Kwa nini Zitto anafaa kuwa rais 2015

NINAAMINI kwamba makala haya yataniletea upinzani mkubwa sana kwa baadhi ya watu ambao hawataki kusikia mtu akisema Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Kabwe Zitto, anafaa kuwa rais.

Kwa bahati mbaya, wengi hawamfahamu vizuri au taarifa walizonazo zinatokana na wale wenye chuki binafsi naye.

Ni muhimu kwa taifa letu kuwa na mijadala mipana kuhusu watu wanaotaka kugombea nafasi kubwa na nyeti hapa nchini kama urais. Rais hawezi kuchaguliwa eti kwa vile ametoka katika chama fulani, dini fulani, ana mwonekano mzuri au kabila fulani.

Rais anachaguliwa kutokana na ajenda anazoleta mezani. Barack Obama alikuja na sera za mabadiliko (change) na atahukumiwa kwa hilo. Ni lazima tujiulize, wagombea wetu watakuja na hoja gani mezani?

Kwa nini Zitto Kabwe?

Katika mojawapo ya maandishi yake, mwanasiasa na mwandishi wa iliyokuwa Urusi, Leon Trotsky, alipata kusema kwamba kiongozi mzuri ni yule mwenye uwezo wa kuandika mawazo yake.

Kwamba ni hatari sana kwa taifa kuwa na kiongozi ambaye hawezi kueleza kwa maandishi ya walau kurasa tatu mawazo yake kuhusu mambo mbalimbali.

Trotsky alikuwa ni mwandishi mzuri na pengine aliandika hivi ili aonekane kama mbadala sahihi wa Vladmir Lenin kuliko Stalin.

Hata hivyo, ukiangalia mifano mbalimbali, utaona ukweli wa mawazo haya ya Trotsky. Julius Nyerere ameandika mara ngapi kuhusu masuala mbalimbali? Thomas Jefferson miongoni mwa marais mahiri kabisa wa Marekani alikuwa mwandishi mzuri.

Angalia maandiko ya Rais wa zamani wa Senegal, Leopord Sedar Senghor. Nilikuwa msomaji mzuri wa makala za Thabo Mbeki katika gazeti la chama cha ANC wakati alipokuwa Rais wa Afrika Kusini.

Na hadi sasa, huwa nafurahia sana kusoma makala za Yoweri Museveni kila anapoandika iwe katika vitabu au magazeti. Hata kama hukubaliani na kiongozi kwenye masuala fulani fulani, inasaidia kama unaona anawaza nini.

Miongoni mwa watu wanaotajwa kuwania urais wa Tanzania, ni Zitto Kabwe pekee ambaye anaandika mara kwa mara kwenye magazeti na mitandao mbalimbali.

Makala zake nyingi zina mwelekeo wa kiuchumi lakini huwezi kulaumu kwa sababu kitaaluma ni mchumi. Hata hivyo,
ameandika pia mambo kuhusu mtazamo wake kisiasa na kijamii.

Natoa changamoto kwa wenzangu mniambie mmeona makala za akina nani wengine wanaotajwa kuwania urais zilizotoka katika magazeti au mtandaoni katika siku za karibuni.

Obama alikuwa hafahamiki sana lakini watu walimfahamu kwa kazi zake bungeni na za kiuandishi wakati alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Harvard. Alikuwa miongoni mwa waandishi wa jarida la chuo.

Unamchaguaje mtu ambaye hawezi kukaa chini na kutafakari kuhusu lolote na kutoa mchango wake kuhusu jambo analolifahamu? Huo ni uchoyo wa kitaaluma.

Zitto pia, pengine, ndiye mwanasiasa ambaye anaweza kufiti kwenye mazingira mengi ya kijamii kuliko wengi wa wanasiasa nchini.

Nimemuona kwenye mikutano au mijadala ya kisomi katika vyuo vikuu ambako alipokewa vizuri tu. Nimemuona katika mijadala ya asasi za kijamii ambapo alifiti vizuri tu (kabla ya kuingia kwenye siasa kindakindaki alifanya kazi za kiharakati).

Nimemuona akizungumza vijijini kwao mkoani Kigoma na ungemuona sawa tu na wananchi hao. Nimemuona mpirani akishabikia klabu ya Simba au timu ya taifa kama shabiki mwingine yeyote.

Nimemuona akichanganya na wale wanaoitwa celebrities katika muziki na filamu na nikamuona amepokewa vizuri tu kiasi cha kuimba nao wimbo wa kumchangia msanii Sajuki aliyekuwa akiumwa.

Amekusanya pia wasanii wa mkoa wake na kutoa wimbo wa kuhamasisha maendeleo ya mkoa huo uitwao Leka Tutigite.

Kwenye hili, Zitto amefuata wosia wa mwanafalsafa Conficus aliyeasa kwamba kiongozi ni lazima awe karibu na jamii na asionekane amejitenga nayo.

