Kengele hizi sasa ni za uamsho kwa CHADEMA

WIKI iliyopita kulikuwa na makala kwenye gazeti la Raia Mwema iliyoandikwa na mtu  anayeitwa Nasir Mshanga katika kurasa za kati za toleo lililopita. Makala hiyo iliwaudhi baadhi ya Watanzania wanaotaka mabadiliko.

Makala hiyo ililenga katika kujenga taswira kwamba CHADEMA ni chama hovyo, na kwamba viongozi wake hawastahili kuaminiwa na Watanzania kuongoza dola.

Huo ni mtazamo wa ajabu kidogo, kwa sababu ukiweka ushabiki wa kichama kando, ukweli unabaki palepale; nao ni kwamba chama kilichojipatia viti 48 vya bunge katika uchaguzi uliopita na kilichosaidia mno kubadilisha namna Watanzania wanavyoitathmini Serikali yao, hakiwezi kuwa cha hovyo kwa namna ambayo Mshanga alijaribu kuwaaminisha Watanzania katika makala ile.

Binafsi, sina matatizo na mtu kutoa gazetini mtazamo wake kuhusu CHADEMA au jambo lolote lile; maana, kwa hakika, magazeti ni viwanja vya majadiliano, maoni, mitazamo na hoja zinazokinzana.

Hata hivyo, nikiri kwamba makala ya Nasri Mshanga ilionyesha chuki ya hali ya juu ya mwandishi huyo kwa CHADEMA, na hasa viongozi wake.

Kuna mahali, kwa mfano, anawakejeli Slaa na Mbowe eti walikamatwa wakiwa na bastola huko Arusha, lakini hasemi lolote kuhusu mbunge wa CCM, Aden Rage, ambaye alipanda jukwaani huko Igunga wakati wa kampeni akiwa na bastola kiunoni!

Vyovyote vile; nimeichukulia makala hiyo ya Mshanga kama ni ya mwana CCM aliyeshikwa na hofu – hofu kwamba chama chake pendwa (CCM) kinakaribia kung’olewa madarakani na CHADEMA.

Na yawezekana kabisa hofu ya Mshanga na wana CCM wa aina yake, inatokana na kwamba wananufaika, kwa namna moja au nyingine, na mfumo wa sasa, na hivyo wangependa kuendeleza status quo.

Lakini kwa upande mwingine, Mshanga alizungumzia kitu kingine ambacho viongozi wa CHADEMA wanapaswa kukitafakari kwa makini: nacho ni tabia ya chama hicho kupoteza muda mwingi kuzungumzia lugha za maandamano; kana kwamba inafikiria inaweza kutwaa dola kwa “nguvu za umma”.

Jambo hilo pia lilijadiliwa vyema katika makala nyingine iliyoandikwa na Mayage S. Mayage kwenye toleo hilo hilo la Raia Mwema yenye kichwa cha habari kinachosomeka: “CHADEMA isonge mbele, inawezekana.”

Katika makala hiyo, Mayage naye ameishauri CHADEMA isipoteze muda na shughuli za uanaharakati, na badala yake ianze kujenga mtandao wa ushindi wilayani na vijijini.

Kwa maneno mengine, CHADEMA kinapaswa kuwa bize, si kupanga maandamano nchi nzima;  bali kuandikisha wanachama vijijini, kufungua matawi hadi ngazi za wilaya na kuweka mitandao ya ushindi.

CHADEMA kinapaswa kutumia muda mdogo kuendesha shughuli za kiuanaharakati kama hizi za kudai Katiba mpya, na badala yake kijikite zaidi katika kufungua matawi wilayani na vijijini na kuandikisha wanachama; huku kikiweka mitandao ya ushindi.

Kisipofanya hivyo, kitajikuta Katiba mpya imepatikana 2014  na uchaguzi wa mwaka 2015 umekaribia, lakini chenyewe hakijajiandaa huko vijijini kushinda uchaguzi huo.

Katika mazingira hayo, kitabwagwa tena na CCM; hata kama kuna Katiba mpya, na hata kama kuna tume huru ya uchaguzi.

Kwa hiyo, pamoja na chuki iliyomo katika makala ya Mshanga, inafaa viongozi wa CHADEMA waichukulie, pamoja na ile ya Mayage, kama ni kengele ya uamsho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 ambao hauko mbali. Maana, hakika, muda unayoyoma kwa kasi kwa CHADEMA kujiandaa vyema kwa uchaguzi huo.

3 thoughts on “Kengele hizi sasa ni za uamsho kwa CHADEMA”

  1. wabhukaba says:

    I concur with Nzinyangwa, at least chadema needs pull up socks on members and not members only also open offices to coordinate party activities. They should leave their offices and go out to mobilize members.

  2. Appofral says:

    get cheap emu ugg boots xAXekIsg [URL=http://www.cheap-uggboots.tumblr.com/ – ugg boots melbourne[/URL – to get new coupon ItZbWtsl http://www.cheap-uggboots.tumblr.com/

  3. Msomaji wetu says:

    Nakubaliana kabisa na Bwana Nzinyangwa. Tatizo kubwa linalo tukabili wananchi tukiachana na umaskini ni uelewa wa mambo na kutojua haki ya kila mwananchi. Nchi yetu ya Tanzania inahitaji mabadiliko makubwa sana, na kama wananchi wake hawana uelewa basi itakuwa ndoto kupata hayo mabadiliko. Chadema inahitaji nguvu ya uhamasishaji wa hali ya juu ili kutimiza malengo ya mabadiliko. It can be done.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *