BAADA ya kumsikiliza kwa makini Rais Jakaya Kikwete akihutubia wakati wa maadhimisho ya miaka 34 ya CCM, nimekumbwa na mfadhaiko mkubwa.
Hiyo inatokana na ukweli kuwa Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa CCCM amechuja kwa kasi ya ajabu na havutii kusikilizwa kwa namna yoyote. Ndani ya Serikali na ndani ya chama amezungukwa na watu asiowaamini na wao pia hawamuamini.
Ana uwezo wa kuwabadili na wao wana uwezo wa kumkwamisha asifanye anachotaka. Hali hii si njema kabisa kwa sababu katika jukwaa tulilokaa na Rais Kikwete mjini Dodoma wakati anahutubia, baadhi ya makada walilala usingizi mzito na hawakujua hata hotuba imeisha saa ngapi.
Ni masikitiko makubwa kumwona mkuu wa nchi anasema maneno asiyoyaamini na zaidi sana akijua fika kuwa hata anaowahutubia hawayaamini wanayoyasikia.
Rais alisema kuwa haijui Dowans; alisema kuwa maneno yaliyosemwa na John Chiligati ndivyo hata yeye alivyokuwa anaamini na kukubali; alisema kuwa msimamo wa MIzengo Pinda ndio msimamo wake.
Msimamo wa sasa wa Rais wetu kuhusu Dowans aliupata alipozungumza na wabunge wa CCM katika semina yao mjini Dar es Salaam. Ndani ya Baraza la Mawaziri na katika kikao cha Kamati Kuu, Rais alikuwa na msimamo tofauti na ule alioutangaza Dodoma. Mwisho wa yote, Rais alisema pia na kuahidi kuwa ana mpango wa kuongoza vikao vya CCM kusafisha safu zake zote za uongozi. Sioni kuwa ana uwezo huo na naamini anajua hawezi kufanya mabadiliko hayo. Nitamwomba radhi rasmi kupitia safu hii siku ikithibika kuwa aliyoyasema siku hiyo ndio ukweli.
Hotuba ya Rais Kikwete siku hiyo imeacha makovu mengi kwa baadhi ya wasaidizi wake wa muhimu. Waathirika wa kwanza wa hotuba ile ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wa pili ni Waziri wa Nishati na Madini. Hawa wawili kwa nfasi zao na mapema sana, walikwishakutangaza nia ya Serikali kuilipa kampuni ya Dowans.
Haiwezekani kuwa walitangaza bila ridhaa ya Rais kwa sababu suala la Dowans ni suala nyeti. Kama walifanya bila ridhaa yake, hawafai kabisa na hata kama wanasita kujiuzulu wasidhani kuna mtu atakayewachukulia tena kwa uzito unaostahili.
Lakini suala la msingi hapa si kujiuzulu kwao, bali ni nini madhara ya kukosa msimamo kwa Rais na kuwageuka wasaidizi wake katika siku zijazo. Kiongozi wako usiyejua msimamo wake ni hatari kwa wasaidizi maana hawana uhakika wa kuwa salama hata kama atakuwa amewapa ruhusa ya kufanya mambo fulani kwa maandishi. Sasa ni gumzo kuu kuwa Rais kawatosa William Ngeleja na Jaji Frederick Werema katika suala la Dowans!
Mwandishi wa habari maarufu hapa nchini, aitwaye Salva Rweyemamu aliwahi kuandika makala ndefu za mfululizo kueleza nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa katika chama chake. Ilikuwa ni wakati wa uenyekiti wa Benjamin Mkapa na Salva akiwa mmoja wa wahariri wa gazeti maarufu la wakati huo alikwenda mbali na kumwita Mkapa kuwa ni “Mungu mtu”.
Wakiristo tunaamini “Mungu mtu” ni Yesu Kristo peke yake, na kwa hiyo Salva alipompa Benjamin Mkapa hadhi hiyo ni ama alikuwa amepotoka au aliamua kumtusi kirejareja.
Hoja ya Salva wakati huo ilizama katika mazoea na utamaduni wa CCM kumpa nafasi kubwa Mwenyekiti wa chama katika maamuzi mbalimbali. Haikufikirika kuwa jambo lolote ambalo Mwenyekiti wa chama hakulipenda lingeweza kufanyika katika CCM.
Kwa mantiki hiyo basi, nguvu binafsi ya Mwenyekiti ndiyo iligeuka kuwa nguvu ya chama. Udhaifu binafsi wa Mwenyekiti nao ukageuka udhaifu wa chama chetu cha CCM.
Dhana hii ina asili katika haiba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na enzi za Zidumu Fikra za Mwenyekiti ambazo Baba wa Taifa mwenyewe alizikosoa na kushauri makada waongeze neno “sahihi” na kwa hiyo salamu ya chama ikawa “Zidumu Fikra Sahihi za Mwenyekiti wa CCM”.
Kwa hali yoyote, Baba wa Taifa na namna yake ya kuongoza (style), akaasisi utamaduni wa kuona nguvu ya chama kuwa unatokana na nguvu ya Mwenyekiti wake. Ili kuifanikisha dhana hii, ilibidi Mwenyekiti wa chama awe ni mtu anayekivaa chama na chama kinamvaa yeye.
Japo ni hatari sana kuendekeza dhana hii, lakini pia kukosekana kwa dhana hii, kwa sehemu kubwa ndiyo sababu ya kusambaratika kwa CCM kimaadili na kimwelekeo. Ndani ya chama chetu, uadilifu, ujasiri na ukomavu wa Mwenyekiti unapotiliwa shaka au inapoonekana kuna wanachama waadilifu kuliko Mwenyekiti, huo unakuwa mwanzo wa mpasuko.
Hali kadhalika nguvu ya chama tawala kimsingi ndiyo asili ya nguvu ya serikali. Kinyume chake pia ni kweli kwamba udhaifu wa chama ndio unageuka na kuwa udhaifu wa serikali.
Hivi sasa wananchi walio wengi ama wanaichukia CCM kwa madhambi yanayofanywa na serikali, au wanaichukia serikali kwa madhambi na udhaifu unaoendelea ndani ya CCM.
Kwa sababu watu walizoea kuona uadilifu ndiyo msingi wa kwanza wa mwanachama wa TANU na CCM, ni vigumu kuwashawishi kuwa udhaifu binafsi wa kiongozi wa CCM hauna uhusiano na chama anachokiongoza.
Nilipomsikia Rais Kikwete akiahidi kukiongoza chama katika mabadiliko makubwa ya kukisafisha, nilijiuliza ikiwa kweli anafahamu mtiririko huu wa kinasaba, yaani kati ya Mwenyekiti na chama na kati ya chama na serikali.
Kwa kuwa mimi binafsi nina shaka kubwa sana na uwezo wa Rais Kikwete kama kiongozi thabiti, nina kila sababu ya kuamini kuwa hakuna lolote litakalotokea kutokana na ahadi ya Rais aliyoitoa kule Dodoma. Na kwa kuwa CCM kwa sasa imesambaratika hata katika sekretariati yake, hakuna uwezekano wa kuongoza vikao vya maamuzi kufikia mabadiliko yanayotarajiwa na wananchi walio wengi.
Enzi ya Mwalimu walikuwapo akina Kingunge Ngombale Mwiru, Pius Msekwa, Mzee Mhina, Daudi Mwakawago na wengine ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuandaa rasimu za mabadiliko muhimu kama haya na kuyaleta mbele ya vikao yakiwa yameiva bila kuingiliwa na ghilba za wenye uchu wa madaraka.
Ikiwa hivi sasa, watendaji wakuu wa chama wanahusishwa na wizi wa kadi na utengenezaji wa kadi bandia wakati wa uchaguzi, ni nani anaweza kuandaa na kuongoza mchakato wa mabadiliko ndani ya CCM?
Kwa kuwa haya yote yanafanyika mbele ya macho ya Mwenyekiti wa chama, ni sahihi kuamini kuwa wote, CCM na Mwenyekiti wake, wanaweza kwenda chini ya mtaro wa historia ya mabadiliko yanayozumgumziwa.
Toa maoni yako