Makala
Kupinga ‘nguvu ya umma’ ni kupinga demokrasia na kutukuza udikiteta
Deusdedit Jovin
Toleo la 259
19 Sep 2012

TUHUMA tata zilizotolewa na kina Samuel Sitta dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ambazo nimezijadili kwa kifupi katika toleo lililopita la gazeti hili, zimenihamasisha kutafakari kwa kina kuhusu changamoto za kiitikadi zinazotukabili katika safari ya kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa rais na wabunge ifikapo mwaka 2015.

Baada ya kutafakari kwa kina nimejiridhisha kwamba kuna haja ya kufanya muhtasari, ufafanuzi na utetezi wa itikadi ya CHADEMA kwa kubainisha kila “hoja au wazo linalotolewa kimantiki”1 ili kusisitiza mafundisho yake ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na vinginevyo.

Kila wazo au hoja ya aina hiyo nitakuwa nairejea kama “tasinifu ya kiitikadi” (ideological thesis) ya CHADEMA. Vyanzo vya “tasnifu za kiitikadi” (ideological theses) za CHADEMA ni Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, Ilani za Uchaguzi, nyaraka za kiutendaji za chama, na pia nyaraka za kielektroniki, kwa maana hotuba mbalimbali za viongozi wa chama.

Na leo, ili kuonyesha ukweli kwamba kina Sitta wanaopinga “nguvu ya umma” wanapinga demokrasia na kukumbatia udikiteta, nimeamua kufanya muhtasari, ufafanuzi na utetezi wa “tasinifu ya kiitikadi” (ideological thesis) ya CHADEMA ifuatayo:

“CHADEMA tunaamini na kutambua kuwa “kuchaguliwa” kuunda utawala wa kuongoza nchi hakumaanishi wachaguliwa kujitwalia mamalaka ya UMMA na kisha kuyatumia mamlaka hayo kuwakandamiza “waliowachagua” kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma.

Hivyo basi, falsafa ya “Nguvu na Mamlaka ya Umma” ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na za haki” (Katiba 2006, ibara ya 3.6 na 3.7).

Katika nyaraka za CHADEMA “tasinifu ya kiitikadi” hii inarejewa kama “tasinifu ya nguvu ya umma” (people’s power thesis) au “tasnifu ya kidemokrasia” (democratic thesis). Ni “tasinifu ya nguvu ya umma” inayoitofautisha CHADEMA na vyama vingine vya siasa vyenye harufu ya udikiteta. Aya zifuatazo zinakusudia kuweka bayana ukweli huu katika upeo usio na shaka.

Demokrasia ni mfumo wa utawala unaozingatia “nguvu ya umma”

Awali ya yote, napenda kuweka bayana kuwa, mafundisho ya CHADEMA kuhusiana na “tasinifu ya nguvu ya umma” hayana tofauti yoyote na mafundisho yanayotolewa na walimu wa sekondari na wakufunzi wa vyuo vyetu wanapokuwa wanafundisha madarasani. Kwa mfano, “tasinifu ya nguvu ya umma” imo katika kitabu kiitwacho “Mwongozo wa Somo la Uraia Kwa Ajili ya Walimu wa Sekondari na Wakufunzi wa Vyuo” kama kilivyochapishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania mwaka 2002 kwa idhini ya Dk. Naomi B. Katunzi. Katika kitabu hiki, “tasinifu ya nguvu ya umma” imejadiliwa katika somo la 11 na 12 kuanzia ukurasa wa 45 hadi 51.

Kwa namna fulani basi, Taasisi ya Elimu Tanzania, Walimu wa Sekondari na Wakufunzi wa Vyuo wanaofundisha somo la uraia, wanafanya kazi ya kueneza itikadi ya CHADEMA. Kwa maoni yangu, hii ndiyo sababu iliyoifanya CHADEMA kupata mteremko katika siasa zake za hivi karibuni.

Mtazamo huu unaungwa mkono na sababu zifuatazo: CHADEMA, walimu wa sekondari, wakufunzi wa vyuo na wanafunzi wao wanakubaliana katika yafuatayo: kwamba, neno “demokrasia” linatokana na maneno mawili yaliyo katika lugha ya Kigriki; kwamba, na neno la kwanza ni, “demos” linalomaanisha “umma”; kwamba, neno la pili ni “kratos” linalomaanisha “nguvu” au “mamlaka”; na kwamba neno “demokrasia” linamaanisha mfumo wa utawala unaozingatia “nguvu ya umma.” Katiba ya CHADEMA (2006) imeyataja wazi wazi maneno “nguvu na mamlaka ya umma (the people’s power)” katika ibara ya 3.1.

Katika ulimwengu wa leo, demokrasia inamaanisha maamuzi ya wengi kupitia wawakilishi wao waliowachagua moja kwa moja na kuwaingiza katika vikao vya maamuzi kama vile Bunge na Baraza la Madiwani. Lakini si hivyo tu. Pia, demokrasia inamaanisha maamuzi ya wengi kupitia wawakilishi wao waliowachagua kwa njia ya mzunguko na kuwaingiza katika vikao hivyo vya maamuzi. Mwakilishi aliyechaguliwa na wananchi kwa njia ya mzunguko ni yule ambaye ameteuliwa na mwakilishi aliyechaguliwa moja kwa moja na wananchi.

Kwa mfano, Rais anachaguliwa moja kwa moja na wananchi; halafu anawateua mawaziri, majaji, na watumishi wengine wa umma. Kwa kuwa, Rais amechaguliwa moja kwa moja na wananchi, uteuzi wake unahesabiwa ni uchaguzi uliofanywa na wananchi kwa njia ya mzunguko kupitia mkono wa Rais.

Mtu aliyechaguliwa moja kwa moja anaweza kuwajibika moja kwa moja kwa mtu aliyemchagua au akawajibika kwa njia ya mzunguko kwa mtu aliyemchagua kupitia kwa mwakilishi wa mtu aliyemchagua au vyote kwa pamoja.

Kadhalika, mtu aliyeteuliwa anaweza kuwajibika moja kwa moja kwa mtu aliyemteua au akawajibika kwa njia ya mzunguko kwa mtu aliyemteua kupitia kwa mwakilishi wa mtu aliyemteua au vyote kwa pamoja. Picha yenye kichwa cha maneno “Uongozi wa Kidemokrasia kwa mujibu wa itikadi ya Nguvu ya Umma” inaonyesha mahusiano yanayopaswa kuwepo kati ya mchaguaji, mteuaji na mteuliwa.

Katika mchoro huu, ambao unawakilisha mtazamo huu wa CHADEMA, Rais anawajibika kwa Bunge na Wapiga kura, kwa maana kwamba Bunge na Wapiga kura wanayo nguvu ya veto dhidi yake muda wowote kupitia kura ya maoni ili kumwondoa madarakani (power of recall through a referendum). Pia, utaona kwamba kwa kuzingatia mtazamo huu wa CHADEMA, madaraka ya Rais katika kuteua watumishi wa mahakama yamefyekwa.

Sasa bunge ndilo lenye mamlaka hayo. Yaani, majaji wanawajibika kwenye bunge. Hii ndiyo njia pekee ya kuachana na urais wa kifalme.

Hiki ndicho kinachomaanishwa na Katiba ya CHADEMA (2006) pale inapotamka maneno yafuatayo: “Hivyo basi, falsafa ya “Nguvu na Mamlaka ya Umma” ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na za haki” (Katiba 2006, ibara ya 3.7).

Mtazamo huu wa CHADEMA ni kinyume kabisa na mtazamo wa itikadi ya kidikiteta. Katika mfumo wa uongozi wa kidikiteta, kuchaguliwa kuunda utawala wa kuongoza nchi kunamaanisha wachaguliwa kujitwalia mamalaka ya UMMA na kisha kuyatumia mamlaka hayo kuwakandamiza waliowachagua kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma.

Lakini, katiba ya CHADEMA inapinga vikali jambo hili kupitia misamiati ifuatayo: “CHADEMA tunaamini na kutambua kuwa “kuchaguliwa” kuunda utawala wa kuongoza nchi hakumaanishi wachaguliwa kujitwalia mamlaka ya UMMA na kisha kuyatumia mamlaka hayo kuwakandamiza “waliowachagua” kwa sababu tu ya kutetea maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma (Katiba 2006, ibara ya 3.6).

Majumuisho na hitimisho

Kwa ujumla, huwa kitaalamu tunasema kwamba “democracy is inversely proportional to dictatorship.” Yaani, kadiri maamuzi na matendo ya kidemokrasia yanavyoshamiri maamuzi na matendo ya kidikiteta yanafifia.

Na kinyume chake ni kweli. Yaani, kadiri maamuzi na matendo ya kidemokrasia yanavyofifa maamuzi na matendo ya kidikiteta yanashamiri. Matendo ya kidikiteta ni matendo ya kuwaburuza watu kana kwamba ni roboti bila kujali kwamba wanayo akili na utashi.

Kwa mfano, wananchi wakiamua kupitia sanduku la kura kwamba huduma za elimu na afya zitolewe kama “faida ya wote” lakini vyombo vya dola vikachakachua matokeo ya kura na hatimaye kuhakikisha kwamba huduma za elimu na afya zinatolewa kama “faida ya wengi” inayobagua wachache, kama kina Sitta wanavyopendekeza, huo unakuwa ni udikiteta. Kwa hiyo, kupinga “nguvu na mamlaka ya umma” ni kupinga demokrasia na kutukuza udikiteta.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Deusdedit Jovin
deus.jovin@gmail.com
+255-0758341483, +255-0684175182

