ILE minong’ono ya muda mrefu na ya chini chini juu ya ukwasi mkubwa wa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, hatimaye imewekwa bayana, na umma wa Watanzania umejua.
Kwa hakika huu ni mwendelezo wa kufichuliwa kwa ufisadi mkubwa unaofanywa na viongozi wenye dhamana ya kutupeleka kwenye ‘ Tanzania yenye Neema’, badala yake wanajineemesha wenyewe.
Wiki iliyopita gazeti moja la kila siku nchini liliandika habari juu ya kuchunguzwa kwa waziri mmoja mwandamizi kuhusiana na ununuzi wenye utata wa rada ya kijeshi, mwaka 2002.
Habari hiyo iliibua hisia na hamu ya wasomaji kutaka kujua waziri huyo ni nani huku wengine wakipitia baraza la mawaziri la mwaka huo na bila shaka Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wakati huo, Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Ulinzi Profesa Philemon Sarungi walikuwa walengwa wakubwa.
Lakini kwa vile Sarungi hayumo katika baraza la mawaziri katika serikali ya awamu ya nne basi aliyebaki kuhisiwa ni Profesa Mwandosya na Chenge.
Lakini wakati Watanzania wakiwa na shauku ya kutaka kujua ni waziri gani, gazeti moja la Uingereza, The Guardian, lilitegua kitendawili hicho kwa kumtaja Chenge kwamba ndiye anayechunguzwa kuhusiana na sakata hilo la rada. Na bila hiana magazeti ya nchini nayo yakalinukuu na kutupasha sisi ambao hatuna uwezo wa kusoma magazeti ya Uingereza kwenye mtandao. Hilo ni jambo jema kutujulisha kwani tunaoumia na mzigo huu wa ufisadi ni sisi Watanzania na si Mwingereza.
The Guardian lilienda mbali zaidi kwa kusema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Chenge ana akaunti katika Kisiwa cha Jersey yenye dola milioni moja (zaidi ya shilingi bilioni 1). Hizi ni dola la Kimarekani, si dola za Zimbabwe!
Chenge na mwanasheria wake aliyeko Ohio, Marekani wamekiri kuwa akaunti na fedha zilizomo ni zake lakini wakakanusha kuwa fedha hizo hazihusiani na kashfa ya ununuzi wa rada. Kwa hiyo hilo la uhalali wa akunti na kiasi cha fedha halina mjadala; ni mali ya Andrew Chenge.
Tunashukuru kwa kukubali maana wengi hukana akaunti zao za kifisadi pale zinapogunduliwa. Ieleweke mapema kabisa kwamba lengo la makala hii si kujadili kama fedha hizo zinatokana na ‘dili’ ya kununua rada ya pauni za Uingereza milioni 28 (zaidi ya shilingi bilioni 70), bei ambayo inasemekana ilizidishwa mno na kuwakamua vilivyo walalahoi wa Tanzania .
Suala la kama fedha hizo zinatokana na hiyo dili ya rada au siyo tuiachie taasisi ya kuchunguza makosa makubwa ya jina-Serious Fraud Office (SFO) ya Uingereza ambayo kwa mujibu wa taarifa zilizopo, ndiyo inachunguza sakata hilo .
Lakini ni kiasi cha kutumia bongo kidogo kujua kwamba mpaka kugundulika akaunti hiyo lazima SFO watakuwa wamefuatilia mlolongo wa malipo ya kibenki (bank transactions) tangu kutoka kwa mnunuzi (serikali) kwenda kwa muuzaji, kampuni ya BAe Systems ya Uingereza mpaka ‘kamisheni’ kubwa ya pauni milioni 12 aliyolipwa kwa siri mfanyabiashara Shailesh Vithlani ‘aliyechonga’ dili hiyo .
Wao si waganga wa kienyeji kwamba walipiga ramli na kugundua kuwa Chenge ana akaunti nje ya nchi tena kwenye kisiwa ya Jersey ! Hao ni wataalamu waliobobea hivyo lazima wawe na uhakika na kile wanachofanya. Lakini hilo tuwaachie SFO, huenda mambo mengi yakaibuka huko mbele kadri uchunguzi utakavyoendelea.
Maana katika sakata hii Wizara za Fedha, Mawasiliano na Uchukuzi na taasisi nyingine kama TCAA, JWTZ lazima zilihusika japo hatujui ni kwa kiwango gani wahusika walinufaika na ununuzi huo tata.
