NIMEOMBA kupeperusha bendera ya Tanzania Bunge la Afrika Mashariki. Machi 12, 2012 Katibu wa Bunge la Tanzania alitoa taarifa kwa umma kuhusu kuanza kwa mchakato wa kupata wabunge tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la tatu la Afrika Mashariki.
Bunge la pili la Afrika Mashariki liliapishwa Juni 05, 2007 kwa kipindi cha miaka mitano, na hivyo kipindi chake kinaelekea ukingoni.
Kupitia taarifa yake, aliwataka Watanzania ambao wanaamini kwamba wanazo sifa za kugombea na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kuanza mchakato wa kuteuliwa kuwa wagombea wa uchaguzi huo, kupitia vyama vyao vya siasa.
Binafsi naamini kwamba ninazo sifa husika. Kwa hiyo nimekiomba Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, kiniteue kama mgombea katika kinyang’anyiro hiki. Baada ya kuwasilisha maombi yangu niliwafahamisha wadu wote kupitia mitandao ya kijamii kuhusu uamuzi huu. Hata hivyo, nimegundua kwamba wadau wengi hawana habari sahihi kuhusu mchakato huu muhimu kuhusu uhai wetu sote.
Katika makala hii ninabainisha taarifa za msingi kuhusu mchakato huu kwa manufaa ya wasomaji.
Ratiba na utaratibu wa uchaguzi
Uchaguzi wa wajumbe watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, katika mkutano wake wa sasa Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Bunge ya Machi 12, 2012, siku ya uchaguzi ni Aprili 17 , 2012 mara tu baada ya Kipindi cha Maswali na Majibu.
Kimsingi, basi, inaonekana kuwa mchakato wa kuwapata wabunge hawa utakuwa na hatua tatu. Kwanza ni uteuzi kupitia vyama vya siasa, ambapo kwa CHADEMA, kikao husika ni Kamati Kuu ya Chama. Hatua ya pili ni uteuzi kupitia kambi za vyama bungeni (caucuses), kila chama kikichuja wagombea wake. Na hatua ya tatu ni upigaji kura wa wabunge wote.
Mbali na utaratibu huu wa uchaguzi, wadau pia wamekuwa wakiniuliza maswali kuhusu majukumu, idadi ya wajumbe na historia ya Bunge la Afrika Mashariki. Hivyo, napenda kutoa majibu kwao wote kwa njia ya makala hii.
Majukumu ya Bunge la Afrika Mashariki
Kulingana na ibara ya 49 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, majukumu ya jumla ya Bunge la Afrika Mashariki ni kama yalivyo majukumu ya mabunge mengine—yaani kutunga sheria na kusimamia serikali kwa njia ya uwakilishi. Kwa usahihi zaidi, Bunge la Afrika Mashariki linayo majukumu yafuatayo:
Kuwasiliana na mabunge ya nchi wanachama kwa lengo la kuhuisha masuala yote yanayohusu Jumuiya. Kujadili na kupitisha bajeti ya Jumuiya. Kupokea na kujadili taarifa ya utendaji wa shughuli za Jumuiya, taarifa ya kamati ya ukaguzi na udhibiti ya Jumuiya, na taarifa nyingine yoyote itakayoletwa kwake na Kanseli ya Jumuiya.
Kujadili masuala yote yanayohusu Jumuiya na kutoa mapendekezo ya utekelezaji kwa Kanseli lakini katika mipaka ya Mkataba wa Jumuiya na kuunda kamati mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake. Kazi nyingine kupendekeza kwa Kanseli jina la Katibu wa Bunge na watumishi wengine wa Bunge la Jumuiya.
Kamati za Bunge la Afrika Mashariki
Na Kazi ya saba ni kuandaa kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli zake, na pia kanuni za kuendesha kazi za kamati mbaimbali. Kuna Kamati za kudumu saba, ambazo ni, Kamati ya Hesabu za Bunge; Kamati ya Kilimo, utalii na maliasili; Kamati ya Jumla; Kamati ya Uongozi wa Shughuli za Bunge; Kamati ya Sheria, Kanuni na Haki za Wabunge; Kamati ya Masuala ya Kikanda na Utatuzi wa Migogoro; na Kamati ya Biasgara, Mawasiliano na Uwekezaji. Wajumbe wa Kamati hizi wanapatikana kwa kuzingatia uwiano sawa kati ya nchi wanachama wa Jumuiya, ambapo kwa wastani, kila kamati inao wajumbe kati ya 12 hadi 15.
Idadi wa wajumbe katika Bunge la Afrika Mashariki
Katika Bunge la Afrika Mashariki kuna jumla ya wabunge 45, tisa kutoka katika kila nchi mwanachama. Huchaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano kupitia mabunge ya nchi wanachama. Mbunge anaweza kuchaguliwa tena baada ya kipindi chake kwisha.
Katika ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tunasoma kwamba Wabunge wa Afrika Mashariki lazima wawakilishe watu wengi kadiri inavyowezekana, kwa kuzingatia vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, makundi yenye mitazamo tofauti kijamii, jinsia na makundi mengine yenye kupigania maslahi ya kisekta katika jamii ya nchi wanachama.
Kwa mujibu wa ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuiya, sifa za kisheria ili mtu aweze kuchaguliwa kama Mbunge wa Afrika Mashariki ni hizi hapa: Mtu ambaye ni raia wa nchi mwanachama; Mtu mwenye sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mujibu wa Katiba ya nchi anakotoka; Mtu ambaye sio Waziri katika serikali ya nchi anakotoka; Mtu ambaye sio mtumishi wa Umma katika nchi anakotoka; na mtu ambaye, kwa namna moja au nyingine, ameonyesha nia au uzoefu wa kukuza na kuhami malengo ya Jumuiya. Hivyo, utaona kwamba, ili mtu kuchagukliwa, uzoefu wa kisiasa sio kigezo cha kisheria.
Mbali na wabunge 45, kuna wajumbe wengine katika Bunge la Afrika Mashariki, ambao hata hivyo, hawana haki ya kupiga kura. Hawa ni pamoja na Mawaziri watano wa Mambo ya Afrika Mashariki katika nchi wanachama; Mwanasheria wa Jumuiya; na Katibu Mkuu wa Jumuiya. Hivyo, kwa mujibu wa ibara za 48 na 50 katika Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, jumla ya wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki ni 52.
Historia fupi ya Bunge la Afrika Mashariki
Bunge la Afrika Mashariki linayo historia ndefu inayojikita katika juhudi za ushirikiano wa siku nyingi wa kikanda katika biashara, uchumi, utamaduni na kadhalika.
Kwa mfano, mwaka 1897 – 1901 Kenya na Uganda zilianza ushirikiano wa kiuchumi kwa kujenga reli iliyoziunganisha. Mwaka 1900 kuliundwa kituo cha pamoja cha forodha. Mwaka 1905 iliundwa Bodi ya Sarafu moja. Mwaka 1909 iliundwa Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki. Mwaka 1919 uliundwa Umoja wa Forodha. Mwaka 1926 ulifanyika mkutano wa Magavana wa Afrika Mashariki. Mwaka 1940 iliundwa Bodi ya Mapato ya Kodi. Pia mwaka huo iliundwa Kanseli ya Pamoja ya Uchumi.
Kutokana na historia hii, mwaka 1967 Jumuiya ya Kwanza ya Afrika Mashariki iliundwa kwa mujibu wa Mkataba wa Kisheria. Kwa mujibu wa mkataba huu Bunge la Afrika Mashariki liliundwa ili kutunga sheria kuhusu yale mambo ya pamoja.
Jumuiya hii ya kwanza ilivunjika mwaka 1977 kwa sababu mbalimbali. Na miaka 20 baadaye, yaani, Apprili 29, 1997, Jumuiya Mpya ya Afrika Mashariki ikazaliwa mjini Arusha, Tanzania. Wanachama waanzilishi walikuwa Tanzania, Kenya na Uganda. Na baadaye mnamo Julai 01, 2007 Rwanda na Burundi zilikaribishwa kama wanachama wapya.
Kwa njia hii, Bunge la Afrika Mashariki, kama chombo kimojawapo cha Jumuiya limefufuliwa upya. Lilizinduliwa rasmi Novemba 30, 2001 kupitia kikao chake cha kwanza.
Sababu za kuomba ubunge wa Afrika Mashariki
Nimeomba kuwa sehemu ya Bunge la Afrika Mashariki ili kuweza kushiriki kikamilifu katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya yetu. Kwa mujibu wa Mkataba huu katika ibara ya tano, Jumuiya yetu inayo malengo yafuatayo:
Kusanifu sera na programu zinazolenga kupanua na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama, kuhusu masuala yanayohusu siasa, uchumi, jamii, utamaduni, utafiti, teknolojia, ulinzi, usalama na sheria, haya yote yakilenga kufanikisha maslahi ya pamoja (ibara ya 5(1)).
Kwa ajili ya kufikia lengo hili kuu, ibara ya 5(3) inatueleza kuwa Jumuiya inakusudia kufanya yafuatayo: kukuza na kuhami uchumi; kuboresha viwango vya maisha ya watu wa Jumuiya; kutunza mazingira kwa kuratibu utumiaji bora wa maliasili kwa faida ya vizazi vijavyo; kupigania usawa wa kijinsia; kupigania haki, usalama na utangamano; na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Kwa wale ambao wamefuatilia historia yangu wanafahamu fika kwamba malengo haya ndiyo yamekuwa sehemu ya kilio changu siku zote. Kwa mfano, wakati wa kampeni mwaka 2010 nilipokuwa nagombea ubunge jimboni Karagwe niliinadi ajenda iliyo katika Ilani ya chama CHADEMA kwa kutumia vokali za “A-E-I-O-U.”
Katika vokali hizi, herufi “A” inawakilisha “Aidiolojia bora kama chombo cha kujenga uzalendo,” herufi ya “E” inawakilisha “Elimu, Mafunzo, Habari na Utamaduni Bora,” herufi ya “I” inawakilisha “Idadi Kubwa ya Miundombinu Mama iliyo Bora,” herufi ya “O” inawakilisha “Ongezeko la Mazao, Kipato na Mali Bora,” na herufi ya “U” inawakilisha “Uhai, Afya, Makazi, Hifadhi ya Jamii na Mazingira Bora.” Waliohudhuria kampeni zangu ni mashahidi.
Lakini sio hivyo tu. Pia kielimu nimekamilika. Ninayo elimu ya Chuo Kikuu katika fani ya TEKNOHAMA tangu mwaka 1998. Umri wa miaka 40 nilionao unatosha. Na uzefu wangu kama mwalimu wa sekondari, na kwa sasa, kama mhadhiri ni sifa nyingine zinazonipa sababu ya kuthubutu.
Toa maoni yako