Katika dunia hii iliyo kijiji, unahitaji rais anayefahamu mawazo na hisia za makundi mbalimbali ya kijamii. Unahitaji pia rais ambaye makundi mengi kadri iwezekanavyo yanaweza kujihusisha na harakati zake.

Majuzi hapa, katika gazeti hili hili, Zitto ameandika makala kuhusu namna Mkoa wa Lindi unavyoweza kuwa Sri Lanka ya Tanzania. Angeweza kuandika kuhusu Kigoma lakini akaandika kuhusu rasilimali za mkoa wa Lindi usio wake.

Hili lilionyesha namna anavyofikiri kama Mtanzania na si kama Mha. Lakini pia ameonyesha namna gani anafahamu matatizo ya Watanzania kiuchumi na utatuzi wake.

Tusisahau pia kwamba Zitto amejikita zaidi katika usomi wa masuala ya madini na nishati. Ninaamini kwamba huko tuendako tunahitaji rais mweledi katika masuala hayo. Huko tuendako, gesi na mafuta yatakuja kuwa rasilimali muhimu zaidi hapa nchini. Nani miongoni mwa wanaotajwa ana uelewa wa mambo haya kuliko Zitto?

Mimi pia ni miongoni mwa wale wanaoitwa romantics katika siasa. Kwamba Zitto ni mtoto wa mkulima. Hatokani na familia zile za “uchifu mamboleo” zinazoanza kujitengeneza hapa nchini.

Za mtoto wa rais mstaafu anayetaka urais. Za mke wa waziri ambaye ni mbunge wa viti maalumu. Bado wapo miongoni mwetu wanaotamani wanasiasa waliojitengeneza wenyewe. Tunaitwa romantics. Zitto anaangukia katika kundi hili la waliojitengeza wenyewe.

Katika umri wake, Zitto ametengeneza urafiki na kufahamiana na watu ambao wanasiasa wengine hata hawawajui. Tumeona mara ngapi Zitto akikutana na watu kama Mahathir Mohamed, yule mwanasiasa aliyeibadili Malaysia kutoka nchi masikini hadi tajiri?

Tumemuona akikutana na akina Keneth Kaunda. Ninafahamu ana mawasiliano ya karibu na Raila Odinga. Zitto anaaminika na karibu wakuu wote wa vyombo vya usalama nchini. Unahitaji mgombea anayeaminika na vyombo nyeti kama hivyo.

Ninafahamu kwamba kuna viongozi wa juu na waliomzidi umri Zitto hapa nchini ambao walikuwa hawafahamiani na viongozi mashuhuri wa kitaifa wa Tanzania na walikutanishwa nao kupitia kwa mwanasiasa huyu.

Watu wengi hawafahamu lakini Zitto ni mwanajumui wa Afrika (Pan Africanist). Huko nyuma ilikuwa miongoni mwa sifa muhimu za mtu kuwa kiongozi. Umujumui, pamoja na mambo mengine, unampa fahari mtu mweusi. Unampa fursa ya kufahamu mtu mweusi alikotoka.

Kwangu mimi, hii ni sifa nzuri kwa kiongozi wa nchi ya kiafrika. Tuliwapenda kina Nyerere na Nkrumah kwa sababu walikuwa wanajumui wazuri. Waliweza kuzungumza na wazungu na kueleza msimamo wao pasipo waoga.

Kama una rais mpenda uzunguni, anayetamani kuwa mzungu na asiyejua nini kilio cha mwafrika, unategemea nini kutoka kwake. Kwangu mimi, uanajumui unamfanya kiongozi kuwa mzuri.

Zaidi ya nusu ya Watanzania wana umri chini ya miaka 30. Itapendeza zaidi kama mtu mwenye maono, elimu, umri na kipawa cha Zitto akawa kiongozi wa taifa la namna hiyo badala ya kuwa na Rais ambaye anawakilisha asilimia 20 ya Watanzania kiumri.

Hebu tumchambue Zitto Kabwe wakti ungalipo. Lakini, kama atawania urais mwaka 2015, na kama Allah atanijalia uzima, kwa chama chochote au kama mgombea binafsi, ana uhakika wa kura yangu.

Nimefungua mjadala

25 thoughts on “Kwa nini Zitto anafaa kuwa rais 2015”

 1. gabriel says:

  kama alah atamjalia Ezekiel! na kweli mamluki huja katika kila rangi. inajulikana zitto yuko kwenye payrol ya ccm. kama anataka urais arudi huko huko aliko na mapenzi nako wakampe. hii makala imehaririwa na zitto mwenyewe.

 2. benedicta says:

  Uliyoyaandika yana ukweli ndani yake, kwani kwa hali ya sasa tunahitaji Rais atayetuongoza akiwa anafahamu nini Tanzania inataka na yeye awe na mtazamo unaoelewa watanzania wanahitaji nini na dira na madhumuni yake kuwania urais yawe wazi. Kwa sasa tuna wengi walioonesha nia ya urais 2015 lakini hatujui nini mitazamo zaidi ya kujua yeye yuko kundi gani.

  Jenerali ulimwengu aliwahi kuandika hatuhitaji mgombea wa urais aliye kama mbwa alionaye gari kisha akalifukuza lakini baada ya kulifikia hajui halifanyie nini zaidi ya kulinusa nusa tu….

 3. Michael says:

  Nikushukuru binafsi kwa wasifu wa Zito ambao awali sikuwa naufahamu. Wasifu wake ni mzuri na ana sifa za kugombea urais. Lakini pengine ni vema ukatoa wasifu wa majina mengine pia yanayotajwa tajwa kuutaka urais. Hii itawafanya Wantazania kuelewa wasifu wa watu hao pia. Tunapochagua ni vema tukawa na majina kadhaa badala ya wasifu wa mtu mmoja. Naamini mwendelezo wa makala haya utatuletea wasifu wa majina mengine yanayotajwa tajwa kuutaka urais.

 4. Mzee says:

  Huu mjadala wa Zitto na umri wa rais tayari umeshafungwa kule Jamii Forums. Fuatilia hapa: http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/367485-kufungwa-kwa-mjadala-wa-ujana-na-urais%3B-ujana-si-dawa-na-uzee-si-ugonjwa.html

  Waandishi kama nyie mnaonunuliwa u kujipendekeza kwa wanasiana msidhani kwa kuandika articles kama hizi mtampaisha Zitto. Watanzania siyo wajinga kama ilivyokuwa zamani.

  Watanzania ndiyo wanaamua rais wao awe nani, sio Zitto au vibaraka wake.

 5. Buluka says:

  Kuandika Makala kwenye Blog au kwenye magazeti siyo kigezo pekee cha mtu kuwa Rais. Vigezo vya kuwa Rais ni vingi. Hata hivyo, wapo watu wengine walioandika na wanaendelea kuandika kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwaelimisha wananchi masuala muhimu, mathalan Generali Ulimwengu, Padri Revotus Karugendo, Prof. Issa Shivji, Saed Kubenea na Dr. W. Slaa.

  Dr. Slaa et al, ameandika kitabu muhimu sana katika historia ya Bunge letu kinachoitwa Bunge lenye meno! Aidha, amefanya mikutano mingi ya kuhamasisha wananchi masuala mbalimbali na pia anakubalika na watu wengi hususan vijana. kama anachoongea ndicho anachomaanisha, Inaonekana ana dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko nchini. Aidha, viongozi waliowengi katika chama chetu Tawala nao wanadhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli. pia ieleweke kwamba maendeleo siyo suala la siku moja, ni mchakato unaojumuisha mambo mengi. Hivyo, kwa wote tunahitaji kiongozi ambaye ni mzalendo, muadilifu, mwenye dhamira ya kweli, asiye na upendeleo na anayeshaurika.

  Kuna usemi usemao ndimu changa haina maji na mwingine unasema bamia iliyokomaa haina thamani! na mwingine unasema ngoma ya watoto haikeshi! Tunapoamua kuchagua kiongozi tuangalie na kuchunguza umakini wa huyo mtu asije kuliangamiza Taifa letu zuri.

 6. twalib kissima says:

  Zito for president, frankly speaking the guy is competent  na kama CDM wanataka kututhibitishia watanzania kwamba ndani ya CDM hakuna ukaskazini wala udini wamsimamishe Zito watakuwa hawana maswahi mengi ya kuulizwa kipingi ch kampeni na watapata muda mwingi wa kuuza sera zao kuiliko kujitetea. viva zito.

 7. twalib kissima says:

  Zito for president, frankly speaking the guy is competent  na kama CDM wanataka kututhibitishia watanzania kwamba ndani ya CDM hakuna ukaskazini wala udini wamsimamishe Zito watakuwa hawana maswahi mengi ya kuulizwa kipingi ch kampeni na watapata muda mwingi wa kuuza sera zao kuiliko kujitetea. viva zito.

 8. Joseph M.Ndatala says:

  Nimeisoma kwa makini sana makala hii na pengine ni moja ya vitu ambavyo naweza kusema leo vimenichukulia muda. Miongoni mwa Viongozi ninaowakubali ni Pamoja na Zito, nafahamu kuwa kila binadamu ana mapungufu yake hata Zito naye anayo yake hata hivyo yapo mapungufu yanayoweza kurekebishwa kama ya Zito.

  Swala la Zito kuibua mijadala ya Urais wakati na maeneo ambayo hayafai kwa wakati huo ni moja ya mapungufu makubwa kwa Kiongozi huyu mahiri na kijana mdogo wa umri wangu, wakati huo akijua pia kwamba hata umri wake kwa mjibu wa Katiba iliyopo hana sifa za kuwa rais.

  Namaliza kwa kusema Zito anafaa kuwa rais wa Nchi kama akitulia na kuwa na weredi wa kuheshimu waliomtangulia ndani ya chama chake si kuanza kuibua maswali hata wengine kumwita CCM, hasa kwa kuwa na mahusiano na JK jambo ambalo kwa mwanasiasa makini sio tatizo maana siasa sio ugomvi. Pamoja sana

 9. jimmy maia domonicus says:

  haya bwana kwa hayo nimekukubali ila kunakitu kimoja nataka nikukumbushe wakati kikwete anatafuta urais kunamwandishi alimpaisha kikwete kama wewe akasema huyuy mtu tukimchagua nchi itanyooka sana tu manake ni mtu wa watu anajua kujichanganya ameshajichanganya sana tu na wabongo kwa hiyi anajua shida zao,lakin toka aingie madarakani imebainika ni kiongozi zaifu ambae hajawahi tokea hapa bongo toka kuwepo kwa dunia na misingi yake dhaifu kupita,alafu dhima ya chama chochote duniani huoga kinapandikiza mapandikizi yanayo igiza upinzani wakweli kiasi kwamba wananchi wanaoongalia picha wanaweza wakawa wanasifu huyu ndie kiongozi na kushangilia kabisa kumbe mwenzenu anaigiza,kwahiyo zito kwa nje ni chadema ila kwa ndani ni ccm pure bila ubishi,ukitaka kujua zitto ni ccm,yeye anajijua ni chadema kwanini akatoe mbinu kwa ccm jinsi ya kujisafisha au kuishauri ccm jinsi ya kushinda uchaguzi 2015?tangulini man ikauza siri za clabu yake kwa mpinzani wake?

 10. Mnyonge Mnyogeni says:

  TUJADILI MAHITAJI YA TANZANIA NA RAIS TUMTAKAE NA SI VYAMA

  Muanzishaji wa hoja ameweka wazi mawazo yake kuhusu sababu zilizomfanya aone ZITO ZUBERI KABWE "ZZK"  anafaa kuwa Rais wa Tanzania.  Amefungua mjadala kwa wengine kueleza mawazo yao kuhusu ZITO na urais wa Tanzania pia akitaka na wengine wajadiliwe kama wanajitokeza.

  Kwa vile hawajitokeza wanasemewa na watu wengine au vyombo vya habari nadhani si busara kuwajadili mawazo yao kwa vile hayako/hawako wazi.

  Mimi kwanza kabisa nimpongeze ZITO kwa ujasiri wa kueleza mapema nia yake na kutoa nafasi ya mjadala mpana kwa watanzania wanopenda na wasiopenda kusikia na kuona mawazo huru. Tangu alipotangaza nia kumekuwa na mijadala mingi yenye kupinga na yenye kukubaliana nae. Wale wanopinga wengi wameangalia zaidi maslahi ya chama "CDM" na wahafidhina ndani ya chama jambo ambalo sioni kama ni kukuza DEMOKRASIA  bali kuidumaza,

  ZITO ametoa wazo lake wakati muafaka kwa watanzania tukizingatia kuwa Mabadiko ya katiba yanaweza kuwa na nafasi ya kuleta mageuzi makubwa iwapo tutayatumia vizuri. Kuhusu umri gani unastahiki kwa mgombea uris, Kama kweli kilo cha vijana wote bila kujali vyama vya siasa wanavyotoka ni kuona hawapati nafasi katika uongozi wa taifa, nadhani ni muda muafaka kuutumia kupata katiba itakayojali maslahi ya vijana katika nafasi ya uongozi.

  Tumekuwa tukiletewa kiongozi ndani ya Box muda mfupi kabla ya uchaguzi na kushindwa kumchambua vya kutosha. mwisho wa yote tunalalamikia utendajin wake na Mwisho wa ukaji wake IKULU, katika kipindi hiki cha siasa za vya vingi. MKAPA mfano alisifiwa na kuonekana NDIE alipoibuliwa na Mwl. Nyerere tuliamini kuwa ndie mwisho wake wote tumetahayari, Hata mwalimu angakuwepo sijui sura yake angeweka wapi Jinsi Mkapa alivyomaliza muda wake aliyoyafanya akiwa IKULU, Pia leo hii tunamlalamikia KIKWETE utendaji wake sababu zinafanana na wale waliombeba na kudai chaguo la MUNGU wamerudi nyuma inawezekana kwa sababu ya kukosa maslahi waliyo Tarajia.

  Kwa hiyo hii ni nafasi kwa watanzania kupata nafasi ya kutosha Kutathmini Uwezo wa kiuongozi Kabla ya kuingia Madarakani. Tumeona wanasiasa wetu wengi ni wale wa kuibuka, Kwa kufuta maslahi yaliyo onekana kweye medani za siasa si wale wenye nia ya kuatumikia watanzania .

  Wanaibuliwa na makundi na kujificha humo ndio maana hutumikia makundi yao yaliyo wawezesha na wananchi kama wanavyodai wakiwa majukwaani, Tunahitaji kiongozi anaejipambanua kutoka katika jamii na mtazamo wake kuelekea jamii mzima anayotarajia kuiongoza,

  KIJAMII, Kiongozi tunaemuhitaji watanzania ni yule ambae makundi yote ya kijamii yanaweza kuunganishwa na yeye bila kujali lolote linalowatofautisha kijamii, na si yule ambaye jamii nyingine imeshampamba kwa sifa za kuipendelea jamii mojawapo au kundi mojawapomla kijamii.

  KIUCHUMI, Kiongozi anefahamu vizuri matatizo ya watanzania kiuchumi na njia madhubuti za kutatua bila kutegemea WAJOMBA KUTOKA NG'AMBO, mwenye mawazo ya kutumia raslimali zilizopo nchini, kwa mipango ya Muda mfupi na mrefu kuwezesha watanzania kufikia daraja linalofanana na Rasilimali walizonazo.

  Kiongozi wa Tanzania awe na mwenendo unaoonekana na wote bila kutiliwa shaka katika mahusiano yake na Makundi mbalimbali ya kijamii kwa mgongano wa maslahi unaojitokeza wawapo madarakani.

  Tujadili kama watanzania na si kama wana CMD, CCM, CUF, NCCR, TLP, UDP na vingine, tutashindwa kutafuta muafaka wa kitaifa kuhusu Tanzania tuitakayo na Rais aneweza kuiongoza kuifikisha huko. Kwa mtazamo wangu ZITO ameonesha kuwa anafaa kwa walijitokeza, Tuwaombe na wengine wanaohitaji wajitokeze wasizuiwe na matamko ya KICHAMA muda huu ni muafaka VYAMA VYA SIASA viache kuogopa RAIS ni wa watanzania sio wa chama cha siasa.

  ZITO MPAKA SASA ANAFAA KUWA RAIS WA TANZANIA kama na wengine wapo WAJITOKEZE umri miaka 35 inatosha kuongoza NCHI.

 11. hamidu says:

  Safi ndugu muandishi ila nafikiri umekosea kitu kimoja ktk utafiti wko uja tafiti vzuri juu ya zito kabwe kwanza umri wke kwamujibu wa katiba harusiwi pili kabwe ni kibaraka wa ccm anae tumiwa kutugawa watanzania wataka mabadiliko ya kweli nafikiri ndio tengemeo la CCM kuigawa chadema ila mkumbushe kitu kimoja maskin watanzania wamechoka na unafiki wke

 12. obeto says:

  Rais ajaye wa Tanzania 

  Mimi sina shida na jina la mtu wala umri wake. Ninachozingatia ni uwezo wa mtu; ukaribu wake na watanzania; umakini wake; uzoefu; uzalendo; uelewa na ujuzi zaidi juu ya mahitaji ya wakati uliyopo na ujao ya watanzania.

  Watanzania wengi ni watu hambao hawapendi mijadala. Katika mijadala tunakua kimawazo na kuhabarika zaidi. Nikiri tu kuwa huu mjadala ulioko mezani umeninufaisha sana kiasi cha kuweza kuchangia mawazo yangu.

  Pamoja na kuzingatia itifaki zote na sheria zitakazokuwepo; Tanzania ni lazima tutafute rais mwenye asili ya kupenda mijadala. Tunapitia kipindi kigumu sana. Kipindi ambacho tunamuhitaji rais mzalendo wa dhati kabisa. Kiongozi mwenye maono. Mchapa kazi. Mwenye maamuzi ya mwisho kwa wakati. Mtu anayesimamia maneno yake. Si kigeugeu. Mwenye uwezo wa kushirikiana hata na wapinzani wake kwenye masuala ya kitaifa.

  Wapigakura nao wanapaswa wabadilike. nashangaa kwa nini wengi hatupendi kujitokeza kupiga kura ilhali sisi ndo mara nyingi tunakuwa wa kwanza kulalamika kwa wazi na kwa kificho!! 

  Nimalizia kwa kutufautiana na mawazo ya wengi.

  Jamani waliowahi kusema kuwa mgombea fulani alikuwa ni chaguo la Mungu hawakukosea hata kidogo. Mungu ni mwema kila wakati. Binadamu kwa asili yake anajifunza vizuri akishuhudia kwa macho yake mwenyewe. "Experience is a good teacher". Mungu alituletea chaguo lake ili tushike adabu; uchaguzi mwingine ukija tusirudie makosa yetu ya awali.

  Eti hata huu ukweli kuna watanzania wenzangu wataubishia na uchaguzi hata uje leo watarudia makosa yale yale ambayo Mungu alishatufunua macho.

  Tuone zaidi ya tunayoyatazama, kuangalia na kuchungulia!!

 13. JOHN B.KASWIZA says:

  Ni kweli Mheshimiwa  Zito Kabwe ana sifa nyingi  zilizotajwa na sizizotajwa  kama  walivyo  wananchi wengine katika  vyama au wasio na  vyama.Ndugu yangu Ezekiel  mawazo yako ni sahihi  kwa  upeo wako na wale wanaokubaliana nawe, ni haki yako  ya  msingi na ambayo  hata  wasiokubaliana  nawe  na  wasiofungamana  na  upande wowote  wanayo.TATIZO KUBWA ULILOKUWA  NALO WAKATI  UKIFANYA  UCHAMBUZI WAKO  NI  KWAMBA" UWEZO WAKO  WA  KUFIKIRI WAKATI UKICHAMBUA JAMBO HILI  ULIKUWA  KATIKA  KIWANGO CHA  CHINI   SANA".Jizuie kufanya MAAMUZI

  katika  mambo ambao  tayari unamafungamano nayo,waachie wengine wasio na mafungamano wafanye vinginevyo hutatenda HAKI  na wala HAKI haitaonekana kutendeka. Kwa kifupi haukutenda haki katika  uchambuzi wako  kwa  sababu  ya kuwa  na  mafungamano (BIAS)."Logically, when someone is biased, hisor her  ability to reason becomes extremely low".

 14. godfrey mwanakatwe says:

  Kwangu mimi binafsi kuandika tu sioni kama ni hoja yenye nguvu sana, Nyerere aliandika sana na maandishi yake mazuri tu yapo mpaka leo lakini hayakutekelezwa na wala hayakueleweka na hayaeleweki mpaka sasa kwa kuwa waliopo hawayatekelezi, na waliokuwa na nyerere hawakuyatekeleza yamebaki kuwa ya nyerere peke yake.Kwangu mimi rais ajaye suala la kuwa na uwezo wa kuandika mawazo yake ni sifa ya ziada tu, nahitaji rais ajaye awe ni mtu ambaye anajua tanzania imetoka wapi, ipo wapi na wapi inatakiwa kwenda. Awe ni rais ambaye anaelewa watanzania wanahitaji nini, na awe tayari kutimiza mahitaji ya watanzania kwa namna yeyote ile na wala siyo kupokea mambo toka mataifa makubwa na kuyaleta tanzania, kuifanya tanzania ndio nchi ya majaribio ya mahitaji ya mataifa makubwa,hapana hatuhitaji rais wa namna hiyo.Ili kutekeleza hayo, tunahitaji rais ajaye wa tanzania azielewe siasa za kidunia zilizopo ili ajue jinsi ya kucheza nazo kuleta tanzania yenye neema, siyo kugeuza tanzania shamba la bibi. Kama zitto anakidhi hayo sina tatizo naye.

 15. pr.magoma kisse says:

  siku zote hakuna mtu ninaemchukia kama mlevi,si kwa sababu ya kelele zake-wako wakimya,si kwa sababu ya matusi-kwangu hizo ni ngonjera;ila zaidi namchukia mlevi kwa sababu hana uwezo wa kufikiri vizuri-ukikataa sintakulazimisha.

  nasikitika kwamba,katika wakati huu tulionao-wakati ambapo tunahitaji zaidi watanzania wazalendo,wenye uwezo wa kuiona tanzania na matatizo (wengine huyaita changamoto) yake kwa uwazi na uhuru;nasikitika kwamba bado tunao watanzania walevi-ambao hawana fikra huru na makini.

  nasikitika kuona kwamba bado tuna watanzania ambao wamefungwa na mikatale ya udini,uchama,ukabila n.k.

  ndugu mwandishi wa makala haya,sijui kama umetumwa au la – ila umenikosha;umenikosha kwa hoja za msingi ulizozitoa.wanaoona kama hauko sahihi,wajibu hoja.

  namalizia kwa kusema hivi,mashabiki na wafuasi wa CHADEMA;msidhani CHADEMA NI MBOWE AU SLAA – CHADEMA NI WATANZANIA,wakiamua lolote laweza kuwa.acheni ULEVI,ACHENI USHABIKI – JADILINI HOJA KWA UMAKINI.

 16. Pierre says:

  Kwa kuwa hatuna vigezo vya kumchagua kiongozi katika nchi yetu hata mwendawazimu anaweza chaguliwa sio jambo la kushangaa.

 17. Eliabu says:

  Siku watanzania tukiacha unafiki katika masuala ya kitaifa, tutasogea toka tulipo sasa. Mjadala ni mzuri na umekuja wakati muafaka kabisa, sijajua ikiwa kuna ulazima wa kutetea upande fulani kwa sababu binafsi zaidi ya zile za kitaifa. Kwangu mimi natamani sana wengi wajitokeze mapema kama Zito ili tuwaweke jamvini kama hivi. Si sawa kumpa nafasi sana Zito eti kwa kuwa kajitokeza bali tuangalie uwezo wake, uzalendo na dhamira yake dhidi ya taifa letu. Wala hatuitaji kumpa mtu Urais kwa sababu za kimihemko kama tulivyofanya 2005.

  Nawasilisha!

 18. Kevin Jakob says:

  Nyerere aliingia madarakani akiwa na umri chini ya miaka 40. Alikuwa na miaka 39. Kagame, Kabila Joseph, Rais wa Swaziland wa sasa wote wameingia madarkani wakiwa na umri chini ya miaka 40. Umri usiwe sana hoja, bali uwezo wa mtu  na upeo wake.

  Zitto ameonyesha uwezo ingawa hajatimiza miaka 40. Sifa kubwa aliyo nayo ni ujasiri wa kukemea uozo. Amelifanya hili hadi kufukuzwa kwa muda bungeni mara kadhaa. Urais wenye dhamira ya kuwakomboa watanzania na uonevu unahitaji jasiri. Nyerere aliaminiwa na watanzania kwa sababu hakuwa na ubinafsi na alikuwa jasiri wa kukemea hata watawala. Je zitto hizo sifa mbili anazo? Ndiyo. Amekemea mara nyingi utawala wa CCM. Amekemea utaratibu wa wabunge kujiongezea posho(si mbinafsi). Huyo ndo kiongozi anayetufaa.

  Endapo Chadema itakamata usukani na kama Zitto hatapata urais basi  aambulie uwaziri mkuu. Ni mtendaji mzuri. Style ya Lowassa vile, tofauti hana kashfa huko nyuma.

  Masuala ya madini na nishati ni nyeti. Yanaweza kuliangamiza taifa. Tumeona jinsi Wizara ya madini na nishati ilivopata wakati mgumu kutokana na uelewa finyu/ufisadi  kuhusiana na mikataba mbali mbali ya madini na nishati. Na taifa letu litaendelea kuwa shamba la bibi likinufaisha wachache na kuwakaanga wengi endapo hatutakuwa makini na suala hili. Zitto kajiandaa kwa kusomea maswala haya na hata kutoa ushauri kwa wizara husika mara kadhaa ili kukosoa kasoro fulani za kiutendaji. Kiongozi tumtakaye lazima awe sensitive na ukandamizaji unaoweza kulikumba taifa letu kutokana na mikataba mibovu kwa kuiweka wazi(siyo kuifanya siri) na kukwepa mitego ya kulikandamiza taifa kama mkataba wa IPTL(kulipa hata kama mitambo haizalishi).

  Mimi sio mwananchama wa CHADEMA lakini kijana Zitto sitasita kumpa kura yangu. Sijawahi kumwona, nasoma habari zake. Navutiwa na hoja pamoja na ujasiri wake.  

  Nimwombe Zitto aendelee na ujasiri huu hata kama atarubuniwa na CCM kama Kabourou alivyogeuka baada ya kurubuniwa. Sasa hivi yuko kimya, cheche hamna tena.

  Kwamba Zitto atakuwa mgombea hilo linategemea na katiba wakati wa uchaguzi na vile vile kauli ya chama chakeCHADEMA. Inawezekana chama hiki kikamsimamisha mgombea mwingine. Hatuwezi kukiamulia na wala Zitto hawezi kukishurutisha. Hili likitokea kuna mawili kwa Zitto: ama kukubali uamuzi huo wa chama chake ama kujiunga na chama kingine ama kuwa mgombea binafsi endapo katiba mpya itakuwa imeruhusu.

  CHADEMA nao wanamgwaya Zitto, kajitangaza kwamba anataka kugombea lakini chama chake hakijamkanya kwa sababu ruhusa rasmi ya kujipigia debe au kujitangaza haijatolewa na chama chake. Wanaona kinachoendelea huku wakitafakari kimya kimya. Wanajua ana uwezo na nadhani hawataki kumtibua kwani hii inaweza kuleta mpasuko wa chama. Lakini katika CHADEMA wapo wanaoutamani urais. Mmoja ni Dr Slaa. Huyu hajatangaza nia ya kugombea. Ni mjanja, anajua taratibu anasubiri ruksa ya chama chake na vile vile kwa kuwa ana maadui nje kujitangaza kunaweza kuharakisha mbinu chafu kutoka kwa maadui wake. Anasubiri wakati muafaka.

  CHADEMA kutomkemea Zitto kwenye vikao rasmi ni kuheshimu uhuru wa mawazo. Ni ukomavu vile vile. Wakati ukifika basi wenye nguvu watapimana ndani ya chama. Lakini ni lazima uongozi wa chama hizho uangalie historia na kukubalika kwa mtu.

  Umri wa Zitto unapaswa kuwa mtaji kwa CHADEMA. Hebu fikiria ni vijana wangapi watamchagua mgombea wa CHADEMA kama mgombea huyo atakuwa kijana! Vile vile uwezekano wa Zitto kuwekewa vipingamizi wakati wa kugombea ni mdogo kwa sababu hana kesi mahakamani. Unapokuwa na kesi mahakamani huo ni mtaji kwa wabaya wako wakati wa kugombea.

  Mungu atusaidie tufanye uamuzi wa kweli katika kuwapata viongozi wetu. Maana uamuzi mbaya ni hasara kwetu. Sisi wenyewe tutaanza kulaani: Oh kwa nini tulimchagua, tungejua nk

  Lakini uchaguzi mzuri unahitaji uelewa. Wengi vijijini wakipewa kanga, kilo ya sukari na fedha kidogo mgombea anapita. Baadaye, kama ni mbovu, hao hao wanaanza kulia. Hayo kwenye nchi zilizoendelea hayapo. Ni sifa za mtu ndo zinampa ushindi, si zawadi anazotoa wakati wa uchaguzi. Ili mgombea wa CHADEMA aweze kupita lazima wananchi vijijini wapigwe msasa mapema kupitia kampeni za uhamasishaji.

  I

   

 19. marina says:

  Huyu ni mtu mmoja tu katoa maoni yake bado wako wengi  watatoa maoni sawa na ya kwake au tofauti

  na mawazo yake.Wakati ukikaribia utatoa majibu.

  Kabwe ni miongoni mwa viongozi wengi wanaofaa kugombea urais,nawataja,Lowasa,Membe,Slaa,Lipumba

  ,Magufuli,Makyembe,Mandosya na wengine wengine siwajui.Mtu akiimba wimbo wake msikilize usimkatishe tamaa. 

   

 20. Msomaji wetu says:

  kweli zitto anafaa kuwa rais 2015 tuachane na uanachama, ushabiki katika siasa bali tuangalie mtu atakaye beba nafasi hiyo nakwa ajili ya mali ya mtanzania, selikali ya tanzania na kujali mtanzania na si raisi wa watanzania kwa niaba ya wazungu. kumbuka tufikiri kabla ya kutenda naningejua huja badaye. kwaiyo tuchague rais anaye faa kuwa kiongozi kwa kutofata itikadi za vyama

 21. Safari says:

  Zito huyu huyu anayesapoti SSRA kuchukua mafao yetu kuneemesha mafisadi au Zito mwingine mimi hapana hapati kura yangu…zito hajengi chama ila anabomoa chama kwa kujiweka mbali na maamuzi mengi ya chama..kuhusu kujua uchumi au kuwa umesoma uchumi sio sifa hata kidogo..kwani JK kasomea nini? je unaweza kumlinganisha na Mkapa katika kukuza na kusimamia uchumi?Mkapa aliangushwa na system mbovu ya kudhibiti rushwa ila kiuchumi alifanikiwa zaidi ya raisi yoyote TZ kwa hiyo kusoma uchumi si hoja kabisa…kuhusu kuwa karibu na watu hamna kitu kwani Kikwete hayuko hivyo wa kwanza kuwahi kwenye misiba…Mimi namtaka raisi mkali, raisi asiyetaka sifa nyepesi nyepesi, raisi anayeweza kutoa order mpaka mbwa wakatetemeka, raisi anayejenga nchi, raisi anyesimamaia maamuzi ya Wanachama wenzake baada ya kupitishwa hata kama hakubaliani nayo kwa sababu huyu tutaweza kumwambia hapana kwa pamoja na akatekeleza sio raisi ambaye yeye anadhani ni mjuvi sana kuliko waTZ wengine! My vote either Magufuli au Slaa only…Najua nikitaja watu hawa mtandao wa wezi unatetemeka

 22. Dr.DAVID GULULI says:

  ni wazi pasipo shaka,mwandishi umekodiwa kufanya hii kazi,dhamira binafsi ya zito mwenyewe wala

  sio kweli kwamba anataka urais,na anajua kabisa hata akipitishwa hawezi kushinda hata nafasi ya pili

  hawezi kupata,kwahiyo huu mpango kamili wa kizandiki na kijasusi unaotumiwa na CCM,kudhoofisha

  nguvu ya chadema kisiasa,kwa hiyo watu acheni kushabikia uhalisia msioujua.Zito ni mvurugaji tu na

  ni pandikizi kwelikweli na ni msaliti numba moja kwa watanzania

 23. Japhet Azariah says:

  kabwe hanauwezo wa kuongoza nchi yetu kutoka kwenye mifumo iliyotengenezwa ya kifisadi na kubebana coz yeye anategemea kubebwa pia, mwandishi kumbuka zitto anafanya hayo yote ili awe raisi, ukimtazama vizuri hata kwenye malumbano yake ya hoja huonyesha kuwafanya watu wamfurahie zaidi na siyo kusimamia muono wake wa kizalendo. Kutangaza nia yake mapema mm nimeitafsiri kwa kuhisi niko sawa na nia yake kuwa, anahitaji watanzania washawishike na vitendo vyake vya kishawishi vya kutoa hoja ili aonekane anafaa kuwa raisi. Sinakumbukumbu vizuri ya alichokifanya kwenye kamati yamadini dhidi ya karamagi. amini usiamini  zitto ni tapeli, hanatofauti na mrema, tuweni makini

   

 24. nelson c.mkude says:

  tapeli wa fikra tu huyo hatuwai leo hata baadae hafai tena.

 25. Sylvester Cosmas Vungu says:

  Japo nimechelewa ,ninawiwa sana kumpongeza mwandishi kwa kuanzisha mjadala huu muhimu kwa mtakabari wa maendeleo ya taifa letu tukufu;ninaamin Zitto Kabwe anaouwezo mkubwa wa kuwa kiongozi mkubwa wa nchi kwa wakati umfaao,ninaona ni vema akaendelea kujiweka karibu na watu mbalimbali ndani na nje ya nchi katika idara mbalimbali ili kujiongezea ujuzi utakaomrahisishia kufanikisha lengo lake hapo baadae,InshaAllah.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *