ya kuneemeka nayo. Zanzibar chunga sana hata vizazi saba vijavyo hamtakuwa mmeanza kunufaika na mirahaba

mwandishi,unajitahidi kukataa ukweli.Naamini kuwa hukufanya utafiti wa kutosha juu ya ulichokiandika kabla ya hapo.endelea na mawazo yako hayo.uchomaji wa makanisa ilikuwa njia mbinu pekee ya watawala kuzima wimbi la madai ya wazanzibari waliowengi juu ya kudai Uhuru wao ulioporwa miaka isiyopungua arobaini iliyopita.
 

Msiwe kama hamjui mnachokifanya, wakristo mmeanza kuwatesa siku nyingi kabla hata ya hii vugu vugu ya leo mnayotaka kuanzisha Al shaabab Tanzania. Hiyo dini yenu ambayo ili isonge mpaka mchome nyumba za ibada za wenzenu tumeiogopa na sidhan kama kuna mwenye akili timamu anayeweza kujiunga. ACHENI HIZO, TANGAZENI DINI YENU KWA USHAWISHI NA WATU WANAWEZA KUJA NA SI KWA KUCHOMA NYUMBA ZA IBADA ZA WENZENU
 

Mimi sidhani kama waliochoma moto makanisa ni wale wanaodai muungano ujadiliwe kwenye uundaji wa katiba mpya. Wale wasiotaka ujadiliwe ndiyo wanaoweza kufanya kitu kama hiki. Tumeona mambo mengi yakifanyika katika nchi hii kuwahamisha watu kutoka kwenye mada ili wajadili kitu kingine.Naona labda muungano una siri kubwa. Ndiyo maana viongozi piga ua hawataki ujadiliwe. Hawajui hila na ujanja ujanja wa kizamani haviwezi kuwasaidia tena!

Kutokukubali ukweli nako ni maradhi. Kukubali kumezeshwa kila kinachoandikwa au kuoneshwa na vyombo vya habari - bila kujua au kujali ajenda ya vyombo hivyo - nako ni wazimu. Kwa nini musiweze kuamini kuwa yanayotokea Zanzibar ni siasa na si dini? Kwa kuwa katikati ya matukio makanisa na mabaa yamechomwa? Mbona pia maduka na magari yalichomwa pia? Kwa nini isiwe ni mkanganyiko wa umasikini, uzalendo na hasira zilizopotea njia?
Nashuku uwezo wenu wa kuchambua na kufikiri. Nataraji haya ni mawazo ya John Bwire tu na si tahriri ya gazeti la Raia Mwema, ambayo kama ndiyo unakuwa ndio msimamo wa gazeti katika kadhia hii. Kama historia ya dini na mjengeko wa kijamii na kitamaduni wa Zanzibar hamuujui kiasi hiki - hata nyinyi wa Raia Mwema - nina kila sababu ya kuamini kuwa Wazanzibari wasioutaka Muungano wako sahihi kukataa kuendelea kuungana na watu ambao, hata wale wenye nafasi za hadhi kubwa kijamii  kama walivyo waandishi na taasisi za habari - wana uwezo mdogo wa uchambuzi wa mambo.

Vurugu za Zanziba na baadaye kule Mbagala Dar es salaam hazitokani na Udini. Vurugu hizo zatokana na ukosefu wa ajira na uchumi duni miongoni mwa vijana.
Haiwezekani kijana mwenye ajira yake inayomlipa Tshs 1,500,000/= au zaidi kwa mwezi akajiingiza kwenye makundi ya vijana wakafanya fujo iwe fujo za kisiasa, kidini au kikabila. Kwa mfano, hata kama ungefanya utafiti wa akina nani wamo kwenye vurugu utakuta ni vijana wa kike au wa kiume au wazee wasiokuwa na ajira wala kazi za maana mtaani. Nimetoa mfano wa kipato cha Tshs 1.5mil kwa mwezi lakini ukiangalia kwa umakini hata kama ni kipato cha chini ya hapo mfano Tshs 300,000 kwa mwezi naamini kijana kama huyu hawezi kuacha kwenda kwenye majukumu ya kumwingizia kipato chake eti anaenda mtaani kuandamana au kuchoma magari na makanisa. HAIWEZEKANI.
Kwa hiyo kusema kwamba ni udini na chuki za kidini siyo kweli. Bali ni chuki za wasio nacho dhidi ya wenye nacho. Huu ndio mzizi wa tatizo.
NINI KIFANYIKE:
Kwanza, Serikali itazame upya mfumo wa Elimu ya Tanzania kuanzia ngazi ya Shule za Msingi. Vijana wanaomaliza darasa la Saba waweze kuruhusiwa kupata ajira moja kwa moja kwenye maeneo yafuatayo: Mahoteli ya Binafsi/Umma, Mabaa, Nyumba za Kulala Wageni, Kuwa wahudumu wa Ofisi za Umma au za Binafsi, Kufanya usafi kwenye majengo makubwa, kufanya kazi za ulinzi kwenye mashule, mahospitali, wapishi, nk. Kazi kama hizi Serikali itamke wazi kwamba zitafanywa na vijana wenye kiwango cha elimu ya Darasa la Saba na vyeti vya darasa la Saba viruhusiwe kutumika kuombea ajira hizo. Kijana aliyemaliza Form Four asiwemo kwenye kada hii ya kazi hizi. Maoni haya nayatoa kwa sababu Kijana aliyemaliza darasa la Saba awe Mwislam au Mkristo hana pa kwenda kabisaaaa. Kama ameshindwa kuendelea na masomo ya Sekondari au VETA (ambayo na yenyewe inataka waliomaliza F.IV siku hizi) basi kijana huyu anageuka kuwa bomu linalosubiri kupasuka wakati wowote kwa sababu yoyote hata iwe ndogo kama ile ya kukojolea Kuraan mtoto wa Mbagala aliyemaliza Drs la 7 juzi tu.
Pili, Vijana wanaomaliza Kidato cha Nne, sera ya taifa iwatazame kwa jicho la tatu. Sera inapaswa kutamka wazi kwamba kila kijana aliyemaliza Kidato cha 4 ataajiriwa moja kwa moja kwa kutumia cheti chake cha F.4 hata kama hajapitia kozi yoyote. Kazi zinazowafaa vijana hawa zitamkwe kwa uwazi ikiwa ni pamoja na hizi zifuatazo: Watendaji wa Vijiji nchini (VEOs), Watendaji wa Mitaa mijini (MEOs), Wahudumu wa Afya mahospitalini, Askari Mgambo, mameneja wa Nyumba za Kulala wageni ukiacha za kitalii, wahudumu wa Ikulu, wahudumu wa ofisi za umma, nk. Vyeti vya Kidato cha 4 vitumiwe kuomba kazi kama hizo na sera ya taifa iruhusu hivyo.
Tatu, vijana waliomaliza kidato cha sita bila ya kujali amemaliza kozi nyingine yoyote waruhusiwe kupata ajira zifuatazo: Ualimu wa shule za Awali na Msingi, Mameneja wa hoteli ikiwemo za kitalii, makarani wa tume ya Uchaguzi (NEC), Sensa, Watendaji wa Kata (WEOs), Makatibu wa Vyama vya Siasa au Ushirika wa kuweka na kukopa, Kuuza maduka, Makarani wa DAWASCO na Mamlaka nyinginezo za Maji Mijini, nk. 
Nne na Mwisho, wote wanaohotimu elimu ya juu (Vyuo Vikuu na vya kati) sera ya taifa itamke wazi kwamba ajira zao zitakuwa kada tofauti na hizo zilizoko kwenye hoja ya kwanza, ya pili na ya tatu. Wao waajiriwe kama maofisa kwenye taaisisi yoyote ya umma au binafsi. Kiwango hicho cha elimu ndicho kitumike kuajiri watu wenye weledi kwenye taaluma husika kama ni waandishi wa habari, watangazaji wa TV na Redio, wawe na taaluma hiyo. Manesi, Madaktari, walimu wa sekondari, vyuo, maofisa watendaji wa mashirika ya umma, mamlaka na wakala wa serikali, makampuni binafsi, migodini, nk. Sera ya ajira itaje waziwazi na waajiri waagizwe kisheria kwamba ajira kama hizo zitashikiriwa na watu wenye kiwango hicho cha elimu. Kwa mfano mtu mwenye elimu ya Chuo Kikuu au Diploma ya chuo chochote ndiye anayeweza kuwa Mtangazaji wa TV/Redio au mwandishi wa habari.
Aidha, ili kutoa ajira zaidi kwa vijana, sera ya taifa itaje wazi kwamba kazi zote za ofisi za umma ziwe za utendaji au za kisiasa zifanywe na watu wenye elimu inayofanana na kazi hiyo. Sera itaje na ilindwe na sheria kwamba hakuna ofisi ya umma itakayoshikiliwa na mtu mwenye umri zaidi ya miaka 60. Iwe Siasa au kazi za utendaji kama mtu ameshatimiza miaka 60 aachie ngazi ili kuwapisha vijana wapate ajira. Hii natamani iwe kwenye kila sekta ikiwemo kwenye vyama vya siasa. Ukomo wa umri uwe miaka 60. Mtu yeyote mwenye umri zaidi ya miaka 60 asigombee nafasi yoyote iwe ubunge, udiwani au Urais. Hii itatoa nafasi zaidi kwa vijana. Watu wenye umri huo watumike kutoa ushauri tu pale inapohitajika.
Taifa likifanya haya; vurugu za kidini, kisiasa au kikabila zitabakia kuwa hadithi tu.
Juma V. Milinga
Mtaalam wa Hifadhi ya Jamii, Uchumi na Maendeleo ya Jamii.
(IFM- ADSAA,& Masters of CED, OUT)

Toa maoni yako