MARA baada ya kuifunga Malawi na kuingia nusu fainali za mashindano ya soka ya kugombea Kombe la Chalenge, kocha msaidizi wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alinukuliwa akisema watasherehekea Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kutetea ubingwa wa michuano hiyo.
“Kwa kuwa tutakuwa tunasherehekea Miaka 50 ya Uhuru tunataka kufanya hivyo kwa kutwaa Kombe la Challenge na kuwapa Watanzania zawadi ya Miaka 50 ya Uhuru,” alisema Jamhuri.
Kana kwamba hiyo haitoshi, kocha huyo aliongeza ya kuwa kwa upande wake binafsi, furaha itazidi maradufu kwa vile alizaliwa tarehe tisa na kwamba angependa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kutetea taji lao walilolitwaa kwenye ardhi ya nyumbani mwaka jana.
Lakini haikuwa hivyo, kwani katika mchezo uliofuata Kilimanjaro Stars iliyaaga mashindano na kuvuliwa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuchapwa mabao 3-1 na Uganda ambayo ilitinga fainali na hatimaye kulibeba kombe hilo baada ya kuifunga Rwanda.
Jamhuri alisema aina ya majigambo ambayo mashabiki wa soka wa Tanzania wamezoea kuyasikia. Mpira Tanzania unachezwa ‘mdomoni’ na kwenye uwanja mpana zaidi wa ‘magazetini.’ Visingizio ni lazima vitafutwe baadaye kuelezea sababu ya kushindwa.
‘Julio’ aliliahidi Taifa ushindi pasi na shaka. Alisema ya kuwa Kilimanjaro Stars imekamilika na ina wachezaji wenye sifa za kuliletea heshima Taifa.
"Nasema wazi ikitokea tumetolewa hakuna visingizio...tumeichagua kwa mahitaji maalumu ndio maana umeona kuna wenye uzoefu wa mashindano mbalimbali na wasio wazoefu lakini wanaweza kufanya kazi wakipewa nafasi.
Akaongeza: "Naamini mtu kama Ibrahim Mwaipopo ni mchezaji mzuri na akipewa nafasi atafanya kazi, hata Mwaikimba (Gaudence) ni mshambuliaji mzuri na huwezi kubisha hilo mfano mzuri mwaka jana alifunga mabao mengi kwenye ligi na hata msimu huu ana mabao ya kutosha."
Kuhusu maandalizi watakayofanya alisema wameanza na mazoezi ya kutengeneza stamina kabla ya kuhamia kwenye mbinu na ufundi.
"Ukweli ni kwamba muda ni mfupi, lakini ninachofanya sasa hivi ni kuwafanyisha mazoezi ya stamina kabla ya kuhamia kwenye mbinu na ufundi mwingi ambayo ndiyo itakuwa staili yetu," alisema Julio.
Hakika maneno ya ‘Julio’ yalitoa picha inayoonyesha ya kuwa Kilimanjaro Stars ingeshindana si kushiriki michuano hiyo. Lakini nini kilichotokea? Ilifungwa mchezo wake wa kwanza na Rwanda kwa bao 1-0, ikaifunga Djibouti (ambayo kila mlevi alikuwa anajifunzia kunyoa) kwa mabao 3-0 na kufungwa na Zimbabwe kwa mabao 2-1.
Hivyo ikaponea kwenye tundu la sindano kutolewa kwani, ililazimika kutinga hatua ya robo fainali kwa mahesabu ya kumpata ‘best looser.’ Kwa maelezo mengine ingekuwa kwenye ‘siasa za CCM’ iliponea kwenye ‘kapu’ kwenda robo fainali.
Ushiriki wa Kilimanjaro katika michuano hiyo uligubikwa na matatizo mawili, la kwanza likizua tatizo la pili: Tatizo la kwanza ni manung’uniko ya baadhi ya mashabiki kuhusu uteuzi wa timu hiyo kwamba ulifanywa ‘kiushikaji’ mno na tatizo hilo ndilo lililosababisha baadhi ya mashabiki kwa makusudi kabisa kuizomea timu hiyo kila ilipocheza.
Je, uteuzi wa timu ulikuwa na kasoro gani? Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti la Mwananchi (kama lenyewe lilivyoandika), mashabiki wa Yanga hawakuridhika na kikosi hicho kwa vile sehemu yake kubwa iliundwa na wachezaji wa timu ya Simba.
Simba ilikuwa na wachezaji sita, Haruna Moshi ‘Boban’, Mwinyi Kazimoto, Shomari Kapombe, Juma Jabu, Juma Kaseja na Juma Nyosso, wakati Yanga ilikuwa na wachezaji watatu: Godfrey Taita, Nurdin Bakari na Shaaban Hassan ‘Kado’.
Lakini, kuwa na wachezaji wengi wa timu moja kwenye timu ya taifa si tatizo, tatizo ni pale uteuzi wa wachezaji hao unapoonekana kufanywa kwa lengo la kuthibitisha kitu maalum au kwa upendeleo kama mashabiki wengi wa Yanga walivyoamini.
Ajabu ni kwamba, zomea zomea hiyo ilikuwa ‘point’ kwa Jamhuri kuelezea ni kwanini Kilimanjaro ilishindwa kutetea ubingwa wake.
Alinukuliwa akisema ya kuwa mgawanyiko miongoni mwa Watanzania katika kuishangilia timu hiyo ndio uliosababisha washindwe kutetea taji lao. Lakini hiyo ni kweli? Bila shaka si kweli, ni kisingizio tu.
Akizungumza baada ya mchezo ambao Kilimanjaro Stars ilitolewa na Uganda mashindanoni, Kihwelo alisema Watanzania wamevuna walichopanda kwenye Challenge!! (kweli?)
Alisema kuna kundi fulani la mashabiki tangu kuanza mashindano hayo walikuwa wakishangilia timu za kigeni na kuizomea Stars, hali aliyodai iliwakatisha tamaa wachezaji wake (!!).
Kocha huyo aliyekuwa msitari wa mbele kuongea na waandishi wa habari kila baada ya mchezo, alisema pia kwamba maandalizi duni kwa upande mwingine ndiyo yaliyochangia kufanya vibaya kwa timu hiyo, kwani walipewa timu muda mfupi kabla ya mashindano. ( Hakuliona hilo alipokuwa anajigamba mwanzoni).
“Hawa Uganda karibu wote ndio hawa hawa waliotoka kushiriki kwenye mashindano ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika, wamekaa pamoja kama timu kwa muda mrefu,” alisema Kihwelo.
Kihwelo alisema hayo akiwa amesahau kwamba hata yeye alikuwa na fursa ya kuchagua karibu kikosi kile kile kilichoitoa Chad kutinga kucheza michuano ya makundi ya fainali za Afrika hivi karibu tu. Kwa makusudi wakaamua kuchagua kikosi kigeni kabisa na kutamba nacho na sasa analaumu alipoangukia!!
Lakini si wote waliokuwa wanakerwa na Kilimanjaro walikuwa wanafanya hivyo kwa sababu tu timu hiyo imesheheni wachezaji wa Simba. Baadhi ya mashabiki wa soka walitoa maoni yao kwenye tovuti ya gazeti la Mwananchi kuelezea jinsi walivyokerwa na timu hiyo.
Wa kwanza alisema: “Timu yoyote inayocheza soka ya kuvutia itapata mashabiki Tanzania. Stars wasijidanganye kuwa watashangiliwa wakati hata pasi tano hawafikishi!!! Watu wanataka burudani, nyie mnakimbia kimbia ovyo uwanjani bila mpango wowote.”
Mwingine alisema: “Timu kama Ethiopia, Malawi, Sudan, Rwanda na Uganda zinaonyesha kabisa zinaujua mpira. Wanapiga pasi za kueleweka, na wanafanya mashambulizi kwa mpangilio. Kwa nini wasijinyakulie mashabiki?”
Mwingine alikwenda mbali zaidi: “Stars wanabutua tu mbele na kukimbia kimbia ovyo. Nani anataka soka la namna hiyo!!! Hawana hadhi kabisa ya kucheza ndani ya uwanja mzuri kama ule. Wanaudhalilisha sana uwanja wetu.”
Hayo ndiyo yaliyokuwa baadhi ya maoni ya mashabiki. Kusema kweli soka letu lilishindwa kutupa zawadi nzuri kwenye kilele cha sherehe za miaka 50.
Hata klabu ya Simba ilishindwa kututoa kimasomaso ilipocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na kufungwa bao 1-0 licha ya kuwapo kwa majigambo kabla ya mchezo huo kuchezwa.
Hebu tubadilike jamani. Ratiba ya michuano ya kuwania kufuzu fainali za Afrika mwaka 2013 inaonyesha ya kuwa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itaanza raundi ya pili kwa kucheza na Msumbiji, mchezo utakaofanyika Dar es Salaam Februari 29 mwakani na marudiano yatakuwa Maputo, Msumbiji kati ya Juni 15 na 17 mwakani.
Maandalizi yaanze mapema. Tuanze ukurasa mpya wakati tukielekea kwenye miaka 50 mingine ijayo ya uhuru wetu. Tuanze Kuthubutu sasa ili Tuweze na Kusonga Mbele.
Toa maoni yako