Maoni ya Wasomaji

hakika mtazamo wako kama mwandishi ni mzuri kisi ila swali langu ni kuwa huwezi kuona kwamba bado tatizo la udikiteta halita ondoka kwa mfumo huo? kwa mfano: kwa kuwa uwezo wa kumtoa rais ambaye atekelezi majukumu yake ni bado yapo kwa wabunge chukulia wabunge wa chama kimoja ndio wengi na upande wa pili na wachache kwa hali hii ya kila chama lazima kijinufaishe kwanza itawezekana vipi? pia huwezi kuona kuwa kutakuwa hakuna ufanisi na maamlaka makubwa yatakuwa kwa wabunge tena wakati mwingine wao ndo wabovu wa kufikilia baadhi ya mambo kama leo tunavyo ona wabunge wetu? kwangu mm naona kuna kila haja ya vyama kuweka baadhi ya mambo ya kimsingi kama elimu kuwa na sera ya pamoja bila kuangalia itikadi za vyama. lazima tuwe na sera ya kitaifa kwa baadhi ya mambo hilo ndo suluhu ya yate. sijaona cha muhimu kwa mfumo huu mwandishi bado hauta komboa taifa letu.

Mr. Twahil, Asante kwa kuuliza swali. Unasema kuwa hujaona cha muhimu katika makala yangu, kwa maana kwamba, mfumo huu ninaoupendekeza bado hautakomboa taifa letu. Umetaja sababu mbili. Kwanza, ni mfumo wa uendeshaji Bunge ambapo kamati ya chama (caucus) chenye wabunge wengi ndiyo inaweka mwelekeo wa maamuzi ya Bunge. Na pili, umetaja udhaifu wa mbunge mmoja mmoja. Kwanza nikiri kwamba dukuduku lako ni la haki. Lakini, umeharakisha kusema kwamba nilichokipendekeza hakitamkomboa mwananchi. Nianze na sababu ya pili. Ni kweli wabunge dhaifu hazaa Bunge dhaifu. Kanuni ya nguvu ya umma ninayoiongelea inataka kwamba wawakilishi wanaochaguliwa na kuteuliwa wawe ni sifa. Na jambo kubwa ni kwamba, mwakilishi asiwe na tatizo tunaloliita “cognitive hazard”. Elimu na uzoefu ni njia nzuri ya kupunguza tatizo hili. Hii maana yake ni kuwa, vigezo vyetu vya wagombea lazima viboreshwe ndani ya Katiba ya nchi, katiba za vyama na sheria za uchaguzi. Tatizo jingine tunaliita “moral hazard”. Na kuhusu sababu yako ya kwanza, ni wazi kwamba caucus za vyama zinatumiwa vibaya kwa sababu ndani yake kuna wabunge dhaifu. Hujaona kina Filikunjombe wanavyobadilisha upepo ndani ya CCM? Kwa hiyo, tukishughulikia tatizo la “cognitive hazard” hili la pili litakuwa limeshughulikiwa kwa njia ya mzunguko. Kuna jambo jingine niseme kuhusu sababu yako ya pili. Kanuni ya nguvu ya umma katika ngazi ya Bunge inataka kwamba cauacus zibanwe ili zilinde maslahi ya taifa. Tunalazimika kubuni mfumo wa kufanikisha jambo hili. Ninalo pendekezo. Kwamba, kwa kila uamuzi unaopitishwa ndani ya Bunge, fomula iwe ni kwamba uungwe mkono na angalau 50% ya wabunge wa kambi ya upinzani na 50% ya wabunge wa kambi ya chama tawala. Maoni yangu yote haya yanazingatia kanuni ya nguvu ya umma. Kwa hiyo, sio sawa kusema kwamba, makala yangu haina maana.

Twahil, kwa bunge sidhani kama litaweka udikteta, logic hapa ni kupigania nguvu ya democrasia. Unajua demokrasia ikiwa imefikia kiwango kinachohitajika inaweka check and balance kwa watawala na watawaliwa. Na hii itapunguza wabunge kushiorikiana kwa jambo lisilokuwa na masilahi kwa uma. Hapa na maanisha nini? Ikiwa demokrasia ipo ya kutosha, ina maana wabunge lazima watakuwa wanatizama wananchi huku wakifanya maamuzi na hii itatokana na kuwepo na mifumo isiyokuwa na lelemama na kiongozi asie faa. Unajua kaka tuendako wabunge watakuwa na party cocus kwa jambo la msingi kwa nchi na kwa msilahi kwa uma sio kwa chama. Sasa ikatokea mkafanya ya chama lakini yanayokinzana na ya wananchi maana yake mifumo mizuri ya demokrasia haitawavumilia kipindi cha uchaguzi kikifika. Lakini mifumo hii lazima iwe imeundwa kwa uangalifu na tena iwe inajisimamia kikamilifu 'independent'. Harafu sina uhakika kwenye demokrasia ya kweli ukapata wabunge wabovu, kama itatokea maana yake kutakuwa na shida somewhere either mifumo ya uchaguzi mibovu, wananchi wanaochagua, elimu, rushwa, ushamba kushabikia bila kupima.

Toa maoni yako