Kinachomtesa Lowassa

MATOKEO ya kikao cha mwisho cha Hamashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichoonekana dhahiri kushindwa kuwawajibisha watuhumiwa wa ufisadi katika chama hicho tofauti na matarajio ya Watanzania wengi, yamedhihirisha mawazo yangu ya siku nyingi kwamba, iwapo Edward Lowassa angeamua kugombea urais mwaka 2005, Jakaya Kikwete asingekuwa Rais wa Tanzania.

Vikao vya CCM vilivyotarajiwa kukamilisha utekelezaji wa ajenda ya kujivua gamba vilivyoanza mara tu baada ya Bunge kumaliza kikao chake cha mwisho mwaka jana, vilitanguliwa na vitisho vya chama hicho kumeguka iwapo Kikwete akiwa Mwenyekiti wake, angeendelea na agenda yake hiyo.

Katika mchakato huo wa kujivua gamba baadhi ya walengwa wa hatua hiyo, wakiwa Lowassa na mwenzake Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, wote wawili ni wajumbe wa Halmashaauri Kuu ya CCM.

Kati ya watu wanaoheshimika hapa nchini, waliomtahadharisha Kikwete (kwa kutoa ujumbe wa vitisho vya chama kumeguka) juu ya dhamira yake hiyo, ni pamoja Jaji Mark Bomani, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya  Tanzania.

Baada ya kuisoma hadhari hiyo kwenye gazeti moja la hapa nchini, nilijiuliza swali moja kwa mshangao; Bomani katumwa na nani kutoa wito huo kwa Kikwete?

Vikao vya CCM vilipomalizika Dodoma na kutanganzwa kwa uamuzi uliopitishwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho juu ya kujivua gamba, ilibainika kwa Watanzania kiwango cha nguvu ya Lowassa aliyonayo ndani ya chombo hicho muhimu chenye jukumu la kupitisha uamuzi wa mwisho ya chama tawala.

Uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya CCM, haukuwa wa ajabu kwangu kwa sababu haukuwa uamuzi wa kwanza kuwashangaza Watanzania.

Wengi wetu naamini bado tunakumbuka hoja ya kulaumiwa kwa Samuel Sitta na hatimaye kutaka aondolewe katika wadhifa wa Spika wa Bunge kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, kwamba hoja hiyo ilianzishwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM. Lakini juhudi hiyo ilikwama kutokana na ajenda yao hiyo kupingwa vikali na wabunge wa CCM.

Hata hivyo, hasira hiyo ya wajumbe hawa wa Halmashauri Kuu ya CCM dhidi ya Sitta ilikuja kujidhihirisha tena baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kutokana na Halmashauri Kuu hiyo kupitisha hoja ya kumweka pembeni Sitta kugombea kwa mara ya pili uspika wa Bunge kwa tiketi ya CCM.

Kama alivyofanya Bomani kumtahadharisha Kikwete juu ya utekelezaji wa hatua ya kujivua gamba,  Chenge akiwa mmojawapo wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi, aliitisha kikao cha waandishi wa habari kupinga hatua ya Sitta kugombea uspika wa Bunge kwa mara ya pili.

Kutokana na mwenendo huu wa Halmashaauri  Kuu ya CCM, ndio maana imenilazimu kueleza fikra zangu za muda mrefu kwamba kama Lowassa angegombea urais mwaka 2005, na kutomwachia rafiki yake kama ambavyo amewahi kutamka, basi leo hii ambaye angekuwa Ikulu ni yeye na si Kikwete.

Na hilo lingewezekana kutokana na mwenendo huu wa Halmashari Kuu ya CCM na sababu nyinginezo ninazoendelea kuzieleza hapa katika safu hii.

Baadhi yetu tunaelewa kwamba Kikwete na Lowassa, wamelelewa na kukua ndani ya chama hicho kwa pamoja tangu ujana wao wakiwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kama ilivyo kawaida ya binadamu, matarajio ya mtu yeyote yule katika mahali pake pa ajira au taaluma yake, ni kufika ngazi ya juu kabisa ya uongozi katika eneo lake hilo.

Kwa maana hiyo, wakiwa wasomi, ni dhahiri kwamba hawa wawili, katika maisha yao ya siasa, walikuwa wakijipanga kuhakikisha kwamba siku moja, wanashika uongozi wa ngazi ya juu kabisa za kisiasa hapa nchini. Hivyo wote wamekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kushika urais wa Tanzania.

Kujitokeza kwao wote kugombea urais mwaka wa 1995, kunadhihirisha hoja hii. Wakati Lowassa alienguliwa kutokana na kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, dhidi ya wasiwasi kuhusu mali alizojilimbikizia; Kikwete alisonga mbele.

Lakini naye kura za Mkutano Mkuu wa CCM, katika duru ya pili ya kumpata mgombea kwa tiketi ya CCM hazikutosha. Benjamin Mkapa akawa mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.

Kwa hamu hiyo ya wote kutaka kushika urais mwaka 1995, naamini kwamba wote wawili walikuwa na lengo hilo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ulipowadia. Lakini kwa makubaliano, kama alivyowahi kutamka Lowassa, aliamua kumwachia mwenzake kwa sababu alijua ana uwezo.

Naamini pia kwamba hakuchukua uamuzi  huo mgumu bila makubaliano maalumu. Kwa maana hiyo, hata baadhi ya makala zilipojitokeza katika magazeti hapa nchini kuonyesha wasiwasi wa baadhi ya wananchi juu ya Lowassa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wake.

Katika hoja yangu ya iwapo Lowassa angeamua kugombea urais mwaka 2005, ndiye leo angekuwa Rais wa Tanzania, kuna maeneo makuu matatu ya kutathmini hoja hii.

Kwanza ni suala la nguvu na mvuto wa ufuasi kwa wote wawili (Kikwete na Lowasa), walionao ndani ya CCM. Katika eneo hili, ndani ya chama chao, hadi mwaka 2005, nguvu zao za kisiasa na ufuasi, hawakuzidiana sana. Naweza kusema walikuwa wakilingana.

Pili, Lowassa mbali ya kuwa mwanasiasa alikuwa mfanyabiashara. Kikwete akiwa mtu mwenye mtazamo wa kushika madaraka ya nchi tu, akiweka kando suala la mali.

Hivyo ni dhahiri kwamba Lowassa akiwa mfanyabiashara mkubwa; angeungwa mkono na wafanyabiashara wengi zaidi ambao wamekuwa wakiifadhili CCM kwa miaka mingi na baadhi yao wakiwa viongozi ndani ya chama hicho.

Mbali ya eneo la pili, eneo la tatu ambalo lingemwezesha Lowassa kuwa na mvuto mkubwa zaidi kukubaliwa kuwa rais wa Tanzania, ni upande wa watumishi wa umma na hasa viongozi serikalini na mashirika yake ambao walijiingiza kwenye biashara wakitumia madaraka waliyonayo.

Kutokana na hali hiyo, wengi wao wangemwona Lowassa ambaye ni mfanyabiashara mwenzao, kuwa ndiye rais wa kufanya nao kazi na si Kikwete.

Mbali ya sababu hiyo kwa upande wa watumishi wa umma, kabla ya uchaguzi wa mwaka 2005, kulijitokeza woga kwamba Kikwete angerejesha serikalini nyumba zilizouzwa na Serikali ya Awamu ya Tatu. Kutokana na woga huo, naamini wengi walionufaika na zoezi hilo, Lowassa angekuwa chaguo lao na si Kikwete.

Kutokana na Kikwete kuelewa vyema yote haya, nguvu za fedha na usawa wa ufuasi wa kisiasa na rafiki yake ndani ya CCM na pia uchu wa madaraka ya urais ambayo Lowassa amekuwa nao kwa muda mrefu, alitumia mbinu ya kumweka karibu naye.

Bila hivyo angekabiliwa na upinzani mkali katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2005. Hili Kikwete alilijua fika na hakuwa tayari kukabiliana na ushindani huo.

Bila shaka, kwa uzoefu wake wa kisiasa na jinsi anavyomwelewa rafiki yake, naamini Kikwete alikuwa pia na wasiwasi kwamba hata kama angepambana naye na kumshinda katika hatua ya uteuzi wa mgombea wa CCM, kwa dhamira ya urais ambayo Lowassa alikuwa nayo, angeweza  kabisa kujitoa kwenye CCM na kujiunga na chama cha upinzani au kuanzisha chama chake ili apate fursa ya kugombea urais.

Yote kati ya hayo mawili iwapo moja lingetokea, ni ukweli ulio wazi  kuwa CCM kisingepona kumeguka. Aliyeweza kuelewa hali hii vyema si mwingine bali ni Kikwete pekee. Hivyo ilimlazimu kuidhibiti hali hiyo kwa njia ya uamuzi wa mgumu wa makubaliano. Na hii ndiyo sababu kuu inayomtesa Lowassa tangu alipolazimika kujiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008.

Ambaye amesoma tathimini hii kwa makini, hatashindwa kuelewa kwa nini ajenda ya Kikwete ya kujivua gamba ilikwama kutekelezwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichopita.

Kwa kifupi ni kwamba wajumbe wake, ambao  baadhi yao ni wafanyabiashara wakubwa, waliamua kumuunga mkono mfanyabiashara mwenzao Lowassa.

Katika makala yangu katika toleo lililopita la gazeti hili, nilieleza kuwa msingi wa ulazima wa kujivua gamba kwa CCM unatokana na chama hicho kuingiliwa na wanasiasa ambao ni wafanyabiashara wenye dhamira ya kujinufaisha binafsi.

Kama nilivyofafanua, kujijenga kwao ndani ya chama hicho kiasi cha kushika nyadhifa za juu za uongozi nchini, ni kwa kipindi cha miongo miwili wakati wa utawala wa Awamu ya Pili na Awamu ya Tatu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nguvu hii ya wafanyabiashara ndani ya CCM, ndiyo iliyokwamisha ajenda ya Kikwete ya kujivua gamba huko Dodoma. Nguvu hii pia ni ukweli ulio wazi kwamba Lowassa, anaitafsiri kuwa ndiyo nguzo yake kuu katika mikakati yake ya kuendesha siasa zake ndani ya CCM ili kufikia lengo lake la kuwa Rais wa Tanzania. Mtazamo huu potofu ni sababu nyingine inayomtesa Lowassa.

Pamoja na matamanio yake yote hayo, Lowassa hana budi kukumbuka kwamba Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi na si ya wafanyabiashara pekee. Hawa ndio watakaoamua nani awe rais wao ifikapo mwaka 2015.

Comments

nadhani makala yako hii umetumwa na haowatu wako - Lowassa na Kikwete, na unataka kutulazimisha tuelewe kuwa Lowassa bado ana mvuto na kuwa inawezekana unamsafisha

Mimi napata wasiwasi na kukata tamaa nionapo juhudi za Lowasa za kutafuta URAIS ifikapo 2015. Wasiwasi wangu ni jinsi Bwana Lowasa anavyowalaghai Watanzania masikini ambao amekuwa akiwaongezea mzigo wa umasikini katika harakati zake za Ufisadikwa kutumia viongozi wa kidini. Inaumiza na haiingii akilini ninapouangalia uhusiano wa Madhebu hasa ya kiristo yakishahabikia kupokea misaada ya fedha kutoka kwa Lowasa ili hali wakijua fika kuwa fedha hizo ni za Wizi kutoka kwa Waumini wao Masikini.Katika mazingira ya watu makini Lowasa anapaswa kuogopwa kama gonjwa la ukimwi.Anatafuta Uongozi si kwa maslahi ya Taifa hili,anatafuta uongozi wa kuwa karibu na raslimali zake ili aweze kuzipora kirahisi na historia yake iko wazi.Nitoe wito kwa Watanzania mmoja mmoja tugundue njama za Lowasa na Magenge yake.

Lowassa hawezi kuwa Rais wa nchi hii.Pamoja na kwamba wafanyabiashara na mafisadi ndio wanamuunga mkono,Watanzania(wakulima na wafanyakazi) hawatakubali kumpa wadhifa huo kwani atawaangamiza.Iwapo CCM watampitisha Lowassa kugombea urais 2015,basi wajue wamekizika chama.Wajifunze na yaliyotokea nchi nyingine kama Zambia,Ivory Coast ,Kenya na kwingineko. 

Watnzania tulisema hatumtaki Maximo katika timu ya taifa leo hii tunalaumu timu mbovu,kosa ni la nani? maana yake ni kwamba hatujapanga la kuchafua maana Baba wa Taifa Mwl. J.K Nyerere aliwahi kunena hivyo. Ninamaamini Lowassa anafaa maana ana maamuzi.

Mimi kwa upande wangu naona Lowassa anafaa kuwa rais wa Tanzania tukimkataa Slaa. Maana yangu ni kwamba Lowassa ni mfuatiliaji na mbinu za CCM kumchafua hazina mantiki kwa mtu ambaye ni intellectual. Tanzania tuweni wakweli tunachotaka ni nini? Kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzie!!!!! Kikwete yuko bize kuchuma mali wakati huu yuko madarakani wakati watu wana njaa na taabu kibao!! Pinda anashindwa kukemea hata wauza mafuta na sukari!! Tuwe na mtu asiye tikisika katika maamuzi. Labda Magufuli,Lowassa Mwanri au Slaa bila hapo tujue maskini wenzetu na wababaikaji wanaoongwa kwa limote contol HAKUNA KITU. Tukithubutu,tutaweza na tutasonga mbele.

Lowasa hata ajisafishe vipi bado ni mchafu tuu! Kweli Watanzania wenzetu tuangalie sana huyu bwana alitiliwa mashaka na baba infact late Nyerere was right! Bado makashfa ya Richmond huyu mtu ni hatari, tapeli, mlafi na mwizi. Tuwe macho bora ile kwetu kwa tusiemjua saaaaaaana kama huyu jamaa.

LOWASA ANAFAA KUWA RAIS. VIGEZO: ANA MAAMUZI YA HARAKA...! KWA MTIZAMO WANGU BORA KUMCHAGUA MWIZI HALAFU TUKATENGENEZA MFUMO ASHINDWE KUIBA. HALAFU WIZI SIO TABIA YA NDANI ANAWEZA NA NADHANI ATABADILIKA NA KUTUFAA..! TOFAUTI NA MTU AKIWA MWOGA/ASIYE NA MAAMUZI/ KIGUGUMIZI KATIKA KILA KITU.. ANAKUWA OVERCONSCIUOOS... TABIA HII NI NGUMU KUIONDOA KAMA ALIVYO KIKWETE. TUMESEMA WEEEEEEEEEEEEE LAKINI WAPIIIIIIIIII! KILA JAMBO KIGUGUMIZI.  LOWASA ANAFAA... AWE RAIS 2015. TUTAZIBA MIANYA YA UFISADI ATUMIKIE WATANZANIA KWANZA.
ANA FAIDA ZAIDI KULIKO KUMPA ASIYE MWIZI HALAFU HANA MAAMUZI KATIKA KILA KITU.

eti mwanri..una uhakika??

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.