Habari
Kina Zitto hatarini
Mwandishi Wetu
Toleo la 191
22 Jun 2011
  • CCM yataka kubadili aliyoanzisha Samuel Sitta

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama, kimeanza kushawishi ili kiongoze Kamati nyeti za Bunge ambazo Spika aliyepita Samuel Sitta, aliziweka katika uongozi wa wabunge wa Upinzani, imefahamika.

Mukama alidokeza mwelekeo huo wa ushawishi wakati akihutubia mamia ya wahitimu wa vyuo vikuu mkoani Dodoma, mwishoni mwa wiki, katika hafla maalumu iliyofanyika ukumbi wa Royal Village, Dodoma na kwamba kazi hiyo itawezekana kwa kuwa tayari wakati huo CCM kitakuwa kimekwisha kujivua gamba na mpango huo utawezeshwa na kuwapo kwa wabunge wake makini.

Kama Mukama ataendelea na ushawishi huo, ni dhahiri kuwa unaweza kufanikiwa kutokana na ukweli kuwa wabunge wengi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wa CCM na kwa kuzingatia mazingira maalumu, kanuni za Bunge zinaweza kubadilishwa.

Ingawa katika maelezo yake kwa wahitimu hao wa vyuo vikuu Mukama hakuweka bayana, lakini kamati za kudumu za Bunge ambazo zimetengwa kwa mujibu wa kanuni kuongozwa na wabunge wa Upinzani ni kamati tatu za kudumu.

Hizo ni Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Kabwe Zitto na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema.

“CCM ina wabunge wengi wasomi na wenye uwezo mkubwa sana kuliko hata wengine. Tunataka chama hiki kiwe wazi zaidi na kuisimamia karibu zaidi Serikali....sasa mimi nashangaa pamoja na kuwa na wabunge wengi hao kamati muhimu wanawapa wapinzani,” alihoji Mukama katika hali inayotafsirika kuwa malengo ya CCM kujivua gamba ni kuimarisha uwazi zaidi na chama hicho kutaka kuisukuma moja kwa moja Serikali katika utendaji, uadilifu na kusikiliza kilio cha wananchi wakati wote.

Hata hivyo, bado haijawekwa bayana kama suala hilo tayari limejadiliwa na Sekretariati ya CCM ambayo pia kama imejadili ni lazima kulifikisha suala hilo kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu yake, ikitarajiwa kuwa ni suala linaloweza kufanywa kwa ‘usiri’ ili kukwepa kile kinachoweza kuelezwa kuwa kuingilia mhimili huru wa Bunge.

Uamuzi wa kamati hizo kutakiwa kuongozwa na Upinzani uliasisiwa na Spika aliyepita Sitta, ambaye aliweka bayana kuwa lengo lilikuwa kusaidia uwajibikaji zaidi na kuondoa mgogoro wa maslahi kwa kuwa hesabu zinazosimamiwa ni za Serikali ya chama tawala.

Hata hivyo, Sitta alishawishi uamuzi huo akirejea taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola katika mazingira ambayo CCM na Serikali ilikuwa imezongwa na kashfa kubwa za kampuni ya kufua umeme ya Richmond iliyosababisha aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili waliopata kuongoza Wizara ya Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Mbali na kashfa hizo, kashfa nyingine zilizoshika kasi ni pamoja na kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) Benki Kuu ya Tanzania.

Kansa ya CCM

Katibu Mkuu huyo wa CCM, katika hatua nyingine alisema hatua iliyochukuliwa na chama hicho ya kujivua gamba inagusa masuala mengi ikiwamo kuondoa kansa ya baadhi ya vigogo kujipangia safu binafsi za uongozi hasa nyakati za uchaguzi wa ndani, akiweka bayana kuwa hayo ndiyo mazingira yanayokitafuna chama hicho katia maeneo mengi, ukiwamo Mkoa wa Arusha.

Mgogoro umekuwa ukirindima mkoani Arusha kati ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), James Millya na Katibu wa CCM Mkoa Mary Chatanda huku taarifa zikieleza kuwa katikati ya mtafaruku huo mkubwa, unaoelezwa kuwa sasa umepozwa, yupo Lowassa ambaye ana waumini katika makundi ya vijana yanayoongozwa na Millya.

“Kuna kansa ya kupanga safu za uongozi katika chama na haya ni matatizo pia yaliyojitokeza Arusha. Kuna rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia wakati fulani wajumbe wote wa huko hawatokani na wanachama bali ni wajumbe wa kiongozi fulani,” alisema Mukama akiwahutubia mamia ya wahitimu hao wa vyuo vikuu mkoani Dodoma, ambao ni wanachama wa CCM.

Udhaifu wa CCM

Kama vile akiachia wenye akili kumaizi, Mkama hakwenda kwenye undani wa suala hilo la magomvi ndani ya CCM na badala yake aliendelea kufichua orodha ya maeneo dhaifu katika kuimarisha chama hicho.

Kwa mujibu wa Mukama, kuna mazingira mahsusi ya udhaifu yaliyoshinikiza chama hicho kujipanga upya katika mwekeleo wa kujivua gamba ambao alisisitiza kuwa ni kipindi cha mpito na si msukosuko.

Maeneo hayo ni mosi; dhuluma za ufisadi, pili; udhaifu wa vyombo vya uamuzi katika chama hicho, tatu; kujipenyeza kwa wafanyabiashara wasio waaminifu na nne; kujilimbikizia vyeo. Maeneo mengine aliyotaja ni kupomoroka kwa utamaduni wa kuwajibishana; kushindwa kusimamia sSrikali yake katika maeneo kadhaa, ikiwamo baadhi ya mikataba ya uwekezaji.

Alisema  ni kutokana na matatizo hayo yote  ndiyo maana hatimaye CCM imebebeshwa mzigo na umma kwamba ni chama kinachobeba mafisadi.

“Ndiyo maana tunatakiwa kufanya mabadiliko ili chama hiki kirejee kuwa chama cha wanyonge. Hata Mwenyekiti wetu (Rais Jakaya Kikwete) amekwishakusema hata kama tukitekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa asilimia 100 kama jamii haina imani nasi katika suala la maadili tutashindwa tu.

“ Na hili limekwishajitokeza. Pale Nyamagana (Mwanza) tumetekeleza Ilani yetu vizuri, lakini tumekataliwa (kukosa ubunge),” alieleza Mukama katika mkutano huo.

Ubunge Viti Maalumu

Mukama ameeleza kuwa yapo makundi mengi maalumu ambayo CCM imeshindwa kujikita na kujipambanua nayo, ingawa pia kuna nafasi maalumu za kufanya hivyo zikiwamo za Ubunge wa Viti Maalumu.

“Kuna makundi mengi ambayo CCM haijaweza kujipambanua nayo, mfano baadhi ya Wabunge wa Viti Maalumu wanaochaguliwa hawana mizizi sawasawa katika makundi hayo,” alieleza Mukama.

Wateule wanaohoji chama

Kwa mara ya kwanza, Mukama ameweka bayana kuwa licha ya kwamba yeye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalumu iliyoundwa na Rais Kikwete kufanyia kazi mchakato wa kujivua gamba, lakini Kikwete aliwateua kutokana na sababu kubwa mbili.

Alitaja sababu hizo kuwa ni kwanza, watu wanaokijua vizuri chama lakini si wenye madaraka kwa wakati huo wa mchakato wa kutafiti namna ya kujivua gamba. Pili, ni timu ya watu wanaoweza kukihoji chama hicho ili baadaye kijijengee uhalali wa kuihoji na kuisimamia serikali.

“Tuliandaa waraka ambao Mwenyekiti aliuita A case for reform . Ameunda timu ya watu wanaokielewa vizuri chama lakini pia wasio na dhamana yoyote katika chama ili wafanye kazi hiyo kwa uhuru...watu wa kukihoji chama,” alisema Mukama.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako