SIKU hizi nina muda wa kutosha kufuatilia majadiliano mbalimbali katika tovuti kadhaa kubwa duniani zinazozungumzia masuala ya Afrika na watawala wetu.
Baadhi ya mijadala hiyo ya mitandaoni iliyonivutia, hivi karibuni, ni ile iliyomhusu Rais wetu, Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Mjadala kuhusu Kikwete ulihusu kile alichokizungumza kwenye mkutano wa hivi karibuni wa uchumi uliofanyika huko Davos, Uswisi na ule wa Kagame ulihusu habari zilizoandikwa kwenye gazeti la Los Angeles Times la huko Marekani kuhusu Rwanda.
Kwenye mjadala kuhusu alichokisema Kikwete huko Davos, wachangiaji wengi walimlaumu kwa mchango wake ‘mwepesi’ kuhusu nini hasa kinacholitatiza bara la Afrika lishindwe kuendelea, na hivyo kuendelea kutegemea misaada ya nchi tajiri duniani.
Katika mkutano huo wa Davos, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, aliwaomba marais wa Afrika waliohudhuria mkutano huo kuueleza mkutano ni kwa nini hali hiyo inaendelea kulikumba bara lao.
Walitangulia kujieleza Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Raila Odinga wa Kenya, na ndipo Rais wetu Jakaya Kikwete alipopewa fursa kuzungumza.
Kwa mujibu wa wachangiaji wengi kwenye mitandao hiyo, Zuma na Raila walijitahidi kujieleza vizuri; lakini Rais wetu, Jakaya Kikwete, ‘aliboronga’, na kwamba aliishia tu kujenga dhana kwamba nchi za Afrika haziwezi kuendelea bila ya misaada ya mataifa tajiri!
Baadhi ya wachangiaji kwenye mtandao waliwalaumu wasaidizi wa Rais Kikwete kwamba hawakumuandalia kitu kizito cha kuzungumza kwenye mkutano huo, na hivyo kumwachia azungumze mwenyewe kutoka kichwani mwake.
Hicho alichokisema Kikwete huko Davos nacho kimewekwa (neno kwa neno) kwenye mitandao na mwananchi mmoja.
Mtazamo huo wa Kikwete huko Davos kwamba Afrika haiwezi kuendelea bila misaada ya mataifa tajiri ndio uliomuudhi Mwingereza mmoja ambaye alimshutumu rais wetu gazetini; huku akitumia lugha ambayo haipendezi – lugha ambayo unaweza kusema ni sawa na kupiga chini ya mkanda.
Huyo Mwingereza alidai alifanya kazi UNDP hapa Tanzania na anaijua vizuri nchi yetu. Kwa mtazamo wake, Kikwete ni rais dhaifu kiutendaji kuliko wengine wote tuliopata kuwanao.
Alichokisema bwana huyo dhidi ya Kikwete kiliwekwa hata kwenye mtandao wa hapa nchini wa Jamiiforum, na watu wamekuwa wakisambaziana habari hiyo hapa nchini kwa njia ya intaneti.
Labda niweke wazi mapema kabisa kwamba nami naungana na wale wote wanaotofautiana na Rais Kikwete kuhusu kile alichokizungumza kule Davos.
Si kweli kwamba Afrika haiwezi kuendelea bila kusaidiwa na mataifa tajiri, na si kweli kwamba Afrika haiwezi kulitupilia mbali bakuli la ombaomba ambalo imekuwa ikilitembeza Ulaya na Marekani kwa zaidi ya miaka 50 sasa.
Lakini nisemi pia kwamba sikushangazwa na kauli hiyo ya Kikwete huko Davos; kwani miaka sita au saba hivi ya uongozi wake, imetuthibitishia sote kuwa si muumini wa dhana ya kujitegemea.
Na ndiyo maana alikwenda Davos na kulalamika ili tuonewe huruma na Wazungu kwa kutamka kwamba Waafrika tunaishi maisha ya shida mno (hand to mouth) na tunahitaji kusaidiwa!
Najua jambo hili kwamba hatuwezi kuendelea bila misaada ya Wazungu linakera baadhi yetu, na ndio maana mimi binafsi sichoki kumtolea mfano Rais Kagame wa Rwanda kama mmoja wa marais Afrika anayethibitisha kwamba nchi inaweza kupata mafanikio katika vita yake dhidi ya umasikini bila misaada ya Wazungu.
Mwezi uliopita niliandika katika safu hii kuhusu mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Rwanda imeyapata katika kampeni yake ya kutokomeza nyumba za udongo katika nchi hiyo, na kuwaomba watawala wetu wakajifunze Rwanda kwa Kagame.
Makala hiyo ilipokelewa vyema na wasomaji wangu wengi, lakini wako wachache waliotofautiana nami; huku wengine wakinipinga kwa kutumia lugha chafu ikiwa ni pamoja na wanaoishi Ughaibuni waliosema eti mimi ni Mtutsi. Mpare na Mtutsi wapi kwa wapi jamani?!
Ni kwa sababu ya hao walionipinga kuhusu Kagame nilifuatilia kwa hamasa kubwa huu mjadala mwingine mitandaoni juu ya kile kilichoandikwa na gazeti la Los Angeles Times la Marekani kuhusu Kagame.
Serikali ya Rwanda ilitangaza, hivi karibuni, kwamba imefanikiwa kupunguza umasikini kwa asilimia 12 katika kipindi cha miaka sita iliyopita; yaani imeushusha umasikini kutoka asilimia 57 hadi asilimia 45.
Mafanikio hayo yamechukuliwa kuwa ni ya aina yake duniani; huku gazeti hilo likiyaita; one of the most stunning poverty drops in the world.
Ni kwa sababu hiyo, Los Angeles Times lilimtafuta mmoja wa wachumi wanaoheshimika duniani anayeitwa Paul Collier ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Uchumi wa Dunia katika Chuo Kikuu cha Oxford na kumuomba ufafanuzi wake juu ya mafanikio hayo ya haraka ya Rwanda.
Matokeo ya mazungumzo hayo ni kuchapishwa kwa habari hiyo kwenye Los Angeles Times iliyobeba kichwa kinachosomeka hivi: How did Rwanda cut its poverty so much? Habari hiyo iliwekwa katika mitandao kadhaa na ikawa ndio chanzo cha majadiliano hayo mitandaoni.
Kimsingi, mchumi huyo wa Oxford University anataja sababu mbili kubwa zilizoiwezesha Rwanda kupata mafanikio hayo makubwa ndani ya miaka sita.
Sababu ya kwanza aliyoitaja ni bei nzuri ya kahawa katika soko la dunia, na kwamba Rwanda iliitumia vizuri fursa hiyo.
Paul Collier anaeleza kwamba Serikali ya Rwanda ilielekeza mapesa iliyoyapata kutoka katika mauzo yake ya nje ya kahawa kwenye miradi ya maendeleo vijijini.
Kama hivyo ndivyo, Mtanzania unashindwa kujizuia kujiuliza; sisi Tanzania tulikuwa wapi tusifaidike na bei hiyo nzuri ya kahawa katika soko la dunia?
Lakini si vigumu kulipata jibu la swali hilo hasa katika mazingira ambayo tunaambiwa kuwa kahawa yetu mkoani Kagera inavushwa kila mwaka kuingizwa nchini Uganda, na kwamba ni Uganda ndio inayoiuza nje kwenye soko la dunia!
Lakini sababu ya pili iliyotajwa na Paul Collier ni kwamba Rwanda ina rais mwadilifu na mchapakazi kweli kweli. Kwa maneno yake mwenyewe Collier alitamka hivi: The President (Kagame) runs a tight ship within government built on performance rather than patronage”.
Msomi huyo wa Oxford University pia alimsifu Kagame kwa kujenga utamaduni wa uchapaji kazi nchini Rwanda, na kwa kuwapangia mawaziri wake viwango wanavyopaswa kuvifikia kila mwaka, na wasiovifikia huwajibishwa.
Si hivyo tu, msomi huyo alisema kwamba Rwanda ndio nchi pekee katika bara la Afrika inayokaribia, japo kidogo, njia iliyofikiwa na nchi za Mashariki ya Mbali kupata maendeleo ya haraka. Alisema hivi:
“Basically, President Kagame built a culture of performance at the top of the civil service –minister well paid but given targets. Rwanda is the nearest that Africa gets to an East Asian-style developmental state.”
Hivyo ndivyo mkurugenzi huyo wa Oxford University anavyomwona Kagame na Rwanda yake, na sisi tuliobahatika kuitembelea Rwanda ndivyo pia tunavyomwona Kagame.
Nirudie kusema tena kwamba Kagame ni mfano hai unaothibitisha kwamba Afrika inaweza kuendelea bila ya kutegemea misaada ya Wazungu; kitu ambacho Rais wetu, Jakaya Kikwete, hakiamini; kama alivyotuthibitisha tena kwa kauli yake ile tata kule Davos.
Kwa hiyo, tunachohitaji Afrika ni kuwa na marais wa aina ya Paul Kagame, na si wa aina ya Jakaya Kikwete na wenzake.
Hawa (kina Kikwete na marais wenzake Afrika) ndio wale waliofurahia na kuchekelea, hivi karibuni, kule Addis Ababa, Ethiopia wakati wa uzinduzi wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) lililojengwa na Serikali ya China kama ‘msaada’ kwa Waafrika.
Kina Kikwete na wenzake hawakuona kuwa ni aibu kubwa kwa AU kujengewa hata ofisi zake na China wakati umoja huo umekuwepo kwa miaka zaidi ya 40!
Kama katika historia ya miaka zaidi ya 40 ya umoja huo, wameshindwa hata kujijengea ofisi tu, watamudu nini?
Na wala marais wale wa Afrika hawakutambua hata kuwa kujengewa jengo hilo na Wachina ni aina fulani ya “rushwa”!
Wangelijua kwamba ni aibu na ni ‘rushwa’ ya aina fulani inayotolewa na nchi hiyo inayosomba na kunufaika na maliasili za Afrika; achilia mbali kubwaga bidhaa zake dhaifu kwenye bara hilo, wasingechekelea walivyochekelea wakati wa uzinduzi ule!
Ni rais mmoja tu barani Afrika ambaye hakuchekelea. Yeye aliiona hiyo kuwa ni aibu kubwa kwa bara letu la Afrika na alitamka hivyo. Rais huyo ni Paul Kagame wa Rwanda, na ndiyo maana sikushangaa Los Angeles Times likimmwagia sifa kemkem.
Hii ndio simulizi yangu ya leo kuhusu ya Jakaya Kikwete huko Davos na ya Paul Kagame huko Los Angeles (LA), lakini nihitimishe hivi:
Kwa miaka 50 tumekuwa tukipokea misaada kutoka kwa Wazungu lakini tumeshindwa kuitumia kujiletea maendeleo na pia imetufanya tushindwe kujitegemea.
Utegemezi huo umetubwetesha kiasi kwamba (kwa mfano) tukipewa msaada wa boti ya uvuvi, mathalan na Sweden, tutataka pia fedha za kununulia mafuta ya boti hiyo zitoke pia Sweden! Hicho ndicho kiwango cha utegemezi tulichokifikia.
Ndugu zangu, tumebweteshwa mno na misaada ya Wazungu. Ole wetu siku Wazungu watakapoanza kutuchoka. Na siku hizo hazipo mbali; maana tumeshaanza kuziona dalili.
Tafakari.
Maoni ya Wasomaji
<p>Binafsi nina creative idea
<p>Binafsi nina creative idea, kwanini mh.Paul Kagame akisaidiwa na baadhi ya mawazili na watendaji wa selikari ambao ni very competent pamoja na kambi ya upinzani ya hapa nchini asipewe ulaji- (yaani tumwombe tumwajiri baada ya kustaafu kwake huko rwanda) hapa tanzania kama uwazili au mtendaji ktk secta za madini, utalii, elimu na viwanda kwa pamoja?? yaani huyu jamaa ashughurike na hizo sectors in totality vile sisi tumeshindwa, mi nafikiri atasolve vitu vingi sana</p>
Bravo Mbwambo! Sema,longa
Bravo Mbwambo! Sema,longa longa...................................................................!
Unachokisema hapa
Unachokisema hapa nakifananisha na makala moja aliwahi kuandika Ayoub Ryoba kwenye gazeti la The Citizen mwaka 2006, sikumbuki toleo namba ngapi; lakini kwa kifupi alitoa mfano wa kujengewa matundu kadhaa ya choo kwenye shule ya msingi na serikali ya Japan na kufanya uzinduzi wa nguvu wa hayo matundu ya choo, na muda mfupi baadaye serikali yetu inaagiza mashangingi kwa mamia hata elfu kutoka Japan kwa gharama kubwa! Tafakari
Huo ndo uzezeta tuliofikia kama nchi, ole wetu....
<p>Mimi miaka yote nimesema
<p>Mimi miaka yote nimesema Kikwete is a joke na watu hawakubali. Nakumbuka mwaka 2005 alipochaguliwa kwa vigelegele na akina Kilaini kumuita chaguo la Mungu niliwaambia huyu jamaa fake. Nakumbuka afisa mwandamizi wa Usalama wa Taifa alinigeukia na kunijibu kwa ukali kwamba Kikwete ndio rais pekee anaeheshimika Afrika (kwa wakati ule). Nilijaribu kumueleza kwamba wote akina Bush na Gordon Brown wakati ule walikuwa hawamheshimu bali wanajua Kikwete ni mtu dhaifu ambaer ukimpa misaada ale na mafisadi ana-sign mikatanba bila kuisoma. Yule bwana alikasirika akaanza kunitafiti nafanya kazi wapi 'anishughulikie'. Bahati nzuri akagundua sio kila mtu ni muwindwa, aliposhtuka kuwa nami ni mwindaji akaniacha nilivyo. Eight years on, kila nilichosema kimetimia na zaidi. MWinyi alikuwa rais goigoi aliyeanzisha udini Tanzania lakini in comparison, the man was more patriotic na alijua anachofanya. At least ali-spearhead process ya liberazation. Nini legacy ya Kikwete? To me, is already the worst ever president Tanzania has always had. Sitazamii kama atakuwepo tena rais mzembe kama huyu Tanzania na sisemi hivi kwa sababu ya dini yake. I hope Salim Ahmed Salim angechukua nchi 2005!!</p>
Bunge au mbunge mmoja kutoa
Bunge au mbunge mmoja kutoa hoja/mswada ya kupinga kauli za JK anazozitoa akiwa kama mkuu wa nchi ingesaidia kuondoa udhaifu wake na vile vile kwa wale watakaofata badae, mfano iyo kauli ya Davos na ile ya mafisadi kwamba wanapesa nyingi ivyo ukiwakamata nchi itayumba. Tunaitaji hoja za ku-rebuke kauli zake
Ndugu Mbwambo nakupongeza kwa
Ndugu Mbwambo nakupongeza kwa makala yako na uvumilivu ulionao katika kutafuta data ili kuelimisha umma juu ya Tanzania na uongozi uliopo. Mimi kwakuwa kazi yangu si mwandishi basi nilishakata tamaa juu ya nchi yangu Tanzania. Niliwahi kutoa maoni yangu kwenye moja ya makala zako mwaka jana mwishoni. Katika makala ile nilisema watanzania hatukumwelewa mwalimu Nyerere aliposema Kikwete bado mdogo. Nikaeleza kwamba mwl aliongea kiutu uzima kwamba huyu ana akili za kitoto. Waingereza wanasema a fool at forty is a fool for ever. Wakati anataka urais na mwl anakataa tayari he was above 40.
Kwa hali ninayoiona ya Tanzania nimekata tamaa kabisa. Sitegemei lolote jema kwa njia ya amani. Na ukiangalia Afrika yote utaona hata pale panapotokea nguvu ya umma kufanya mabadiliko, bado wanasiasa watakao shika dola watavuruga kabisa. Angalia hali ya Misri, Syria na Libya.
Nakuomba endelea kuandika labda hata sisi tulio kata tamaa twaweza inua mioyo tena.
Tutamkumbuka Kikwete katika
Tutamkumbuka Kikwete katika yafuatayo.
Raisi wa kwanza Tanzania kwenda kukutana na akina BoysIImen
Rais wa kwanza Tanzania kwenda kupiga picha na 59cent.
Rais aliyeruhusu dola ya marekani kutumika Tanzania kwa kua shilingi ya Tz inashuka thamani kila siku.
Raisi wa kwanza Tanzania kusafiri sana nje ya nchi (Vasco Dagama)
Raisi aliyekwepo aliyesimamia sera ya elimu kwa zaidi ya 50% wanafunzi kufeli kidato cha nne.
Raisi aliyekaa kimya madaktari wakigoma na kusababisha vifo kibao vya Watz
Raisi aliyeshindwa kutoa msimamo wake kuhusu Dowans
Raisi aliyepewa Phd nyingi sana kupita wote Tanzania.
Raisi aliye iweka Tanzania gizani kwa mgao hatari wa umeme.
Raisi anayependa kusifiwa na Wamarekani.
Na mengine mengi tutamkumbuka pia.
MUNGU IBARIKI TANZANIA KAMA ALIVYOTUFUNDISHA BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE
Haki ya Mungu hili
Haki ya Mungu hili limeniumiza badala ya kunifurahisha. Kweli unayosema wengine watayapinga ndugu mbwambo. mimi nimezaliwa tanzania, nikasomea huko kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu sasa nafanya kazi Rwanda. Nasema hivi kama watu wengine wanakutukana eti waandika hivo kwakuwa wewe ni mtutsi, tuwaulize kama akina Prof. paul from oxford relate to Tutsi too! or simply the IMF, World bank and even the Tycoon Bilgates who has just invested in Rwanda. Ukifika hapa Rwanda nakujionea kwa macho yako angalau kwa wiki moja utashangaa. Umeshaona the Kigali cith master plan that will be positioned in future? huwezi amini anaetaka nimtumie ashangae. waafrica tunaweza kama tukitaka. nimeishi uganda, na nimeshi kenya kwa masomo na baadae nikafanya kazi huko; kweli waafrika tunaendekeiza udhaifu usio msingi maana hata huko mambo mengi ni hovyo lakini nadhani kwa robotatu ya miaka yangu nilioishi Tanzania, basi nasema sio Kikwete wakumlaumu bali ni watanzania wote mimi pia nilimchagua kwamara ya kwanza lakini mara ya pili mh! Kama fikra za wengi zisipo zingatia mambo muhimu sijui nini kitatukia. Kwa swala la Kagame, huyo hata ukidhani anapewa sifa za bure wajisumbua labda wale wazembe wakufikili na kutazama maana ukiingia ndani ya nchi ya Rwanda utaamini kuwa the Guy (Kagame) really mean what he say and is a man that walk the talk.