HAKUNA ubishi kwamba kilimo ndiyo sekta kubwa kuliko zote Tanzania kwa kuangalia mchango wake katika pato la taifa, ajira, na mauzo nchi za nje.
Ni kweli pia kwamba masikini wengi nchini wanaishi vijijini wakitegemea kilimo kuendesha maisha yao. Katika mazingira kama haya kuwekeza katika kilimo ndiyo njia pekee ya kuchochea kukua kwa uchumi na kupunguza umasikini. Na hicho ndicho kilikuwa kiini cha kaulimbiu ya kilimo ni uti wa mgongo.
Kaulimbiu ya “kilimo ni uti wa mgongo” wa uchumi ni ya siku nyingi. Ni mojawapo ya kauli alizotumia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuhamasisha shughuli za kilimo katika miaka ya 1960 na 1970.
Kwa sababu ya dhamira ya kweli ya kuinua maisha ya wananchi aliowaongoza, kauli hiyo iliandamana na vitendo, na kweli katika kipindi hicho kilimo kilipamba moto na rekodi iliyowekwa wakati huo ya uzalishaji na mauzo nchi za nje kutokana na sekta ya kilimo haijawahi kuvunjwa hadi leo.
Maendeleo ya kijamii yanayoripotiwa katika mikoa ya Kagera na Kilimanjaro kipindi hicho ni ushahidi wa kutosha jinsi kilimo kinavyoweza kubadilisha maisha ya watu.
Lakini kwa Mtanzania yeyote ambaye huwa anasumbua ubongo wake kufikiri anajua kwamba kaulimbiu hiyo kwa sasa ni mzaha mkubwa. Watu wamefikia hatua ya kudhihaki wakisema maana ya kaulimbiu hiyo ni kwamba kilimo ni ugonjwa wa uti wa mgongo, ndiyo maana kinasusiwa. Pili, wanasema kilimo ni uti wa mgongo kwa vile uti wa mgongo hukaa nyuma, hauonekani, kwa hiyo hata kilimo cha Tanzania hakionekani; kimesahaulika.
Kutokana na hali hii, dalili ziko wazi kwamba kilimo kinaanza kuonekana kama mzigo mkubwa kwa Taifa kukiendesha. Kuna watu wanaoanza kufikiri kwamba kilimo kinakwamisha kasi ya maendeleo hivyo wangefurahi kuona Serikali inaachana na kilimo na kujikita zaidi katika kuendeleza viwanda kama njia ya kuondoa umasikini Tanzania.
Nilipata kumsikia waziri mmoja katika Serikali ya Awamu ya Tatu akiwaeleza wanafunzi wa chuo kikuu fulani nchini katika mhadhara kwamba enzi za kuweka mkazo kwenye kilimo zimekwisha, hizi ni enzi za viwanda. Na katika kuthibitisha hoja yake alitoa mfano wa nchi za Ulaya na Marekani ambako kilimo huchangia sehemu ndogo ya pato la taifa. Pia katika Bunge la Bajeti la mwaka huu, 2008, nilimsikia mheshimiwa mmoja akisema “Kutegemea kilimo ni kupitwa na wakati….”
Aliendelea kuponda kilimo huku wabunge wakishangilia kwa jinsi alivyokuwa anajenga hoja yake. Na baada ya mchango wake alipongezwa na Spika kwa kusema “Mh .... kwa jinsi unavyojieleza kuna vitu vingi vinaburudisha; nilitamani uendelee lakini kanuni haziruhusu”.
Kwa vile kauli hizi zinatoka kwa watu ambao wako karibu na viongozi wakuu wa nchi, hakuna shaka huo ndio ushauri ambao wanatoa kwa viongozi hao. Ndiyo maana si jambo la nadra kusikia kiongozi mkubwa wa nchi akitamba katika mikutano kwamba uchumi unaendelea vizuri kwa vile mchango wa kilimo unazidi kushuka katika pato la taifa.
Wale wanaoshangilia kupungua kwa mchango wa kilimo katika pato la taifa na wale wenye mawazo kama ya mbunge na waziri niliowataja juu, siwatofautishi na mbunge mmoja wa Uganda aliyewahi kutoa kioja bungeni katika kujenga hoja ya kuondoa umasikini katika nchi yake.
Mbunge yule baada ya kuona kwamba katika mji wa Kampala, ambao umezungukwa na vilima, watu wanaoishi katika vilima ni matajiri na wale wanaoishi mabondeni ni masikini, alishauri serikali iandae utaratibu wa kuhamishia vilimani wale wanaoishi mabondeni ili waweze kuendelea kama wenzao.
Hapa kwetu ni sawa na kusema, watu wenye hali duni wanaoishi maeneo kama Manzese, Dar es Salaam wahamishiwe Masaki na Oysterbay ili waendelee kama watu wanaoishi maeneo hayo.
Mantiki ni ileile kwa upande wa mchango wa kilimo katika pato la taifa. Ni kweli kwamba kadiri nchi inavyoendelea mchango wa kilimo katika pato la taifa hupungua. Lakini inabidi kilimo kiwe kinakua kwa kasi kama asilimia 8-10 kwa mwaka bila kutetereka ndipo sekta nyingine zitakua haraka na kukipita na hivyo mchango wake kuendelea kupungua kadiri muda unavyokwenda.
Tanzania kilimo kinakabwa koo ili mchango wake upungue katika pato la taifa ili tuonekane tunaendelea. Hakuna cha kushangilia, Tanzania kilimo kinakua kwa asilimia 3-4 kwa mwaka wakati idadi ya watu inaongezeka kwa wastani wa asilimia 3 kwa mwaka.
Nafahamu kwamba kwa mantiki hiyohiyo, viongozi wa Tanzania, kama walivyo viongozi wengi wa Afrika, wanatamani sana maendeleo ya viwanda na miji ya nchi za magharibi, na wanafikiri kwamba wale wamefikia kiasi hicho cha maendeleo kwa vile wana viwanda.
Hivi kipi ni sahihi? Wanaviwanda kwa sababu wameendelea au wameendelea kwa sababu wana viwanda? Kwa kushindwa kujua kipi kinatangulia na kipi ni matokeo, viongozi wetu wanafikiri tunaweza kuruka tukaingia katika ulimwengu wa viwanda. Ndiyo maana serikali nyingi za Afrika, Tanzania ikiwamo, zilijenga viwanda vikubwa mara baada ya uhuru.
Viko wapi viwanda hivyo? Vimekufa. Ziko sababu nyingi zinazoweza kuwa zilisababisha viwanda hivyo kufa, lakini kubwa ni kwamba viwanda hivyo havikujengwa kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi wa wakati huo. Walichotakiwa kufanya ni kutambua sekta mama (inayoajiri wananchi waliowengi) na kuiendeleza ili viwanda vikue kuanzia chini vikiwa vidogo huku vikiwa na mizizi imara katika sekta hiyo. Na hiyo ndiyo siri ya maendeleo ya viwanda katika nchi zilizoendelea. Wengine sekta mama zao zilikuwa misitu (Finland), nafaka (Marekani na Kanada), bandari (Singapore), huduma (Uswisi) na madini (Afrika Kusini). Kwa Tanzania, sekta hiyo ni kilimo (nafaka, mifugo, misitu na uvuvi).
Labda nitumie fursa hii kueleza kwa nini bidii zozote za kuendeleza viwanda kwa kutelekeza kilimo hazitaendeleza uchumi na kupunguza umasikini Tanzania. Wote tunafahamu kwamba asilimia 70-80 ya Watanzania wanaishi vijijini wengi wao wakitegemea kilimo ambacho hakina tija hivyo ni masikini wa kipato. Katika mazingira kama haya huwezi kuwa na viwanda vya maana kwa ajili ya soko la ndani kwa vile ni asilimia 20-30 tu ya watu ina kipato cha maana kuweza kununua bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivi, labda kama viwanda hivyo vinajengwa kwa ajili ya kuuza bidhaa nje ya nchi tu.
Lakini kiuchumi tunaambiwa katika ulimwengu wa ushindani nchi haiwezi kuwa na soko la nje imara wakati soko la ndani linalegalega. Soko la ndani ni muhimu kwa viwanda, kwanza, kwa kupata uzoefu, na pili kama sponji ya kufyonza mishtuko ya kibiashara nje ya nchi.
Katika mantiki hiyo, utaona wazi kwamba kasi ya kukua kwa uchumi wetu inakwamishwa na kuwa na watu wengi wasio na kipato cha maana, ambao tumekwisha kuona hapo juu kwamba ni asilimia zaidi ya 70 na wengi wao ni wakulima.
Ukimuuliza mtu ambaye si mkulima na wala maisha yake hayategemei kilimo moja kwa moja juu ya namna anavyoathirika na umasikini wa wakulima, anaweza kukwambia umasikini wao haunihusu kwa vile ni daktari wa watu, mwandishi wa habari, rubani, mcheza mpira, profesa wa chuo, mfanyakazi wa benki ama mtumishi wa umma.
Ukimuuliza anaonaje kipato chake kazini au katika shughuli zake, atakwambia hapa kipato ni duni sana. Ukimdadisi kwanini unapata kidogo atakwambia roho ya kinyonyaji ya mwajiri.
Ukweli si hivyo, kinachotokea ni kwamba kipato cha mwajiri hakitoshi kwa vile wanunuzi ni wachache. Kwa mfano, kama kampuni ya magazeti inauza nakala 5,000 kila siku kwa sababu wanunuzi ni sehemu ya wale asilimia 20 wenye uwezo wa kununua. Lakini kama hawa asilimia 80 ambao ni masikini wangekuwa na kipato, kampuni ya magazeti ingeuza nakala 50,000. Kipato kingeongezeka na mwandishi angelipwa vizuri zaidi. Au tuseme mtu ni mcheza mpira, analipwa laki nne kwa mwezi. Hii ni kwa sababu wanaoingia viwanjani kuangalia mpira ni sehemu ya asilimia 20 wenye uwezo. Kama masikini wangekuwa na kipato wangejaza viwanja na wachezaji wangelipwa vizuri. Rubani angesafirisha abiria wengi zaidi, daktari mwenye hospitali binafsi angetibu wagonjwa wengi zaidi badala ya kufia majumbani kwao na watumishi wa umma wangepata masilahi mazuri zaidi kwa vile walipa kodi wangekuwa wengi zaidi. Biashara zingechangamka na viwanda vingeongeza uzalishaji kwa vile soko lingekuwapo. Na hilo ndilo lingeongeza kasi ya kukua kwa uchumi na umasikini kupungua.
Kwa maelezo hayo hapo juu tunajifunza vitu viwili muhimu. Kwanza, mjadala wa nini kifanyike kupunguza umasikini wa wakulima unamgusa kila mtu bila kujali kazi anayofanya. Pili, sisi kama jamii tusipopata njia ya kufanya kupunguza umasikini wa kipato kwa wakulima, nchi kuendelea litakuwa ni jambo la muujiza.
Ni wazi Serikali inalijua hilo na mataifa mengi ya Afrika yanalijua hilo. Ndiyo maana kuna mikakati mingi ya kuwekeza katika kilimo na mabilioni yanatumika katika kazi hiyo. Suala la kama uwekezaji huo ni wa kimkakati au ni upotezaji wa fedha na mali za umma na wafadhili ni kitu kingine na nitaligusia tena baadaye.
Kwa upande wa Muungano wa Afrika (AU) nchi wanachama zinasisitiza suala la kuwekeza katika kilimo kama njia ya kuanzia katika kuondoa umasikini wa watu wa bara hili. Ndiyo maana walipitisha Azimio la Maputo. Azimio hilo lilitokana na ukweli kwamba sekta ya kilimo, kwa muda mrefu, itaendelea kuwa injini ya kukua kwa uchumi katika mataifa mengi ya Afrika hasa kusini mwa jangwa la Sahara. Pamoja na ukweli huo, waliona kwamba uwekezaji katika kilimo katika eneo hili umeendelea kuwa chini sana ukilinganisha na maeneo mengine duniani.
Kwa mfano, Ulaya pamoja na kwamba kilimo kinachangia asilimia mbili tu ya pato la taifa, uwekezaji katika sekta hiyo ni asilimia 50 ya bajeti ya nchi zilizo katika muungano wa Ulaya.
Kwa afrika ambako kilimo kinachangia kati ya asilimia 20 na 50 ya pato la taifa, uwekezaji umekuwa asilimia 5.6 ya bajeti za nchi hizi.
Matokeo kilimo kimeendelea kukosa tija hivyo kushindwa kuondoa umasikini na kuchangia kasi ya maendeleo ya uchumi. Kwa kuzingatia ukweli huu ndipo wakuu wa nchi za AU, katika mkutano wao wa kawaida Julai 2003, mjini Maputo, wakaazimia kwamba nchi zote wanachama watenge angalau asilimia 10 ya bajeti zao kwa ajili ya kilimo na maendeleo vijijini – hilo ndilo linaloitwa “Azimio la Maputo”.
Kwa bahati mbaya tangu kupitishwa kwa Azimio hilo ni nchi sita tu mpaka sasa ambazo zimeitikia wito huo. Nchi hizo (kiwango kinachokwenda kwenye kilimo katika mabano) ni Niger (20%), Ethiopia (16.8%), Bukina Faso (13.7%), Chadi (12%), Mali (11%), na Malawi (11%). Kwa bahati mbaya hakuna nchi ya Afrika Mashariki ambayo imefikia kiwango kilichoazimiwa. Kwa mfano, Kenya imefikia asilimia 7.5, Tanzania asilimia 6, Uganda asilimia 3.5, na Burundi asilimia 2.
Binafsi namshukuru Mungu kwamba Tanzania haijaongeza sana bajeti yake katika kilimo kufikia hizo asilimia zilizopendekezwa na AU. Naomba nisieleweke kwamba napinga ongezeko hilo na hivyo kujichanganya katika hoja, napenda niseme mapema kabisa kwamba ingawa suala la kutenga kiasi kikubwa cha bajeti katika kilimo linapigiwa upatu, hatuna budi kuelewa kwamba kutenga fedha ni kitu kimoja na namna ya kutumia hizo fedha ni kitu kingine. Hivyo, kabla fedha hazijaongezwa ni vizuri kujiuliza ni kiasi gani cha fedha hiyo ndogo inayotengwa kwa sasa kinatumika kwa malengo sahihi yenye kuleta tija katika sekta ya kilimo.
Yawezekana kabisa sehemu kubwa ya fedha hii inatumika kununua na kuendesha magari ya kifahari, kugharimia makongamano na warsha, na kulipa posho za vikao. Hivyo kuongeza bajeti ya kilimo itakuwa ni kuongeza magari ya kifahari na idadi ya makongamano. Jiulize hapa Tanzania ni mikutano mingapi inaenedelea kila siku kwenye mahoteli ya kifahari katika fukwe za Dar es Salaam, Bagamoyo na Mwanza, katika miji maarufu kama Arusha, Morogoro na Dodoma, eti wanajadili namna ya kuondoa umasikini hasa wa mkulima.
Maudhui ya mikutano mingi kama hii niliyowahi kuhudhuria ni yaleyale – Tanzania ni nchi iliyobarikiwa sana; ina mabonde mazuri yenye rutuba. Hilo tayari tunalijua, tunataka njia ya kutumia fursa hizo kuleta maendeleo ya watu.
Yawezekana hali ndiyo hiyo hata katika mataifa mengi ya Afrika – fedha zinazotengwa kwa ajili ya kilimo haziendi kwenye kilimo. Ndiyo maana hata zile nchi tulizotaja hapo juu kwamba zimeitikia wito wa kuwekeza asilimia 10 ya bajeti zao katika sekta ya kilimo, tija katika sekta hiyo haijawa na tofauti kubwa na ya zile ambazo hazijafanya hivyo.
Mfano, Kenya, Eritrea, Guinea, Nigeria na DRC, zimeshuhudia sekta zao za kilimo zikikua kwa zaidi ya mara mbili hata bila kufikia asilimia 10 iliyokubaliwa Maputo.
Kuna mifano ya matumizi yasiyo makini ya fedha zinazolenga kuendeleza kilimo hapa Tanzania. Nilipata bahati ya kuongea na kiongozi mmoja wa wilaya fulani kuhusu wanachofanya kutekeleza tamko la Rais la kufanya Mkoa wa Morogoro kuwa ghala la chakula la Taifa. Akaniambia kwamba wanaendelea vizuri na maandalizi; wamekwisha kununua luninga za kutosha, magari yamekwisha kuandaliwa, na watumishi (posho) wako tayari kwa kuzunguka vijiji vyote katika wilaya yake wakionyesha video za kilimo bora. Kazi hii ilitarajiwa kutumia shilingi bilioni moja. Matarajio ya mkakati huo ni kwamba baada ya hapo wakulima watalima vizuri zaidi na Morogoro itakuwa Ghala la Chakula la Taifa! Hivi ni kweli wakulima hawalimi vizuri kwa sababu hawajui mbinu za kilimo bora? Kama si mkakati wa kifisadi, sina woga kusema kwamba huu ni uvivu wa kufikiri.
Mfano mwingine wa matumizi ya fedha za kilimo ambayo tija yake inatiliwa shaka ni ruzuku katika pembejeo, hasa mbolea. Januari 2006 nilipata bahati ya kufanya utafiti wa masoko ya mazao ya kilimo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini chini ya udhamini wa Taasisi ya Utafiti wa Sera za Chakula (IFPRI).
Katika utafiti huu mambo mengi yalijitokeza toka kwa wakulima lakini kubwa zaidi lilikuwa suala la hujuma katika mbolea ya ruzuku.
Katika vijiji vyote tulivotembelea: Lyamukena, Kiumba, Mtwango, Igongolo, Manga, Tunduma Mjini, Majengo, Maporomoko, Mwaka, Katete, Namore na Chindi, wakulima walilalamikia bei kubwa ya mbolea.
Kwangu suala hili nililipokea kwa mshangao kwa vile nilijua kwamba mikoa hii ilikuwa chini ya mpango wa mbolea ya ruzuku. Hii ilinifanya kutafuta habari zaidi kuhusiana na suala hili. Niligundua hujuma kubwa iliyokuwa ikiendelea. Kwa uzalendo wa hali ya juu niliweka wazi mbinu zote zinazotumika kufanikisha hujuma hii. Ilikuwa ni siri iliyowazi kwamba mbolea ilikuwa inavushwa kwenda nchi za jirani, na sehemu nyingine iliishia katika maduka ya wauza pembejeo.
Hivyo ndivyo mabilioni yaliyotengwa katika bajeti kwa ajili ya kuendeleza kilimo yanavyotumika. Takumbuke kwamba lengo kuu la kuanzisha programu ya mbolea ya ruzuku lilikuwa ni kuwezesha Taifa kuondokana na tatizo sugu la uhaba wa chakula kwa kuwawezesha wakulima wa mahindi kupata mbolea.
Lakini tangu mpango huo ulipoanzishwa uzalishaji wa mahindi haujabadilika pamoja na mabilioni yote yaliyotumiwa katika mpango huo, karibu bilioni 30 katika miaka miwili ya mwanzo.
Inaendelea
Toa maoni yako