Kizungumkuti cha mishahara Mererani

IDADI kubwa ya wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite katika machimbo ya Mererani wilayani Simanjiro  wapo hatarini  kukosa ajira iwapo serikali  itatekeleza  agizo  la kuwataka  wamiliki wa migodi kuwalipa wachimbaji mishahara wachimbaji hao wadogo.

Mwishoni mwa mwezi Februari serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexender Mnyeti alitangaza kuwa sheria za kazi zinaelekeza wachimbaji  wadogo kulipwa mishahara ya kati ya shilingi  400,000 kwa migodi mikubwa na shilingi 250,000 kwa migodi midogo.

Aidha, mishahara hiyo pia itakatwa tozo zote za kodi  za serikali na mifuko ya hifadhi jamii na gharama za matibabu kwa wachimbaji wadogo.

“Kila mmiliki wa mgodi atawajibika kuwalipa mishahara wachimbaji wake kama inavyoelekeza sheria ya ajira, na mimi nasimamia sheria hivyo nitasimamia pia na utekelezaji wake,” alikaririwa akisema Mnyeti.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa wa Manyara wamiliki wa  migodi yote wamepewa hadi Aprili Mosi ili kuanza utekelezaji wa mpango huo.

Hoja za wenye migodi

Wakizungumza na Raia Mwema Jumatano viongozi  wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA), walieleza kuwa  iwapo mpango huo utatekelezwa  migodi mingi itafungwa kutokana na wamiliki wake kutokuwa na uwezo wa kulipa mishahara wachimbaji wadogo.

Katibu wa Marema tawi la Mererani Aboubakar Madiwa aliambia gazeti hili kuwa agizo hilo la serikali kwa wamiliki wa migodi halitekelezeki kwa mazingira ya uchimbaji wa Tanzanite kwa sasa.

“Wamiliki wengi hawana uwezo wa kuwalipa wachimbaji wadogo, kutokana na wengi kuwategemea “wafadhili”  wanatoa fedha za kuhudumia migodi kwa kwa asilimia 90,” alisema Madiwa.

Aliongeza: “ Utaratibu uliozeleka kwa wachimbaji wadogo wa madini ya vito na hata dhahabu ni wa kulipana kwa asilimia (parcent) ambapo hutegemeana na makubaliano yaliyopo kwenye mkataba.”

Alisema agizo hilo litaleta athari kubwa sana kwa wachimbaji wadogo na wamiliki kwani migodi mingi  itafungwa na wachimbaji wadogo watarudi makwao na hivyo kukosa ajira.

Ingawa hakuna takwimu rasmi kuhusu idadi ya wachimbaji wadogo waliko Mererani inakadiriwa kufikia wachimbaji kati ya 4000-5000  ambao huingia na kutoka eneo hilo.

Kwa mujibu wa Katibu huyo wa Marema hata hivyo wameunda Kamati ya watu 12 ili kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Manyara kujaribu kulipatia ufumbuzi  suala  hilo  na tayari mapendekezo na ushauri umetayarishwa kwa maandishi.

“Kamati inahusisha viongozi wa dini, wazee wenye busara, wamiliki wa migodi, na viongozi wa Marema, na tuna matumaini kuwa tutayapatia ufumbuzi matatizo yanayotukabili,” alisema Madiwa.

Naye Mwenyekiti wa Marema Sadick Mneney alieleza kuwa kwa kipindi sasa hali za wamiliki wa migodi kifedha si nzuri kutokana na kukabiliwa na changamoto nyingi  kuliko miaka ya nyuma.

Alisema changamoto kubwa ni kupanda kwa asilimia 100 kwa gharama za uchimbaji, hasa ununuzi wa vifaa, vitendea kazi na kuwahudumia wachimbaji wadogo kwa chakula kila siku.

Akitoa mfano alisema: “ Mgodi wenye wachimbaji kati 15-20 gharama za kuhudumia si chini ya milioni 10-15 kwa mwezi, kiasi ambacho wamiliki wengi hawana na hutegemea ufadhili au kuuza mali wanazomiliki ili kuendelea na uchimbaji.

“Kwa mgodi wenye wachimbaji 100-400 unazungumzia gharama ya shilingi milioni 50-100 kwa mwezi, hizi ni fedha nyingi sana, na bado hakuna uhakika wa kupata madini, wengine tumechimba kwa zaidi ya miaka 15 hatujapata.”

Alisema changamoto nyingine ni ya kuongezeka kwa gharama inatokana na migodi mingi kufikia hata urefu wa kilomita 1.5 ndani ya ardhi hivyo kuhitaji ziada ya rasilimali watu na fedha katika kuihudumia.

Alizitaja baadhi ya gharama za uchimbaji, kuwa ni baruti, mafuta (cotex), umeme, mafuta dizeli na vilainishi vya mashine, chakula cha wachimbaji, maji pamoja na matibabu.

“Kama kweli agizo hilo litatekelezwa sioni “future” ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite. Watabaki wamiliki wachache ambao wataajiri watu 5 hadi 10 na vijana wengi watarudi makwao,” alisema Mwenyekiti huyo.

Neema iliyogeuka laana

Tanzania  inatajwa  kuwa ni kati ya nchi za Kiafrika zilizojaliwa neema ya kuwa na  utajiri mkubwa wa madini ambayo yapo katika maeneo mbalimbali  ya ardhi yake ambayo hata hivyo kwa kiasi kilichochimbwa bado Taifa halijafaidika ipasavyo.

Katika maeneo mengi neema hiyo ya uwingi wa madini imegeuka “laana”  kutokana na serikali kukosa sera mathubuti ya kusimamia shughuli za uchimbaji, migogoro baina ya wanaoitwa wawekezaji na wachimbaji wadogo ambayo imegeuka kuwa chanzo vifo na uharibifu wa mali kutokana na vurugu za mara kwa mara.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Nishati na Madini  za mwaka 2014-2015  hadi  sasa madini yaliyochimbwa ardhini hayajafikia hata asilimia kumi ya madini yote yanayotakiwa kuchimbwa.

Takwimu hizo zinaoonyesha kuwa Tanzania ina madini ya aina mbalimbali yakiwamo madini ya chuma (tani 103 milioni), dhahabu (tani 2,222 milioni), shaba (tani 13.65 milioni) na nikeli (tani 209 milioni).

Kwa upande wa madini ya vito  takwimu zinabainisha kuwa bado kuna utajiri wa kutisha  katika maeneo mbalimbali nchini ambao bado haujaanza kuvunwa.

Miongoni mwa madini hayo  vito kwa mujibu  wa takwimu hizo ni  almasi (tani 50.9 milioni), Tanzanite (tani 12.60 milioni), makaa ya mawe (tani 911 milioni) na madini ya viwandani kama chokaa ambayo ni tani 313 milioni.

Takwimu hizo ziliwahi kuthibitishwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo George Simbachawene wakati akijibu maswali Bungeni kuhusu utajiri wa madini  Mei 29 mwaka 2015 mjini Dodoma.

Kati ya madini ya vito ambayo yamepata umaarufu mkubwa ni Tanzanite ambayo yanachimbwa pekee  duniani  katika eneo la Mererani Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara.

Hata hivyo, pamoja na dosari hizo serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imechukua hatua kadhaa madhubuti kufanya marekebisho makubwa katika sekta ya madini ambapo mwaka jana iliunda kamati maalumu za Bunge kuchunguza madini ya Almasi na Tanzanite.

Kamati ya kuchunguza mianya ya utoroshwaji wa madini Tanzanite iliongozwa na Doto Biteko ambayo iligundua “madudu” mengi  na Rais Dk. Magufuli alichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kujenga ukuta kuzunnguka eneo lote la Mererani.

Malalamiko na taarifa ya Kamati ya  Biteko yanahalalishwa na takwimu za Wizara ya Madini  na Nishati mwaka  pamoja na tovuti kadhaa za kimataifa mwaka 2013-2014 zinaoonyesha kuwa Kenya imeuza katika soko la dunia madini ya Tanzanite yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni zaidi ya 135 (zaidi ya bilioni 200) na kuizidi Tanzania huku India ikuza madini yenye  thamani ya Dola milioni  500.

Kwa mujibu wa takwimu hizo Tanzania ambayo ndiyo pekee inayozalisha madini hayo duniani  imeuza katika soko la dunia Tanzanite yenye  thamani ya dola za Kimarekani milioni  38 tu na kiasi cha baadhi ya wadau ikiwamo Marekani kuhoji inakuwaje Tanzania iwe ya mwisho katika mauzo wakati ndiyo mzalishaji  pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *