Michezo
Kwa nini ni muhimu kumpigania Sajuki
Ezekiel Kamwaga
Toleo la 238
9 May 2012

JUMA Kilowoko maarufu kwa jina la Sajuki, miongoni mwa waigizaji mahiri wa filamu hapa nchini yu taabani. Habari kuhusu masahibu yanayomkuta sasa zimeenea mahali pengi hapa nchini kama moto wa nyikani.

Kwa wasiomfahamu vizuri, nadhani nitakuwa sijakosea kama nikisema kwamba miaka miwili au mitatu iliyopita, alikuwa miongoni mwa waigizaji bora zaidi watano wa kiume waliopo nchini hivi sasa kwenye tasnia ya filamu za Kitanzania (Bongo Movies).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, hususani mkewe, Wastara Juma (naye mwigizaji mahiri), Sajuki anasumbuliwa na ugonjwa kupungukiwa damu mwilini. Ugonjwa huu umemfanya ashindwe kabisa kuendelea na fani yake.

Kushindwa kwa Sajuki kuigiza ni kitu kimoja lakini la kutisha ni ukweli kwamba ugonjwa wake huo hauwezi kutibika hapa nchini na kama hatapata matibabu muafaka ughaibuni (na Mungu apishilie mbali), basi kuna uwezekano wa kumpoteza kijana huyu.

Zinahitajika walau shilingi milioni 26 hivi ili aweze kupata tiba muafaka ya ugonjwa wake. Kwa hali halisi ya familia yake, kiasi hicho ni kikubwa mno na haitaweza kukikusanya. Na ndiyo maana ni muhimu mno kwa Watanzania kuingilia kati.

Lakini, je, ni kwa nini ni muhimu kwa Watanzania kupigania maisha ya kijana huyu? Nitaeleza.

Tasnia ya filamu

Pengine watu hawajafanya utafiti kujua athari lakini tasnia ya filamu nchini imekumbwa na misukosuko mingi tangia mwanzoni mwa mwaka huu. Misukosuko hiyo inahatarisha ustawi wa sekta hii muhimu sana.

Mwaka huu kumekuwapo na taarifa za uhusiano mbovu baina ya wasanii wenyewe, kuvunjika kwa ndoa ya mwigizaji maarufu, kifo cha Steven Kanumba, kesi ya Lulu na sasa ugonjwa huu wa Sajuki.

Watu hawawezi kuipenda tasnia ambayo kuna mabifu kila kukicha, ndoa za wasanii zinazovunjika hovyohovyo (Marekani sawa lakini nchi zetu bado ndoa ni kitu kitakatifu), kuondokewa na msanii kipenzi (Kanumba) na kuripotiwa zaidi kwa masuala ya kesi ya tuhuma za mauaji ya msanii kuliko kazi za wasanii.

Kama Sajuki atashindwa kusaidiwa, itajengwa picha kwamba jamii ya Watanzania haiwajali wasanii wake. Katika mazingira hayo, nani mwingine atataka kujihusisha na sanaa hizo?

Hata wasanii waliobaki nao watajiuliza maswali mengi sana kuhusu umuhimu wao kwa jamii. Wanaweza kupata mawazo kwamba wanapendwa wakiwa wazima tu.

Kama Sajuki atasaidiwa na kupona, watu wengi watasisimshwa na taarifa hiyo. Watu wengi zaidi wenye vipaji watataka kujiunga na sekta hii na kuongeza ubora wa filamu zetu. Hii ni kwa sababu wataona watu wanawajali waigizaji wetu.

Lakini, kama Sajuki ataachwa ateketee, nani atataka tena kuwa mwigizaji? Tusisahau pia kwamba Sajuki na mkewe Wastara pia wana kampuni ya filamu ambayo ilikuwa ikitoa filamu walau mbili kwa mwezi kabla matatizo hayajamkuta gwiji huyu.

Kumtelekeza kunamaanisha kuna vijana ambao watapoteza ajira zao. Kunamaanisha kwamba kuna watu wangeweza kabisa kuajiriwa lakini hawataajirika kwa sababu kampuni itakuwa imekwisha. Ni athari pia kwa tasnia ya filamu nchini ambayo kimsingi bado ni changa.

Ugonjwa wa Sajuki

Watu wawili wanapendwa sana nchini Marekani kwa sababu ya aina ya magonjwa waliyowahi kuumwa au wanayoumwa. Muhammad Ali, yule gwiji wa masumbwi anasumbuliwa na ugonjwa unaoitwa Parkinson. Rais wa zamani wa Marekani, Ronald Reagan, alikufa baada ya kusumbuliwa sana na ugonjwa wa Alzeiheimer.

Ingawa watu hawa wawili wameteswa sana na magonjwa hayo, kuumwa kwao kumesababisha jamii ya Wamarekani kuyafahamu na kujua namna ya kujikinga nayo.

Ugonjwa unaomsumbua supastaa na wenyewe unakuwa ‘supastaa’ vilevile. Si wengi walikuwa wanaufahamu ugonjwa huu wa kuishiwa damu unaomsumbua Sajuki. Watu watajifunza sasa msanii huyu aliupataje na namna gani watu wanaweza kujikinga.

Katika jamii ya kishirikina kama Tanzania, ni muhimu mno kwa magonjwa kama ya Sajuki kufahamika ili kuondoa dhana za watu kulogana. Ni muhimu sana kwa msanii huyu kusaidiwa akapona ili watu wajue ugonjwa wake unaponyeka tena kwa njia za kisayansi kabisa.

Ndoa ya Sajuki

Ndoa ya Sajuki na Wastara ni miongoni mwa zilizo maarufu baina ya wasanii. Kwa wasiofahamu, Wastara alipata ajali ya gari miaka michache iliyopita na akapata ulemavu wa miguu wa kudumu baada ya kukatwa mguu mmoja.

Pamoja na hali yake hiyo, Sajuki aliendelea kuishi na mkewe huyo katika mazingira magumu. Ni mapenzi hayo ya dhati kwa mkewe ndiyo yaliyomfanya Sajuki aheshimike na kupendwa sana na watazamaji wa filamu.

Katika dunia ya sasa ambapo mapenzi feki yamechukua nafasi kubwa –Wastara na mumewe huyu walikuwa kielelezo kuwa ikrari mapenzi ya kweli yapo.

Na Wastara amekuwa mstari wa mbele kumpigania mumewe huyu apate tiba. Itakuwa maumivu ya namna gani kuona mapenzi haya ya kweli yakikatishwa kwa jambo ambalo Watanzania wana uwezo mkubwa wa kulitatua.

Ni muhimu Sajuki asaidiwe ili vijana na wazee wafahamu kuwa penzi la kweli lina malipo yake. Kama Sajuki angemkimbia Wastara kwa sababu ya ulemavu, leo hii yeye angekuwa mgeni wa nani?

Tukimtelekeza Sajuki, jitihada zote hizi za Wastara na wasanii wenzake waliofikia hatua ya kutoa wimbo kwa ajili zitakuwa zimepotea.

Serikali

Mara baada ya msiba wa Kanumba, serikali ilitoa kiasi cha Sh milioni 10 za Kitanzania kwa ajili ya kugharamia msiba. Zaidi ya kiasi hicho, ilitoa pia msaada wa vyakula na vinywaji. Vema.

Nafikiri serikali ina wajibu sasa wa kumsaidia Sajuki angali akiwa mzima. Kama iliweza kutoa milioni 10 kwa ajili ya msanii aliyechukuliwa na Mungu, bila shaka inaweza kutoa zaidi kwa ajili ya msanii anayepigania kuokoa maisha yake.

Inaweza kumsafirisha. Inaweza kumpeleka katika hospitali hiyo ya India alikoenda kwa gharama zake mara ya kwanza na ninajua serikali haiwezi kushindwa kutoa milioni 26!

Kama serikali yetu iko kwa ajili yetu, basi inapaswa nayo ijitokeze kumuokoa kijana huyu. Isisubiri hadi wakati wa kutoa rambirambi.

Nitumie nafasi hii kuwapongeza wabunge Halima Mdee, January Makamba, Zitto Kabwe na Esther Bulaya, kwa kuungana na wasanii kutoa wimbo wa kusaidia kumchangia Sajuki ujulikanao kwa jina la Nimepoteza Mboni Yangu.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Ezekiel Kamwaga
ezepolka@yahoo.com
+255-718814875

Mwandishi ni msomaji wa Raia Mwema, vilevile ni Msemaji wa Timu ya Soka ya Simba

Maoni ya Wasomaji

Sajuki ni mwenzetu, Tumsaidie. Nia tunayo, uwezo tunao. Let's unit to save his live. Wenye kuomba na wamwombee sana.

Toa maoni yako