Lakini hiyo si hoja kama nilivyokwisha kusema. Hoja hapa ni ukwasi mkubwa alionao waziri Chenge. Ni ukwasi ambao umeshtua umma wa Watanzania. Katika nchi masikini kama hii waziri mmoja anapokuwa ana dola milioni moja tena kwenye benki ya nje ya nchi, inatisha na kushtua sana. Bilioni moja! Tena hiyo ni akaunti moja tu ya nje ambayo imegundulika. Hatujui ana akaunti ngapi huko nje kama Uswisi na huko Marekani ambako mpaka ameweka wakili wake.
Kuna sababu gani ya waziri au ofisa yeyote wa serikali kuwa na wakili Marekani? Anahofia nini hicho mpaka kuwa na wakili wa kimataifa ambaye anamlipa fedha nyingi za kigeni wakati tuna mawakili mahiri hapa hapa. Si bure. Na hizo ni za nje ya nchi, nina hakika kwamba lazima hapa nchini ana akaunti nyingine tena nyingi. Hizo nazo zitakuwa na mamilioni ya pesa.
Ni vigumu Chenge pamoja na utumishi wake wa muda mrefu (miaka 30) kutushawishi hizo dola milioni moja amezipataje. Atueleze ana biashara gani ya kimataifa inayomwingizia fedha za kigeni. Atueleze kama ni fedha halali, je amezitaja kwenye Tume ya Taifa ya Maadili ya Viongozi? Kama hajazitaja ni kwanini?
Atueleze kwanini amefungua akaunti nje ya nchi badala ya hapa nchini? Je, haoni hicho ni kigezo cha kufanya fedha hizo ziitwe haramu kwa mujibu wa sheria mpya ya fedha haramu? Kwa hakika maswali ni mengi mno ambayo umma wa Watanzania unasubiri Chenge (na si mwanasheria wake wa Marekani) ayajibu. Sijawahi kusikia kwamba Chenge ni mfanyabiashara zaidi ya kuwa mkurugenzi katika katika kampuni tata ya Tangold kwenye mradi uliojaa mizengwe wa kuchimba dhahabu wa Buhemba ambao nao sokomoko lake liko mbioni kulipuka.
Kuna watu wameitumikia nchi hii kwa miaka mingi tena kwenye nyadhifa za juu lakini wamestaafu bila hata kuwa na pikipiki. Kwa vyovyote vile, Chenge hawezi kutushawishi kwamba fedha hizo zinatokana na utumishi wake wa muda mrefu.
Imani ya wananchi kwa Chenge ilianza kupungua baada ya mikataba mibovu ya madini na ile ya kubinafsisha mashirika ya umma. Wengi wakiwamo wabunge wanadhani kuwa kuna ushiriki (role) wake katika mikataba hiyo ambayo serikali ya awamu ya nne iliagiza kupitiwa upya ili pande zote mbili zinufaike.
Hata hivyo, ukwasi wa Chenge ulianza kujulikana wazi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 alipogombea na kushinda ubunge wa jimbo la Bariadi Magharibi dhidi ya Isaac Cheyo wa UDP.
Kwa wapiga kura wa huko wanajua jinsi ubabe wa pesa ulivyotumika. Pili ni kwenye uchaguzi wa mwaka jana wa CCM. Na hilo pia nawachia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na wapambe wengine. Haikushangaza kwa nini aliingia Kamati Kuu (CC).
Wananchi wengi walishangazwa na kupinga pale Rais Jakaya Kikwete alipomteua tena kuwa waziri baada ya kuvunja Baraza la Mawaziri Februari mwaka huu.
Lakini hilo ni moja. La pili linaenda kwa Rais Kikwete ambaye kwa kweli anaelekea kukabiliana na changamoto nyingi wakati huu. Kuibuka kwa kashfa hiyo hakika kunazidi kuiweka serikali yake katika wakati mgumu na kushusha imani ya wananchi kwa serikali yake.
Ingawa kashfa ya rada haikutokea wakati wa utawala wake, kama ilivyo EPA, kitendo cha yeye kumwamini na kumteua Chenge kuwa waziri kunafanya wananchi wadadisi uwezo na umakini wake.
Rais ana vyanzo vingi vya habari vinavyoweza kumfanya ateue wasadizi wake ambao ni waadilifu. Kitendo cha wananchi kuguna na kuhoji kwa nini amteue tena Chenge ni dhahiri kinaonyesha kuna tatizo katika utawala wake au mfumo nzima.
Kama wananchi wanakosa imani na mtu halafu rais anamteua kuwa waziri lazima kuna walakini. Ina maana rais wetu, yote hayo alikuwa hayajui? Au?
Hata kama si fedha za rada, kitendo cha waziri kuwa na akaunti nje ya nchi yenye shilingi bilioni moja kinatosha kumtilia shaka na kutomchagua.
Au rais atueleze alimteua kwa vigezo vipi? Je, alifadhili kampeni zake au ni mtu wake wa karibu kama tulivyozoea kuambiwa? Na kama ni ukaribu unatokana na nini? Maana huwezi kuwa karibu na mvuta bangi wakati wewe huvuti! Pia inakuwaje wananchi wanakuwa na shaka na mtu fulani na baadaye shaka yao inathibitika lakini rais na mfumo wake wanashindwa kupata mashaka au uthibitisho huo mapema kabla ya kufanya maamuzi kama hayo ya uteuzi?
Nchi inakwenda wapi kama wananchi ‘wanaona’ kuliko utawala? Hakika jambo hili linazidi kushusha si tu umaarufu wa serikali ya Kikwete bali hata yeye mwenyewe. Wananchi wanaanza kuona anakumbatia ‘marafiki’ ambao wanaandamwa na tuhuma za ufisadi. Mwisho wa siku watu wataanza kuhoji usafi wake mweyewe iwapo amezungukwa na marafiki wa aina hiyo.
Na hili la Chenge ni moja tu kati ya mengi ambayo tayari tumeyashuhudia. Swali hapa ni vipi Rais Kikwete atamaliza uoza wote huu?
Wakati masuala ya ufisadi yanazidi kupamba moto na kuibuka kila kukicha, suala la Muafaka wa Zanzibar ni mzigo mwingine unaomsubiri Rais Kikwete.
Tunasubiri kuona ile kauli yake wakati akihutubia Bunge, Desemba 30, 2005 kwamba: I might be wearing a smiling face but I am firm on issues (Naweza kuonekana mtu wa kutabasamu tu, lakini nina msimamo kwenye mambo ya msingi).
Mwisho ushauri wa bure kabisa kwa Rais Kikwete: wakati umefika aamue moja, urafiki/ ukaribu wa kimaisha/kikazi au kuwatumikia Watanzania waliomchagua kwa kishindo (asilimia 80.2) mwaka 2005.
Ni ukweli ulio wazi kwamba wananchi wengi wameng’amua kwamba wengi wanaohusishwa na ufisadi ni wanamtandao ambao walimsaidia kuingia madarakani.
Sasa wakati umefikia achague kusuka ama kunyoa. Aweke mbele maslahi ya Taifa au maslahi ya marafiki na waliomfadhili kwenye uchaguzi.
Wananchi wanajua kinachoendelea hivyo si watu wa kudanganywa muda wote:you can’t cheat all the people all the time. Huu ni wakati wa maamuzi mazito.
Na watu walikwisha kufanya maamuzi mazito, yeye hatakuwa wa kwanza, mifano ya karibuni kabisa ni ya Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika, au Rais wa Ukraine Viktor Yushchenko ambaye aliingia madarakani mwaka 2004 kwa Mapinduzi ya Chungwa (Orange Revolution) lakini mwaka mmoja baadaye (2005) aliamua kuvunja Bunge na kumtimua Waziri Mkuu wake ambaye alikuwa mtu wake wa karibu sana Bi. Yulia Tymoshenko baada ya ufisadi mkubwa na kuporomoka kwa uchumi.
Wengi waliohusishwa na ufisadi ni marafiki zake wa karibu waliokuwa wakiongoza naye maandamano ya umma pale Kiev lakini ilifikia hatua akaamua kuweka urafiki pembeni na kuweka mbele maslahi ya taifa. Akawatema na kulazimika kumteua hasimu wake kisiasa Viktor Yanukovych kuwa Waziri Mkuu.
Hii ni aina ya mifano kuonyesha kwamba mambo yanapokwenda mrama, inabidi ufanye maamuzi yenye maslahi ya taifa na si kuangalia huyu ni nani, ama tukoje naye.
Swali moja la kujiuliza ni je, katika mazingira haya tutafika kwenye Tanzania yenye neema tuliyoahidiwa mwaka 2005? Tukumbuke umebaki mwaka mmoja na nusu kufikia Uchaguzi Mkuu. Je, Rais Kikwete atakuwa na miujiza gani katika kipindi hiki kifupi? Niseme tu kwamba kwa awamu hii ya kwanza tusahau neema tuliyoahidiwa. Labda kama atapata awamu nyingine!
Toa maoni yako