RIPOTI ya Umasikini na Mandeleo ya watu ya 2007 inayotolewa na kitengo cha kuangalia maendeleo ya MKUKUTA cha Wizara ya Fedha na Uchumi, inaonyesha kwamba kati ya mwaka 2001 na 2007 idadi ya watu wanaoishi katika umasikini Tanzania imeongezeka kwa milioni moja toka millioni 11.7.
Inathibitisha pia kwamba umasikini unapungua kwa kasi ya kuridhisha mijini kuliko vijijini. Mfano, wakati kwa Dar es Salaam umasikini umepungua toka asilimia 28.1 mwaka 1991 hadi asilimia 16.2 mwaka 2007, vijini umasikini umepungua kwa asilimia tatu tu toka asilimia 40.8 hadi asilimia 37.4 katika kipindi hicho.
Kwa mwenendo huu wa mambo malengo ya Maendeleo ya Milennia ya kupunguza umasikini wa kipato hadi asilimia 19 ifikapo 2015 na malengo ya MKUKUTA ya kupunguza umasikini wa kipato hadi asilimia 19 ifikapo mwaka 2010 yamekwisha kushindikana.
Hiyo inatuonyesha kuwa mbinu zinazotumiwa na Serikali na wadau wengine kukuza uchumi na kupunguza umasikini zimeshindwa. Sasa basi kuna haja ya kujaribu fikra mpya, pengine ambazo si za kawaida.
Kabla sijapendekeza njia mbadala ya kuleta mapinduzi kwenye kilimo, nianze kwa kuchambua mapungufu yaliyomo katika mikakati na mbinu zinazotumika kuendeleza sekta ya kilimo Tanzania. Udhaifu wa kwanza wa mikakati hiyo ni kushindwa kuzingatia ukweli kwamba kilimo si shughuli ya kudumu ya kiuchumi ya watu walio wengi!
Ni shughuli ya mpito kuelekea katika shughuli za uchumi ambazo ni imara zaidi. Ndiyo maana tumekwisha kusikia mara nyingi kuwa mojawapo ya kipimo cha maendeleo ya kilimo ni kuwa na wakulima wachache wenye uwezo wa kulisha watu wengi zaidi.
Wakulima wakiwezeshwa kupata kipato kizuri kutoka katika kilimo, sheria ya kimaumbile inasema watahama kilimo na kuanzisha shughuli nyingine zisizotegemea kilimo moja kwa moja, mfano, huwekeza katika viwanda vidogo vya usindikaji, usafirishaji, biashara ya huduma kama hoteli ama duka, na baadaye huhama kilimo kabisa.
Watu wengi zaidi huajiriwa katika biashara hizi kwa maana hiyo wanaolima huzidi kupungua. Wale wanaoacha shughuli za kilimo wanakuwa sehemu ya soko la wanaobaki katika kilimo. Kadiri watu wanavyohama shughuli ya kulima ndivyo wanaobaki katika shughuli hiyo huzalisha zaidi kwa vile wanunuzi, yaani soko (wale wasiolima) lipo na ardhi iliyoachwa na wale walioondoka ipo. Uwezekano wa kutumia zana za kisasa katika kilimo (mechanisation) huongezeka kuliko hapo awali ambapo kulikuwa na vishamba vidogovidogo. Inafika mahala ambapo mkulima mmoja anaweza kulisha watu wengi zaidi na mchango wa kilimo katika pato la taifa hupungua.
Kwa mantiki hiyo basi, mikakati yenye lengo la kuendeleza kilimo inabidi ilenge kwenye kuweka mazingira ya kuongeza kasi ya watu kuhama kilimo. Hapa simaanishi kwamba watu wahamishwe kwa nguvu bali kwa kuwawezesha kupata kipato ambacho, kama tulivyoona hapo juu, kitawafanya wahame wenyewe kwa kujua au kutokujua.
Kushindwa kutambua ukweli huo matokeo yake miradi mingi ya kilimo nchini hulenga katika kufanya maisha ya wale walio kwenye kilimo yavumilike, wapate unafuu fulani wa maisha na wala si kuwabadilisha hasa. Hebu fikiria mradi wa mabilioni ya fedha unaishia kugawa kuku wawili au watatu kwa kaya kadhaa, au kukopesha mbuzi/ng’ombe mmoja, au kujenga banio dogo tu la kumwagilia ekari 15-20 hivi, au kujenga soko dogo la kuuzia mazao ya kilimo, au tuseme kuwapa wakulima maji ya kunywa ya bomba.
Vitu hivyo vitawapa unafuu wa maisha lakini haviwezi kuleta mabadiliko ya msingi tunayotazamia katika kilimo. Kwa kifupi mipango yetu mingi hailengi mbali (not ambitious), inaweka malengo mepesi mno. Hata linapokuja suala la kujilinganisha (benchmarking) tunajilinganisha na wale waliokaribu na sisi; wasiofanya vizuri (low performers).
Tunajisifu, eti angalia hatuko mbali sana na jirani zetu au mataifa mengine yanayoendelea – kwa mtindo huo tunajikwamisha wenyewe. Ni vizuri tukalenga mbali. Na hivi ndivyo wenzetu wa Magharibi walivyoendeleza nchi zao. Ile mifereji ya maji tunayoona huko, barabara za juu na chini ya ardhi havikutokana na kuwa na malengo mepesi kama yetu.
Hapa wengine watasema sisi ni masikini; fedha haitoshi kufanya mambo makubwa. Kama hiyo ni kweli basi tukae chini tupange vizuri kimkakati tufanye nini, tuache nini kwa fedha finyu iliyopo. Kama fedha haitoshi ina maana gani kutekeleza miradi husika nchi nzima? Nafikiri ingekuwa busara kuelekeza fedha hiyo katika mojawapo ya mabonde mazuri yanayofaa kwa kilimo cha mpunga angalau tukajitosheleza kwa mchele. Rais Jakaya Kikwete alipotangaza kwamba Morogoro litakuwa ghala la chakula la Taifa nilidhani ulikuwa mwanzo mzuri.
Udhaifu mwingine katika kuendeleza kilimo ni kwamba mikakati imetawanyika mno. Inajaribu kushughulikia wakulima wote na mazao yote kwa mbinu moja. Tukianza na hili la wakulima. Si sahihi wakulima wote wakawekwa katika kapu moja na baadaye ukawapo mkakati wa kuwaendeleza kama kundi moja.
Ni vizuri wakulima wakawekwa katika makundi, kwa kuzingatia ukubwa wa biashara yao katika kilimo, mfano, tukawa na wakulima wakubwa, wa kati, na wadogo wadogo. Hii itatusaidia kujua tunapoleta mkakati fulani ni kundi lipi hasa linalengwa.
Kwa mfano, serikali inaposema banki ya Rasilimali Tanzania (TIB) itaimarishwa ili iwakopeshe wakulima, tujue ni kundi gani hapa linalengwa. Tunapoanzisha mpango wa ruzuku kwenye pembejeo tunalenga wakulima wa kundi lipi hasa. Hoja hii itaeleweka vizuri zaidi baadaye kidogo.
Kwa upande wa mazao, mikakati iliyopo inajaribu kushughulikia mazao yote kwa uzito sawa. Mara kabeji, mara karoti, hoho, kahawa, pamba, vanilla, pilipili, iriki, fenesi, machungwa, mchele, mahindi na mtama. Sina maana kwamba baadhi ya mazao si muhimu lakini ukweli ni kwamba yana uzito tofauti kimkakati.
Ikumbukwe kwamba sehemu kubwa ya Tanzania ipo kati ya meta 0 na meta 2,000 juu ya usawa wa bahari. Kwa maana hiyo, nchi hii inaweza kuzalisha mazao ya aina zote, na mifugo ya kila aina iliyopo duniani. Hali hii badala ya kuwa baraka imegeuka kuwa balaa kwa nchi.
Hebu tujiulize kama Tanzania ingejikuta iko katika sehemu ambayo kijiografia ina uwezo wa kuotesha mazao mawili au matatu tu. Naamini kilimo chetu kingeendelea kwa kasi kwa vile tusingetawanya rasrimali, tungezielekeza katika mazao hayo machache kuliko ilivyo sasa tunavyotawanyika bila kuwa matokeo ya maana.
Ndiyo maana nchi kama Misiri inazalisha ngano na mchele wa kutosha hadi kuuza nchi za nje wakati inategemea mto mmoja tu – Mto Nile. Israel pamoja na kuwa jangwani, inaweza kuvuta maji toka Bahari ya Galilaya na kujitosheleza kwa chakula na matunda na kuuza ziada nje ya nchi.
Sisi pamoja na mito yote hiyo hatuwezi kujitegemea kwa chakula. Maji ya mito yanaachiwa kwenda baharini bila mpango wowote wa kuweka mabwawa ya udhibiti kuyafanya yawe maeneo mahsusi ya kuzalisha mazao. Hivyo hatunabudi kuyaweka mazao yetu katika makundi na baadaye tuwe na mkakati tofauti kwa kila kundi la mazao.
Vilevile, mikakati yetu imeshindwa kutambua kwamba matatizo yanayokabili sekta ya kilimo yana uzito tofauti, hivyo utatuzi wake unahitaji vipaumbele tofauti. Yawezekana kabisa kwamba yale yenye uzito mkubwa yakishughulikiwa inavyostahili mengine yatakwisha yenyewe. Kwa uzoefu wangu, ukiachilia mbali majanga ya asili, changamoto kubwa katika sekta ya kilimo iko katika mfumo wa masoko.
Soko ndilo injini ya kuendesha mfumo mzima wa uzalishaji kwenye biashara ya aina yoyote. Iwapo wakulima wangepata soko la uhakika la bidhaa zao, wangekwenda wenyewe kutafuta mbolea, mikopo, mbegu bora, trekta, utaalamu, teknolojia ya umwagiliaji na madawa ya kuua wadudu na magugu.
Ikumbukwe kwamba kutumia pembejeo za kisasa ni kuongeza gharama za kuzalisha, hivyo soko la mazao ya kilimo lazima litoe bei itakayorudisha gharama hizo. Wakati umefika kutumia sehemu kubwa ya fedha za miradi ya kilimo kushughulikia changamoto za masoko. Tukifanya hivyo zile za uzalishaji zitashughulikiwa kiurahisi.
Mashirika yasiyo ya kiserikali, mfano, MVIWATA na FaidaMali, na baadhi ya wafadhili, wamekwisha kutambua ukweli huo na wamejikita katika kushughulikia changamoto za masoko ya mazao ya kilimo kwa njia ya value chain development kama njia muafaka ya kuendeleza kilimo.
Toa maoni yako