Kuchaguliwa kwa Trump: Urais wa Marekani sio biashara ya familia, asema Obama

Rais Barack Obama na Rais Mteule Donald Trump walipokutana katika ikulu ya White House mara baada ya uchaguzi nchini Marekani.

RAIS wa Marekani Barack Obama amesema alimshauri mrithi wake Donald Trump kutojaribu kuiendesha ikulu ya nchi hiyo “jinsi ambavyo mtu anaweza kuisimamia biashara ya familia.”

Katika mahojiano na shirika la utangazaji la BBC, Barack Obama alisema kwamba Trump lazima “aheshimu” taasisi za Marekani.

“Baada ya kuapishwa,” alisema, “unasimamia taasisi kubwa zaidi duniani.”

Alionya kwamba kuna tofauti baina ya kuongoza na kufanya kampeni.

“Kuna miji mikubwa ya dunia na masoko ya mitaji na watu duniani kote ambao wanachukulia kwa umakini sana kile ambacho Trump anasema,” alisema Obama.

Obama pia alizungumzia kuhusu ripoti ya idara za kijasusi za Marekani kuhusu shambulizi la kimtandao la Urusi na jaribio la kujaribu kushawishi kampeni za urais wa Marekani.

Alisema kwamba alikuwa “amedharau” madhara ya mashambulizi ya aina hiyo.

“Nadhani nilidharau kiasi ambacho, katika kizazi hiki cha sasa cha habari, inawezekana kutolewa kwa habari za uongo… na zinaweza kuwa na athari kwenye jamii yetu.”

Alisema kwamba mazungumzo yalikuwepo na Trump ambayo walizungumzia juu ya umuhimu wa kuwa na imani na idara za kijasusi za nchi hiyo.

“Inaweza kutokea wakati ambapo njia pekee ambayo unaweza kufanya uamuzi mzuri ni kama unaimani kwamba mfumo unafanya kazi vizuri,” alisema.

Wiki iliyopita Trump alisema kwamba alikuwa “mshabiki mkubwa” wa idara za kijasusi, baada ya miezi kadhaa ya kutilia mashaka uhusika wa Urusi katika udukuzi wakati wa kampeni za uchaguzi. Lakini baadae aliibua maswali juu ya jinsi chama cha Democratic kilivyojibu mashambulizi hayo ya kimtandao.

“Ni jinsi gani na kwa nini  wanauhakika kuhusu udukuzi kama hawajawahi kamwe kuomba kuchunguzwa kwa kompyuta? Kitu gani kinaendelea? Trump aliuliza kwa njia ya Twitter.

Trump ataapishwa Januari 20.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *