Michezo
Kwani Maximo nani asikosolewe?
Ibrahim Mkamba
Toleo la 032
4 Jun 2008

NATOA maoni yangu leo nikijua nitakosana na marafiki zangu kadhaa wakubwa na watu ninaowaheshimu sana lakini kwa kuipenda sana nchi yangu na kwa kutambua ninayo haki kikatiba kutoa maoni, naomba niseme ninachokusudia.

Naomba nitangulie kusema kwamba, maoni yangu hayahusiani na matokeo ya sare ya nyumbani dhidi ya Mauritius.

Matokeo hayo ni ya kuridhisha kwa kuzingatia jinsi wenzetu walivyofanya maandalizi ya nguvu Ufarannsa yaliyojumuisha mechi za majaribio na timu kubwa za nchi hiyo wakati sisi tukiishi kwa matumaini tu ya "lazima Mauritius tuwafunge mengi" bila kufanya lolote la maana la maandalizi ya mechi hiyo!

Zaidi ya hayo,sare ni moja ya matokeo matatu ya mechi, mengine yakiwa ni kushinda na kushindwa.

Maoni yangu yatakayonikosanisha na baadhi ya ninaowaheshimu yanamhusu Marcio Maximo, kocha wetu wa timu ya Taifa.

Kocha wetu huyu anaabudiwa mno, anapewa hadhi inayozidi stahili yake na baadhi yetu tunaogopa mno kumkosoa kwa kuwaogopa Watanzania wenzetu!

Kocha wetu huyu anaabudiwa kwa sababu imekuwa ni dhambi kubwa mno kusema makosa yake ingawa ni binadamu kama wengine asiyeweza kukwepa kutenda makosa.

Ukisema kocha wetu amekosea jambo fulani, unakuwa umetenda dhambi isiyosameheka!

Kwa hiyo, ili uingie peponi, jilazimishe kuongea pongezi tupu kuhusu kocha wetu huyo!

Kocha wetu anapewa hadhi inayozidi stahili yake. Hata timu yetu anayofundisha ikiharibu kazi, tunafanya kila liwezekanalo kutafuta wa kumbebesha lawama lakini si kocha wetu huyo.

Hali tuliyonayo nchini kwa sasa ni kwamba kila mtu ana uhuru wa kikatiba wa kusema chochote ili mradi havunji sheria lakini chochote hicho kisiwe kumkosoa Maximo!

Ninaamini hivyo kwa sababu, kila mara tunaambiwa tumuache kocha afanye kazi yake, tusimuingilie.

Yaani, tuache kusema makosa yake? Cha kushangaza, zuri lolote likitokea kuihusu timu yetu ya Taifa, wote tunatakiwa tuungane, kupongezana na kushangilia mafanikio.

Kwa nini mshikamano huu uwe kwenye kupongezana tu wakati kwenye kukosoana tunafumbana midomo?

Tena wakati mwingine tunafumbana midomo kwa msingi wa mtoa maoni huyu alicheza soka, huyu hakucheza, huyu alifundisha soka timu ya taifa akashindwa kupata mafanikio na kadhalika.

Inawezekana Mtanzania huyo alifundisha bila mafanikio kwa sababu alikuwa hana msaada wa Serengeti Breweries inayomwaga pesa za kutosha sasa kwa maendeleo ya timu yetu ya Taifa.

Inawezekana mtoa maoni huyu hakuchezea Yanga wala Simba lakini alichezea CIBA ya Magu au Mazulia ya Kilosa.

Asipojua chochote kuhusu soka, hatoi maoni ya soka. Kwani viongozi wote wanaoongoza soka letu walicheza soka la kuwafanya watambulike kupitia soka lao?

Naomba tusidanganyane, hakuna kocha duniani asiyeelezwa kitu na wadau mbalimbali wa soka hata kama kocha huyo ni maarufu kiasi gani.

Kinachofanyika, na ninachokubali, mwenyewe atachambua cha kufuata na cha kuacha na halazimishwi achukue kipi au aache kipi, maamuzi ni yake tu.

Mbona hata hapa, Maximo alimchagua Haruna Moshi kwenye timu ya Taifa baada ya maneno ya wadau na matokeo yake yakawa mazuri?

Nani atakataa kwamba mchezaji huyo alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu hiyo baada tu ya kujiunga nayo?

Alitoa pasi ya bao la Nizar Khalfan dhidi ya Senegal mjini Mwanza katika sare yetu na Senegal ya 1-1.

Siku hiyo angeweza kusogea na mpira huo kuelekea golini na kujaribu golini mwenyewe.

Ni mchezaji huyo aliyetoa pasi safi kwa Erasto Nyoni aliyefunga bao Burkina Faso na timu yetu kupata ushindi wa ugenini wa hilo bao moja dhidi ya wenyeji Burkina Faso.

Haruna alifanya hivyo mahali ambapo angeweza kupiga mwenyewe golini. Ni Haruna Moshi huyo huyo aliyetoa pasi kwa Abdi Kassim aliyefunga bao dhidi ya Uganda katika mechi ya uzinduzi wa uwanja wetu wa kimataifa.

Bila maneno ya wadau, ni wazi Maximo, timu ya Taifa na Watanzania wote wangekosa huduma hiyo nzuri ya Haruna Moshi kwenye timu yetu ya Taifa.

Leo hii wote tunauona mchango mkubwa kwa timu yetu ya Taifa wa mchezaji mwenye kiwango cha juu, Mrisho Ngassa.

Makocha wote wa timu pinzani za nje waliomuona mchezaji huyo wanasema, kiusahihi kabisa, kwamba kijana huyo anaweza kucheza soka popote duniani!

Mchezaji huyo, ameingia kwenye timu yetu ya Taifa kupitia juhudi za Watanzania wengi kuomba mchezaji huyo ajumuishwe kwenye timu hiyo.

Kama tulisema alikosea kuwaacha nje ya timu ya Taifa kina Haruna Moshi na Mrisho Ngassa na alipokubali

kufanya tulivyomshauri matokeo yakawa mazuri, hatupaswi kuzibwa midomo kusema kwamba anakosea kuendelea kumuacha nje ya kikosi chake Juma Kaseja kwa sababu ya utovu wa nidhamu usiokwisha.

Nani mwenye nidhamu nzuri mwenye umri unaozidi kidogo miaka 20 ambaye hajafanya kitendo cha utovu wa nidhamu kufikia umri huo, hasa anapojihusisha na soka?

Wengi walishafanya hivyo, waliadhibiwa na sasa wamekuwa mfano mzuri kwa wengine kwa nidhamu bora.

Ni wazi Kaseja akirudishwa kundini sasa atakuwa mwalimu wa nidhamu kwa wenzake.

Maneno ya wanaomtaka Kaseja kwenye timu ya Taifa yataonekana ya muhimu siku Ivo Mapunda atakapopata dharura katika mechi yenye umuhimu mkubwa kwetu.

Hapo ndipo itakapokuwa balaa kwani wachezaji wa akiba wa nafasi yake, hawaaminiki na makocha wao, wachezaji wenzao na Watanzania wengine.

Matokeo yake, hata wenyewe hawajiamini. Atakayecheza badala ya Mapunda ni wazi atakosa kujiamini, ikizingatiwa umuhimu wa mechi hiyo kwa Taifa, ukubwa na ukali wake, hasa ikiwa ya ugenini.

Nawasihi sana Watanzania wenzangu, tuache Maximo aambiwe chochote cha maana na Mtanzania yeyote yule kama anavyofanyiwa kocha yeyote yule duniani.

Mwenyewe ndiye mwenye maamuzi ya mwisho ya nini cha kufanya. Kufumbana midomo huku baina ya Watanzania na Watanzania kunafanya watu waogope kusema lolote la maana kuhusu timu yetu ya Taifa kwa kuogopa shutuma, matusi, kejeli na kutengwa kwa sababu kufanya hivyo kunaonekana na baadhi ya Watanzania wenzetu kama kufuru kubwa!

Ukweli ni kwamba kumwambia kocha wetu Maximo amekosea mahali si dhambi wala uhaini bali ni upendo wa dhati kwake, kwa timu yetu ya Taifa na kwa nchi yetu kwa ujumla.

Uhuru huo tu wa kusema, ndiyo utarudisha upendo wa asilimia zote wa Watanzania kwa timu yao ya Taifa.

Sehemu yetu wamepunguza upendo kwa timu hiyo kwa kutengwa wanapomkosoa kocha wetu na kuwafanya wajione kama si sehemu ya Taifa hili. Mungu Ibariki Tanzania.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako