Kilimo cha mjini chaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa

UZALISHAJI wa mbogamboga katika wilaya mbalimbali za jiji la Dar es Salaam sasa umeendelea kuathirika kutokana na uhaba wa maji, hali iliyosababisha kupungua kwa mavuno.

Hatua hii inakuja baada ya kuadimika kwa mvua katika maeneo mbali mbali ya nchi, ikiwemo Dar es Salaam, kwani wakulima wengi hutegemea maji ya kwenye vijito vidogo vidogo kama chanzo cha maji ya umwagiliaji.

Baadhi ya wakulima waliozungumza na Raia Mwema wamesema kwamba, kukosekana kwa maji imekuwa ni janga kubwa kwa biashara zao kwani vipato vyao vimeathirika kutokana na kupungua kwa mavuno.

Katika maeneo ya masoko mbalimbali ya mitaani, bei za mazao ya bustani ikiwemo mboga mboga sasa zimeendelea kuongezeka kutokana na kupungua kwa uzalishaji.

Wakulima walisema kupungua kwa mavuno ya bidhaa za mbogamboga kumeathiri vipato vyao, hali inayoisababisha kushindwa kumudu gharama za maisha ikiwemo kununua chakula ma matumizi mengine ya msingi.

Tatizo ya ukosefu wa mvua lilianza katikati ya mwaka jana, hali iliyosababisha kukauka kwa baadhi ya mito, ambayo maji yake hutumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

Kwa Upande wa maeneo ya Mbagala, ambako wengi ya wakulima wengi wanategemea mto Mziga kama chanzo cha maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, hasa wa mboga mboga, hali sio shwali kwani hivi sasa umekauka, na kupoteza matumaini ya wakulima hao.

Mto huo ambao kwa mwaka mzima huwa haukosi maji, mwaka huu hali imekuwa tofauti kwani umekauka kabisa, hali inayowafanya wakulima wengi watumie maji ya kununua kutoka kwa wasambazaji binafsi.

Wasambazaji wa maji binafsi katika maeneo hayo, wanatoza shilingi 2,000 kwa mita moja ya mraba ya maji (lita 1,000), kiwango ambacho ni sawa na shilingi 2 kwa lita.

Hii ni ghali zaidi ikilinganishwa na maji yanayosambazwa na Mamlaka ya Maji Safi na Salama jijini (DAWASCO) ambayo kwa mujibu wa sheria hutoza maji kwa gharama ya shilingi 1,775 kwa mita moja ya mraba.

Musa Kadingi (27) ambaye ni mkulima wa mbogamboga maeneo ya Mbagala anasema kukosekana kwa maji imekuwa ni tatizo kubwa kwao kwani hata vipato vyao vimeathirika na wanatumia gharama kubwa kuzalisha.

Kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, bei ya bidhaa hizo kwa wanunuaji wa jumla nazo zimapanda kwa takribani mara mbili, hali inayosababisha ongezeko la bei ya rejareja kwa wateja.

Kadingi alisema kwamba kutokana na kuisha kwa maji kwenye mto mzinga, hivi sasa wanatumia kaji kidogo sana kulima na wale wenye uwezo zaidi basi hununua maji ya kumwagilia kwa wasambazaji binafsi wenye visima vya maji katika maeneo ya karibu.

Alisema kwamba kupungua kwa uzalishaji, imesababisha pia kupungua kwa vipato vya wakulima wengi na wengine ambao hawana uwezo wa kununua maji, sasa wameacha kabisa kulima.

“Nilikuwa napata zaidi ya Sh300,000 kwa mwezi kutokana na kilimo cha mchicha, nyanya chungu na bamia lakini hivi sasa Napata nusu ya kipato hicho,” alisema kwenye mazungumzo na Raia Mwema.

Alisema kupungua kwa mapato hayo ni matokeo ya kupungua kwa uzalishaji, pamoja na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, hasa upatikanaji wa maji ya kutosha.

Kwa mujibu wa wakulima wengi kwenye maeneo hayo, ukosefu wa mvua pia umesababisha kuongezeka kwa magonjwa wa mazao yao hasa nyanya chungu, ambazo sasa zinaathiriwa na tatizo la ukungu mwekundu.

Japokuwa ugonjwa huo wa mboga ambao haujatambuliwa na wakulima wengi, madhara yake tayari yameshaathiri wakulima wengi kwani wakati mwingine mazao mengi yamenyauka.

“Tumajeribu kutumia dawa mbalimbali za kunyunyizia lakini hali imekuwa ni mbaya kwani ugonjwa umeongezeka na mazao mengi yameathirika,” alisema mkulima huyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) hivi karibuni kiwango cha mvua katika msimu wa mwaka huu wa masika ni kidogo kwenye maeneo mengi ya nchi hali inayoweza kusababisha ukame.

TMA ilitahadharisha kwamba endapo Watanzania hawatazitumia kwa busara mvua chache zinazotarajiwa kunyesha nchini.

Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), juu ya mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi uliopita, ulisema licha ya maeneo mengi ya nchi kutarajia mvua za wastani, maeneo mengine mvua zitakuwa kubwa.

Baadhi ya maeneo hayo ni kanda ya Ziwa Viktoria, mikoa ya Kagera, Simiyu na mikoa ya kusini mwa nchi ukiwemo Lindi, Ruvuma, Mtwara na Mashariki mwa mkoa wa Mbeya.

Mkurugenzi Mkuu wa wa Mamlaka hiyo, Dk. Agnes Kijazi, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba kwa mwaka huu mvua za masika zitakuwa chache kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Dk. Agnes alisema pia licha ya mabadiliko hayo, ambayo wengi walitarajia unafuu wa hali ya hewa katika kipindi hiki ambacho maeneo mengi likiwemo jiji la Dar es Salaam joto limekuwa juu, kuna uwezekano wa kuwepo vipindi vichache vya mvua kubwa kwenye baadhi ya maeneo.

Alisema katika utabiri wa msimu wa vuli walioutoa Oktoba, mwaka jana, walisema maeneo mengi ya nchi yangekuwa na mvua za wastani na juu ya wastani, huku wakiutaja mkoa wa Ruvuma pekee kuwa na mvua ya chini ya wastani.

Mkulima mwingine, Novatus Jackson (46) ambaye amekuwa akijishughulisha na kilimo hicho kwa miaka zaidi ya saba alisema kwamba anayaona mabadiliko hayo kila mwaka na hali inazidi kuwa mbaya.

“Nilianza kulima hapa mwaka 2009 na miaka ya zamani maji yalikuwa sio shida, lakini sasa hivi kumekuwa na uhaba mkubwa wa maji kutokana na kupungua kwa mvua,” alisema Jackson.

Kwa mujibu wa mkulima huyo, miaka ya nyuma, mvua ilikuwa inanyesha mara mbili kwa mwaka lakini mwaka juzi na mwaka jana hali haikuwa nzuri kwani kumekuwepo na uhaba wa mvua.

“Kipindi kile wakati mvua ziko nyingi, mto mzinga ulikuwa haukauki mara kwa mara kwani maji yalikuwa ya kutosha mwaka mzima, lakini sasa hali imebadilika na mto umekauka kabisa,” alisema.

Mto Mzinga ambao vyanzo vyake viko maeneo ya Kongowe, na mkoa wa Pwani (Mkuranga na Kisarawe) ambao miaka kadhaa ulikuwa ukifurika sasa limebakia korongo tu na hamna maji kabisa.

Hata hivyo, bado kuna maeneo machache ambayo yana maji, lakini ongezeko la mahitaji ya maji kwa sasa kwa ajili ya kilimo, ufugaji na ujenzi, linatishia uwepo wa maji hayo kwa muda ambao watu wanasubiria mvua za msimu.

Kutokana na hali hii, mamia ya akina mama ambao wanategemea eneo hilo kama chanzo cha bidhaa kwa ajili ya biashara yao ya uchuuzi wa mboga nao pia wameathirika kwani hivi sasa wanapata bidhaa hizo kwa bei ghali.

Wauzaji nao wanalalamika kwamba, kutokana na kuongezeka kwa bei ya jumla ya bidhaa hizo, bei ya rejareja nayo imeongezeka hali inayosababisha kupungua kwa wateja ama kupunguza kiwango cha bidhaa wanazonunua kwa siku.

“Sisi tuna mitaji midogo sana na kupanda kwa bei ya jumla ya bidhaa za mbogamboga imetuathiri kwa kiasi kikubwa kwani tunashindwa kukuza biashara zetu,” alisema Tatu Musa, muuza mboga maeneo ya Mbagala.

Japokuwa bei ya mboga katika maeneo mbalimbali bado haijaongezeka kwa kasi, kiwango cha mboga ambacho kinapatikana kwa sasa ni kidogo ikilinganishwa na kipindi cha mwaka jana.

“Ukubwa wa fungu la mchicha la shilingi mia tatu sasa sio tena kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kwani umepungua sana na wateja wengi wanalalamika,” alisema muuzaji huyo.

One thought on “Kilimo cha mjini chaathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa”

 1. ZALIA MSHUMBUSI says:

  Hili ni janga kwa taifa maana si Dar tu bali maeneo mengi mboga zimekuwa ghali.

  Nashauri serikali au wafadhili wangejikita katika uchimbaji wa visima virefu katika

  maeneo ya mashamba ili kuwezesha umwagiliaji wa uhakika kwani si rahisi kwa wakulima

  wengi kumudu gharama za uchimbaji wa visima virefu au hata marambo makubwa kwa ajili

  ya umwagiliaji. Kwa imani yangu serikali ikifanya hivyo kilimo kwa njia ya umwagiliaji kitakuwa

  na tija. Hapa sizungumzii visima vya maji kwa ajili ya maji ya kunywa vijijini nazungumzia visima na

  mabwawa ya maji kwa ajili ya mashamba ili kuchochea ukuaji wa uchumi katika kilimo na ufugaji

  kwani inasikitisha sana wakati mwingine unapopita mashambani na kuona mazao yamekauka kisa

  mvua haikunyesha wakati unaelezwa kuwa eneo husika lina maji ya kutosha katika miamba ardhini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *